Sunday, April 6, 2008

CUF yatoa masharti kwa JK

Chama cha Wananchi (CUF) kimeto masharti kwa Rais Jakaya Kikwete ili kuyanusuru mazungumzo ya kusaka mwafaka huko Zanzibar.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, amemtaka Rais Kikwete kufanya kila analoweza kuhakikisha kuwa chama chake (CCM) kinasaini makubaliano yaliyofikiwa na kamati ya mazungumzo, kabla CCM haijatumbukiza suala la kura ya maoni.
Iwapo Kikwete atashindwa kulitekeleza hilo, Profesa Lipumba amemtaka atekeleze sharti la pili ambalo ni kuwakutanisha Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad, na Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, kujadili suala hilo.
Lipumba alisema kuwa Kikwete hawezi kushindwa kufanya hilo hasa ikizingatiwa kuwa hivi karibuni tu alifanikiwa kuwakutanisha mahasimu wakubwa huko Kenya, Rais Mwai Kibaki na Raila Odinga katika mgogoro wao wa matokeo ya uchaguzi.
CUF imetoa msimamo huo baada ya rais Kikwete kukiomba chama hicho kurejea katika meza ya mazungumzo, kupitia hotuba yake kwa taifa aliyoitoa wiki iliyopita.
Aidha, katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, amekiandikia chama hicho, kukifahamisha kilichojiri katika kikao cha CC na NEC ya CCM huko Butiama na kukitaka warudi waendelee na mazungumzo hayo.
Lakini CUF ilishatangaza kuwa hakipo tayari kushirikiana na CCM kufanya kile ilichokiita ‘usanii wa kisiasa’ kikimaanisha utekelezaji wa pendekezo ya upigwaji wa kura ya maoni kuhusiana na mfumo wa utawala huko Zanzibar.
Kwa upande mwingine CUF imetangaza maandamanao ya nchi nzima ili kuonyesha msimamo wake katika suala hilo.
Kwa mujibu wa Lipumba, maandamano hayo yatawahusisha pia viongozi wengine wa vyama vya upinzania na yamepangwa kuanza Jumamosi ijayo huko Zanzibar kabla hayajahamia kwenye mikoa mingine.

No comments: