Thursday, November 6, 2008

Serikali yaanza kuikana TRL

Serikali imeaonyesha dalili za kuitosa Kampuni ya Reli nchini (TRL). Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akizungumza Bungeni wakati akijibu maswali ya papo kwa papo leo, ameitaka kampuni hiyo kutimiza wajibu wake kwa mujibu wa mkataba ulioingia.
Alisema kuwa si wajibu wa serikali kutoa fedha kila mara kampuni hiyo inapopatwa na matatizo. Serikali imewahi kutoa fedha mara mbili kulipia mishahara ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, ambao walitishia kugoma baada ya mwajiri wao kushindwa kuwalipa nyongeza za mishahara kama walivyokubaliana.
Aidha, Pinda amesema yanayojitokeza hivi sasa ndani ya TRL ni funzo kubwa kwa serikali, ambayo inatakiwa kuwa makini wakati mwingine itajkapokuwa inatafuta mwekezaji.
Maneno hayo ya Pinda yanadhihirisha kiburi cha serikali, ambayo licha ya kuonywa wakati wa mchakato wa kumpata mwekezaji ambaye ni kampuni ya RITES kutoka India, ilikataa kusikiliza ushauri.
Matokeo yake, mwekezaji huyo ameshindwa kukifanya kile ambacho watumiaji wa reli hiyo walikitarajia kutokana na ahadi zake na serikali yenyewe, ambayo ilitamba kuwa imempata mwekezaji makini atakayelifufua lililokuwa Shirika la Reli nchini (TRC).
Tangu mwekezaji huyo alingie nchini, TRL imekuwa ikikumbwa na migogoro ya kazi mara kwa mara na hali ya usaifiri imezorota sana. Mara baada ya kuingia, mwekezaji alifunga baadhi ya njia (kama ile ya Tanga) na kuzusha malalamiko kutoka kwa wadau ambao walisema kuwa matarajio yao ni kuona mwekezaji akifufua na si kufunga reli.

No comments: