KWA muda wa wiki takriban mbili sasa kumekuwa na taarifa ambazo zinatia madoa taasisi mbili muhimu nchini; jeshi la Polisi pamoja na Magereza. Taarifa hizo zinahusu ukiukwaji wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa dhidi ya watu ambao wapo chini ya himaya ya ulinzi wa taasisi hizo.
Katika moja ya taarifa hizo, inadaiwa kuwa mtu aliyekamatwa kwa tuhuma za mauaji ya mkewe huko Mwanza, alipigwa na askari akiwa katika kituo cha polisi na kufariki dunia.
Kwa upande mmoja, askari wanaotuhumiwa kufanya hivyo wamekanusha na kutoa taarifa kuwa mtu huyo alifariki akiwa hospitali kutokana na kipigo alichokipata kutoka kwa wananchi wenye hasira kabla hajakamatwa na askari hao.
Lakini kwa upande mwingine, mashuhudaa, akiwamo kiongozi wa serikali ya mtaa, wanasema kuwa mtu huyo hakupigwa na wananchi wenye hasira kama askari wanavyoeleza.
Maelezo ya mashuhuda wengine ambao ni au walikuwa mahabusu katika kituo ambacho marehemu alipelekwa, wanadai kuweko kwa tukio la mtuhumiwa huyo kupigwa na askari na kufariki akiwa kituoni hapo.
Kutoka Kibaha kuna taarifa nyingine za mtuhumiwa kufariki akiwa mikononi mwa Polisi. Kama inavyodaiwa kutokea Mwanza, mtuhumiwa huyu naye anadaiwa kufariki kutokana na kipigo cha askari ambao kimsingi walipaswa kumlinda asidhurike.
Kama kawaida, askari polisi wamekanusha kuhusika na kifo hicho wakidai kuwa walimfikisha mtuhumiwa hospitali akiwa mahututi. Lakini maofisa wa hospitali nao wanakana kuhusika na kifo hicho wakisema kuwa mtu huyo alifikishwa kwao akiwa tayari ameshafariki dunia.
Kutoka Singida Jeshi la Magereza limejikuta katika wakati mgumu na kuingia lawamani kwa madai kuwa lilishindwa kumpatia huduma za matibabu ya haraka mfungwa mmoja aliyekuwa akitumikia adhabu ya kifungo cha 10 gerezani kwa kosa la unyang’anyi.
Inaelezwa kuwa mfugwa huyo alipigwa na askari hadi kuvunjika kiuno na mgongo alipokuwa akifanya kazi kwenye gereza wilayani Iramba.
Inadaiwa kuwa baada ya kupigwa, mfungwa huyo aliachwa kwa muda wa mwaka mmoja bila kupewa matibabu yanayostahili, hali iliyomsababishia kupooza.
Kwa upande wake, Jeshi la Magereza mkoani Singida linaeleza kuwa mfungwa huyo alitumbukia kwenye shimo na kuvunjika mguu na kiuno wakati alipokuwa anafukuzwa na wafungwa wenzake katika harakati za kutoroka.
Lakini haijaelezwa wazi kwa nini mfungwa huyo aliachwa bila matibabhu yanayostahili kwa muda wa mwaka mmoja, licha ya haja ya kupatiwa matibabu hayo kuelezwa na daktari aliyemchunguza baada ya kuumia.
Inavyofahamika ni kuwa hata kama mfungwa huyo aliumia wakati anatoroka, bado anayo haki na anastahili kupatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata na hatimaye ashtakiwe kwa kosa analodaiwa kulifanya.
Matukio haya si ya kwanza ya aina hii kuripotiwa dhidi ya Jeshi la Polisi na Magereza. Lakini kwa kipindi sasa habari zinazofanana na hizi zilianza kupotea na kutuaminisha kuwa taasisi hizo mbili zilikuwa zimeanza kubadilika na kuzingatia misingi ya haki za binadamu.
Kuibuka upya kwa taarifa hizi, ingawa bado hakuna uthibitisho kuwa yaliyotokea yamesababishwa na watendaji katika taasisi hizo, kunastahili kufanyiwa tathimini ya kina.
Ni mapema mno kuvilaumu vyombo hivi lakini matukio haya yanatulazimisha kuanza kuhoji iwapo taasisi hizi zimeanza tena mchezo wa kuwaua wahalifu?
No comments:
Post a Comment