Thursday, August 15, 2013

SerikaliSerikali isiwachochee wanaofanya uchochezi



Watanzania wengi wameshitushwa na kujeruhiwa kwa katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda huko Morogoro. Sheikh Ponda alijeruhiwa katika tukio lililohusisha askari polisi ambao wanasema walikuwa na lengo la kumkamata baada ya kiongozi huyo wa Waislamu kumaliza kuhutubia mkusanyiko wa Baraza la Iddi.


Taarifa zilizopo ni kuwa Sheikh Ponda alipigwa risasi begani. Lakini bado kuna utata wa nani hasa alifyatua risasi hiyo iliyomjeruhi Ponda. Polisi wanakanusha kuwa walimjeruhi Sheikh Ponda wakati waumini wake na ndugu wa karibu wanasisitiza kuwa risasi iliyomjeruhi kiongozi na ndugu yao ilifyatuliwa na askari polisi aliyekuwa kwenye gari la polisi na ambaye alikuwa amevalia sare za polisi.

Kwa kuwa polisi wenyewe wanakiri kuwa walifyatua risasi hewani katika tukio hilo kwa lengo la kuwatawanya wafuasi wa Ponda waliokuwa wanawazuia wasimkamate kiongozi wao, basi, hivi sasa Jeshi la Polisi linaweza kuchukuliwa kama mtuhumiwa namba moja wa kujeruhiwa kwa Sheikh Ponda.

Tukio hili limeamsha hasira miongoni mwa waumini wa Kiislamu kwa sababu wanaamini kuwa haikuwa sahihi na sawa kwa Jeshi la Polisi kutumia nguvu kiasi hicho kwa ajili ya kumkamata kiongozi wao. Lakini watetezi wengine wa haki za binadamu nao wanalaumu tukio hili, nao wakilinyoonyeshea kidole Jeshi la Polisi.

Hili si mara ya kwanza la mtu kujeruhiwa au hata kuuawa kwa risasi katika matukio yanayohusisha Jeshi la Polisi. Kuhusika kwa polisi katika matukio kama hayo huko nyuma, kunaweza kuwafanya watu wengi kuamini kuwa hata katika tukio hili, polisi wanahusika na risasi iliyomjeruhi Ponda.

Polisi imekanusha kumjeruhi Ponda, lakini imekiri kutumia risasi za moto kukabiliana na wafuasi wa Sheikh Ponda. Na hapa ndipo lawama zinapojikita. Kwa nini Polisi walitumia risasi za moto katika tukio ambalo walikuwa na uwezo wa kulishughulikia kwa namna nyingine ambayo isingehatarisha maisha ya mtu yoyote na bila kuamsha hasira za watu.

Kwa kutumia risasi za moto katika tukio hili, pamoja na mambo mengine, serikali imechochea hasira za wafuasi hawa wa Ponda. Hasira hizi zinaweza zisiwe halali lakini bado Jeshi la Polisi litakuwa na lawama kwa kuamsha hasira hizi. Ilichokifanya Polisi ni kama kuwachochea watu ambao inawatuhumu kufanya uchochezi.

Ni kweli kuwa Jeshi las Polisi lilikuwa likimtafuta Ponda. Haijaelezwa kama Polisi walimtumia Ponda wito wa kuitwa Polisi kwa sababu anahitajika huko. Hakuna pia taarifa iwa Ponda alikuwa amekataa kutii wito huo. Kama hilo halikufanyika, Polisi wasikwepe lawama kwa kulishughulikia suala hili kinyime na weledi unavyowataka wafanye.

Lakini hata makachero wa Polisi wanafahamu kuwa kumkamata kiongozi huyu mbele ya wafuasi wake ni jambo la kusababisha fujo. Kwa kuwa makachero hawa walishamuona Ponda wakati alipohutubia mkutano huo was Morogoro, walikuwa na uwezo wa kumfuatilia kimya kimya hadi katika eneo na mazingira ambapo angekuwa ameachana na wafuasi wake na kumkamata.

Taarifa kuwa Ponda alikuwa anakwenda Morogoro kuhutubia baraza hili la Iddi zilipatikana siku kadhaa kabla ya tukio hilo. Hivyo, Polisi wangeweza kuweka vizuizi njiani ili kumkamata Ponda wakati akisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekes Morogoro. Lakini polisi waliona hayo yote hayaifai isipokuwa kuwachochea wafuasi wake kwa kumkamata kiongozi wao mbele yao.

Lakini kwa upande wa pili naomba niwasihi pia wafuasi wa Sheikh Ponda. Ni kweli tukio hili linakasirisha sana. Lakini kama tulivyoshuhudia katika matukio kadhaa, polisi wamehusika sana na kuwajeruhi au hata kusababisha vifo. Hivyo, si vizuri kupandisha hasira kutokana na matukio haya ya polisi.

Ni kweli kuwa unaweza usivumilie matukio kama haya lakini matokeo ya kufanya hivyo hayawezi kujenga. Kama watu watapatwa na hasira na kuamua kulipiza kisasi kwa matukio haya, madshara yake yatakuwa makubwa sana.

Hali hiyo inawezsa kuifanya jamii isiishi kwa amani na utulivu unaotakiwa ili kuiwezesha kuzalisha. Kwa maana nyingine, ninachokisema kuwa hatupaswi kulipiza jino kwa jino kwa sababu kufanya hivyo kutaathiri sana hata maisha yetu sisi tunaolipiza.

Lakini hii haina maana kuwa iwapo wananchi watakuwa wavumilivu taasisi za serikali ziendelee kuwanyanyasa na kuwatesa wananchi bila sababu za msingi. Uvumilivu huu unaweza kufikia kikomo na itakapofikia hatua hiyuo, hali itakuwa mbaya sana.

Polisi na serikali kwa ujumla wana mtindo wa kuwaambia wananchi kuwa kazi ya kulinda amani I mikononi mwa kila mmoja. Leo ngoja niwakumbushe askari polisi na watumishi wengine katika vyombo vya dola nchini. Kazi ya kulinda amani si ya wananchi peke yao.

Askari nao wana wajibu mkubwa katika kuhakikishga amani inadumu. Na hawapaswi kulifanya hilo kwa kutumia nguvu. Utulivu na amani katika jamii unakuja kwa kuhakikisha kuwa haki inatendeka.

Askari wetu wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa wanatenda haki kwa wananchi. Ndio wana nguvu za dola lakini hawapaswi kuzitumia nguvu hizo kuwaonea au kuwanyanyasa wananchi. Kufanya hivyoi ni kuvuruga amani.

Kwa hakika nchi itatumia rasilimali kidogo sana kudumisha amani iwapo Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola vitaamua kushirikiana na wananchi. Lakini, kama vyombo vya dola vikijiona kuwa vyenyewe vina nguvu kuliko wananchi katika jukumu hili la kutunza amani, siku zote wataendelea kutumia risdasi za moto hata katika matukio madogo masdogo ambayo yataendelea kumaliza maisha ya watu, kusababisha ulemavu na mbaya zaidi kuchochea hasira.

Jambo hili litasababisha mzunguko wa matukio ya uharibifu wa amani kuendedlea bila kikomo.

No comments: