Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kiongozi wa Timu iliyoteuliwa na Rais Kikwete kuchunguza wizi wa mabilioni ya EPA, Johnsom Mwanyika ametoa taarifa ambayo inaibua maswali mengi bila kujibu maswali yaliyoibuliwa awali.
Katika taarifa hiyo, ambayo kimsingi haina kipya, Mwanyika amewataka watanzania na wanahabari kuwa na uvumilivu wakati Timu yake ikiendelea na kazi ya uchunguzi.
Kwa kudhihirisha kuwa hataki kutoa taarifa mpya, Mwanyika amejificha chini ya kivuli cha kuogopa kuharibu wa upelelezi unaoendelea.
Anasema: “Timu inaona ni vyema kutotoa taarifa ambazo zitaathiri kazi ya uchunguzi inayoendelea. Tunapenda kuusihi Umma na Wanahabari kuwa na subira wakati kazi hii inaendelea.”
Aidha, alishindwa kutaja majina ya watuhumiwa ambao tayari wamerejesha sh bil 50 walizoiba. Mwanyika anasema hawezi kuwataja kwa sababu wao ni makampuni na utu wao unatambuliwa kisheria tu.
Taarifa kamili ya Mwanyika hi hii hapa:
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TIMU YA RAIS YA UCHUNGUZI WA FEDHA ZA EPA
TAARIFA KWA UMMA
Kama mnavyofahamu tarehe 08 Januari, 2008 Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete aliunda Timu inayojumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili, pamoja na mambo mengine, kuchunguza na kuchukua hatua za kisheria kwa makampuni na watuhumiwa wa upotevu wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mheshimiwa Rais alituagiza kuwa tuwe tumekamilisha kazi hiyo katika kipindi cha miezi sita.
Taarifa hii ya tatu inatolewa kufafanua na kutoa taarifa ya namna kazi inavyoendelea kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais takriban miezi miwili iliyopita.
Timu inapenda kuufahamisha umma kuwa pamoja na majukumu mengi iliyopewa, kwa sasa Timu imejikita katika kufanya uchunguzi wa kitaalam na wa kina. Kwa msingi huo, pamoja na fedha zinazorudishwa, ni vyema Umma na Wanahabari wakafahamu kuwa kazi ya uchunguzi haijafika mwisho na kwa sasa Timu inaona ni vyema kutotoa taarifa ambazo zitaathiri kazi ya uchunguzi inayoendelea. Tunapenda kuusihi Umma na Wanahabari kuwa na subira wakati kazi hii inaendelea.
Hata hivyo, Timu inapenda kuuhakikishia Umma na Vyombo vya Habari kuwa kazi hii ya uchunguzi inaendelea vizuri na Timu inapata ushirikiano mzuri kutoka kwa makampuni na wamiliki wanaohusika na upotevu wa fedha za EPA.
Vilevile tunapenda kuukumbusha Umma na Wanahabari kuwa Timu imepewa miezi sita ya kufanya kazi na hatimaye kuwasilisha Taarifa kwa Mheshimiwa Rais. Huu ni mwezi wa pili tangu Timu ianze kazi yake. Kwa msingi huo, Timu inawasihi Umma na Wanahabari kuwa na subira kwani Wahenga walisema SUBIRA YAVUTA HERI. Tunawahakakishia kuwa kazi inaendelea vizuri na heri yaja kwani tulichonacho hadi sasa katika uchunguzi si haba.
Vilevile Timu inapenda kutoa ufafanuzi kuhusu maswali na malalamiko ya kutokamatwa kwa waliohusika. Tunapenda kuueleza umma kwamba uchunguzi wetu hadi hivi sasa unaonyesha kwamba wahusika wakuu ni makampuni. Kisheria, makampuni hayo ni mtu yaani ‘Legal Person’. Hata hivyo, makampuni hayo ni tofauti na mtu wa kawaida. Kampuni katika maana hii, inajitegemea yenyewe.
Kwa msingi huo, ikiwa kampuni imefanya kosa, kuna utaratibu wa kufuata kisheria. Kazi inayofanyika hivi sasa, ni uchunguzi wa kina kuhusu maafisa wa makampuni hayo ili kufahamu ni kitu gani kilichosababisha hali hiyo kutokea. Uchunguzi huu unaendelea na ndiyo utakaotuwezesha kujua hatua za kisheria zitakazochukuliwa.
Timu inapenda kuutarifu Umma na Wanahabari kuwa itaendelea kutoa taarifa ambazo inaamini hazitaathiri uchunguzi unaoendelea mara kwa mara.
Imetolewa na Johnson P.M Mwanyika,
Mwenyekiti wa Timu
9 Machi, 2008
No comments:
Post a Comment