Uchaguzi Kenya na mustakabali wa EAC
Wakati wa ukusanyaji wa maoni kuhusu haja ya kuharakisha uundwaji wa Shirikisho la Afrika Mashariki, asilimia 75 ya watanzania walipinga wakisema hakukuwa na haja ya kuharakisha uundwaji wa shirikisho. Katika hao waliopinga, wapo waliohusisha hali ya amani na utulivu katika nchi za Kenya na Uganda na kueleza wasi wasi wao kuwa huenda ikaathiri shirikisho hilo.
Walitilia wasiwasi hali na mifumo ya kisiasa na kueleza kuwa haiendani na hali na mifumo ya kisiasa inayofuatwa na Tanzania. Baadhi ya viongozi waliwabeza wananchi hawa, wakisema kuwa hiyo ni hofu tu.
Walihakikisha kuwa hali ya kisiasa katika nchi hizo si sababu ya kuhofu. Lakini viongozi na wananchi wa Kenya wameamua kuonyesha kwa vitendo kuwa hofu hiyo iliyoonyeshwa na watanzania wengi na kuopuuzwa na badhi ya viongozi ni hofu halisi ambayo inapaswa kzuingatiwa kwa makini.
‘Sarakasi’ zilizofanywa katika uchaguzi mkuu wa Kenya hadi hivi sasa zimesababisha vifo vya zaidi ya watu 160. na hakuna anayejua kuwa idadi hiyo ni halisi au la kwa sababu hali ya mawasiliano imekuwa ngumu kiasi kwamba kuna uwezekano wapo wengi waliokufa lakini hawajatambuliwa.
Katika hatua iliyofikiwa nchini humo kutokana na uchaguzi mkuu, ni rahisi kumlaumu kila mtu. Lakini kwa ujumla, viongozi wa serikali na upinzani, wanasiasa na wananchi, wanapaswa kubeba lawama kutokana na machafuko yaliyotokea.
Wanachopigania ni matokeo ya uchaguzi. Wakati rais Kibaki, serikali yake pamoja na chama chake cha PNU wanatangaza kuwa wameshinda kihalali (sijui kama wanaamini hivyo), wapinzani, wakiongozwa na raila odinga wa ODM, wanadai kwa nguvu kuwa wameporwa ushindi wao.
Mabishano haya ndiyo yaliingiza wananchi mitaani, hasa baada ya kuapishwa kwa Kibaki, dakika chache tu baada ya kutangazwa kwa matokeo katika mazingira ya kutatanisha.
Polisi, waliotakiwa kulinda usalama, waliwapiga watu risasi katika kile kinachoelezwa kutuliza ghasia. Habari zilizopo zinaonyesha kuwa polisi hawakushambuliwa na silaha za moto na watu waliokuwa wanafanya fujo. Ni sehemu moja, Kisumu, ambako inaelezwa kuwa polisi waliwapuiga risasi wananchi wlaiowarushia mawe.
Inashangaza kuwa wakati wana zana nyingi za kutuliza ghasia bila kulazimika kupiga risasi za moto, polisi wanawesza kujibu mashambulizi ya mawe kwa risasi za moto!
Kwa upande mwingine, Odinga anafahamu kuwa ana wafuasi wengi nchini humo. Huu ni mtaji wa kisiasa ambao ameamua kuutumia kufikia malengo yake, kuwa kiongozi wa Kenya. Inatia moyo kuwa anahubiri amani, akiwataka wafuasi wake kuacha kufanya fujo na kuwa watulivu.
Lakini wakati huo huo, anawahimiza kushiriki katika maandamano ya amani kushinikiza Kibaki aachie ngazi. Odinga ameshawajaza wafuasi wake ujumbe kuwa kura zai zimeibwa, na anajua wazi kuwa katika mazingira ya siasa za mgawanyika kama zilizopo Kenya, haiwezekani kwa wafuasi wake kuwa wartulivu huku wakifahamu fika kuwa kura zao zimehujumiwa.
Hawawezi kuwa watulivu hasa bada ya msimamo na tabia zinazoonyeshwa na Kibaki, chama chake na serikali yake. Jinsi anavyong’ang’ania madaraka wakati ushahidi uliopo unaonyesha kuwa ushindi wake ni wa kupikwa.
Wafuasi wa Odinga hawawezi kutulia sasa wakati baadhi ya Tume ya Uchaguzi (ECK) wameanza kutoa maelezo yanayozidi kuthibitisha kuwa matokeo yaliyotangazwa yalikuwa na mushkeli.
Wajumbe wanne wa tume hiyo waliwaambia waandishi wa habari kuwa kuna umuhimu wa kuunda chombo kingine huru kuchunguza kile kilichotokea kwa sababu inavyoonekana kuna kasoro nyingi katika ujumlishaji wa matokeo.
Hata kama mwenyekiti wa ECK, Samuel Kivuitu atajitokeza kukanusha taarifa hizo, bado haitaondoa ukweli kuwa wajumbe hao wameongezea tu kwenye kasoro ambazo zilishaelezwa awali na waangalizi wa uchaguzi huo kutoka nje na ndani ya Kenya.
Serikali imeaanza jitihada za kutuliza hali ya mambo. Lakini inachokifanya hakiwezi kufanikiwa kwa sababu mazingira yanaonyesha wazi wazi kuwa ushindi wa Kibaki una kila aina ya dosari, si halali.
Katika mazingira hayo, Odinga, ambaye amekuwa akiipigania nafasi hiyo kwa miaka mingi, hawezi kukubaliana na ameshaonyesh hilo. Inafahamika kuwa mazungumzo ndio njia bora zaidi ya kumakliza tofauti baina ya watu wanaopingana. Kutokana na vurugu hizo, Odinga aliombwa kukutana na Kibaki ili kuzungumza na kumaliza tofauti zilizojitokeza.
Sharti kubwa alilolitoa ni kuwa Kibaki ajiuzulu kwanza na ndipo atakapokaana naye mza moja na kujadili. Anasema kua kukaa na Kibaki wakati akiwa bado anashikilia wadhifa wake wa urais, ni sawa na kukubali kuwa ameshinda kihalali wakati yeye (Odinga) anaamini kuwa Kibaki hakuingia madarakani kihalali.
Haya yanakumbushia yaliyowahi kutokea Zanzibar katika chaguzi. Mara zaote, Chama cha Wananchi (CUF) kimekuwa kikitoa madai baada ya uchaguzi kuwa kimeporwa ushindi. Jitihada zilifanywa kila mara kuwaleta CUF kaatika meza ya mazungumzo pamoja na mshindi. Lakini mara zote, CUF wamekataa kwa kusema kuwa kukaa meza moja na mtu huyo, ni sawa na kukubali ushindi wake.
Kilichotokea katika mabishano hayo bado ni kidonda ambachio kinaiumiza Tanzania hadi hivi leo. Katika uchaguizi wa mwisho, rais Abeid Aman karume aliapishwa saa chache tu baada ya matokeo kutangazwa kama ambavyo Kibaki ameapishwa dakika chache tu baada ya kutangazwa kwa matokeo.
Kama ilivyowahi kutokea kwa Zanzibar, mtiririko wa matukio katika uchaguzi unafanana na wa Kenya. Kila chama kilianza kujitangazia matokeo yake mapema huku tume ya uchaguzi nayo ikitoa matokeo yake. Inapofika wakati fulani karibu na mwisho, kama ambavyo CUF na CCM waliandika kwa tume ya uchgauzi kulalamikia matokeo, ODM na PNU nao walilalamika kwa tume kuwa wananyongwa.
Polsii na vikosi vya usalama vilitumika kuhalalisha matokeo ya uchaguzi zanizbra kama ambavyo sasa polisi na vikosi vya usalama vinavyotumika kuhalalisha ushindi wa Kibaki Kenya.
Lakinimkuna tofauti kubwa. Wananchi wa Kenya inaonekana wana mwamko mkubwa. Inaweza kuwa mwamko huo umejengwa kutokana na ukabila wao na watu wa kabila fulani wanaamua kulinda maslahi ya mgombea wa kabuila lao. Lakini kinachoonekana ni mwamko wao wa kutokubali kuibiwa.
Hali hii ni tofauti na watanzania ambao ishindi wa chama cha siasa hauna maana sana kwao kiasi cha kuwa tayari kupoteza maisha wakiutetea.
Na hiki ndicho walichokuwa wakikielezea watu waliokuwa wakipinga uharakishwaji wa uundwaji wa shirikisho la Afrika Mashariki, ingawa hakukieleweka wakati ule.
Watanzania wanauogopa mwamko huo wa wakenya wa kuwa tayari kupoteza maisha kwa ajili ya ushindi wa kiaisa. Wanaogopa kwa sababu hawajaiona mipaka ya mtu huyo aliye tayari kufa kwa ajili ya siasa. Wanajiuliza mpaka hivi sasa, kama yupo tayari kufa kwa ajili ya siasa, ambayo haina uhusiano wa moja kwa moja na kuleta sahani ya ugali mezani kwake, atafanya nini katika suala linalohusiana moja kwa moja na maisha yake, kwa mfano ajira.
Wakati wakenya wameonyesha kwa vitendo kuwa hofu ya watanzania kuhisna na siasa za Kenya ni halisi, inakuja changamoto nhingine. Pamoja na yanayotokea Kenya, bado dhamira ya kuunda Shirikisho la Afrika mashariki itaendelea.
Lakini, matukio haya yamethibitisha hofu ya watanzania na nidhahiri kuwa yatakuwa ni rejea pale ambapo watanzani watatakiwa kufikiri tena kuhusiana uundwaji wa shirikisho.
Wakati tunafikiri jinsi ya kuisadia Kenya kumaliza changamoto za uchaguzi wake mkuu, inapaswa tufikirie pia athari ya yaliyotokea katika dhamira yetu ya kuunda shirikisho la Afrika Mashariki. Tutafanya makosa makubwa iwapo tutaamua kufunika kombe ili mwanaharamu apite.
Huyo mwanaharamu hatopita, na kama akipita hatokwenda mbali, na atarudi kuja kutuandama. Hivyo ni uamuzi wetu iwapo tumshughulikie sasa hivi au tuendelee kuahirisha tatizo.
No comments:
Post a Comment