Sunday, January 6, 2008

BREAKING NEWS: WAHARIRI WASHAMBULIWA

Katika kile kinachoweza kuelezewa kuwa ni hujuma mbaya kabisa nchini, wahariri wawili wa gazeti la Mwana Halisi, wameshambuliwa siku ya Jumamosi kati ya saa 3 na saa 4 usiku.
Mhariri Mkuu wa gazeti hilo, Saed Kubenea ndiye aliyeathirika zaidi baada ya kumwagiwa tindikali usoni na taarifa zilizopatikana hivi punde kutoka Hosptali ya taifa Muhimbili alikolazwa, zinaelezwa kuwa amepoteza uwezo wake wa kuona.
Watu hao watatu, ambao mmoja alikuwa na panga, mwingine rungu na mwingine chupa iliyokuwa na rtindikali, waliwavamia wahariri hao ofisini kwao wakati walipokuwa wakiendelea na kazi ya kuandaa gazeti.
Walianza kugonga mlango baada ya kushindwa kuufungua na Kubenea alidhani kuwa ni wageni wa kawaida hivyio aliondoka kwenda kuwafungulia huku akiwataka wagomge polepole lakini alipofungua na kuona zana zao, alirudi ndani kwa kasi akiandamwa na yule mwenye chupa ya tindikali.
Wakati Kubenea akivamiwa na watu hao na kumwagiwa tindikali, Mhariri wa Habari wa gazeti hilo linalotoka mara moja kila wiki, Ndimara Tegambwage, alivamiwa na wale wawili na mmoja akaanza kumshambulia kwa panga.
Katika purukushani hiyo walimjeruhi Tegambwage, ambaye pia huandikia safu ya SITAKI katika gazeti la Tanzania Daima Jumapili.
Inaweza kuwa ni ajali ya kawaida lakini mazingira yake yanatia shaka kubwa sana. Tangu lianzishwe, Mwana Halisi limejidhihirisha katika jamii kama gazeti ambalo lipo mstari wa mbele kufumua na kuandika maovu yanayofanywa na viongozi kadhaa.
Gazeti hilo limejijengea sifa ya kutomung'unya maneno pale linapokuwa na habari fulani. Habari zake huandikwa kwa kutaja kila kitu pamoja na majina halisi ya wahusika. lakini kutokana na ujasiri huo, Mwana Halisi, wahariri na waandishi wake wamejijengea uadui na kundi fulani la watu na vitisho kwao viligeuka kuwa suala la kawaida.
Kubenea na Tegambwage labda hawakuwa na habari kuwa waliokuwa wakiwatishia walikuwa wanaandaa nini mkapa maswahibu haya yalipowakuta.
Wakati tunawaombea Kubenea na Tegambwage, ni wakati wa kuangalia waaandishi wanafanya nini ili kujilinda dhidi ya njama na hujuma kama hizi.

1 comment:

Anonymous said...

Kazi ya Rostam na Lowassa. Hamna mjadala.