Monday, November 5, 2007

Kutoka asilimia 80 hadi kuzomewa

USEMI wa Rais Jakaya Kikwete, alipochukua uongozi wa nchi, kwamba anakusudia kuendesha uongozi wake akijenga katika yale yaliyofanywa na mtangulizi wake, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, unaweza kuwa na tafsiri nyingi sana. Wakati alipotoa msemo huo, (utabakia kuwa msemo mpaka utekelezaji wa yaliyoahidiwa utakapoanza kuonekana), wengi waliufasiri chini ya matumaini yao juu yake na kuuona kama sehemu ya ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

Wakati huo watu tayari walikuwa wameshayapima kwa undani yale yaliyofanywa na mtangulizi wake. Hivyo matumaini ya watu wengi yalikwenda kwenye muendelezo wa hayo na ndiyo maana watu walimuamini sana Kikwete alipoahidi kuwaletea kila mmoja wao maisha bora.

Na watu walifahamu nini kuhusu mtangulizi wa Kikwete? Walikuwa wakimfahamu Mkapa kama mtu ambaye alitumia muda wake wa uongozi kujenga uchumi wa Tanzania. Walimfahamu hivyo kutokana na yale yaliyofanyika ambayo yalikuwa yanaonekana dhahiri. Haikuhitajika kuwa na darubini au hadubini kuyajua hayo.

Katika kipindi cha miaka kumi ya kuwepo kwake madarakani, jambo kubwa na la msingi ambalo Mkapa alilifanya ni kufanikiwa kuutengamanisha uchumi mkuu (macro-economy).

Huu ulikuwa ni msingi ambao ulimjengea sifa ndani na nje ya nchi. Hapa nchini, hivi sasa, sifa hii ya Mkapa, pamoja na nyingine nyingi, zimeanza kupata tafsiri nyingine baada ya upande wa pili wa shilingi ya mambo aliyoyafanya Mkapa akiwa madarakani, kuanza kuwekwa wazi.

Tumesikia upande mmoja tu unaotoa tuhuma hizo, hatujasikia Mkapa mwenyewe anasema nini. Na haiyumkini kuwa tutamsikia akisema. Lakini hata kama tunapaswa kufanya uamuzi kuhusu tulichokisikia na ushahidi wake, na kuamua kuwa Mkapa aliyafanya yote anayotuhumiwa kuyafanya, haitafuta sifa zake, ikiwamo hii ya kuujenga uchumi mkuu.

Pamoja na mabaya yake yote (na kwa hakika anayo mabaya kwa sababu yeye ni binadamu tu), sifa hiyo itaendelea kuwepo na kudumu, hata kama baadhi ya watu hawatakubaliana na hilo.

Nalichukulia hili la kujenga uchumi mkuu kama msingi wa yote aliyoyafanya Mkapa, kwa sababu hilo ndilo jambo ambalo lilikuwa na mwelekeo wa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Na kwa watu wa kawaida, iwapo watapata mahitaji yao muhimu, mambo mengine wala hayatawasumbua sana.

Iwapo mtu ana uhakika wa mlo kila siku, anapata uwezo wa kulipia ada watoto wake, anaweza kuipatia familia mahitaji yake yote muhimu na mwisho wa siku kuweza kuweka akiba, hata kama Mkapa aliiba mamilioni mangapi, hayatamuathiri sana kisaikolojia.

Ila itamuuma sana iwapo maisha yake yatakuwa ya shaka. Kila mara, anapokuwa na uhitaji wa kitu fulani alafu akakosa uwezo wa kukipata, mawazo yake yatamfanya aamini kuwa wizi uliofanywa na Mkapa ndio unaomsababishia leo hii akikose kitu hicho.

Na ukiangalia alipofikia Mkapa katika kuujenga uchumi, aliwafikisha Watanzania mahali pa kuleta matumaini. Na ninarudia kusema kuwa ndiyo maana Kikwete alipoahidi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania akijenga katika yale aliyoyakuta, watu walimuamini sana. Walimuamini kwa sababu waliyaona hayo ambayo yamejengwa na Kikwete kuyakuta. Waliona kuwa ilibakia kazi ndogo tu ya kuufanya uchumi mkubwa uujenge uchumi mdogo (micro-economy), ambao kimsingi ndio unaomjaza mtu mafedha mfukoni.

Na kwa jinsi ilivyokuwa, uwezo wa uchumi mkuu wakati Mkapa anaondoka madarakani, ulionyesha dhahiri kuwa kazi ya kuujenga uchumi mdogo ni rahisi kwa kiasi fulani kwa sababu misingi ilikuwa imeshajengwa.

Mfumuko wa bei ulikuwa umeshuka kutoka tarakimu mbili na ulikuwa ukizidi kushuka. Hii ilimaanisha kuwa uwezo wa mtu kununua (purchasing power) ulikuwa ukiongezeka.

Akiba ya fedha za kigeni nchini ilikuwa ya kuridhisha, iliyotoa uhakika wa uchumi wa nchi kuhimili misukosuko ya muda mfupi na wa kati iwapo itabidi.

Makusanyo ya kodi yalikuwa yakiongezeka kila mwezi na kwa hakika kila mwisho wa mwaka, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ilikuwa ikitangaza kuvuka malengo iliyojiwekea.

Hii inamaanisha kuwa nchi ilikuwa na uwezo wa kulipia zaidi ya sehemu ya bajeti ambayo ilijipangia kulipia na mapato ya ndani, ndiyo maana kila mwaka asilimia ya utegemezi katika bajeti ilikuwa ikipungua.

Thamani ya sarafu yetu ilikuwa inajizatiti. Ni kweli kuwa ilikuwa ikishuka, lakini si kwa kasi ambacho tunaishuhudia hivi sasa. Hii ilionyesha kuwa mambo hayakuwa mabaya sana.

Lakini leo hii, takriban miaka miwili baada ya Kikwete kuingia madarakani tupo wapi? Mfumko wa bei unaelekea kwenye tarakimu mbili, kule ambako Mkapa alitutoa. Hapa mtu unaweza kujiuliza ni jinsi gani Kikwete anajenga uongozi wake katika yale aliyoyafanya Mkapa.

Ushahidi kwamba mfumko wa bei unapanda, unatolewa na Benki Kuu kila mwezi. Lakini hata katika maisha ya kawaida, hili linaonekana. Bei za bidhaa zimepaa kiasi kwamba watu wameanza kujiuliza maswali mengi yanayokosa majibu.

Mtafaruku kuhusu bei ya saruji wala bado haujatulia. Bei za vyakula zinabadilika kwa kasi kuliko kinyonga anavyoweza kubadili rangi zake. Kibaya zaidi ni kuwa mabadiliko hayo yanahusisha si tu kupanda, bali kupanda kwa tofauti kubwa mno. Leo si ajabu ukakuta bidhaa ikiwa imepanda bei mara mbili ya uliyoiona jana.

Lakini serikali imekuwa haiishiwi na visingizio na kutoa matumaini kwa kutumia takwimu. Tulitarajia kuwa hali ingekuwa mbaya mwaka jana baada ya msukosuko uliotokana na kukosekana kwa umeme. Lakini wakati wa tatizo hilo, serikali yenyewe iliwatoa Watanzania wasiwasi na kuwaeleza kuwa kila kitu kilikuwa kimedhibitiwa ipasavyo.

Na kama kawadia yao wakatumia takwimu, zilizoonyesha kupanda kwa makusanyo ya kodi ya kila mwezi kuhalalisha kauli yao kuwa kila kitu kipo sawa. Hamkujua kuwa kutoyumba kwa uchumi wa nchi kulitokana na misingi ya kuweka akiba ya kutosha fedha za kigeni kulikofanywa na Mkapa.

Leo hii uchumi wa nchi upo matatizoni. Hakuna kiongozi wa serikali au chama anayetaka kukiri hili hadharani. Wengi wanauchukulia uchumi kama sehemu ya siasa wanazopiga majukwaani. Na ndiyo maana tunaumia na tutaendelea kuumia iwapo viongozi wetu wataacha kuuona uchumi kama siasa.

Ndio wanauona uchumi kama siasa. Hii inatokana na jinsi wanavyotukoga. Haiwezekani mtu apange safari, akiwa ametinga magwanda ya kijani kibichi na nyeusi, akitumia gari la serikali, alafu anasema kuwa anaelezea uzuri wa bajeti huku hotuba yake ikianza na salamu za kidumu chama.

Uchumi haujui chama, unajua mipangilio na mambo kimahesabu. Ni utaalamu wa kimahesabu, si ujuzi wa kupiga domo jukwaani. Wanaweza kuwa mabingwa wa kuelezea uzuri wa bajeti kwa lugha tamu, zinazonakshiwa na vikorombwezo na vichekesho, lakini kama hesabu za kiuchumi hazijakaa sawa, kesho yake itajionyesha wazi kwa mfumko wa bei kupanda.

Hayo maneno matamu hayawezi kuifanya thamani ya shilingi isishuke. Thamani ya shilingi itaendelea kushuka na tofauti kati ya riba ya kuweka na kukopa kupanuka iwapo tutaishia kutoa maneno matamu jukwaani bila kuchukua hatua za kuidhibiti hali hiyo.

Iwapo watafanya mambo yanayotakiwa kudhibiti viashiria vya uchumi, wala hawatahitaji wajuzi wa kutunga mashairi ili kuwashawishi watu. Kila kitu kitaonekana dhahiri; hali ya mambo itabadilika, maisha yatazidi kuwa bora na hapo hata wasipowaambia Watanzania lolote, watafahamu kwa kweli serikali yao ipo kazini.

Miaka miwili iliyopita, asilimia 80 ya Watanzania waliichagua serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyopo madarakani. Huu ni ushindi ambao hadi hii leo bado umewalevya baadhi ya watu ndani ya CCM, kiasi kwamba hawaachi kuutajataja kana kwamba shida za Watanzania zitamalizwa na asilimia 80.

Hivi hawa viongozi wameshawahi kujiuliza kwa nini hao asilimia 80 waliowachagua juzi tu, leo wanaanza kuwazomea majukwaani? Yanatokea haya mara nyingi sana, na yanapaswa kuwa somo kwa viongozi wetu.

Lakini wao inaelekea wameamua wasiyaone. Inatisha sana kuwa wanaozomewa ni wao, lakini wakitoka hapo wanakanusha kuwa hawakuzomewa! Hivi ni kuwa wamelewa sana madaraka kiasi kwamba kelele za kuzomewa wao wanaziona kama za kushangiliwa? Siamini.

Kuzomea huku ni aina fulani ya wananchi kutoa hasira zao. Na namna yao ya kueleza manung’uniko yao. Lengo lao ni kutaka kilio chao kisikiwe na viongozi. Lakini viongozi wasiposikia kuzomea huko, na hata kufikia hatua ya kukanusha kuwa hawakuzomewa, wananchi watajua kuwa salamu zao hazijafika.

Watatafuta njia na mbinu nyingine ya kufikisha kilio chao. Na huu ndio utabiri ambao CCM siku zote imekuwa wakiambiwa lakini hawataki kuamini. Kwamba ipo siku, wananchi ambao wanajihisi kudharauliwa kwa kiasi cha juu na viongozi wao, ambao wakiwafikishia ujumbe na kilio chao hawakisikii, wataamua kutafuta njia na mbinu nyingine ya kufikisha kilio chao. Watafanya nini? Ni vigumu kujua sasa.

Lakini ni dhahiri kuwa chaguo la watakachokifanya litakuwa si kuwakumbatia viongozi wasiowasikia.

pnyanje@yahoo.com
pnyanje@gmail.com

1 comment:

Anonymous said...

Nimefurahi kuanzishwa kwa hii Blog but nashauri itangazwe zaidi ili ichangamke kama JAMBO FORUM ambayo mimi binafsi inanipatia habari nyingi na za kunifanya nichunguze mbivu na mbichi. jitahidi peter na hongera sana najua utawashinda wote na ninaamini hivo.ntakuwa naipitia kila siku.kila laheri Jenifer Daniel