Tuesday, January 29, 2008

Wabunge Wadai Ripoti Kamili ya Ernst & Young

SASA inaelekea mambo yataanza kunoga. Wabunge wameshaanza kuidai ripoti kamili iliyoandikwa na kampuni ya Ernst & Young kuhusiana na ubadhirifu uliobainika katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), iliyopo Benki Kuu (BoT).

Wabunge walitoa msimamo wao huo jana, mara baada ya Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, kumaliza kuwasilisha bungeni kauli ya serikali ambayo ilikuwa ni taarifa kuhusu ripoto ya ukaguzi wa EPA.

Wabunge waliona huo ni mwanzo wa ubabaishaji kwani alichokiwasilisha Meghji ilikuwa ni muhtasari wa kilichomo katika ripoti ya Ernst & Young, na hatua ambazo rais Jakaya Kikwete na Wizara yake imezichukua baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo.

Taarifa hiyo ya Meghji, haina tofauti sana na taarifa ambayo ilitolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, ikielezea kilichobainika katika ukaguzi uliofanywa na Ernst & Young na hatua ambazo rais Kikwete alizichukua.

Baada ya kumaliza kusoma kauli hiyo, Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP) na Christopher ole Sendeka (Simanjiro-CCM), walisimama wakitaka mwongozi wa Spika kuhusiana na suala hilo.

Alipopewa nafasi ya kusema, Cheyo alieleza kuwa taarifa iliyoeasilishwa na Meghji ni nzuri, lakini akabainisha kuwa ni finyu mno ukilinganisha ya ripoti ya Ernst & Young.

Aidha, Cheyo alihoji iwapo ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) itawasilishwa Bungeni na kutaka tipoti hiyo, pamoja na taarifa ya Meghji, vyote vijadiliwe na wabunge kwa kina

Kwa upande wake, Sendeka aliposimama, alibainisha kuwa kilichowasilishwa na Waziri Meghji ni muhtasari tu.

Huku akimwelekea Spika, ole Sendeka alisema: “Naomba kama itakubalika uielekeze serikali ilete taarifa kamili ya mkaguzi (Ernst & Young) na bunge lipate fursa ya kuijadili kwa kina.”

Kwa kuoinyesha kuwa wanaunga mkono yanayowasilishwa na wenzao, wabunge wengi walikuwa wakishangilia kwa kupiga makofi wakati wabunge hao wawili walipokuwa wakiwasilisha hoja zao.

Akijibu maombi hayo, Spika Samuel Sitta alikubaliana na hoja za wabunge hao na kusema kuwa yote waliyaomba yamo katika mchakato wa mashauriano baina ya ofisi ya Spika na serikali.

Aliwakumbusha watoa hoja na wabunge wengine kwua tangu awali, alishakubaliana na hoja iliyowasilishwa na Lucy Mayenga (Viti Maalum-CCM), akitaka ripoti ya hesabu za BoT za mwaka 2005/06 iwasilishwe bungeni na kujadiliwa na wabunge wote.

“Hoja hii bado ni hai na taarifa iliyotolewa leo si kipingamizi. Naamini kuwa katika wakati huu wa uwazi na ukweli serikali imeeshasikia hoja zenu na itazitafakari ipasavyo na bila shaka tutafikia mahali pazuri,” alisema Spika Sitta.

Katika taarifa aliyoiwasilisha jana Bungeni, pamoja na kubainisha yaliyogunduliwa na Ernst & Young katika ukaguzi wa EPA na hatua zilizochukuliwa na rais, meghji alisema kuwa wizara yake nayo imechukua hatua kadhaa.

Alisema kuwa baada ya kupata ripoti hiyo, Wizara ya fedha imeiagiza Mamlaka ya Mapato cnhini (TRA), kufanya uchunguzi wa kina kubaini mienendo ya ulipaji kodi wa makampuni yote yaliyohiska katia kashfa ya EPA.

Aidha, Meghji alisema kuwa iwapo itabainika kuwaepo kwa ukwepaji wa kodi, TRA imetakiwa kuchukua hatua za kisheria.

Pia wizara yake imeielekeza BoT kufanya uhcunguzi wa kina na kuwasilisha taarifa serikalini kuhusu hatua zilizochukuliwa kwa mabenkiya biashara yaliyohusika na kupokea fedha kutoka makampuni yaliyotajwa kuhusika katika kashfa ya EPA, iwapo sheria, taratibu na kanuni kuhusu udhibioti wa fedha haramu zilizingatiwa.

Aidha, akifafanua hatua ya rais Kikwete kuwaagiza Mwanasheria Mkuu wa serikali (AG), Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kuchunguza zaidi suala hilo, unalenga kupata ushahidi wa kisheria utakaowezesha kufunguliwa kwa mashtaka dhidi ya watu na kampuni zote zilizohusika katika kashfa ya EPA.

No comments: