Wednesday, November 7, 2007

Joto Hili la Kidini Linatisha

SASA ni dhahiri kuwa mamlaka zinazohusika zinapaswa kuchukua hatua kuhakikisha kuwa masuala ya kidini yanawekwa katika mukhtadha unaofaa ili kuepusha migongano mikubwa kijamii.

Kuna kila dalii kuwa migongano mikubwa ya kijamii, ikisababishwa na tofauti za kidini ipo njiani na mtu anayefuatilia kwa makini malumbano na matukio kutokana na kuhusiana na hoja ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, atabaini hilo.

Uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuliweka suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi katika Ilani yake ya uchaguzi unaweza kutajwa kuwa ndicho chanzo cha migongano hii inayozidi kukua.

Uamuzi huo ndio uliowafanya baadhi ya Waislamu, mwishoni mwa mwaka jana, waanzishe haratakati, kama aina ya shinikizo, wakiitaka serikali iharakishe uundwaji wa Mahakama hiyo kama ilivyoahidiwa katika Ilani.

Mmoja wa wanaharakati maarufu wa kidini, Sheikh yahya Hussein, aliitisha mkutano katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na kutoa historia ya suala hilo, kwa lengo la kuonyesha kuwa hakukuwa na ubaya wowote kwa Tanzania kuwa na mahakama ya aina hiyo.

Lakini suala hilo limepata sura mpya tangu Mchungaji Chritopher Mtikila wa Kanisa la Wokovu Kamili, aibuke siku za hivi karibuni na kufungua kesi Mahakama Kuu, akiitaka isitishe harakati zozote za taasisi yoyote, ikiwemo Serikali, kuanzisha Mahakama ya kadhi, kwa kuwa hatua hiyo inakinzana na katiba na nchi.

Tangu hapo, suala hilo limetawaliwa na vitisho na mabishano ya jazba, wakati mwingine bila kujali kuwa suala hilo tayari limeshafikishwa mahakamani.

Hali hiyo labda ndiyo iliyosababisha Mtikila aandike barua yenye maneno makali kwenda wa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na kusababisha akamatwe na polisi, ahojiwe na hatimaye kufikishwa mahakamani, akikabiliwa na kesi ya uchochezi.

Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa kesi mbili zinazohusiana na uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, makundi kadhaa ya kidini yameendelea kutoa maoni yao kuhusiana na suala hilo, na sasa taasisi nyingine zimeanza kuhusishwa katika kile kinachoonekana kutaka kuupanua mjadala wa kidini nchini.

Katika taarifa yake, Umoja wa Wainjilisti wa Kikristo Tanzania (Uwakita), sasa unalilaumu Jeshi la Polisi, kwa kuonyesha kile umoja huo unachokiita upendeleo wa kidini.

Uwakita unaamini kuwa Jeshi la Polisi wamekuwa wepesi kushughulikia Wakristo wanaotoa vitisho na kuwaachia Waislamu (tena baadhi yao viongozi) kwa kutoa vitisho na uchochezi wa aina hiyo hiyo.

Kauli hii ya Uwakita inatokana na hatua ya Jeshi la Polisi kumkamata, kumhoji na kunfungulia mashtaka Mtikila. Kwa mujibu wa Bullegi, Umoja huo unaamini kuwa Jeshi la Polisi halitendi haki linapowashughulikia viongozi wa kidini wanaortuhumiwa kutoa kauli zinazoashiria uchochezi na uvunjifu wa amani.

Umoja huo unasema kuwa kinachoendelea hivi sasa ni matokeo ya kufumbiwa macho kwa mihadhara ya dini ya Kiislamu, iliyoibuka enzi za utawala wa Awamu ya Pili, chini ya rais Ali Hassan Mwinyi.

Hili linadhihirishwa na matukio na kauli kadhaa za viongozi wa dini. Kabla ya kufikia hatua ya kuandika barua kwa Lowassa, Mchungaji Mtikila alikuwa ametishiwa maisha yake mara kadhaa na baadhi ya viongozi wa Kiislamu, tena wengine wakitumia vyombo vya habari, bila wahusika kuchukuliwa hatua zozote na Jeshi la Polisi, licha ya Mtikila kufikisha malalamiko yake.

Sheikh Yahya Hussein amewahi kutamka kuwa bila Mahakama ya Kadhi, damu itamwagika, lakini hajaeleza damu itakayomwagika ni ya nani. Haya si maneno ya kupuuza.

Yapo matamshi yaliyotolewa na Sheikh Khalifa Khamis na Ponda Issa Ponda, kuwa watamkata kichwa Mchungaji Mtikila kwa kutoa maoni yake juu ya Mahakama ya Kadhi.

Kwa maelezo yoyote yale, mwenendo huu wa mambo unaonekana dhahiri kuanza kulipeleka Taifa hili kule lisikostahili kwenda.

Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni moja ya vyanzo vya tatizo hili na kimsingi viongozi wake na wale wa serikali wanapaswa kukaa na makundi ya kidini ili kuliweka suala hili sawa.

CCM inatambua kuwa, Serikali ya Tanzania kwa maelekezo ya waasisi wake waliokuwa wakitambua vyema athari za masuala ya kidini iliweka bayana kutokuwa na dini na hivyo kutojihusisha moja kwa moja na masuala yote ya kiimani.

Uamuzi chama hicho tawala, kwa sababu inazojua, iliamua kwa vitendo kukiuka misingi ya kisera na kimuelekeo wa waasisi wake ambao siku zote imekuwa ikitamba kuwaenzi na sasa taifa limeanza kuonja machungu ya maamuzi haya mabaya.

Kwa kutambua hilo, viongozi wetu wanapaswa kuchukua kila hatua ya wazi inayowezekana kuyaweka chini makundi yote ya kidini na kuiondoa serikali kuchukua mwelekeo wa kiimani kwa maslahi ya taifa hili ambao msingi wake tulishajengewa na waasisi wetu.

Si kwamba Mahakama ya Kadhi ni mbaya, la hasha. Kwa Waislamu ni chombo muhimu sana katika utekelezajiw a imani yao. Hivyo kuanzishwa kwake ni kwa manufaa makubwa kwao. Lakini kuanzishwa kwa Mahakama hii kusigeuke kuwa zahma kwa watu wengine.

Zipo njia mbazo zikitumika, kuna uwezekano wa kuwanzisha Mahakama ya Kadhi, bila kuathiri utendaji wa Serikali na imani za watu wengine. Utafutwe upenyo huo ili susla hili lisilete madhara kwa jamii.

No comments: