Rais Jakaya Kikwete anasema kuwa haelewi nini kinasababisha mfumko wa bei, tujiandae sasa kwani kuna uwezekano akaja na sababu kama hiyo atakapotakiwa kueleza kwa nini deni la taifa linaongezeka.
Ripoti ya Benki Kuu inaonyesha deni la jumla la Taifa liliongezeka mwezi Oktoba na kufikia dola za Marekani milioni 6,894 kutoka kiasi cha dola za Marekani milioni 6,453.5 mwezi uliotangulia.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya hali ya uchumi iliyowekwa kwenye tovuti ya BoT hivi majuzi, hilo ni ongezeko la dola za Marekani milioni 440.5, sawa na asilimia 6.8.
Ongezeko hilo linatokana na madeni mapya, kubadilika kwa viwango vya ubadilishaji fedha na limbikizo la riba katika madeni ya nje.
Ripoti hiyo inabainish apia kuwa katika deni hilo, asilimia 76.6 ni deni la nje na asilimia 23.4 ni deni la ndani.
Deni la nje limeongezeka kwa asilimia 6.8 na kufikia dola za Marekani milioni 4,940.4. katika kiasi hicho, dola milioni 4,010.2 zilikuwa ni deni halisi wakati dola milioni 1,268.2, sawa na asilimia 18.4 ya deni lote, lilitokana na malimbikizo ya riba.
Orodha ya taasisi za serikali zilizo madeni inaonyesha kuwa Serikali Kuu ndiyo inayoongoza kwa kuwa na deni linalofikia dola milioni 3,192.4 sawa na asilimia 79.6 ya deni lote ikifuatiwa na sekta binafsi ambayo inadaiwa dola milioni 647 (asilimia 16.1) na taasisi za umma zinadaiwa dola milioni 170.8 sawa na asilimia 4.3.
Ripoti hiyo inaionyesha kuwa katika mwezi huo, malipo ya madeni ya nje yalifikia dola milioni 3.8. kati ya kiasi hicho, dola milioni 2.2 zilikuwa malipo ya madeni halisi na dola milioni 1.6 zilikuwa ni malipo ya malimbikizo ya riba.
Kuhusu deni la ndani, ripoti hiyo inabainisha kuwa nalo liliongezeka na kufikia sh bilioni 1,885.3 ilipofika mwisho wa Oktoba, 2007 ikilinganishwa na deni la sh bilioni 1,860.8
lililorekodiwa mwezi mmoja kabla.
Katika kiasi hiki, dhamana za serikali zilikuwa ni asilimia 99.6 ya deni lote huku taarifa ikionyesha kuwa mabenki ya biashara ndio wakopeshaji wakubwa kwa serikali kwa kuikopesha asilimia 43.7 ya deni lote.
Kuhusu mfumko wa bei, taarifa hiyo inabainisha kuwa ulishuka na kufikia asilimia 7.1 mwezi Oktoba ikilinganishwa na asilimia 8.3 iliyorekodiwa mwezi Septemba.
No comments:
Post a Comment