(Habari hii ni kwa hsiani ya Tanzania Daima)
ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ukiwaona Ditopile Mzuzuri, amefariki dunia jana asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk. Meshack Massi, Ditopile alifariki dunia ghafla jana, saa 3 asubuhi akiwa katika Hoteli ya Hilux, iliyopo mjini hapa.
Dk. Massi alisema Ditopile alifariki dunia akiwa katika hoteli hiyo alipokuwa akiangalia televisheni.
Alisema jana asubuhi alipokea ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (SMS) kutoka kwa uongozi wa hoteli hiyo ambako Ditopile alikuwa amepanga kuwa hali yake si nzuri na wangehitaji msaada wa daktari.
“Nikaagiza haraka wauguzi kwenda kumpima, baadaye nikaona wanakuja na gari ndogo na tulipompima tukabaini alikuwa amefariki dunia,” alisema Dk. Massi.
Mwili wa marehemu ulisafirishwa jana kwa gari la jeshi lenye namba 1759 JW 04, kwenda jijini Dar es Saalam ambako umehifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, ukisubiri mipango ya mazishi.
Habari zinaeleza kuwa uchunguzi wa mwili huo unatarajiwa kufanyika katika Hospitali ya Lugalo, kwani chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika.
Mdogo wa marehemu, Selemani Ditopile, akizungumza na Tanzania Daima jana jioni, alisema marehemu anatarajiwa kuzikwa kesho katika makaburi ya familia yaliyopo Kinyerezi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Akizungumzia kifo hicho, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Said Kalembo, alisema juzi Ditopile alimpigia simu akimfahamisha kwamba yupo mkoani Morogoro na kwa kuwa alikuwa amefika usiku walitafuta nyumba ya kulala.
“Kesho yake hatukuonana, lakini alipomaliza shughuli zake alirudi katika hoteli hiyo. Jana baada ya kuamka akiwa na mkewe wakiwa wanaangalia televisheni ghafla alizidiwa na kuomba msaada wa kidaktari.
“Hata hivyo, baadaye alipomuangalia kwenye viganja vya mkono, vilikuwa vyeupe,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Aidha, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Thobias Andengenye, alisema walipokea simu ya Dk. Massi iliyoeleza kuwa katika chumba cha ICU mkoani hapo kulikuwa na mwili wa Ditopile.
Alisema taarifa kutoka kwa ndugu aliokuwa nao zinaeleza marehemu alikuwa na ndugu zake wawili, akiwemo mdogo wake, Selemani Ditopile na mkewe Tabia.
“Walifika mkoani hapa Aprili 18, saa 6 usiku na kufikia katika hoteli hiyo kwa ajili ya mapumziko, tayari kwa safari kesho yake kwenda kwenye mashamba yake yaliyopo Mgongolwa, wilayani Mvomero,” alisema kamanda huyo wa Polisi.
Alisema siku iliyofuata walikwenda shambani huko ambako walirudi saa 12 jioni na waliporudi waliwatembelea ndugu na jamaa mkoani hapa, kisha wakarejea hotelini hapo kulala na Ditopile alikuwa amelala chumba namba 106, wakiwa na mpango wa kurejea Dar es Salaam jana.
“Alfajiri inadaiwa marehemu huwa na tabia ya kuswali, kwa hiyo baada ya swala yeye na mkewe huyo walikaa kuangalia televisheni, ambapo mkewe alipitiwa usingizi kidogo, alipoamka akajaribu kumwamsha lakini hali yake haikuwa ya kawaida,” alisema.
Alisema baadaye alimjulisha shemeji yake na kuanza kutoa taarifa kwa ndugu na jamaa ndani na nje ya mkoa sambamba na kuomba msaada katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ambaye aliwasili mjini hapa jana asubuhi, alisema ameguswa na msiba huo kwa kuwa alimfahamu Ditopile kwa muda mrefu na wamekuwa pamoja jeshini na serikalini.
Alisema kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi ni msiba mkubwa, kwa kuwa alikuwa na mchango mkubwa katika chama na alikuwa akirekebisha kasoro mbalimbali za chama.
Ditopile ambaye pia alikuwa mwanasiasa alifunguliwa kesi ya kumuua kwa kumpiga risasi, dereva wa daladala, Hassan Mbonde, katika tukio lililotokea makutano ya Barabara ya Bagamoyo na Kawe, Dar es Salaam. Tukio hilo linadaiwa kutokea jioni ya Novemba 4, mwaka 2006.
Katika kesi hiyo ambayo awali ilikuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kabla ya kuhamishiwa Mahakama Kuu, Ditopile alikuwa akitetewa na Wakili, Nimrod Mkono.
Baada ya kesi hiyo ya kuua bila kukusudia kuhamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, mahakama ilipanga kutajwa kesi hiyo kwa mara ya kwanza Aprili 24, mwaka huu.
Tukio hilo la mauaji linadaiwa kutokea baada ya gari la mwanasiasa huyo kugongwa na daladala, na kisha dereva akakataa kushuka kushuhudia uharibifu alioufanya.
Kutokana na kitendo hicho, Ditopile-Mzuzuri, anadaiwa alichomoa bastola, akawa anagonga gonga dirisha ili dereva ashuke chini, ghafla, risasi ilifyatuka na kumuua papo hapo.
Kutokana na kukabiliwa na kesi hiyo, siku moja kabla ya kufikishwa mahakamani, Novemba 5 mwaka 2006, Dipotile alimwandikia barua Rais Jakaya Kikwete akiomba kujiuzulu wadhifa wa mkuu wa mkoa. Rais Kikwete alikubali ombi hilo Novemba 7.
Katika barua hiyo Rais Kikwete alisema: “Kuomba kwako kujiuzulu wadhifa wako wa mkuu wa mkoa ni uamuzi wa busara na hekima. Unatoa fursa kwa taratibu stahiki za kisheria kufanyika bila ya vizuizi visivyokuwa vya lazima. Ni heshima kwa taifa letu linalozingatia utawala wa sheria.
“Hivyo napenda kukuarifu kuwa nimekubali ombi lako la kujiuzulu wadhifa wa mkuu wa mkoa. Kwa mara nyingine tena pole kwa yote. Usiache kumshukuru na kumuomba Mungu.”
Katika barua yake ya kuomba kujiuzulu, Ditopile alisema tukio hilo lilikuwa linapingana na dhamira na wajibu wa kazi yake ya ukuu wa mkoa.
Baada ya Ditopile kujiuzulu ukuu wa mkoa, mwanasiasa mkongwe, Abeid Mwinyimusa, aliteuliwa kushika wadhifa huo.
Uteuzi huo wa Mwinyimusa ulianza Novemba 28, mwaka 2006, na aliapishwa Desemba 4, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment