KATI ya watu waliotakiwa wawe na furaha baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kutengua uteuzi wa aliyekuwa gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Daudi Ballali, ni Dk. Wilbrod Slaa, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Karatu.
Lakini hali si hivyo kwa Dk Slaa. Kilichofanywa na Rais Kikwete hakijamridhisha kiasi cha kutosha. Anaamini kuwa sehemu iliyoshughulikiwa ni ndogo sana.
Kwamba Rais ametangaza uamuzi aliochukua kutokana na sababu alizozitoa, lakini kilichoelezwa ni sehemu ndogo sana ya tatizo kubwa lililopo.
“Tumeikubali taarifa, tunafurahi kuwa baadhi ya hatua zimewekwa hadharani, lakini serikali haijawa wazi kwa kiwango yenyewe ilichoahidi.
“Tuliambiwa kuwa ripoti ya uchunguzi uliofanywa na kampuni ya Ernst & Young itawekwa hadharani yote. Lakini walichofanya ni kutoa taarifa iliyotokana na sehemu ya ripoti, hilo silo walilotuahidi,” hivyo ndivyo anavyoeleza Dk. Slaa kuhusu kutoridhishwa na uwazi wa serikali kuhusu ripoti ya uchunguzi wa Ernst & Young.
Kingine kinachomfanya Dk. Slaa asifurahie sana hatua ya Rais Kikwete ni kuwa hata hicho kilichoelezwa katika taarifa, hakijibu sehemu kubwa ya matatizo yeye na wapinzani wenzake waliyojaribu kuyaonyesha.
Kipimo chake katika hili ni majina ya kampuni zilizotajwa kuhusika na kashfa ya akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA). Wakati akitangaza kwa waandishi wa habari taarifa ya serikali na hatua Rais Jakaya alizozichukua baada ya kukasirishwa na kuhuzunishwa ripoti hiyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, aliyataja makampuni 22 kuwa yalihusika na malipo yenye kutia shaka ya EPA.
Lakini Dk. Slaa anasema kuwa hiki ni kiinimacho kwa sababu kampuni zilizotajwa zinahusisha watu wadogo sana na sehemu ndogo sana ya ubadhirifu ambao yeye ana taarifa nao.
“There is no way (haiwezekani), deep green isionekane humu, uchunguzi uliofanywa EPA unahusisha 2005/06. Mimi ninazo taarifa kuhusiana na nini kampuni hii imefanya, nina hadi cheque number (namba za hundi) zilizotumika kulipa mabilioni katika kampuni hii.
“Lakini inavyoonekana wao walichokitoa (katika taarifa ya Luhanjo) ni kile walichotaka kukitoa, kile ambacho kilistahili kutolewa kimefichwa “wamewataja watu wadogo sana,” anasema.
Katika sakata hili la ubadhirifu BoT na kashfa ya mafisadi, historia itaendelea kumuonyesha Dk. Slaa kama muasisi wa hoja hizo. Ingawa kabla yake kulikuwa na taarifa zilizosambaa chini chini kuhusiana na tuhuma za ufisadi na ubadhirifu, lakini yeye ndiye aliyeibua mambo hayo hadharani.
Aliposimama bungeni na kueleza mambo hayo, wapo waliomdhihaki wakidhani kuwa ulikuwa ni mchezo wa kisiasa uliozoeleka wa wapinzani kuwarushia makombora watu walio upande wa pili.
Lakini Dk. Slaa hakukatishwa tamaa na kejeli, dharau na masimango mengine yaliyotoka hata kwa viongozi wakuu serikalini (wako hata waliosema kelele za mlango hazimnyimi mwenye nyumba usingizi). Dk Slaa aliamua kusimama kidete akitetea hoja yake, akitumia taarifa alizozikusanya kutoka katika mtandao wa intaneti na vyanzo vingine.
“Ndiyo, nilitumia taarifa za kwenye intaneti kwa sababu nilijua kuwa zinaruhusiwa kisheria wakati (viongozi wa serikali) walipoleta sheria ya kutaka vyanzo vya intaneti vitumike kama ushahidi mimi nilipinga bungeni, lakini kutokana na wingi wao (wabunge wa CCM) waliipitisha, na nikaamua kuitumia hiyo hiyo,” anasema.
Utata kuhusu ushahidi wa Dk. Slaa uliotoka katika intaneti ulipingwa hata na Spika, Samuel Sitta, ambaye katika hatua fulani alionekana kuwa na shaka na ushahidi huo.
Lakini hii ni kama ilimchochea Dk. Slaa na kueleza nia yake ya kuandaa hoja binafsi, akilitaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza tuhuma alizokuwa nazo.
Lakini Dk. Slaa hakufanikiwa kuiwasilisha hoja hiyo bungeni. Anaeleza sababu za kushindwa kuwasilisha hoja hiyo kuwa alipata taarifa mapema kuwa hoja hiyo ingezimwa.
“Sikutishwa na mtu. Nilipata taarifa kuwa hoja itazimwa, kulikuwa na tarifa zilizonifikia kuwa kiongozi mmoja serikalini alikuwa ametahadharishwa kuwa asije akaiacha hoja hii ikatua bungeni kwa sababu serikali haikuwa na majibu wakati ule.
“Walijiandaa kuikwamisha kwa namna yoyote na mimi nikaona kuwa iwapo nitaiwasilisha haitatendewa haki. Nikatafuta mahali muafaka pa kuipeleka na matokeo yake yameshaonekana,” anaeleza kwa kujiamini.
Maelezo haya ya Dk. Slaa yanamaanisha kuwa uamuzi wake pamoja na viongozi wenzake wa kambi ya upinzani kuichukua hoja hiyo na kuipeleka kwa wananchi, wakiifanya ajenda yao kuu katika mikutano ya hadhara iliyofanyika mikoa kadhaa nchini, ndiyo mahali muafaka alikoipeleka hoja hiyo.
Walianzia katika viwanja vya Mwembeyanga, Dar es Salaam, ambako Dk. Slaa alifanya kile ambacho watu wengi waliamini kuwa hakiwezi kufanywa na mwanasiasa wa Tanzania.
Siku hiyo, Dk. Slaa aliweka hadharani majina ya viongozi kadhaa wa serikali na chama, si tu akiwatuhumu kwa ufisadi, bali akiorodhesha tuhuma za kila mmoja wao.
Huko nyuma wanasiasa wa upinzani wamewahi kutaja majina mawili matatu ya watu wanaowatuhumu kwa ubadhirifu wa mali za umma lakini hoja hizo hazikupata mashiko.
Hii ya Dk. Slaa ilikuwa ni tofauti. Jitihada za watuhumiwa kutaka kujisafisha zilibakiwa kuwa matishio ambayo hayakumteteresha Dk. Slaa na wenzake.
Lakini Dk. Slaa alipata wapi ujasiri wote huu? Au ni namna nyingine ya kujitafutia umaarufu?
“Ndugu yangu, ukiyavulia nguo maji ya baridi huna budi kuyaoga. Mimi nilishayavulia nguo maji haya na hivyo nililazimika kuyaoga. Katika hili ninatimiza wajibu wangu kama mwakilishi wa wananchi, wala sitafuti jingine lolote, niliwaomba wananchi niwatumikie, wakanichagua na sasa natimiza ahadi ya kuwatumikia,” anasema.
Anaeleza zaidi kuwa ujasiri mwingine aliupata kutokana na kuwa na taarifa za uhakika kuhusu kile alichokisema.
Kwamba alikuwa na uhakika na taarifa alizokuwa nazo kwa sababu zilizotokana na taarifa za serikali yenyewe pamoja na vyanzo vingine. Dk. Slaa ni miongoni mwa wabunge na wanasiasa wenye tabia ya kusoma sana.
Yeye mwenyewe anaeleza kuwa hutumia muda wake mwingi kuperuzi habari mbalimbali kwenye intanet na ana muda maalumu wa kupitia rekodi za serikali na tafiti mbalimbali kuhusu masuala anayoyafuatilia.
Akisisitiza kuhusu usahihi wa taarifa alizo nazo kuhusu watu na makampuni anayoyatuhumu kwa ufisadi, anasema katika kutafuta taarifa za kampuni anazozituhumu, alifika ofisi za wakala wa kuandikisha kampuni (Brela) alikopata ushahidi wa yale aliyokuwa akiyafuatilia.
“Nilijifunza kufanya hivi baada ya sisi (wapinzani) kudharauliwa sana bungeni na kukejeliwa kuwa hatujui kufanya ‘research’ (utafiti) na sisi tukakiri kuwa kweli bado ni wachanga sana na tunajifunza, lakini katika uchanga wetu haya ndiyo tuliyoweza kuyafanya na bado tunaendelea,” anasema.
Anaeleza kuwa jambo lililomtia matumaini kuendelea na mapambano ya kuwataja hadharani watu waliojihusisha na ufisadi ni kilichotokea baada ya kutaja majina yao, ambapo walijitokeza Watanzania anaowaeleza kuwa wenye uchungu na nchi yao na ari ya kulitetea taifa lao, na kumpelekea taarifa nyingine nyingi za jinsi fedha za umma zinavyotafunwa na wachache.
“Hili ni kundi la Watanzania ambao wameanza kutuamini (wapinzani) kuwa tumedhamiria kupambana na maovu na ufisadi katika jamii,” anaongeza kuwa kati ya hao waliowasiliana naye ni watumishi kutoka serikalini, baadhi yao kutoka idara nyeti za serikali.
“Hawa si kwamba wametoa siri za serikali, kwa mujibu wa sheria namba 3 ya mwaka 1988 kifungu cha 10. Walichofanya ni kutoa taarifa za wizi na si siri za serikali, hivyo sheria hiyo haiwezi kutumika kuwabana.
“Ndiyo maana baada ya kupitia shida zote hizi na nyingine nyingi, sijaridhika na kilichotokea na kumweka nje Dk. Ballali. Wapo wengine wengi ambao nina ushahidi nao kuwa walihusika katika sakata hili, nao washughulikwe na kuwekwa pembeni.
“Hii si siasa, tunapigania maslahi ya nchi na ndiyo maana hata walipovamiwa wahariri wa ‘MwanaHalisi’ kila mtu alilaani, kwa sababu ule ulikuwa ni uvamizi dhidi ya demokrasia. Na ufisadi nao hivyo hivyo, hauna rangi ya chama cha siasa, unaumiza Watanzania wote na kuneemesha wachache.
“Tutaendelea kudai ripoti ya ukaguzi wa Ernst & Young iwekwe hadharani yote ili wananchi wajionee wenyewe kilichomo na hapo ndipo watakapogundua maana halisi ya kilichoonekana kuwa ni kelele za wapinzani.
“Sisi tunaonekana kama tunapiga kelele (kama zile za mlango zisizoweza kumkosesha mwenye nyumba usingizi, sasa ana hiyari mwenye nyumba kutengeneza mlango au auache mlango uendelee kumpigia kelele)…tunakejeliwa sana, lakini nataka niwahakikishieni Watanzania kuwa tuna uhakika na tunachokisema, sisi si wendawazimu hadi tuwe tunaropoka mambo ambayo hatuna uhakika nayo,” anasisitiza Dk. Slaa.
Huku akionyesha wazi kuwa na shauku ya ripoti hiyo kuwekwa hadharani ili Watanzania wote wafahamu kilichomo, anasema serikali inapaswa kuiweka hadharani kama ilivyowaahidi wabunge wakati ilipotoa maelezo kuhusu uchunguzi huo.
Lakini pia Dk. Slaa anawakumbusha watawala kuwa wao si waamuzi wa mwisho wa mambo yanayohusu maslahi ya taifa, walichokabidhiwa ni dhamana ya kuwaonyesha watanzania kule wanakotakiwa kwenda na si kuwafanyia maamuzi yote.
Hata hivyo, katika mazingira ya kawaida, Dk. Slaa anaweza kuwa anahatarisha maisha yake kwa sababu anapingana na watu wenye uwezo wa kufanya chochote kutokana na uwezo mkubwa wa kifedha waliojikusanyia.
Ingawa yeye mwenyewe anaonekana kutotishika na ukweli huo, watu wengi sasa wanaonekana kufuatilia zaidi mwenendo wa maisha yake, hasa wananchi wa chini ambao amekuwa akiwaita mawakili wa kesi yake.
“Ndiyo maana nimeamua sasa kuwa kila ninachokifahamu kuhusiana na ufisadi nakieleza hadharani, hivi ninapozungumza na wewe nimetoka kuhutubia mkutano wa hadhara na tangu juzi nafanya mikutano hiyo katika jimbo langu.
“Natumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi yote ninayoyafahamu kuhusiana na ubadhirifu na ufisadi ili kama likinitokea lolote, wawe na taarifa zote na wataamua wenyewe cha kufanya,” anasema.
Dk. Slaa alifanya mahojiano haya kwa njia ya simu akiwa jimboni kwake Karatu, baada ya kutolewa kwa taarifa za Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa Ballali kuwa gavana.
Rais alifikia uamuazi huo baada ya ripoti ya uchunguzi uliofanywa na kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya Ernst & Young kubaini kasoro kubwa katika akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA) katika mwaka wa fedha 2005/06.
Katika maamuzi hayo, baada ya kutengua uteuzi wa Dk. Ballali, Rais Kikwete alimteua aliyekuwa Naibu Gavana, Profesa Benno Ndulu, kuchukua nafasi hiyo.
Aidha, Rais alimpa miezi sita Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa kushirikiana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuendesha uchunguzi dhidi ya wale wote waliohusika na upotevu wa fedha kupitia akaunti hiyo na kuwachukulia hatua.
Hatua zitakazochukuliwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa fedha zote zilizoibwa kupitia EPA zinarejeshwa.
Pia aliitaka bodi ya BoT kufanya vikao na kuwashughulikia wafanyakazi walio chini ya mamlaka yake walioshiriki katika kashfa hiyo ya EPA.
Ili kuhakikisha kuwa EPA haiendelei kuwa mrija wa mapato kwa wajanja wachache, Rais Kikwete alisitisha ulipaji wa madeni kwa kutumia akaunti hiyo mpaka hapo utaratibu mzuri utakapoandaliwa.
No comments:
Post a Comment