Thursday, June 12, 2008

Kuna nini ndege za Jeshi?

DUNIA imeshuhudia mwezi wenye ajali za ndege ambazo zinaweza kuweka rekodi kutokea katika nchi zinazokaribiana katika kipindi kifupi.

Ilianza helkopta ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuanguka na kuripuka katika eneo la Oljoro mkoani Arusha. Helkopta hiyo iliyokuwa ikitoka Arusha kurejea Dar es Salaam ilikuwa imewabeba watu sita ambao wote walikufa.

Wakati watanzania wakiutafakari ajali hii kubwa, zikapatikana habari nyingine kutoka Kenya kuwa ndege ndogo aina ya Cessna 210, iliyokuwa imewabeba watu wanne, wakiwamo mawaziri wawili, nayo ilianguka na kusababisha vifo vya watu wote waliokuwamo dnani yake.

Waliokufa kutokana na ajali hiyo ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Barabara wa Kenya, Kipkalya Kones na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndabni, Lorna Loboso.

Chini ya muda wa saa 24 tangu kutokea ajali hiyo, ndege ya abiria, iliripuka na kuwaka moto wakati ilipokuwa inatua katika uwanja wa ndege wa Khartoum nchini Sudan, ambayo inapakana na Kenya kwa upande wa kaskazini.

Inahofiwa kuwa watu wote zaidi ya 100 waliokuwemo kwenye ndege hiyo wamefariki. Majanga haya matatu kutokea katika nchi zinazopakana, katika kipindi cha saa chache tu, ni lazima yataushtua ulimwengu.

Ajali iliyotokea Arusha imetupotezea wapiganaji mahiri wa JWTZ. Yumo rubani wa helkopta na msaidizi wake, yupo pia fundi na msaidizi wake pamoja na mke wa mmoja wa maofisa wa jeshi. Pia alikuwemo kijana mwanafunzi, ambaye hakuna mwenye uhakika elimu yake ingemfikisha wapi.

Kwa wote waliopoteza ndugu hao, na hakika ni watanzania wote, ningependa kutoa salamu za pole nyingi sana. Kwa vyovyote vile, huu ni msiba mkubwa kwao na kwa taifa lililopoteza watu hao muhimu katika harakati za kujiletea maendeleo.

Lakini ajali hii ni ya pili kutokea katika kipindi kisichozidi miezi sita, zikihusisha helkopta za jeshi. Ajali hizo zote zimetokea mkoani Arusha. Helkopta ya kwanza ilianguka ikiwa na watu 10 ndani yake wakati wakiwa katika harakati za mkupiga picha. Helkopta hii, iliyokuwa imewabeba pia raia wa Marekani, ilianguka katika maeneo ye Ziwa Natron.

Yapo maswali mengi kuhusiana na helkopta hiyo ya jeshi kutumika katika shughuli za kiraia. Inaelezwa kuwa picha zilizozokuwa zinapigwa zinahusiana au sijui niseme zilikuwa zinahusiana na masuala ya utalii.

Lakini zipo taasisi zinazohusiana na utalii ambazo zina ndege zake zenyewe. Inashangaza kwa nini wizara husika ilishindwa kuzitumia ndege hizo na kwenda kukodi helkopta ya jeshi. Watu wengi walihoji inakuwaje siku hizi jeshi limejiingiza katika biashara ya kukodisha ndege zake?

Katika mlolongo wa matukio ya ajali kuhusisha ndege za jeshi, ilianguka pia ndege ya jeshi muda mfupi baada ya kuruka katika uwanja wa ndege wa Dodoma.

Kwa bahati nzuri, katika ajali hizi mbili za awali, hakuna mtu aliyepotesza maisha juu ya kupata majeraha, uharibifu wa mali na usumbufu uliotokana na ajali hizo.

Kwa watu wanaofuatilia rekodi za usalama katika nyanja za usafiri, inaelezwa kuwa ndege ni usafiri salama kuliko aina nyingine za usafiri. Hivyo, inapotokea ndege zilizonunuliwa na taasisi moja zikipata ajali katika kipindi kifupi cha chini ya miaka mitatu, mtu unaweza kupata mashaka, hasa chanzo cha ajali hizo kinapoelekea kuwa hakihusiani na hali mbaya ya hewa.

Ndege iliyoanguka Dodoma ilianguka wakati hali ya hewa ni nzuri tu. Na ingawa ripoti kuhusus chanzo cha ajali hiyo haijawekwa hadharani, haiwezekani kuwa hali mbaya ya hesa ilikuwa chanzo cha ajali hiyo.

Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa helkopta iliyoanguka Ziwa Natron. Na hii iliyotokea juzi Oljoro, simulizi za mashuhuda zinaonyesha kuwa chanzo kinaweza kuwa matatizo ya kiufundi ya ndege hiyo.

Walioshuhudia wanasema kuwa walishuhudia moja ya mapangaboi ya helkopta hiyo likichomoka wakati ikiwa angaki, kabla ya helkopta hiyo kuanguka.

Hali hii inaleta shaka kuhusiana na uimara wa ndege hizi. Ikizingatiwa kuwa ununuzi wake ulizingirwa na tuhuma za ukiukwaji wa taratibu na rushwa, ni wakati sasa wa kufanhya uchunguzi wa kina kuhusiana na nini hasa Tanzania iliuziwa katika mchakato huo.

Tunaweza kusema kuwa tulinunua ndege kumbe tuliuziwa makanyaboya ya ndege na ndio maana leo zimekuwa chanzo kikubwa cha misiba kwa sababu zinaanguka hovyo.

Wakati wataalamu wakiendelea na uchunguzi kuhusiana na chanzo cha ajali hii ja juzi na nyinginezo (kama haujakamilika) inafaa pia kuanzisha uchunguzi mwingine kuangalia uimara wa ndege za jeshi ambazo zilinunuliwa pamoja na hizi zilizoanguka.

Tufanye hivi kama tahadhari ya chochote ambacho kinaweza kutokea kwani mlolongo wa ajali hizi unatulazimisha tuwe watabiri kuhusiana na ndege hizi. Haitashangaza sana iwapo ikitokea ajali nyingine kuhusisha ndege ya jeshi kwa sababu watu walishazoea ajali kuzihusu ndege hizo.

Hili limeshajionyesha kuwa ni suala linalohusu maisha ya watu, si suala la kulifanyia mzaha au siasa. Kama yalifanyika makosa huko nyuma ni vema yakasahihishwa hivi sasa ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa nnhdege hizo.

Hakuna mwenye uhakika nani atazitumia. Kama ziliweza kutumika kupiga picha kwa ajili ya shughuli za utalii, kwa nini zitashindwa kutumiwa na kiongozi yeyote mkuu serikalini kusafiri nazo?

No comments: