Tuesday, January 8, 2008

POLISI WANATUZUGA?

Akizungumzia tukio la kushambuliwa kwa wahariri wawili wa Mwana halisi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya dar es Salaam, Kamishna Alfred Tibaigana amesema kuwa watu wawili wamekamatwa. Mmoja wa watu hawa ni mzee wa miaka inayokarinia 70! Mwingine amekamatwa kwa sababu amekutwa na kofia yenye damu! Sijui Polisi wana ushahidi uliowashawishi wawakate watu hawa lakini kama ushahidi wenyewe ndio huu ambao Tibaigana anausema, nina wasiwasi sana kwamba Polisi wanatuzuga.
Itashangaza sana iwapo mzee wa miaka hiyo awe ndiye aliyepambana kijasiri na kufanikiwa kuchomoka na kukimbia.
Na huyu mwenye kofia yenye damu, hivi kama akiwa ni mchinja mbuzi wa kule Vingunguti, polisi wanataka kutushawishi vipi?
Sasa hivi ndio Tibaigana anashituka na kuunda timu ya watu saba, inayioongozwa na yeye mwenyewe kulishughulikia tatizo hili. Sijui kama anafahamu kuwa anachokifanya ni kutibu tatizo ambalo tayari limeshatokea.
Alikuwa na nafasi ya kuzuia jambo hilo lisitokee. Mmoja kati ya walioshambuliwa, saed Kubenea, mara kadhaa ametoa taarifa polisi kuwa alikuwa si tu akipokea ujumbe wa vitisho, bali kulikuwa na majaribia ya kumdhuru.
Tibaigana na watu wake labda walidhani kuwa Kubenea anatafuta umaarufu au vipi? Wakadharau na kumuacha hivihivi mpaka alipopatwa na makubwa. Tunashukuru Mungu kuwa ameanza kuona tena na tunaamini kuwa huko India alikopelekwa, atapatiwa matibabu yatakayomrudishia afya yake kama awali.
lakini hili linafaa kuwa funzo kwa polisi kuwa mtu anapotoa taarifa za kutishiwa maisha yake, ifahamike kuwa maisha yake yapo hatarini. Na kwa kuwa ni kazi ya polisi kulinda raia na mali zake, wanawajibika kuyalinda maisha ya mtu huyo kwa gharama yoyote ile kwa sababu yeye ndiye anayelipa kodi inayowalipa wao mshahara kwa kazi ya kumlinda.

1 comment:

Anonymous said...

Nakubaliana nawe. Tangu tukio hilo limetokea nami nimejiuliza sana iwapo kulikuwa na hatua yoyote iliyochukuliwa na polisi tangu Bwana Kubenea alipotoa taarifa za kutishiwa maisha. Ilichokifanya Polisi kwa sasa ni kukumbuka shuka wakati kumeshapambazuka, na hii haitusaidii sisi wanahabari zaidi ya kutupa shaka endapo kweli Jeshi hili la polisi lipo tayari kutusaidia tukiwa na matatizo yahusianayo na taaluma yetu, ama la. Namwombea Kubenea pamoja na Mzee Ndimara (zero-in) uponyaji wa haraka.