Thursday, April 17, 2008

Chenge Ayaita Mabilioni Visenti!

WAZIRI wa Miundombinu, Andrew Chenge, amezungumzia kwa mara ya kwanza, tuhuma nzito za kumiliki kiwango kikubwa cha fedha kinachokadiriwa kuzidi dola za Marekani milioni moja katika akaunti moja nje ya nchi.
Chenge alilazimika kuzungumzia suala hilo jana muda mfupi tu baada ya kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Qatar, akitokea China alikokuwa ameongozana na Rais Jakaya Kikwete katika ziara ya kiserikali.
“Tusubiri uchunguzi ukamilike... kama ukithibitisha, hata hivyo vijisenti itajulikana vilipatikanaje,” alisema Chenge na kusababisha mshangao kwa wanahabari waliokuwa wakizungumza naye nje ya chumba cha wageni mashuhuri uwanjani hapo (VIP).
Alipoulizwa iwapo kwake yeye kiasi hicho cha zaidi ya dola milioni moja ambazo ni zaidi ya shilingi bilioni moja za Kitanzania anazohusishwa nazo anaziita vijisenti, Chenge alijibu swali hilo kwa kusema: “Kila mtu ana viwango vyake.”
Akizungumza akiwa katika hali ya utulivu, tofauti kabisa na ilivyo kawaida yake ya kujibu maswali kwa mkato, Chenge alikiri kwamba tuhuma hizo dhidi yake ambazo kwa mara ya kwanza ziliandikwa katika gazeti maarufu na linaloheshimika la nchini Uingereza la The Guardian mwishoni mwa wiki iliyopita ni nzito na zilizomshtua.
Pamoja na kujaribu kujibu takriban kila swali aliloulizwa, Chenge alikataa kuelezea chochote kwa undani kuhusu kuwa na fedha hizo au njia alizozipata au iwapo kulikuwa na uhusiano wowote kati ya tuhuma hizo na kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi mwaka 2002, akisema kufanya hivyo kwa wakati huu kunaweza kuingilia uchunguzi unaofanywa na taasisi mbalimbali za dola ambazo hata hivyo hakuzitaja.
Hata hivyo alisema amekuwa kiongozi serikalini kwa muda mrefu, akishika nyadhifa tofauti, akiwa ameshika nafasi ya Uanasheria Mkuu wa Serikali kwa miaka 10, hivyo fedha alizokuwa akilipwa zilikuwa halali.
“Tuhuma za ufisadi dhidi yangu ni nzito mno… inabidi nipate muda wa kukaa na kutafakari kwanza, na ukweli wa mambo utajulikana baada ya vyombo vya dola vilivyopewa kazi ya kunichunguza kumaliza kazi yake na hapo nitakuwa na muda wa kujibu,” alisema Chenge.
Aliahidi kutoa ushirikiano wote unaotakiwa kwa taasisi zinazomchunguza kuhusiana na tuhuma hizo zinazomhusisha na umiliki wa mabilioni hayo ya fedha nje ya nchi katika Kisiwa cha Jersey.
Alisema iwapo atakutwa na hatia baada ya uchunguzi huo kukamilika, basi hatakuwa na njia nyingine zaidi ya kuwajibika.
Aidha, Chenge, mmoja wa wanasiasa ambao wamekuwa wakiandamwa tangu aliporejeshwa katika Baraza la Mawaziri katika mabadiliko ya Februari mwaka huu, alisema alikuwa akitarajia kuwasiliana na mwanasheria wake ili kuangalia uwezekano wa kuchukua hatua zinazofaa.
“Nimechafuliwa jina langu sana. Sasa inabidi nipate muda wa kukaa na mwanasheria wangu Joe Mbuna, ili kufanya tathmini ya mambo yaliyoandikwa na vyombo vya habari na kuchuja yale mazuri na mabaya ili niweze kuchukua hatua za kisheria kwa mambo ambayo yameniharibia sifa zangu,” alisema Chenge.
Pamoja na hilo alisema, hata yeye anasubiri kwa hamu majibu ya uchunguzi unaofanywa na Taasisi ya Kuchunguza Makosa Makubwa ya Jinai ya nchini Uingereza (SFO) ambayo itachambua ukweli wa mambo, na kueleza matokeo yatakayotokana na kazi hiyo.
Katika hatua moja, Chenge alizielezea tuhuma hizo kuwa ni zenye mwelekeo wa chuki dhidi yake, akiwataka wale wanaomchukia mtu kutotumia hisia zao kumsingizia.
“Nimeshangazwa sana mambo haya, lakini kila mtu ana haki yake ya kusema na kwa hili nasema mnyonge nyongeni lakini haki yake mpeni… huwezi kumuumbia mtu tuhuma hivi hivi tu.
“Suala hapa (katika uchunguzi wa SFO) naloliona kuwa kubwa na muhimu ni hili ununuzi wa rada kutoka BAE, sasa hili la kusema kwamba Chenge ana fedha nyingi sioni kama lina nafasi, kwa vile hata mimi mwenyewe ninayo nafasi yangu na rekodi nzuri katika utendaji kazi. Nimekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miaka 10, naelewa mambo yangu nilivyoyafanya.”
“Napenda kuwahakikishia ndugu zangu kwamba, hii ni sehemu ya maisha kwa mtu… lakini jamani nchi hii tunaipeleka wapi?” alihoji Chenge.
Alipoulizwa na waandishi wa habari kama yuko tayari kujiuzulu uwaziri, ili kurejesha imani ya serikali kwa wananchi, Chenge hakukubali wala kukataa, bali alisisitiza kwamba anasubiri uchunguzi dhidi yake ukamilike kwanza kabla ya kufikia hatima yake.
“Unapouliza ndugu yangu kwamba nijiuzulu wadhifa nilionao kwa sasa, nashindwa nikujibu nini? Mimi nasubiri mchakato mzima ukamilike… nawaomba muendelee kuwa wavumilivu,” alisema Chenge.
Alipoulizwa kuwa kurudi kwake nchini mapema kunatokana na tuhuma hizo, alikanusha suala hilo na kubainisha kuwa, ratiba aliyopangiwa ilihusu kuambatana na Rais Kikwete huko China na baadaye yeye arejee nyumbanji wakati rais akielekea Marekani.
Jumamosi ya wiki iliyopita, gazeti linaloheshimika nchini Uingereza, la The Guardian liliandika kuwa katika uchunguzi huo wa SFO iligundulika akaunti moja inayohusishwa na Chenge ikiwa na zaidi ya dola za Marekani milioni moja, zilizoko katika akaunti moja, katika Kisiwa cha Jersey.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, SFO inamchukulia Chenge kuwa mtu anayeweza akawa shahidi muhimu katika uchunguzi mzima wa zabuni ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE ya nchini Uingereza.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, SFO inatarajia kuanza upya kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo ili kuangalia iwapo zina uhusiano wowote na zile zinazoaminika kutolewa kwa njia ya rushwa wakati Tanzania iliponunua rada ya kijeshi kutoka nchini humo kwa paundi milioni 28, ambazo ni sawa na shilingi bilioni 70, mwaka 2002.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, inaaminika kwamba, uchunguzi huo wa SFO unatarajia kuanza katika kipindi cha wiki sita zijazo.
Kwa mujibu wa habari hizo, uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba, moja ya mambo yanayofuatiliwa ni kujua iwapo fedha hizo zinazoaminika kuwa za Waziri Chenge zilizowekwa katika akaunti moja iliyoko katika Kisiwa cha Jersey zina uhusiano wowote na zile zilizotoka katika Kampuni ya BAE System inayotuhumiwa kuinyonya Tanzania kwa kuiuzia rada hiyo kwa bei kubwa kuliko ilivyotakiwa.
The Guardian katika habari yake hiyo iliyowekwa katika mtandao wa intaneti, linaripoti kuwa, taarifa hizo zinakuja ikiwa ni miaka mitatu sasa tangu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) kwa kushirikiana na SFO na taasisi za uchunguzi za Uswisi na Jersey zilipoanza kuchunguza kuhusu kashfa nzima ya ununuzi wa rada.
Gazeti hilo lilimkariri Waziri Chenge akikiri kwamba fedha hizo ni zake na akatumia fursa hiyo kukanusha kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha hizo na kashfa nzima ya ununuzi wa rada, uliofanywa wakati yeye akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Jambo la wazi linalotaka kuonekana hapa ni kwamba mimi nilipokea kwa lengo la kujinufaisha mwenyewe fedha za rushwa kutoka BAE. Huu ni uongo,” alisema Chenge.
Aidha, gazeti hilo lilimkariri Chenge akisema kuwa, wakati rada hiyo ilipokuwa ikinunuliwa yeye alihusika kwa kiwango kidogo sana katika mchakato mzima, kwani jambo hilo lilishughulikiwa na wizara nyingine na uamuzi ukaidhinishwa na Baraza la Mawaziri.
Mbali ya hilo, gazeti hilo lilimkariri mwanasheria wa Chenge anayeishi Cleveland, Ohio, nchini Marekani, J Lewis Madorsky, akikanusha kwa niaba ya mteja wake huyo, kuwapo kwa uhusiano wowote kati ya fedha zake na tuhuma zozote.
“Wakati tukitambua kuwa masuala hayo yalitokea muda mrefu uliopita, tunaweza tu tukathibitisha kuwa, tuhuma zozote za ukiukwaji wa sheria, ukiukwaji wa maadili, kutenda isivyo sawa na mambo mengine ya hivyo dhidi ya mteja wetu, ni mambo ambayo kimsingi tunayakanusha kwa nguvu kubwa,” alisema mwanasheria huyo wa Chenge.
Hata hivyo, gazeti hilo liliandika uchunguzi huo dhidi ya Chenge unamfanya yeye kuwa tu shahidi muhimu, kwani wanaielenga zaidi BAE ambayo inadaiwa ilimlipa wakala mmoja wa Tanzania mamilioni ya fedha ili kujenga ushawishi wa rada iliyokuwa ikiiuza kununuliwa.
Wakala huyo ambaye amekuwa akitajwa kwa muda mrefu na ambaye sasa anaaminika kukimbia nchini na kutafutwa na polisi wa kimataifa ni, Shailesh Vithlani.

No comments: