Sunday, November 11, 2007

Uchaguzi Zanzibar Ulikuwa huru?

MCHAKATO wa Uchaguzi Mkuu uliopita Visiwani Zanzibar ulitawaliwa na malalamiko mengi. Kati ya hayo yapo, na kwa hakika malalamiko mengi, yalielekezwa kwa Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC).

Malalamiko hayo yalihusu mwenendo wa uchaguzi huo, katika masuala kama uandikishwaji wa wapiga kura, uendeshwaji wa vituo vya kupigia kura na kuvunjwa kwa haki za wapiga kura.

Katika suala la uandikishwaji wa wapiga kura mathalan, yalikuwepo malalamiko kuwa wapo watu waliokuwa wamejiandikisha zaidi ya mara moja. Hili, kwa kiasi fulani lilikubaliwa na ZEC, wakalifanyia kazi na kutoa taarifa kuwa takriban watu 5,000 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja.

Lilikuwepo pia suala la kuandikishwa kwa watu ambao walikuwa hawajafikisha umri rasmi wa kujiandikisha (miaka 18).

Yapo malalamiko yaliyoelekezwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) hasa kuhusiana na matumizi ya vyombo vya dola. Ilidaiwa kuwa sehemu nyingi vyombo hivyo vilitumika kukandamiza wapinzani, hasa wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ndicho chenye wafuasi wengi wa upinzani visiwani humo.

Wakati huo, mengi ya madai haya, pamoja na mengine mengi yalikanushwa kwa nguvu zote na taasisi ambazo zilituhumiwa. ZEC ni mojawapo ya taasisi ambazo zilikanusha kasoro kadhaa walizotuhumiwa.

Vyombo vya dola navyo vilikanusha kuhusika na unyanyasaji wowote dhidi ya vyama na wapiga kura. ZEC ilikaa kimya wakati vyombo hivyo vya dola vikikanusha kuhusika na kuvunja taratibu za uchaguzi.

Lakini Tume hiyo ilipomaliza muda wake wa kuwa madarakani, iliandaa ripoti ambayo imewasilishwa kwa Rais Amani Karume, aliyewateua wajumbe na mwenyekiti wake. Kwa bahati nzuri sana, ingawa si yote, lakini mambo muhimu yaliyomo katika ripoti hiyo, yamewekwa hadharani.

Pamoja na hongera hiuzo, lakini lazima mshangao unaosababishwa na ripoti hiyo uonyeshwe wazi. Kikubwa kinachoshangaza ni kuwa kasoro nyingi zilizokuwa zimeanishwa wakati wa uchaguzi, ambazo ZEC na taasisi nyingine ilizikanusha, ndizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinabainishwa kwenye ripoti ya ZEC.

Kwa sababu rekodi ya ZEC kukanusha mambo haya bado zipo, na sasa wanaibuka na ripoti inayoonyesha kuwa yale waliyoyakanusha yalitokea kweli, inabidi waje na msimamo ambao utatuweka sote kwenye uelewa mmoja kuhusiana na mambo hayo; yalitokea au hayakutokea? Ufafanuzi huo unatakiwa kwa sababu baadhi ya yaliyomo kwenye ripoti yanazua maswali mengi ambayo majibu yake hayapaswi kuwa ya kufikirika.

Mathalan, katika ripoti yao ZEC wanabainisha kuwa jumla ya watu 1,197 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja. Lakini ripoti za awali zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 5,000 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja. Kimetokea nini mpaka namba hii ikabadilika kiasi hiki?

Pia inapaswa ielezwe kinagaubaga, hao watu waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, wamechukuliwa hatua gani? Inafahamika wazi kabisa zipo sheria zinazoharamisha mtu kujiandikisha katika daftari wa kudumu la wapiga kura zaidi ya mara moja, pamoja na mambo mengine sheria hiyo imepanga adhabu kwa mtu au watu watakaobainika kutenda kosa hilo. Inapaswa ielezwe hapa watu hao ambao ZEC imebaini kuwa wamejiandikisha zaidi ya mara moja wamechukuliwa hatua gani.

Hili linapaswa kuelezwa kwa sababu kuna tetesi kuwa kati ya watu waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja ni vigogo serikalini. Haiyumkini hawa wakaachwa hivi hivi. Hii ni kwa sababu iwapo wao hawakuona haya kutaka kuliingiza Taifa katika madhila yanayotokana na njama za kuvuruga uchaguzi, Serikali nayo haipaswi kuona haya kuwashughulikia ipasavyo.

Aidha, ripoti ya Tume hiyo yenye kurasa 70, imetoa lawama kali kwa vikosi vya SMZ, vikiwemo KMKM, JKU, Zimamoto, mafunzo na Valantia kwamba viliingilia kazi za ZEC. Vikosi hivyo vinashutumiwa kuwa wakati mwingine vilifanya maamuzi yanayohusu ulinzi wakati wa uchaguzi bila kuihusisha Tume.

Baya zaidi, ZEC inaeleza kuwa vikosi hivyo vilishiri katika kuwaandikisha askari bila ya kuihusisha Tume. Sote tunafahamu kuwa jukumu la uandikishaji wapiga kura ni la Tume, iwapo askari au mtu yeyote anataka kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, analazimika kufuata taratibu zilizowekwa.

ZEC inaeleza kinagaubaga kuwa pamoja na kuchukua hatua ya kuwaita viongozi wa vikosi hivyo, lakini walikataa katika nyakati walizoombwa ili kwenda kurekebisha hali mbaya ya mambo iliyokuwa ikijitokeza wakati wa uandikishaji wapiga kura hasa katika mkoa wa Mjini Mgharibi.

Ripoti imesema viongozi wa Serikali za mitaa (Masheha) ambao ni
mawakala wa Tume hiyo, wakati wa uandikishaji wapiga kura walisikiliza ziadi maelekeo ya wakubwa wao kutoka Serikali za Mikoa na kupuuza maelekezo ya Tume hiyo.

Imeelezwa katika ripoti hiyo kwamba kuna baadhi ya vyama vya siasa
Vilifanya mbinu ya kuandikisha watoto wadogo chini ya umri wa miaka 18 kwenye daftari, huku wakijua kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Ripoti hiyo ilisema mbali kukubali kusaini maadili ya uchaguzi, baadhi ya vyama viliyavunja maadili hayo kwa sababu hayakuwa na nguvu za kisheria. Ndiyo maana sasa ZEC inapendekeza maadili ya uchaguzi yawe ni sehemu ya sheria za uchaguzi.

ZEC inagusia pia mambo nyeti likiwemo la taasisi yenye mamlaka ya kuongeza au kupunguza majimbo ya uchaguzi. Kwa mujibu wa Tume hiyo, suala hili lina utata wa kikatiba. Wakati Tume inaamini kuwa yenyewe ndiyo yenye mamlaka ya kufanya hivyo, lakini kwa utaratibu uliotumika, Baraza la wawakilishi ndilo lililopitisha uamuzi kuhusiana na suala hilo.

Kasori hizi pamoja na nyingine zilisababisha mivutano ambayo ilihatarisha uchaguzi huo. Lakini uchaguzi Zanzibar haukuishia mwaka 2005. Tunatarajia kuwa utafanya uchaguzi mwingine mwaka 2010 na nyingine nyingiz zitafuatia.

Ni vema tukaangalia tunakokwenda ili kujiepusha na matatizo yoyote ambayo yanaweza kutukwamisha katika jitihada zetu za kujenga taifa tajiri.

Hatupaswi kuangalia nyuma kwani tukifanya hivyo tunaweza kujikuta tunajiuliza maswali ambayo kimsingi yanaweza kutufanya tuone giza mbele na kushindwa kujua njia ambayo tunapaswa kuienenda.

Hata hivyo, yapo ambayo tunapaswa kujiuliza kwa ajili ya kuweka msimamo wa pamoja na kupanga mustakabali utakaotufikisha tunapokusudia kwenda. Ni lazima tujiulize na kupata jibu la iwapo hivi uchaguzi huo uliofanyika ukigubikwa na kasoro hizo zote, ulikuwa huru na wa haki kama ilivyoelezwa?

No comments: