Friday, February 1, 2008

Masuala Nyeti Yapigwa Danadana Bungeni

KIU ya watanzania kufahamu hatma ya hoja nyeti zinazosubiri maamuzi ya Bunge itabidi kusubiri kwa wiki moja zaidi.
Hii ni kutokana na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kutangaza kuwa masuala hayo nyeti, hayatajadiliwa Bungeni wiki hii hadi atakaporejea kutoka Marekani.
Spika Sitta alitangaza kuwa atakuwa na ziara ya wiki moja nchini Marekani alikoalikwa na Baraza la Wawakilishi na kutoa maelekezo kuwa katika muda ambao hatokuwepo, masuala nyeti yaliyo Bungeni yatapaswa kusubiri.
Alisema kuwa anatarajia kuondoka Jumatatu na kurejea Alhamisi hivyo Naibu Spika, Anne Makinda, atakaimu nafasi yake lakini kati ya majukumu yake hayatahusisha kushughulikia masuala hayo nyeti.
Sitta aliyataja masuala hayo kuwa ni pamoja na suala la ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoangalia mchakato wakuipata kampuni ya Richmond Development (RDC) ya Marekani, iliyopewa kandarasi ya kuzalisha umeme za dharura wakati taifa lilipokabiliwa na upungufu wa nishati hiyo mwaka juzi.
Pia aliitaja hoja nyingine nzito kuwa ni lile linalohusiana na sakata la kashfa ya akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA) ya Benki Kuu (BoT).
“Sikutaka Naibu Spika akurupuke na kuvamia masuala haya nyeti, itabidi yasubiri mpaka pale nitakaporejea… tunayo wiki nzima ya kuyaangalia haya,” alisema.
Hata hivyo, dalili za kupigwa danadana kwa suala la EPA zilianza kuonekana mapema Bungeni jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu, pale ambapo masuali kuhusiana na suala hilo yalipozuiliwa na Spika, kwa maelezo kuwa suala hilo bado linajadiliwa.
Wakati fulani, Spika alizima swali la nyongeza lililoulizwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF), ambaye baada ya Naibu Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo kubainisha kuwa suala la EPA linafanyiwa kazi kutokana na maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete.
Aliposimama kuuliza swali la nyongeza, Hamad Rashid alikumbusha kwua kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, taasisi hiyo ambayo ni moja ya mihimili ya utawala, haizuiliwi kujadili suala ambalo linachunguzwa na taasisi nyingine, ukiacha masuala ambayo yapo mahakamani.
Lakini Spika badala ya kumwita Mkulo kujibu suala hilo, alisimama na kutoa maelezo kuwa alishatoa maelezo awali kuwa majadiliano kuhusu suala hilo yanaendelea na atalitaarifu Bunge hatma ya majadiliano hayo.
Baada ya jitihada za Hamad Rashid kugonga mwamba, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisimama kwa lengo la kuuliza swali la nyongeza, na kwa kudhani kuwa anakusudiakuuliza swali kuhusiana na suala hilo, Spika alimzuia akisema kuwa maelezo aliyoyatoa yameizima hoja hiyo kuendelea kuhojiwa.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mapema wiki hii, Spika aliliambia Bunge kuwa ndani ya wiki huii angetoa taarifa kuhusiana na matokeo ya mashauriano kati ya ofisi yake na serikali kuhusiana na suala la kuwasilishwa Bungeni kwa ripoti kamili iliyoandaliwa na kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu ya Ernst & Young kuhusiana na EPA.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili nje ya Bunge baada ya kipindi cha maswali na najibu, Zitto alisema kuwa lengo lake la kusimama halikuwa kuulizia masuala ya EPA.
“Inaonekana mzimu wa EPA umevawaa serikalini, kila kitu wao wanaona kama EPA… mimi sikutaka kuulizia kuhusu EPA, hoja yangu ilikuwa ni kuwa Naibu Waziri hakujibu swali lililoulizwa.
“Swali liliuliza kuhusu Debt Conversion Scheme, hizi ni fedha ilizoliwa na wafanyabishara waliouziwa madeni, hilo ndilo lililoulizwa lakini waziri alikwepa kulijibu hilo,” alisema Zitto.

No comments: