Wednesday, February 6, 2008

BREAKING NEWS: Lowassa ananuka Richmond

Kamati teule ya Bunge, iliyopewa kazi ya kuangalia mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura kati ya kampuni ya Richmond Development ya Marekani na serikali, imemkuta waziri Mkuu, Edward Lowassa, akiwa mchafu kimaadili na kumshauri kujiuzulu.

Kwa maneno yake, kamati hiyo inahitimisha: “Kamati teule haikufurahishwa hata kidogo na taarifa zinazomgusa moja kwa mowa moja Mhe waziri Mkuu katika kuipendelea Richmond Development Company LLC. Hata hivyo, Kamati teule imetimiza wajibu wake kwa uwazi na ukweli kama ilivyoagizwa na Bunge letu tukufu.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa nafasi aliyonayo Mhe. Waziri Mkuu katika uendeshaji wa shughuli za serikali na uongozi wan chi kwa ujumla, ni wajibu wake yeye mwenyewe kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huu na wajibu wake kikatiba ndani na nje ya Bunge.

“Vile vile ni wajibu wa Bunge ambalo linathibitisha uteuzi wake kwa mujibu wa Ibara ya 51 inayothibitisha uteuzi wake, kuangalia ikiwa matokeo ya uchunguzi huu hayajaathiri hadhi na uzito wake ndani ya Bunge.”

Kwa maneno mengine, Kamati hiyo iliyokuwa inaongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela-CCM) ilikuwa inamtaka waziri Mkuu kujiuzulu kutokana na kuhusika kwake na kashfa hiyo.

Aidha, iwapo Lowassa angeshindwa kuchukua uamuzi wa kumwajibisha kwa kumpigia kura ya kutokwua na imani naye.

Kwa ujumla, Kamati hiyo imebaini kuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, wanahusishwa moja kwa moja na kuipatia kampuni hiyo kazi ya kuzalisha umeme wa dharura wakati ikiwa haina sifa.

Aidha, wengine wanaotajwa katika ripoti hiyo na kushauri wawajibishwe kutokana na ushiriki wao katika sakata hilo ni waziri wa sasa wa Nishati na Madini, nazir Karamagi, katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Ather Mwakapugi pamoja na Kamishna wa Madini, Bashir Mrindoko.

Wengine ni Mwanassheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, ambaye kwa mujibuw a ripoti hiyo ameonekana kutojua alichokuwa anakifanya wakati baadhi ya viongozi wakiwa wanatekjeleza njama za kupindisha sheria na taratibu ili kuhakikisha kuwa Richmond inapatiwa kazi hiyo.

Uchunguzi wa Kamati pia ulibaini kuhusika kwa aliyekuwa waziri katika serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, jinsi ambavyio naye alishiriki katika kuhakikisha kuwa Richmond inapata kazi hiyo.

Inaelezwa katika ripoti hiyo kuwa Dk. Msabaha aliamua kukiuka maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na mchakato wa kuipata kampuni itakayozalisha umeme wa dharura, na kuilazimisha Tanesco kupindisha taratibu na kuikumbatia Richmond ingawa ilidhihirika wazi kuwa haikuwa na sifa ya kupata kazi hiyo.

Hata hivyo, Msabaha anakaririwa na ripoti hiyo akisema kuwa katika suala hilo, yeye amefanywa kuwa kondoo wa kafara tu.

Mtiririko wa ripoti hiyo unaonyesha kuwepo kwa maelekezo na maagizo kutoka kwa Lowassa, kwenda kwa Dk. Msabaha kuhakikisha kuwa Richmond inapatiwa kazi hiyo kwa njia yoyote ile.

Pia ripoti hiyo imeonyesha jinsi Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Nchini (Takukuru), kwa jinsi ambavyo ilitumia mamlaka yake kuficha ukweli wa mambo na kuisafisha Richmond pamoja na viongozi wasio waadilifu walioileta kampuni hiyo.

Kwa msingi huo, Kamati hiyo imependekeza kuwa uongozi wa Takukuru ufanyiwe mabadiliko makubwa ili kulinda hadhi ya taasisi hiyo muhimu katika mapamvbano dhidi ya rushwa.

No comments: