Tuesday, August 26, 2008

Nyaronyo ataka kumrithi Chacha Wangwe

Mmoja wa wahiriri wa gazeti la Kulikoni, Nyaronyo Mwita Kicheere, amejitosa kwenye mbio za kuwania Ubunge wa jimbo la Tarime kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Nyaronyo anakuwa mwanachama wa saba wa chama hicho kuchukua fomu hiyo kuwania kujaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Cha cha Wangwe, aliyefariki hivi karibuni kwa ajali ya gari eneo la Pandambili mkoani Dodoma.
Wanachama wengine sita wamechukua fomu hizo wilayani Tarime, kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Chadema, lakini Nyaronyo aliomba kuchukulia fomu hizo jijini Dar es Salaam na kukubaliwa.
Nyaronyo alichukua fomu jana katika ofisi za Makao Makuu ya Chadema na kuaeleza kuwa ameamua kugombea nafasi hiyo, akisukumwa na dhamira inayomtaka sasa kusema moja kwa moja na wahusika bada ya kuona kauli zake anazoziandika katika magazeti hazipatiwi majibu.
Alisema kuwa amekuwa akiandika mambo mengi katika magazeti, akijinasibu kuwa yeye alikuwa mwandishi wa kwanza kuandika masuala ya Richmond, lakini inaelekea viongozi hawasomi makala anazoziandika.
Kwa hiyo, sasa anataka kupata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja kupitia Bungeni.
Nyaronyo aliwahi kuwa katibu wa Wangwe katika harakati za kusaka ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2005.


Monday, August 25, 2008

Hotuba ya Kikwete Bungeni yaota mbawa


Ule mpango wa Bunge kuijadili hotuba ya rais jakaya Kikwete, aliyoitoa Alhamisi iliyopita, umefutwa. Mpango huo mumefutwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa hotuba hiyo bado haijakamilika kutengenezwa.
Taarufa zinasema kwua wakati rais anahutubia, aliongeza maneno mengi sana ambayo hayakuwamo kwenye nakala ya hotuba iliyokuwa imechapishwa. Kwa hiyo, kilichofanyika ni kuongeza maneno hayo aliyoyasema, ambayo yapo nje ya hotuba na kuipeleka Ikulu ili ikahakikiwe.
Lakini habari nyingine zinasema kwua hotuba hiyo imezuiliwa baada ya serikali kuona msimamo wa wananchi uko kinyume na kilichosemwa na rais. Pia inadaiwa kuwa maneno ya Spika Sitta, aliyoyatoa baada ya Kikwete kumakliza hotuba yake, yaliyokuwa na mwelekeo wa kuisema serikali, nayo yamechangia kwa serikali kuweka shinikizo la kuzuia hotuba hiyo kujadiliwa na wabunge.
Inaelekea pia serikali imetishwa na msimamo na maoni ya wananchi kuhusisna na hotuba hiyo, na kuhofia kuwa iwapo wabunge watapata nafasi ya kuijadili, hiyo itakuwa ni fursa kwa wabunge ‘mafyatu’ kuilipukia serikali bila hofu

Kikwete ziarani Marekani

Rais jakaya Kikwete anaondoka leo kwenda Marekani kwa ziara ya siku tatu. Taarifa rasmi ya ziara yake iliyotolewa na ikului inasomeka ifuatavyo:

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini leo (Jumatatu, Agosti 25, 2008) mchana kwenda Marekani kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais George W. Bush.

Ziara hiyo inalenga kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa karibu zaidi kati ya Tanzania na Marekani, na shughuli zote za Rais Kikwete wakati wa ziara hiyo zinalenga kufanikisha jambo hilo.

Malengo makuu ya ziara hiyo yatakuwa ni kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili hasa katika nyanja za elimu, afya na uchumi.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake keshokutwa, Rais Kikwete atahudhuria hafla ya mfuko wa kwanza katika Marekani kujishughulisha na masula ya elimu miongoni mwa Wamarekani wenye asili ya Afrika na Waafrika wa The Phleps Stokes Fund.

Kwenye hafla hiyo, Rais atazungumzia hali ya elimu ya Tanzania, mafanikio yake na changamoto ambazo zinaendelea kuikabili sekta hiyo.

Baada ya hapo, Rais Kikwete atahudhuria mkutano kuhusu sekta ya afya na hasa jinsi ya kupambana na kuufuta ugonjwa wa malaria nchini kwenye kituo cha maendeleo cha Center for Global Development.

Wakati wa mkutano huo pia zitataganzwa juhudi mpya na misaada mingine ya Marekani katika kupambana na malaria katika Tanzania.

Baadaye siku hiyo hiyo, Rais atakwenda kwenye Bunge la Marekani, ambako itatangazwa rasmi kuwa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha wanyamapori cha International Conservation College kitajengwa Arusha.

Kwenye siku yake ya pili ya ziara hiyo, Rais Kikwete atakwenda Makao Makuu ya Shirika la Misaada la Marekani la USAID, ambako itatangazwa rasmi kuwa Marekani itatoa msaada wa kiasi cha dola za Marekani milioni 20 kusaidia maendeleo ya kilimo na usalama wa chakula nchini.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa atatia saini makubaliano ambako Marekani itasaidia usimamizi katika sekta za maji na nishati kupitia EWURA.

Rais pia atashiriki katika majadiliano kuhusu masuala mbalimbali ya sekta ya elimu, na baadaye kushuhudia tangazo ambako Marekani itaipa Tanzania msaada katika sekta hiyo ya elimu.

Msaada huo utakuwa wa vitabu vya kufundishia masomo ya sayansi wa kiasi cha dola za Marekani milioni 1.5, na kiasi cha dola 500,000 kwa ajili ya kufundishia walimu na ujenzi wa maabara tatu za kufundishia lugha ya Kiingereza.

Rais anatarajiwa kukutana na wawezekaji maarufu katika Marekani.

Kwenye siku ya tatu ya ziara yake, Rais Kikwete atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais George W. Bush katika Ikulu ya nchi hiyo ya White House.

Baada ya shughuli hiyo ya White House, Rais Kikwete atakwenda kwenye kituo maarufu cha waandishi wa habari katika Marekani cha National Press Center ambako Marekani itatangaza misaada zaidi kwa Tanzania katika nyanja ya afya, na hasa katika kupambana na ugonjwa wa ukimwi na magonjwa ya mlipuko.

Chini ya msaada huo wa kupambana na ugonjwa wa ukimwi, Marekani itasaidia ujenzi wa vituo viwili vya kisasa kabisa vya watoto, na pia itasaidia kuongeza uwezo wa Tanzania katika kupambana na magonjwa ya mlipuko.

Jioni ya siku hiyo ya tatu ya ziara hiyo, Rais Kikwete atahudhuria mchezo wa kikapu wa WNBA kati ya timu za Washington Mystics na Chicago Sky kwenye uwanja wa Veriton Center.

Wakati wa mechi hiyo, itatangazwa rasmi kuanzishwa kwa “Diplomasia ya Mpira wa Kikapu” ambayo itaanza kufanya kazi rasmi mwezi ujao (Septemba) wakati ujumbe wa wachezaji nyota wa mpira wa kikapu wa Marekani utakapotembelea Tanzania.


Salva Rweyemamu,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

25 Agosti, 2008