Monday, March 31, 2008

Mashaka Yaanza Zanzibar

Kile kilichokuwa kikihofiwa siku zote, sasa kinaweza kutokea. Hali ya mambo kisiwani Zanzibar imeanza kuwa ya wasi wasi kutokana na maamuzi yaliyofikiwa katika kikao cha NEC ya CCM huko Butiama.

Kinachoonekana kikuweka rehani kisiwa hicho ni kukengeuka kwa CCM na kuamua kupindisha kilichokubaliwa katika kamati ya Mazungumzo na kutaka ifanyike kura ya maoni kuhusu kuanzishwa kwa serikali ya Mseto visiwani humo.

Katika kile kinachoashiria kuwa hali ya mambo imeanza kuwa mbaya, wajumbe wa Baraza la wawakilishi wa CUF, waliacha kuendelea na vikao vya baraza na kwenda katika makao makuu ya chama chao ambajko ulifanyika mkutano.

Habari kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa wajumbe hao wametakiwa na wanachama wao kususia vikao vyote vya baraza la wawakilishi.

Aidha, kuna taarifa pia kuwa wanaCUF wamewataka wabunge wao kutohudhuria vikao vya Bunge, linalotarajia kuanza kukutana mjini Dodoma wiki ijayo.

Wajumbe hao wa CUF walitoka Barazani wakiongozwa na Mnadhimu wa kambi ya upinzani, Soud Yussuf Mgeni, muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu kumalizika.

Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma na Haki za Binaadamu wa CUF, Salum Bimani alisema kwamba kikao hicho kiliitishwa baada ya viongozi wa chama na wajumbe wa Baraza hilo kupewa ujumbe wa simu kutoka kwa wanachama kuwataka wasusie mara moja vikao vya Bunge na Baraza la Wawakilishi.

Tayari watu kadhaa wameshaanza kuonyesha wasi wasi wao kutokana na maamuzi yaliyofikiwa na CCM , ambayo yabnaonekana kurudisha nyuma hatua iliyokubaliwa na Kamatio ya Mazungumzo ambayo iliwashirikisha wajumbe kutoka CCM na CUF.

Katika mazungumzo hayop, ilikubaliwa kuwa iundwe serikali ya mseto Zanzibar, ambapo chaka kitakachoshinda uchagzui kitatoa rais na kile kinachofuatia kitatoa waziri Kiongozi.

Lakini suala hili limekuwa likipingwa miaka yote ya wahafidhina walio ndani ya CCM Zanzibat na wamejiapiza kuwa kamwe hawatoiruhusu CUF katika serikali yao.

Biomani alisema kuwa CUF kimepokea maamuzi ya NEC lakini kitatoa maamuzi yake Jumanne kupitia mkutano na waandishi wa habari, ambao utahutubiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Wakati huo huo, uamuzi wa NEC ya CCM kuwa suala hilo liamuriwe kupitia kura ya maobni, limezua mjadala visiwani hapa, huku baadhi ya watu wakipinga wazo hilo.

Katibu wa TADEA, Juma Ali Khatib, alisema suala la kuitisha kura ya maoni juu ya serikali ya pamoja visiwani humu si muafaka kwa sasa kwa sababu muda uliobakia ni mdogo.

Alieleza kwamba Kamati ya Mazungumzo ya CCM na CUF ilipaswa kulitambua hilo mapema, kwa vile linagusa katiba na sheria za uchaguzi.

Naye Mkurugenzi wa Habari wa NCCR-Mageuzi, Ali Omar, alisema kwamba wakati muafaka umefika kwa Rais Jakaya Kikwete kutangaza kuwa ameshindwa kutatua mpasuko wa kisiasa wa Zanzibar.

Alisema kwamba kwa kuzingatia kuwa suala la serikali ya mseto linahusu maslahi ya taifa halikupaswa kurejeshwa kwa wananchi kwa vile hatua hiyo ni sawa na kupoteza muda.

“NCCR-Mageuzi tunavyoona Rais Kikwete ameshindwa kutekeleza ahadi yake ya kumaliza mpasuko wa kisiasa kama alivyoahdi katika Bunge,” alisema kiongozi huyo.

mwisho

Wednesday, March 19, 2008

Timu ya Pinda Yakamilisha Kazi

Timu iliyoteuliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kupitia kwa kina mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa Richmond, imemaliza kazi yake na kukabidhi ripoti.
Pinda amesema kuwa hivi sasa, serikali inaipitia ripoti hiyo kabla ya kutoa maamuzi kutokana na mapendekezo ya Timu hiyo.
Katika ripoti yake, Kamati teule ya Bunge iliyokuwa na wajumbe watano chini ya uenyekiti wa Dk. Harison Mwakyembe, ilipendekeza watumishi kadhaa wa umma, walio katika ngazi za juu serikalini, wachukuliwe hatua kutokana na uzembe uliosababisha taifa kupata hasara kupitia mkatana huow a Richmond.
Mtumishi mmojawapo mkubwa wa umma ambaye kamati hiyo imependekeza awajibishwe ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, John Mwanyika, kutokana na kile kilichoelezwa na kamati kuwa ni kushindwa kwa ofisi anayoiongoza kuishauri vema serikali katika suala hilo.
Pia, pamoja na kushauri hatua zichukuliwe dhidi ya Mkurugenzi wa Takukuru, kamati hiyo inapendekeza pia taasisi hiyo imulikwe baada ya kutoa taarifa iliyoonyesha kuwa kimsingi hakukuwa na tatizo lolote la ufisadi katika mkataba wa Richmond.
Tayari aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na mawaziri wawili, Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, walishajiuzulu nyadhfa zao baada ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo Bungeni.
Kukamilika kwa ripoti hiyo kunafanya idadi ya ripoti kuhusiana na sakata la Richmond kufikia tatu baada ya timu nyingine iliyohusisha wanasheria wa Bunge kuipitia mikataba baina ya Tanesco na makamopuni binafsi ya kzualisha umeme, ukiwemo wa Richmond.
Wataalam hao wa washeria walibaini kwua mikataba na makampuni matano baina ya sita ilikuwa inafanana kwa kiasi kikubwa na kuleta wasi wasi wa umahiri wa watu walioandika au kuidhinisha mikataba hiyo.

Friday, March 14, 2008

BOT sasa yaiogopa EPA!

Baada ya moto uliowaka sasa inaonekana kuwa akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA) ni moto kweli kweli na Benki Kuu imeonyesha dhamira ya kutaka kujitoe kuendesha akaunti hiyo.

Gavana wa BoT, Benno Ndulu amesema leo kuwa tayari BoT imeshawasiliana na mtaalamu, ambaye ni kampuni moja kutoka nchini kutoka nchini Ufaransa, ili aje kufanya tathmini itakayosaidia kuamua iwapo akaunti hiyo iendelee kubaki BoT au la.

Lakini Ndulu amesema kuwa kimsingi, EPA si sehemu ya shughuli za BoT na ndio maana wanataka kuiondoa akaunti hiyo chini yao.

Gavana Ndulu amesema kuwa kampuni hiyo itatakiwa kukamilisha kazi yake kabla ya katikati ya mwaka huu ili uamuzi wa wapi akaunti hiyo iwekwe ufanywe. Inaonekana kuwa lengo lake ni kuhakikisha kuwa unapoanza mwaka mpya wa fedha mwezi Julai, shughuli za akaunti hiyo zikabidhiwe kwa taasisi inayostahili kuiendesha.

Awali, kabla ya kuhamishiwa BoT, akaunto hiyo ilikuwa ikiendeshwa na NBC.

Baada ya kuhamishiwa BoT, wajanja wachache, kwa kutumia nyaraka za kughushi na ulaghai, walichota kisi cha sh bilioni 133 kutoka katika akaunti hiyo.

Wizi huo ulibainishwa na wanasiasa, hasa wa upinzani walipozungumza bungeni, ingawa viongozi wa serikali walijipanga kukanusha.

Hata hivyo, mbinyo wa wapinzani uliendelea hadi serikali kulazimika kuialika kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu wa Ernst & Young ambayo mwishoni mwa mwaka jana ilithibitisha kuwa kweli wajanja wamejichotea mabilioni kutoka katika akaunti hiyo.

Thursday, March 13, 2008

BREAKING NEWS: Mwekezaji TRL asalimu amri

Mwekezaji katika Kampuni ya Reli nchini (TRL) amesalimu amri na kukubali kutekeleza madai ya watumishi ambao jana walianza mgomo kushinikiza waongezewe mishahara.

Habari zinaeleza kuwa mwekezaji huyo (Shirika la Rites na India na Serikali ya Tanzania) amekubali kuwaongezea mishahara ya kima cha chini wafanyakazi hao kutoka kima wanacholipwa hivi sasa cha sh 86,000 hadi sh 160,000 kwa mwezi.

Aidha, mwekezaji huyo ameahidi kuwa ifikapo Agosti mwaka huu, ataongeza kima hicho cha chini na kufikia sh 200,000. watumishi hao waligoma wakitaka nyongeza ya mishahara wakidai kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakiahidiwa nyongeza hiyo lakini hawajaipata.

Msimamo huo uliomaliza rasmi mgomo, ulifikiwa leo katika kikao baina ya wafanyakazi hao, mwekezaji pamoja na serikali kupitia Wizara ya Miundombinu.

Hali ilianza kuwa mbaya katyika reli hiyo kwani mgomo huo ulisitisha shughuli zote za safari za treni. Moja ya treni ambayo iliondoka juzi dare s Salaam ikielekea mikoa ya Dodoma, tabora, Kigoma na Mwanza, ilikwama ilipofika mjini Dodoma, baada ya watumishi waliokuwa wakiiendesha kugoma kuendelea na safari.

Hali hiyo ilisababisha mtafaruku mkubwa baada ya baadhi ya wabiria kuandamana hadi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambaye alipojadiliana na wafanyakazi hao, alishindwa kuwashawishi waendelee na safari baada ya wenzao wa tabora kueleza kuwa hawapo tayari kuipokea treni hiyo.

Jambo hilo liliwafnay abiria waliokuwa na hasira kuanza kurusha mawe wakiwalenga watumishi wa treni hiyo waliokuwa katika injini na kuwalazimisha askari walioitwa kulinda usalama kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Monday, March 10, 2008

BREAKING NEWS: TRL kwafukuta

Jitihada za kuwazuia wafanyakazi wa Kampuni ya reli nchini kufanya mgomo zimegonga mwamba. Muda mfupi uliopita, wafanyakazi wa kampuni hiyo ambayo ilikodishwa na serikali mwaka huu, wametoa notisi ya saa 48 kwa mwajiri wao, awaongezee mshahara.

Iwapo mwajiri atashindwa kutekeleza ombi hilo, wafanyakazi hao wamejiandaa kufanya mgomo nchi nzima na madhara ya mgomo huo yanaweza kuhatarisha hali ya uchumi wa nchi na kusababisha mvugano katika jamii.

Hii ni kwa sababu Reli hiyo ndiyo tegemeo la usafiri kwa mikoa mingi ya bara hivyo iwapo itashindwa kufanya kazi kutokana na mgomo huo, kuna uwezekano mkubwa bidhaa nyingi zikakosekana katika mikoa kadhaa.

Sakata la wafanyakazi hao lilianza mara tu baada ya mkodishaji, kampuni ya rites ya India, alipoingia kuanza kazi mwanzoni mwa mwaka huu.

Baada ya kuja kwa mkodishaji huyo anayemiliki sehemu kubwa ya hisa za kampuni hiyo, wafanyakazi walitaka kulipwa mafao yaao ya miaka iliyopita na kuanza mkataba upya na mwajiri huyo.

Lakini madai hayo yalitawaliwa na mizengwe na kabla halijapatiwa ufumbuzi unaoeleweka, wafanyakazi walikuja na dai jingine wakitaka nyonmgeza ya mishahara.

Dai hilo la pili ndilo lililozaa notisi iliyotolewa jana na iwapo haitatekelezwa hadi Jumatano, wafanyakazi hao wamesema kuwa watagoma.

Sunday, March 9, 2008

Mwanyika azusha maswali mapya kashfa ya EPA

Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kiongozi wa Timu iliyoteuliwa na Rais Kikwete kuchunguza wizi wa mabilioni ya EPA, Johnsom Mwanyika ametoa taarifa ambayo inaibua maswali mengi bila kujibu maswali yaliyoibuliwa awali.

Katika taarifa hiyo, ambayo kimsingi haina kipya, Mwanyika amewataka watanzania na wanahabari kuwa na uvumilivu wakati Timu yake ikiendelea na kazi ya uchunguzi.

Kwa kudhihirisha kuwa hataki kutoa taarifa mpya, Mwanyika amejificha chini ya kivuli cha kuogopa kuharibu wa upelelezi unaoendelea.

Anasema: “Timu inaona ni vyema kutotoa taarifa ambazo zitaathiri kazi ya uchunguzi inayoendelea. Tunapenda kuusihi Umma na Wanahabari kuwa na subira wakati kazi hii inaendelea.”

Aidha, alishindwa kutaja majina ya watuhumiwa ambao tayari wamerejesha sh bil 50 walizoiba. Mwanyika anasema hawezi kuwataja kwa sababu wao ni makampuni na utu wao unatambuliwa kisheria tu.


Taarifa kamili ya Mwanyika hi hii hapa:

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

TIMU YA RAIS YA UCHUNGUZI WA FEDHA ZA EPA

TAARIFA KWA UMMA

Kama mnavyofahamu tarehe 08 Januari, 2008 Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliunda Timu inayojumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili, pamoja na mambo mengine, kuchunguza na kuchukua hatua za kisheria kwa makampuni na watuhumiwa wa upotevu wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mheshimiwa Rais alituagiza kuwa tuwe tumekamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miezi sita.

Taarifa hii ya tatu inatolewa kufafanua na kutoa taarifa ya namna kazi inavyoendelea kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais takriban miezi miwili iliyopita.

Timu inapenda kuufahamisha umma kuwa pamoja na majukumu mengi iliyopewa, kwa sasa Timu imejikita katika kufanya uchunguzi wa kitaalam na wa kina. Kwa msingi huo, pamoja na fedha zinazorudishwa, ni vyema Umma na Wanahabari wakafahamu kuwa kazi ya uchunguzi haijafika mwisho na kwa sasa Timu inaona ni vyema kutotoa taarifa ambazo zitaathiri kazi ya uchunguzi inayoendelea. Tunapenda kuusihi Umma na Wanahabari kuwa na subira wakati kazi hii inaendelea.

Hata hivyo, Timu inapenda kuuhakikishia Umma na Vyombo vya Habari kuwa kazi hii ya uchunguzi inaendelea vizuri na Timu inapata ushirikiano mzuri kutoka kwa makampuni na wamiliki wanaohusika na upotevu wa fedha za EPA.

Vilevile tunapenda kuukumbusha Umma na Wanahabari kuwa Timu imepewa miezi sita ya kufanya kazi na hatimaye kuwasilisha Taarifa kwa Mheshimiwa Rais. Huu ni mwezi wa pili tangu Timu ianze kazi yake. Kwa msingi huo, Timu inawasihi Umma na Wanahabari kuwa na subira kwani Wahenga walisema SUBIRA YAVUTA HERI. Tunawahakakishia kuwa kazi inaendelea vizuri na heri yaja kwani tulichonacho hadi sasa katika uchunguzi si haba.

Vilevile Timu inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu maswali na malalamiko ya kutokamatwa kwa waliohusika. Tunapenda kuueleza umma kwamba uchunguzi wetu hadi hivi sasa unaonyesha kwamba wahusika wakuu ni makampuni. Kisheria, makampuni hayo ni mtu yaani ‘Legal Person’. Hata hivyo, makampuni hayo ni tofauti na mtu wa kawaida. Kampuni katika maana hii, inajitegemea yenyewe.

Kwa msingi huo, ikiwa kampuni imefanya kosa, kuna utaratibu wa kufuata kisheria. Kazi inayofanyika hivi sasa, ni uchunguzi wa kina kuhusu maafisa wa makampuni hayo ili kufahamu ni kitu gani kilichosababisha hali hiyo kutokea. Uchunguzi huu unaendelea na ndiyo utakaotuwezesha kujua hatua za kisheria zitakazochukuliwa.

Timu inapenda kuutarifu Umma na Wanahabari kuwa itaendelea kutoa taarifa ambazo inaamini hazitaathiri uchunguzi unaoendelea mara kwa mara.

Imetolewa na Johnson P.M Mwanyika,
Mwenyekiti wa Timu
9 Machi, 2008

Tuesday, March 4, 2008

Butiama Kuitikisa CCM

HALI ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) si shwari na taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, makundi ya kisiasa ndani ya chama hicho yameshaanza kujipanga kwa ajili ya kushtakiana ndani ya vikao vikubwa viwili vitakavyoitishwa baadaye mwezi huu.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kwamba, wajumbe wanaounda makundi hayo ambayo yamechipua kutokana na Kashfa ya Richmond wameshaanza kufanya mashauriano ya namna ya kukabiliana wakati wa vikao vya Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Maandalizi ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kinatarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu huko Butiama ambako ndiko nyumbani na mahali alikozikwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani ya makundi hayo mawili, moja likiwa ni lile lililofanikisha kuanguka kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na jingine linalojaribu kumsafisha yeye na wenzake wengine kadhaa tayari yanaonyesha mwelekeo wa kujipanga, tayari kukabiliana na mwenendo huo wa mambo.

Mmoja wa makada maarufu wa chama hicho anayetoka katika kundi linaloshangilia kuanguka kwa Lowassa, Nazir Karamagi na kusakamwa kwa mfanyabiashara Rostam Aziz anasemakuwa tayari walikuwa wameshajipanga kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.

Mwana CCM huyo ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, alisema tayari wameshaanza kufuatilia kile walichokiita nyendo za Lowassa na wana CCM wenzake wengine wanaomuunga mkono ili kuweza kupata msingi imara wa kujenga hoja zao dhidi ya kundi hilo.

Kada huyo machachari wa CCM alisema miongoni mwa hadidu za rejea ambazo watazitumia kummaliza Lowassa, Rostam, Karamagi na wanasiasa wenzao wa kundi hilo ni kauli walizozitoa nje ya Bunge dhidi ya ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Kwa mujibu wa kada huyo, watu kadhaa wenye msimamo kama wake tayari wameshaanza kukusanya vielelezo na kujenga hoja ambazo wanaamini wakizitumia zitasaidia kuzima jitihada zozote zinazoonekana kuanza za Lowassa na wana CCM wenzake kujisafisha.

Mbali ya Lowassa, kundi hilo linataka pia chama hicho kitoe karipio kali dhidi ya Rostam na Karamagi kutokana na kile wanachokieleza kuwa ni kukitia doa chama na serikali kwa sababu tu ya kuweka kwao mbele maslahi ya kibiashara kuliko ya umma.

Habari zaidi kutoka ndani ya kundi hilo la kwanza zinaeleza kwamba, iwapo mkakati wao huo utakwama ndani ya chama, basi hatua itakayofuata itakuwa ni kuupeleka bungeni ambako wataitumia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwachukulia hatua Lowassa na wenzake kadhaa wanaodaiwa kutoa kauli ambazo zinaonyesha dharau kwa Bunge.

Wakati kundi hilo la kwanza likijipanga kwa ajili ya kupigilia msumari wa mwisho katika kile wanachokiona kuwa ni ‘jeneza la kisiasa’ la akina Lowassa, Rostam na Karamagi upande wa pili nao unaonekana kujipanga kwa ajili ya kulikabili kundi hilo la kwanza.

Habari zinaonyesha kuwa, nalo limeanza kukusanya vielelezo kadhaa ambavyo wanataka kuvitumia kwa lengo la kukishawishi chama chao kuwa Kashfa ya Richmond ilikuwa na lengo la kuwadhalilisha, kuwaumiza na kuwamaliza kisiasa.

“We will definitely hit back (Ni wazi kwamba tutajibu mapigo). Hatuwezi tukakaa kimya wakati tukijua waziwazi kwamba watu hawa wameazimia kutuumiza kwa malengo ya kisiasa.

“Hii si haki hata kidogo, mtu unazushiwa uongo wa wazi halafu watu wanakuwa washangiliaji. Ni jambo baya kwamba taasisi za kisheria zimefanya ‘mob justice’ (zinachukua sheria mikononi).

“Hili hatuwezi kukubali liendelee. You wait and see,” alisema mmoja wa wanasiasa hao waliotajwa katika sakata la Richmond ambalo lilisababisha Lowassa ajiuzulu uwaziri mkuu huku Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha wakijiuzulu nyadhifa zao za uwaziri.

Monday, March 3, 2008

BREAKING NEWS: JENGO LA USHIRIKA LAUNGUA

Sehemu ya jengo maarufu la ushirika, zilimo ofisi mbalimbali imeungua kwa moto usiku wa kuamkia leo. Habari zinapasha kuwa ingawa haijathibitishwa na mamlaka husika, chanzo cha moto huo kinaweza kuwa umeme.
Mashuhuda wanapasha kuwa usiku umeme ulikatika katika jengo hilo na uliporejea baadaye, waliona cheche za moto kana kwamba kuna mtu alikuwa anachomelea vyuma . baada ya muda kidogo waliona moshi mzito ukifuka sehemu hiyo na moto mkubwa kuzuka.
Takriban ofisi 15 zimeungua na mojawapo ni ofisi ya Prince bagenda, ambaye alikuwa katika harakati za kuanzisha gazeti jipya lililotarajiwa kuwa mitaani kwa mara ya kwanza Ijumaa ijayo (bado haijaelezwa kuwa mipango ya kulitoa Ijumaa imefuitwa).
Akizungumza eneo la tukio, Bagenda alisema kuwa vitu vilivyokuwa katika ofisi yake vina thamani ya zaidi y ash milioni 250. vuti hivyo vinajumuisha na kompyuta na vifaa vingine vinavyohusiana na uandaaji wa gazeti.
Aidha, alisema kuwa ndani ya ofisi hiyo ndimo ilimokuwa inaendeshwa mipango ya kuanzisha TV na radio.
Wamiliki wa ofisi zilizoungua wamesema kuwa watatoa taarifa hapo baadaye.
Waziri wa Mambo ya ndani, Lawarence Masha, alifika eneo la tukio leo asubuhi lakini hakutaka kuzungumza chochote bkwa maelezo kuwa hajapatiwa taarifa za kutosha kuhusiana na ajali hiyo.