SASA watanzania wanapaswa kujiandaa na hali ngumu itakayotokana na kushindwa kukua kwa uchumi kwa kasi ambayo ilitarajiwa kuleta nafuu katika maisha.
Kudumaa kwa hali ya uchumi kutatokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, jambo ambalo mara kadhaa Rais Jakaya Kikwete amekuwa akilielezea kama moja ya sababu kubwa zinazoikwamisha serikali yake kutekeleza kwa kasi ahadi ya kumletea kila mtanzania maisha bora.
Kwamba kupanda kwa bei ya mafuta ni kidonda kwa uchumi wa nchi inathibitishwa na ukweli kuwa bajeti ya serikali ya mwaka 2007/08, iliyopitishwa mwezi Agosti mwaka jana, haikufikiria wala kuweka tahadhari ya kukua kwa bei ya mafuta kama moja ya matatizo ambayo yanaweza kusababisha matatizo katika utekelezaji wa bajeti.
Licha ya kutoweka tahadhari hiyo katika bajeti, pia mipango ya nchi kuhusiana na uchumi, tangu kuanza kwa mageuzi ya kiuchumi, haijawahi kufikiria bei ya mafuta kama kigezo muhimu katika upangaji wa mipango hiyo.
Licha ya kuwa suala la bei ya mafuta linafahamika kwa wataalamu wanaoandaa mipango ya uchumi wa nchi, hakuna sehemu katika mipango hiyo panapoonyesha jinsi nchi ilivyojiandaa kukabili kikwazo hicho.
Suala la bei ya mafuta limekuwa likitajwa tu kama tatizo linaloikwamisha serikali ambayo viongozi wake wengi, akiwamo rais Kikwete, wanaishia kusema kuwa serikali haina lolote la kufanya kuhusiana na bei hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya utafiti wa uchumi ya ESRF, Dk. Lunogelo Bohela, ameniambia kuwa upangaji wa mipango kama vile MKUKUTA, MKURABITA na mingineyo, haukuzingatia bei ya mafuta kama moja ya vikwazo vinavyoweza kukwamisha utekelezaji wake.
Katika mahojiano nami, Dk. Bohela alibainisha kuwa huo ni upungufu mkubwa katika masuala ya uchumi, kwani athari za bei ya mafuta kwa uchumi wa nchi kama Tanzania, ambayo inategemea nishani hiyo katika uzalishaji, ni kubwa sana na ilipaswa kutiliwa maanani.
“Hadi hivi sasa bado tunategemea mafuta kama nishati ya msingi ya uzalishaji, tunatumia umeme kwa kiasi fulani lakini hata huo umeme nao sehemu yake unazalishwa kwa mafuta, hivyo tutake tusitake bado mafuta yataendelea kuwa ndio msingi wa uchumi wetu,” alisema.
Dk. Bohela alisema kuwa ilitarajiwa kuwa gesi asilia ingesaidia kupunguza utegemezi wa mafuta lakini haijafanya hivyo kwa sababu hivi sasa bado uwekezaji katika eneo hilo haujafikia kiwango kikubwa.
Akielezea matarajio yake kuhusiana na kufikiwa kwa malengo ya kukua kwa uchumi yaliyowekwa, baada ya bei ya mafuta kufikia rekodi ya dola za Marekani 100 kwa pipa na kutoonyesha dalili za kupungua, Dk. Bohela alisema kuwa itakuwa vigumu sana kwa Tanzania kufikia malengo hayo mwaka huu.
“Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita bei ya mafuta imeongezeka maradufu… inavyoonekana ni kuwa bei haiwezi kupungua, itandelea kupanda tu na hii itatuathiri sana.
“Sana sana, iwapo tutajitahidi kuchukua tahadhari kuzuia athari za kupanda kwa bei mafuta, tunachoweza kufanya ni kuhakikisha kasi ya kukua kwa uchumi ina-stabilise (inabaki kama ilivyo), yaani ibakie ileile ya mwaka uliotangulia, lakini sina matarajio makubwa sana kuwa tutaweza kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi katika hali hii,” alisema.
Dk. Bohela, ambaye ni mtaalamu wa uchumi katika nyanja ya kilimo, alisema kuwa kungekuwa na nafuu kubwa iwapo nchi ingekuwa inategemea malighafi nyingi kutoka nchini.
Alisema kuwa iwapo viwanda vinavyozalisha bidhaa nchini vingekuwa vinatumia malighafi nyingi za ndani, hiyo ingepunguza gharama za uzalishaji na kufanya bei ya bidhaa zinazozalishwa kuwa ya chini na kuleta unafuu kwa walaji.
“Hii gharama ya uzalishaji ndiyo kimsingi inayosababisha kupanda kwa mfumko wa bei za bidhaa… tuna bahati mbaya kwamba tunategemea nishati ya mafuta kutoka nje na pia malighafi kutoka nje,” alisema.
Akifafanua madhara ya kupanda kwa bei ya mafuta, alisema kuwa licha ya kuongeza gharama za uzalishaji, lakini kupanda kwa bei ya nishati hiyo kutaongeza pia gharama za usafiri na usafirishaji.
Akitoa ushauri, Dk. Bokela alisema serikali inaweza kuanzisha mazungumzo na moja ya nchi marafiki zinazozalisha mafuta na kukubaliana bei maalum ya upendeleo ambayo Tanzania itakuwa ikuziwa.
“Hii imeshawahi kufanyika huko nyuma na nadhani inaweza kufanyika hivi sasa kwa sababu tutaumia sana iwapo tutaendelea kutegemea mafuta kupitia soko la dunia,” alisema.
Mara kadhaa, rais Kikwete ameelezea kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia kama moja ya sababu zinazoikwamisha serikali kutekeleza mipango yake ipasavyo.
Katika hotuba zake, Kikwete husema kuwa bei ya mafuta katika soko la dunia imeiweka serikali kwenye hali mbaya kwa sababu haina uwezo wa kufanya lolote kuhusiana na udhibiti wa bei hiyo.
No comments:
Post a Comment