WASIWASI na woga umeanza kuwatesa baadhi ya viongozi serikalini, na wafanyabiashara wakubwa wanaotajwa kuhusika katika kashfa ya upotevu wa mabilioni ya shilingi dhidi ya siri nzito aliyonayo moyoni, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Daudi Ballali.
Inaaminika kuwa kokote aliko, Dk. Ballali, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Jakaya Kikwete mapema wiki hii, anayo siri nzito moyoni mwake, na iwapo atapata nafasi ya kuiweka hadharani, mwenendo wa kashfa hizo unaweza kubadilika na kuharibu kabisa upepo wa kisiasa, utawala na biashara hapa nchini.
Aidha, siri hiyo inaelezwa kuwa ni nzito kiasi kwamba inaweza pia kuwaharibia watu wengi na hata kuchafua kabisa rekodi zao licha ya sifa nzuri walizonazo sasa.
Dk. Ballali ameamua kutumia siri hiyo kama turufu ya kujilinda na kujihakikishia usalama wake dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Ballali analinda siri hiyo kwa hali na mali ili kuhakikisha inamsaidia kabla haijavuja na kwamba ameamua kwenda hatua kadhaa mbele akitumia siri hiyo kama kinga dhidi yake na mtego dhidi ya maadui zake.
Watu walio karibu naye walieleza kuwa, baada ya kuona hali ya mambo imeanza kugeuka, Dk. Ballali aliamua kumtafuta wakili na kuandika maelezo ya kina kuhusu kile anachokifahamu katika sakata zima la akaunti ya madeni ya nje (EPA).
Kwamba katika maelezo hayo, Dk. Ballali ametoa sehemu ya siri hiyo, huku akitaja majina ya kampuni na watu ambao kwa namna moja au nyingine walihusika katika mipango ya sakata zima la upotevu wa fedha za EPA.
Aidha, taarifa hiyo ya Ballali iliyohifadhiwa kwa wakili huyo ambaye hajatajwa, ina maelezo ya kina pia kuhusu watu ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa na mkono wao katika maamuzi kuhusu EPA, lakini ushiriki wao huo unaweza usionekane katika uchunguzi wa kawaida.
Baada ya kutoa maelezo hayo, Dk. Ballali ambaye mpaka sasa hali ya afya yake inaendelea kuwa kitendawili, inadaiwa kuwa alitoa maelekezo kwa wakili huyo na watu wengine wa karibu yake, kuhusu wanachopaswa kufanya iwapo atafikwa na jambo lolote ambalo aidha yeye mwenyewe au mtu mwingine wa karibu yake atalitilia shaka.
Dk. Ballali ameelezwa kufanya hivyo kama jitihada zake za makusudi za kuhakikisha kuwa hafanywi kuwa mbuzi wa kafara katika mchezo ambao ulihusisha wachezaji wengi.
Kwamba lengo lake kubwa la kufanya hivyo, ni kutaka kuhakikisha kuwa, baadhi ya watu waliohusika katika mchezo huo hawamtumii yeye kwa aidha kujisafisha kwa namna yoyote ya kujivua madhambi waliyokuwa nayo katika kashfa hiyo na kumvika yeye.
Kasoro zilizobainika katika akaunti ya malipo ya madeni ya nje ndani ya BoT, zilihusisha watu wengi, akiwemo Ballali na wengine anaowafahamu moja kwa moja na wale ambao hawafahamu.
Lakini, baada ya Kampuni ya Ernst & Young kukamilisha ripoti yake na Rais Kikwete kutoa maamuzi, inaonekama kuwa Ballali ndiye alikuwa mchezaji mkuu katika mchezo huo ambao kuibuliwa kwake kumelitikisa taifa na mataifa ya nje.
Hata katika akili ya kawaida, inaonyesha kuwa Dk. Ballali hakuwa peke yake katika suala hili, bali wapo wengine wengi, hususan vigogo kuliko Ballali.
Hayo yanatokea wakati haijawekwa wazi Dk. Ballali yupo katika hali gani au yupo wapi hasa.
Kinachoshangaza, wakati kulazwa kwa gavana huyo wa zamani wa BoT hakukustahili kuwa siri, hakuna aliyekuwa tayari kutoa taarifa za kina tangu alipoondoka nchini kwenda Marekani kutibiwa, takriban miezi minne sasa.
Awali ilidaiwa kuwa, amekwenda Marekani kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake lakini alipokuwa huko ikatolewa taarifa kuwa anaumwa na amelazwa. Baadaye kidogo zikaja taarifa kuwa amefanyiwa upasuaji mubwa.
Tangu uteuzi wake ulipotenguliwa, watu wengi wamekuwa wakitaka Dk. Ballali arejeshwe Tanzania na kushitakiwa sambamba na watu wengine watakaobainika kuhusika na kashfa ya EPA.
Dhamira hiyo ya wengi hailengi kuona tu kuwa kiongozi huyo anashtakiwa, bali wanaamini kuwa, akiwa nchini, anaweza kutoa maelezo mengi na ya kina kuhusu EPA na masuala mengine yaliyomo katika kashfa zinazoelekezwa BoT.
Dk. Willibrod Slaa, ambaye ni muasisi wa tuhuma za ubadhirifu BoT, ni mmoja wa watu wanaoamini kuwa Dk. Ballali ana mengi ya kueleza kuhusu ubadhirifu huo.
Dk. Slaa alisema kuwa, yaliyoelezwa na serikali baada ya kupokea ripoti ya uchunguzi wa EPA uliofanywa na Ernst & Young, ni sehemu ndogo tu ya ubadhirifu mkubwa ambao umefanywa na baadhi ya watu waliopo madarakani na wafanyabiashara.
Dk. Slaa alikwemda mbali zaidi kwa kusema kuwa yeye binafsi anafahamu ubadhirifu uliofanywa kupitia kampuni nyingine kama vile Deep Green, Meremeta na Tangold na iwapo serikali itaendelea kuwa na kigugumizi cha kusema kuhusu hayo, itafika siku ataamua kuyaweka hadharani.
No comments:
Post a Comment