Monday, April 21, 2008

Andrew Chenge ajiuzulu

(Habari hii ni kwa hisani ya Tanzania Daima)

WAZIRI wa Miundombinu, Andrew Chenge, amejiuzulu wadhifa huo kuanzia jana kwa kile alichoeleza kuwa ni kulinda masilahi ya taifa.
Chenge, ambaye anakabiliwa na tuhuma za kumiliki zaidi ya dola milioni moja za Marekani katika akaunti yake iliyopo Kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza, jana alimwandikia Rais Jakaya Kikwete barua ya kuomba kujiuzulu, ambayo rais aliiridhia.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima jana usiku, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alithibitisha rais kupokea barua ya Chenge ya kuomba kujiuzulu wadhifa wake.
Alisema rais aliridhia barua hiyo, huku akimkariri akisema kuwa kwa mazingira ya wakati huu uamuzi huo unafaa kuchukuliwa.
Aidha, mkurugenzi huyo akikariri barua ya Chenge, alisema amefikia uamuzi huo ili kulinda masilahi ya nchi pamoja na kwamba uchunguzi wa suala hilo bado unaendelea.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa uamuzi huo wa Chenge umefikiwa baada ya mashauriano kati yake na Rais Kikwete.
Taarifa hizo zinaeleza kuwa kufikiwa kwa uamuzi huo hakumaanishi kukiri tuhuma hizo, bali kutambua uzito wa tuhuma zinazomkabili.
Aidha, habari zinaeleza kuwa uamuzi huo wa Chenge umechangiwa na dhamira yake ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kuzungumzia kwa kina tuhuma hizo.
Wiki iliyopita, gazeti la The Guardian la nchini Uingereza liliandika kuwa, katika uchunguzi wa SFO iligundulika akaunti moja inayohusishwa na Chenge ikiwa na zaidi ya dola za Marekani milioni moja iliyopo kwenye Kisiwa cha Jersey.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, SFO inamchukulia Chenge kuwa mtu anayeweza kuwa shahidi muhimu katika uchunguzi wa zabuni ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE System ya nchini Uingereza.
Gazeti hilo liliandika kwamba, SFO inatarajia kuanza upya kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo, ili kuangalia iwapo zina uhusiano na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka nchini humo kwa paundi milioni 28 ambazo ni sawa na sh bilioni 70, mwaka 2002.
Hata hivyo, inaaminika kwamba uchunguzi wa SFO unatarajia kuanza katika kipindi cha wiki sita zijazo ingawa ule wa awali ulionyesha kuwa moja ya mambo yanayofuatiliwa ni kujua iwapo fedha zinazoaminika kuwa za Chenge zina uhusiano na zile zilizotoka katika Kampuni ya BAE inayotuhumiwa kuinyonya Tanzania kwa kuiuzia rada mbovu kwa bei kubwa kuliko ilivyotakiwa.
The Guardian katika habari yake hiyo iliyowekwa katika mtandao wa intaneti, linaripoti kuwa, taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.
Gazeti hilo lilimkariri Waziri Chenge akikiri kwamba fedha hizo ni zake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Akizungumzia kwa mara ya kwanza tuhuma hizo Jumatano iliyopita, Chenge aliwataka Watanzania kusubiri uchunguzi dhidi yake unaofanywa na SFO.
“Tusubiri uchunguzi ukamilike... kama uthabiti ukithibitisha hata hivyo vijisenti, ijajulikana vilipatikanaje,” alisema Chenge nje ya chumba cha wageni mashuhuri (VIP) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, akitokea nchini China.
Kutokana na kauli yake ya kuziita mabilioni ni vijisenti, wananchi walionyesha kukerwa na kauli hiyo kwa maelezo kuwa ni dharau, na kwamba huenda atakuwa akimiliki fedha zaidi ya hizo.
Pamoja na hayo, baadhi ya vijana wanaotoka katika vyama kadhaa vya upinzani mjini Dodoma walitangaza azima yao ya kuandamana, ili kumzuia asiingie bungeni wiki hii.
Kutokana na hali hiyo, Chenge alilazimika kuwaombva radhi Watanzania ambao walikwazika au kuumizwa na kauli hiyo.
Chenge alisema halikuwa lengo lake kuwakera wananchi kwa kauli hiyo iliyozua mjadala kiasi cha baadhi ya makundi ya watu wa kada tofauti kutoa maoni yao wakimtaka Rais Jakaya Kikwete amwajibishe.
“Mimi si Mzaramo. Hiki ni Kiswahili. Sisi wengine kule Usukumani kusema vijimambo, au vijisenti, vijitoto hivi ni kawaida kwa desturi zetu.
“Ndiyo maana napenda kusema wazi kwamba iwapo kuna Watanzania niliwaumiza kwa kauli ile niliyoitoa kwa nia njema kabisa na wala si kwa lengo la kuwakejeli, naomba radhi kwa hilo,” alisema Chenge.
Chenge ni waziri wa nne kujiuzulu katika kipindi cha miezi miwili baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha kujiuzulu kutokana na kutajwa katika kashfa ya mkataba tata wa kuzalisha umeme wa dharura wa Kampuni ya Richmond.
Mawaziri hao isipokuwa Dk. Msabaha ni miongoni mwa orodha ya mafisadi 11 iliyotajwa na kambi ya upinzani, Septemba 15 mwaka jana katika viwanja vya Mwembe Yanga.
Aidha, Chenge alikuwa ni miongoni mwa wanasiasa walioandamwa hasa baada ya kurejeshwa tena serikalini, wakati wa mabadiliko ya mawaziri yaliyotokana na kuvunjika kwa Baraza la Mawaziri, Februari mwaka huu.

No comments: