HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa Daudi Ballali kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inadhihirisha kuwa kulikuwa na makosa makubwa katika taasisi hiyo nyeti. Ukubwa wa makosa hayo unaweza kuonekana kupitia hatua hiyo ya rais ambayo kwa namna yoyote ile ni hatua kubwa mno.
Hatua yake ya kuagiza vyombo kadhaa kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watu wengine waliohusika na kashfa hiyo, inadhihirisha pia kuwa Ballali si mhusika pekee katika sakata hili. Wapo wengine wengi tu ambao baadhi yao ni rahisi kuwatambua kutokana na nafasi zao.
Mtu asiyeweza kukwepa kunukia tuhuma hizi moja kwa moja ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha. Kwa mujibu wa wadhifa huo, mtu huyo ndiye anayehusika kuidhinisha malipo ambayo serikali inayafanya. Kwa Kiingereza yeye anaitwa ‘Paymaster General.’
Kashfa iliyomng’oa Ballali inahusiana na malipo. Ni malipo ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyopo BoT. Kwa sababu malipo haya yalifanywa na serikali ni dhahiri kuwa ‘Paymaster General’ aliidhinisha yafanyike.
Malipo yaliyotiliwa shaka na kuchunguzwa ni yale yaliyofanyika kipindi cha 2005/2006 wakati huo Gray Mgonja akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha pamoja na Peniel Lyimo. Lyimo alikwishaondolewa wizarani hapo lakini Mgonja bado anaendelea na wadhifa wake huo hadi hivi sasa.
Iwapo tunataka kupata maelezo ya kina kuhusiana na malipo haya, Mgonja na Lyimo wanaweza kutusaidia sana. Watatusaidia kwa sababu wao au mmoja wao - kulingana na mgawanyo wa kazi zao - ndio walioidhinisha malipo haya.
Kwa kawaida ‘paymaster general’ anaidhinisha malipo baada ya kujiridhisha kuwa malipo hayo ni halali na yanatolewa kwa kufuata taratibu zote za kiserikali zilizopo. Itashangaza sana iwapo ‘paymaster general’ akaamua kutoa tu fedha na kuzilipa bila kufuata taratibu hizo.
Kwa maana hiyo, Mgonja na Lyimo wanayo nafasi nzuri ya kutueleza Watanzania nini hasa kilifanyika katika malipo haya. Wala wasikwepe hili kwa namna yoyote ile kwa sababu wao ndio walihusika kuidhinisha malipo hayo.
Watueleze ilikuwaje wakakubali kuidhinisha malipo ya mabilioni haya ya fedha za wavuja jasho na kututia hasara kiasi hicho? Umakini wao uko wapi katika kuidhinisha malipo ya fedha zetu? Iwapo waliweza kuidhinisha malipo haya yenye kutia shaka, watashindwaje kuidhinisha malipo mengine mengi tu tusokuwa na habari nayo?
Uchunguzi uliofanywa unahusu mwaka 2005/2006 lakini akaunti ya EPA imefanya kazi kwa miaka mingi na Mgonja na Lyimo (pamoja na wengine) wamekuwapo wizarani wakiidhinisha malipo kupitia akaunti hii kwa miaka hiyo yote.
Inashangaza kuwa Mgonja bado anaendelea kuwapo madarakani hadi hivi sasa, wakati kasoro kubwa kama hii imeshajitokeza na Rais ameshawaonyesha Watanzania kuwa kuna kasoro kubwa kiasi cha yeye kutengua uteuzi wa gavana.
Kuna uwezekano kuwa gavana alihusika na wizi uliogunduliwa lakini pia kuna uwezekano kuwa hakuhusika. Kama alihusika hiyo ni sababu tosha ya Rais kusikiliza na kutekeleza maombi ya watu wanaotaka Ballali arudi nchini kuja kukabili mashtaka kuhusiana na kadhfa hiyo ya EPA.
Lakini kama hakuhusika, alipaswa kuwajibika kwa sababu yeye kama kiongozi wa taasisi nyeti, alipaswa kubaini ujanja huo uliofanywa na watu wengine na kuuzuia.
Ndiyo maana tulimwamini kuwa gGavana wa BoT. Hata kama hakuhusika, kutokea kwa wizi huu kunamaanisha kuwa Ballali hakuifanya kazi yake ipasavyo. Na ndiyo maana Rais hakuona kigugumizi na kuchukua hatua ya kutengua uteuzi wake mara moja.
Sasa ndugu yetu Mgonja, wewe ndiye uliyeidhinisha malipo ya mabilioni hayo yote; hivi hauoni tu kuwa nawe unahusika kwa karibu mno na kashfa hii? Au unataka hadi Rais atengue uteuzi wako pia? Hata kama hukuhusika, kwa nini usiwe mstaarabu na kuamua kuachia ngazi ili ule uchunguzi aliosema rais ufanyike uje ukusafishe?
Mgonja anatakiwa kutambua kuwa watu wanaomwangalia na kumpima katika hili, wanarejea tuhuma nyingine alizowahi kutupiwa huko nyuma naye akashindwa kuzitolea majibu ya kuridhisha.
Watu bado wanakumbuka kuwa jina lako lilikuwamo kwenye orodha ya viongozi waliotuhumiwa kwa ufisadi. Wewe mwenyewe ulikaririwa kuwa utashitaki kwa sababu umepakaziwa. Lakini hadi leo haijajulikana kesi yako imekwama wapi!
Hilo lina tafsiri kubwa sana machoni pa Watanzania na sasa inapobainika kuwa ulikuwapo katika Wizara ya Fedha kama ‘paymaster general’ wakati malipo ya EPA yanafanyika mwaka 2005/2006, Watanzania wamepata kitu kingine cha kukupima.
Hata kama ulitumiwa kuidhinisha malipo hayo bila ya wewe mwenyewe kujua, unatakiwa kuwajibika kwa sababu utakuwa ulishindwa kufanya kazi yako vema na kubaini kuwa malipo hayo yalikuwa na mushkeli.
Ningependa kukushauri kuwa uwe muungwana na ujiondoe haraka iwezekanavyo kwa sababu hata ufanye nini, utaendelea kunukia marashi ya EPA. Hilo hauwezi kulikwepa.
No comments:
Post a Comment