Wednesday, November 7, 2007

Tuogope kwenda Muhimbili?

KATIKA kipindi cha wiki mbili zilizopita, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imejiwekea rekodi mbili tofauti ambazo zitachukua muda mrefu kuvunjwa.

Kwanza iliibuka kashfa ya kuuzwa maiti. Ingawa watawala hospitalini hapo walijitahidi kulifunika suala hilo, lakini kila mwenye akili alifahamu kuwa kuna kosa kubwa la kitaaluma lilifanyika.

Ilibainika kuwa mtu aliyepewa dhamana ya kuangalia chumba cha kuhifadhia maiti, aliigeuza kazi hiyo kuwa ni aina fulani ya kujipatia ulaji. Labda ni katika muendelezo wa falsafa ya ‘kila mtu atakula mahali pake.’

Watu walibainisha kuwa si ajabu tukio limetokea kwani mtu aliyepewa jukumu la kuangalia chumba hicho, hana taaluma husika.

Katika utetezi wao, watawala hospitalini hapo walitaka jamii ielewe kuwa suala la kuuza maiti ni la kawaida. Sawa, ni la kaida. Lakini, kuna taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa katika kutekeleza suala hilo ambalo ni la kawaida. Je zilifuatwa? Kama zilifuatwa, manung’uniko yalitokea ya nini?

Lazima kuna jambo hapa, kwani haiwezekani suala lifanyike kwa kufuata taratibu zote alafu lije lizue manung’uniko. Kwa bahati mbaya sana, mtu aliyehusika na kashafa hii alitetewa na wakubwa nab ado anaendelea ‘kutesa’ kwenye nafasi yake.

Kwa kuwa uongozi ulikiri kuwa mtu huyo kweli aliuza maiti bila kufuata taratibu, itawawea vigumu watu kuamini sasa kuwa anapoendelea na kazi yake hatouza tena maiti bila kufuata taratibu. Huo ndio mtindo wake wa maisha kazini, hiyo ndiyo tabia yake, kutuambia kuwa atakuwa amebadilika kwa muda wa siku hizi chache zilizopita, tena bila kumchukulia hatua yoyote, itakuwa ni kutuongopea.

Huyo mtu hafai kuwepo katika chumba hicho. Maiti, pamoja na kuwa thamani yake ya uhai inakuwa imetoweka, lakini ni kitu ambacho bado kina thamani katika utu wa mtu. Haivumiliki kwa ndugu ambao wanajiandaa kumzika marehemu wao, wagundue kuwa maiti yake haipo. Uongozi Muhimbili unapaswa kufikiria upya juu ya kumuachia ofisa huyu wa chumba cha kuhifadhi maiti kuendelea na kazi hiyo.

Kana kwamba hiyo haitoshi, hospitali hiyo kubwa kuliko zote nchini imejiwekea rekodi nyingine. Kwa sababu ambazo zitaelezwa siku chache zijazo (kama zitakuwa ni za kweli au za kutetea uzembe haijalishi sana kwa sababu makosa yameshafanyika), madaktari hospitalini hapo waliamu kumchua mgonjwa aliyekuwa anaumwa goti, wakamfanyia operesheni ya kichwa. Na pia, wakamchukua yule aliyekuwa anahitaji matibabu ya kichwa, wakaenda kumfanyia upasuaji wa goti. Hatuna haja ya kusubiri maajanu na tisa ya dunia, haya yanatosha kuwa na sifa hiyo!

Tumeshaelezwa kuwa tutulie tusubiri matokeo ya uchunguzi unaofanywa na kamati iliyoundwa. Kamati hiyo bila shaka itaangalia sana mambo ya kitaluma na kujaribu kutafuta sababu ni nini kilisababisha makosa hayo yakatokea.

Lakini hata kwa mtu wa kawaida, ni vigumu sana kuamini kuwa lililotokea lilikuwa ni bahati mbaya tu. Si kwamba hakuna bahati mbaya, lakini iwapo taratibu zote kuhusiana na hatua za kumfanyia mgonjwa upasuaji zingefuatwa, hili lisingetokea.

Kimsingi taratibu hizo zimewekwa ili kuzuia makosa kama hayo. Haielezeki kuwa pamoja na taratibu hizo zote, bado suala hilo limetokea. Rekodi ya muda mrefu ya kutotokea kwa suala hilo, inaweza kutumika kama utetezi kuonyesha utendaji mzuri wa hospitali hiyo.

Lakini kwa upande wa pili, rekodi hiyo ya utendaji inaonyesha ni jinsi gani madaktari hao walivyo wazembe kwa sababu rekodi ya hospitali ni kufanya vizuri, hivyo makosa yanaweza kutokea tu kutokana na uzembe.

Suala la kuuza maiti lilitokana na kutofuatwa kwa taratibu na sasa suala hili la kuchanganya upasuaji wa wagonjwa, dalili zinaonyesha kuwa limetokana na kutofuatwa kwa taratibu. Huku kutofuatwa kwa taratibu ambako kunaibuka katika hospitali hii kubwa ndiko kunakonifanya nijiulize kuwa hivi sasa tunapaswa kuogopa kwenda Muhimbili? Kwa sababu yule jamaa aliyepasuliwa kichwa wakati anahitaji operesheni ya goti tu, hajaamuka hadi hivi sasa!

No comments: