Tuesday, March 4, 2008

Butiama Kuitikisa CCM

HALI ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) si shwari na taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa, makundi ya kisiasa ndani ya chama hicho yameshaanza kujipanga kwa ajili ya kushtakiana ndani ya vikao vikubwa viwili vitakavyoitishwa baadaye mwezi huu.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kwamba, wajumbe wanaounda makundi hayo ambayo yamechipua kutokana na Kashfa ya Richmond wameshaanza kufanya mashauriano ya namna ya kukabiliana wakati wa vikao vya Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Maandalizi ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, kinatarajiwa kufanyika baadaye mwezi huu huko Butiama ambako ndiko nyumbani na mahali alikozikwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Vyanzo vya habari vya kuaminika kutoka ndani ya makundi hayo mawili, moja likiwa ni lile lililofanikisha kuanguka kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na jingine linalojaribu kumsafisha yeye na wenzake wengine kadhaa tayari yanaonyesha mwelekeo wa kujipanga, tayari kukabiliana na mwenendo huo wa mambo.

Mmoja wa makada maarufu wa chama hicho anayetoka katika kundi linaloshangilia kuanguka kwa Lowassa, Nazir Karamagi na kusakamwa kwa mfanyabiashara Rostam Aziz anasemakuwa tayari walikuwa wameshajipanga kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo.

Mwana CCM huyo ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho, alisema tayari wameshaanza kufuatilia kile walichokiita nyendo za Lowassa na wana CCM wenzake wengine wanaomuunga mkono ili kuweza kupata msingi imara wa kujenga hoja zao dhidi ya kundi hilo.

Kada huyo machachari wa CCM alisema miongoni mwa hadidu za rejea ambazo watazitumia kummaliza Lowassa, Rostam, Karamagi na wanasiasa wenzao wa kundi hilo ni kauli walizozitoa nje ya Bunge dhidi ya ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe.

Kwa mujibu wa kada huyo, watu kadhaa wenye msimamo kama wake tayari wameshaanza kukusanya vielelezo na kujenga hoja ambazo wanaamini wakizitumia zitasaidia kuzima jitihada zozote zinazoonekana kuanza za Lowassa na wana CCM wenzake kujisafisha.

Mbali ya Lowassa, kundi hilo linataka pia chama hicho kitoe karipio kali dhidi ya Rostam na Karamagi kutokana na kile wanachokieleza kuwa ni kukitia doa chama na serikali kwa sababu tu ya kuweka kwao mbele maslahi ya kibiashara kuliko ya umma.

Habari zaidi kutoka ndani ya kundi hilo la kwanza zinaeleza kwamba, iwapo mkakati wao huo utakwama ndani ya chama, basi hatua itakayofuata itakuwa ni kuupeleka bungeni ambako wataitumia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwachukulia hatua Lowassa na wenzake kadhaa wanaodaiwa kutoa kauli ambazo zinaonyesha dharau kwa Bunge.

Wakati kundi hilo la kwanza likijipanga kwa ajili ya kupigilia msumari wa mwisho katika kile wanachokiona kuwa ni ‘jeneza la kisiasa’ la akina Lowassa, Rostam na Karamagi upande wa pili nao unaonekana kujipanga kwa ajili ya kulikabili kundi hilo la kwanza.

Habari zinaonyesha kuwa, nalo limeanza kukusanya vielelezo kadhaa ambavyo wanataka kuvitumia kwa lengo la kukishawishi chama chao kuwa Kashfa ya Richmond ilikuwa na lengo la kuwadhalilisha, kuwaumiza na kuwamaliza kisiasa.

“We will definitely hit back (Ni wazi kwamba tutajibu mapigo). Hatuwezi tukakaa kimya wakati tukijua waziwazi kwamba watu hawa wameazimia kutuumiza kwa malengo ya kisiasa.

“Hii si haki hata kidogo, mtu unazushiwa uongo wa wazi halafu watu wanakuwa washangiliaji. Ni jambo baya kwamba taasisi za kisheria zimefanya ‘mob justice’ (zinachukua sheria mikononi).

“Hili hatuwezi kukubali liendelee. You wait and see,” alisema mmoja wa wanasiasa hao waliotajwa katika sakata la Richmond ambalo lilisababisha Lowassa ajiuzulu uwaziri mkuu huku Karamagi na Dk. Ibrahim Msabaha wakijiuzulu nyadhifa zao za uwaziri.