NIMESHANGAZWA, na kwa muda sasa nimekuwa nikijiuliza swali ambalo sipati jibu lake; Kwa nini ni rahisi kuwatofautisha Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yussuf Makamba na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete? Si kuwatofautisha kwa umri, umbo, wajihi au sura, bali kwa kauli na hoja wanazotoa kuhusiana na chama wanachokiongoza na masuala makubwa yanayolihusu taifa.
Itakumbukwa kuwa nchi imegubikwa na mjadala kuhusiana na ufisadi na rushwa. Mjadala huu ulipamba moto kuanzia katikati ya mwezi Septemba, pale Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Dk. Wuilbrod Slaa, alipoamua kuyataja majina 11 ya viongozi wa serikali, akiwatuhumu kwa ufisadi.
Wakati majina haya yanatajwa, Rais Kikwete alikuwa nje ya nchi. Kabla ya waliotajwa hawajajitokeza hadharani, Kingunge Ngombale Mwiru (labda kwa niaba ya serikali) na Aggrey Mwanri, akitumwa na CCM wakati huo akiwa Katibu wa Uenezi, walitolea ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo. Watu wengi sasa wanajua walichokisema kilikuwa na mantiki gani.
Alipopata fursa ya kulizungumza hili, Kikwete alitoa kauli ambayo licha ya kutafsiriwa tofauti, lakini ujumbe wake mkuu ulikuwa thabiti; kuwa taarifa kuhusiana na tuhuma hizo zimefika serikalini na sasa zinafanyiwa kazi.
Na ndio maana akawataka waliotoa tuhuma watulie na kuviachia vyombo vingine vifanye kazi zake. Alisema si busara kwa watoa tuhuma wakajivika majoho ya taasisi nyingine. Wao wameshatekeleza wajibu wao kama raia wema. Hakumtisha mtu wala kumkejeli.
Makamba naye alipata nafasi ya kulizungumzia hili mjini Dodoma.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa ukimya wa CCM katika tuhuma zinazotolewa na wapinzani, zinatokana na busara waliyonayo viongozi wa chama hicho.
Aliendelea kusema kuwa viongozi wa chama hicho wanajua siri nyingi sana za hao wanaokirushia makombora. Kwa hiyo, iwapo kama CCM wakiamua kuwaumbua wapinzani, hata vyama vyao vinaweza kufa.
Lakini wiki chache kabla ya hapo, baada ya rais Kikwete kirejea toka Marekani ambako alikuwa wakati majina ya wanaotuhumiwa kwa ufisadi yalipotajwa kwa mara ya kwanza, alitoa kauli iliyoonyesha kuwa yanayosemwa yameifikia serikali na yanafanyika kazi. Na ndio maana akawataka baada ya kazi ya kutoa tuhuma, waviachie vyombo vingine kufanya kazi zake.
Kikwete alikuwa akizungumzia hoja za ufisadi lakini Makamba ameamua kuachana na hoja za ufisadi, sasa anaangalia boriti lililo katika jicho la mtoa tuhuma.
Inashangaza Makamba anamaanisha nini anaposema kuwa viongozi ndani ya CCM wanazifahamu siri nyingi za wapinzani wanaotoa tuhuma? Anawatisha, anawapa rushwa, anawakejeli au ndio kujibu mapigo huko?
Wakati ambapo mwenyekiti wake alishatoa msimamo wa serikali (unaweza vilevile kuwa wa chama), Makamba alipaswa kuwa mwangalifu sana na anachokisema kuhusiana na suala hili.
Ingekuwa vema iwapo Makamba angeelezea kwanza kutuhumiwa kwa viongozi wa Serikali ya chama chake, na jinsi wasivyohusika au wanavyohusika na ufisadi, alafu akatoa maelezo yanayotosheleza kujibu sakata la mikataba ya madini kabla hajageuka na kuanza kuwachambua wapinzani.
Labda aeleze kuwa hizo siri za wapinzani zitasaidia vipi kujibu hoja kuhusu tuhuma za ufisadi na rushwa katika mikataba. Kwa bahati mbaya sana, Makamba anazungumzia kuhusu siri za wapinzani wakati ambapo kumekuwa na taarifa zinazosambazwa kupitia mtandao wa intaneti kuhusiana na kashfa za baadhi ya viongozi wa wapinzani.
Taarifa hizo zinasambazwa kupitia barua pepe na moja ya taarifa hizo jina la msambazaji lifanana na la Makamba. Anataka tuelewe nini? Au ndio siasa yenyewe hiyo?
No comments:
Post a Comment