Thursday, April 3, 2008

HOTUBA YA JK MACHI 2008

HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE MKUTANO NA VIONGOZI NA WANACHAMA WA CCM NA JUMUIYA ZAKE, DIAMOND JUBELEE
02 APRILI, 2008

Ndugu Wana-CCM Wenzangu;
Viongozi na Wanachama Jumuiya za CCM;
Ndugu Wananchi;

Kama mjuavyo tumejiwekea utaratibu wa Rais kuzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi. Lakini, kwa mwisho wa mwezi wa Machi nilishindwa kufanya hivyo kwa sababu ya kulazimika kwenda Mererani, Mkoani Manyara ambako kumetokea maafa makubwa kwa wachimbaji wa madini. Maafa hayo yalisababishwa na mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zilizonyesha katika eneo hilo usiku wa tarehe 28 kuamkia tarehe 29. Nilikwenda kuwafariji wenye migodi, wachimbaji na familia zao kwa maafa yaliyowakuta. Pia nilikwenda kuona shughuli za uokoaji na uopoaji wa miili ya wale waliofariki.
Kwenye hotuba yangu ya mwezi Machi, nilikuwa nimepanga kuongea na Watanzania kuhusu mambo mawili. Mambo hayo ni Ushiriki wa Majeshi ya Tanzania kama sehemu ya Jeshi la Umoja wa Afrika nchini Comoro na tatizo la mauaji ya ndugu zetu Maalbino kwa imani za kishirikina. Awali nilikuwa na wazo kuwa maadam tarehe 31 Machi imeshapita basi niache na hotuba ipite. Lakini, baada ya kusikia kueleweka vibaya kwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM kuhusu Mazungumzo ya Muafaka baina ya CCM na CUF nikaona ipo haja ya kuzungumza. Niitumie fursa hii kuzungumzia yale mambo mawili niliyoyakusudia, na pia nizungumzie maafa ya Mererani na uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuhusu mazungumzo ya Muafaka baina ya CCM na CUF.


Tanzania Kupeleka Majeshi Comoro
Ndugu Wananchi;
Tanzania imepeleka wanajeshi wake 924 kuungana na wanajeshi wa Sudan, Senegal na Libya katika Jeshi la Umoja wa Afrika lililoundwa kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho la Visiwa vya Comoro kurejesha mamlaka yake katika Kisiwa cha Nzuani. Jamhuri ya Shirikisho la Visiwa vya Comoro inaundwa na visiwa vitatu, yaani Ngazija (Grand Comoro), Nzuani (Anjouan) na Mwali (Moeli). Kwa mujibu wa mfumo wao wa utawala, kila kisiwa kina Serikali yake ya ndani inayoongozwa na Rais, na kuna Rais wa Shirikisho anayekaa na kufanyia kazi mjini Moroni, kwenye Makao Makuu ya Taifa la Comoro.
Urais wa Shirikisho unashikiliwa kwa mzunguko baina ya raia wa visiwa hivyo vitatu. Rais wa sasa ni Mheshimiwa Abdallah Sambi ambaye anatokea Kisiwa cha Nzuani. Uchaguzi ujao wa Urais unaenda kwa mtu wa kisiwa kingine.. Kipindi cha Urais wa Shirikisho na wa Visiwa vinavyounda Shirikisho ni miaka mitano.
Mwezi Aprili, 2002 uchaguzi wa Marais wa Visiwa vya Ngazija, Mwali na Anzuan ulifanyika. Kipindi cha miaka mitano cha Marais hao kiliisha rasmi tarehe 13 Aprili, 2007. Kwa mujibu wa utaratibu na Katiba ya Comoro uchaguzi wa Rais hufanyika ndani ya siku 90 baada ya kipindi cha uongozi cha Rais kumalizika. Katika kipindi hicho cha siku 90, Spika wa Bunge huwa Kiongozi wa muda. Kwa mujibu huo wa Katiba, tarehe 14 Aprili, 2007, Marais wa visiwa vya Ngazija na Mwali waliachia madaraka kwa Maspika wa Mabunge ya Visiwa vyao, lakini Bw. Mohamed Bakari, Rais wa Kisiwa cha Nzuan akakataa na kudai kuwa ataendelea kuwepo mpaka baada ya uchaguzi. Akamfukuza Spika ili kutengeneza mazingira ya kutokuwepo mtu anayestahili kuchukua nafasi yake. Rais wa Shirikisho alitumia mamlaka yake ya Kikatiba kuteua mtu mwingine badala ya Spika aliyeondolewa kibabe na Bwana Mohamed Bakari. Lakini naye huyo pia Bwana Bakari akamkataa.
Rais Abdallah Sambi aliamua kwenda Nzuani kumuona na kuzungumza na Bw. Mohamed Bakari na viongozi wengine ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo usiokuwa wa lazima. Bwana Mohamed Bakari akafunga kiwanja cha ndege cha Ouani, Nzuani na kuweka magogo uwanjani hapo hivyo ndege ya Rais wa Shirikisho ikashindwa kutua.
Aidha, Bwana Mohamed Bakari akaamuru kuteremshwa bendera za Shirikisho na kukamatwa kwa askari 30 wa Jeshi la Shirikisho. Mmoja wakamuua, watatu wakawajeruhi, na 26 wakawanyang’anya silaha na kuwafukuza kisiwani humo.
Baada ya hapo, Umoja wa Afrika ukaingilia kati na kufanya mazungumzo na Bwana Mohamed Bakari kumtaka aheshimu Katiba aondoke madarakani na kuruhusu taratibu stahiki zifanyike. Imefanyika mikutano tisa (9) ya namna hiyo; miwili Pretoria, mwili Cape Town, mitatu Addis Ababa na miwili Nzuani. Mikutano yote hiyo haikufanikiwa.
Ndugu Wananchi;
Bwana Mohamed Bakari alikaidi mara zote kuondoka na kufanya mambo kuwa magumu zaidi. Alikaidi uamuzi wa Rais wa Shirikisho ulioungwa mkono na Umoja wa Afrika na kutaka uchaguzi Nzuani usifanyike tarehe 10 Juni, 2007. Sababu ya agizo hilo ni kutaka uchaguzi huo ufanyike siku ambayo Serikali ya Shirikisho na Umoja wa Afrika utakuwepo kusimamia. Bwana Mohamed Bakari akakaidi na kuendelea kufanya uchaguzi huo chini ya usimamizi wake yeye mwenyewe. Kwa kutumia madaftari ya shule, akaendesha uchaguzi na kutangaza kuwa amepata ushindi wa asilimia 85. Mahakama ya Katiba ya Comoro ikakataa kuutambua uchaguzi huo, lakini yeye akaendelea kula kiapo na kuendelea kuwa Rais wa Nzuani kwa kipindi cha pili cha miaka mitano.
Umoja wa Afrika ukaendelea na juhudi za kumtaka aachie madaraka kuruhusu taratibu za Kikatiba zifuatwe na uchaguzi halali ufanyike. Kama nilivyosema hapo awali, mikutano tisa iliyofanywa (wa mwisho ulikuwa mwezi Februari, 2008) haikuzaa matunda.
Kwa sababu ya ukaidi wa dhahiri wa Bw. Mohamed Bakari, ndipo katika kikao kilichopita, Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika walikubali ombi la Rais Abdallah Sambi la kuunda Jeshi la Umoja wa Afrika kusaidia Jeshi la Comoro kurejesha mamlaka ya Serikali ya Shirikisho katika kisiwa cha Nzuani. Iliamuliwa kuwa, Baraza la Amani na Usalama la AU lishirikiane na Kamisheni ya Afrika kutafuta nchi zitakazotoa majeshi ya kufanya kazi hiyo. Kwa kushirikiana na Serikali ya Comoro ndipo zikaombwa nchi nne yaani Libya, Senegal, Sudan na Tanzania kuchangia wanajeshi kwenye Jeshi la UA.
Baada ya kupokea uamuzi huo wa Baraza la Amani na Usalama la UA, tulijadiliana na kufanya mashauriano na wahusika mbalimbali na hatimaye tukakubaliana kuwa tuyakubali maombi hayo. Tumefanya hivyo kwa kutambua wajibu wetu kwa UA na wajibu wetu kwa nchi jirani ya Comoro ambayo wetu wake na wetu wana mahusiano makubwa hata ya kinasaba. Lakini pia kwetu sisi kama Mwenyekiti wa AU tunao wajibu wa kuhakikisha maamuzi muhimu kama haya ya kuhakikisha kuwa nchi ya Comoro haimeguliwi tena kama ilivyofanywa huko nyuma.
Ndugu Wananchi;
Kama mnavyofahamu, operesheni maalum ya kumng’oa Bwana Mohamed Bakari na utawala wake ilianza rasmi alfajiri ya tarehe 24 Machi, 2008 na siku iliyofuata, yaani tarehe 25 Machi, 2008, majeshi ya Umoja wa Afrika yakiongozwa na Tanzania yaliweza kukamilisha zoezi hilo bila umwagaji wa damu au uharibifu wa mali. Hakuna mtu aliyeuawa wakati wa operesheni hiyo. Bwana Mohamed Bakari ametoroka na kiongozi wa muda Nzuani amepatikana kwa mujibu wa Katiba ya Comoro. Ameanza kazi ya kuliongoza taifa kwenye uchaguzi utakaofanyika mwezi Mei, 2008.
Majeshi yetu yataondoka kwa awamu mbili: Awamu ya kwanza yataondoka mwisho wa mwezi huu na ya pili mara baada ya uchaguzi. Umoja wa Afrika una dhamana ya kugharamia operesheni hii. Kiasi cha fedha kimetolewa na UA unaendelea kutoa. Pale ambapo tutalazimika kutumia fedha zetu tumeelewana kuwa UA utatufidia.
Kwanini Tanzania Imeshiriki
Ndugu Wananchi;
Operesheni hii imefanikiwa. Ni heshima kwa UA na ni heshima kwa nchi yetu kuwa sehemu ya mafanikio haya. Kwa niaba yenu napenda kuitumia nafasi hii kuwapongeza Wanajeshi wetu kwa kazi nzuri waliyoifanya. Imeliletea jeshi letu heshima kubwa na sifa kwa nchi yetu. Kabla ya operesheni ile kwanza kulikuwa na hofu kubwa hasa ya kutokea vifo na uharibifu wa mali. Mkuu wa Majeshi yetu Jenerali Davis Mwamunyange alinihakikishia kuwa wameiandaa kisayansi kuepuka hayo yote. Na kweli ndivyo ilivyotokea. Nawashukuru na kumpongeza Mkuu wa Majeshi na Maofisa Wakuu Wanadhimu Makao Makuu ya Jeshi katika operesheni hii huko Comoro kwa kazi nzuri iliyotukuka. Nawapa pole kwa magumu yote waliyokabiliana nayo. Nawapa pole kwa msiba uliowapata wa kumpoteza mwenzao mmoja aliyezama majini pale Kisiwani Mwali siku moja kabla ya majeshi yetu kuondoka kuelekea Nzuani. Ajali haina kinga.. Kila mtu ana siku yake na namna yake ya kuondoka. Tuzidi kumuombea marehemu wetu huyo kwa Mwenyezi Mungu aipokee roho yake na kuiweka mahala pema peponi, Amin.

Tatizo la Mauaji Yanayotokana na Imani za Kishirikina
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kuliongelea ni kuhusu mauaji ya ndugu zetu wa jamii ya albino yanayofanyika hapa nchini. Niseme mapema tu kwamba jambo hili ni la aibu kubwa kwa jamii yetu. Ni jambo la hatari kwa amani na usalama wa watu wetu.
Ndugu Wananchi,
Mauaji yanayotokana na imani za kishirikina ni tatizo la muda mrefu kabla na wakati wa ukoloni na imeendelea hata baada ya nchi yetu kupata uhuru.
Uzoefu unaonyesha kwamba baadhi ya wahanga wanaoathirika ni akina mama vikongwe ambao hutuhumiwa kuwa ni wachawi, kwamba wanawaroga watu wengine na kuwaua. Mauaji ya namna hii yamejikita sana katika mikoa ya Kanda ya Ziwa mikoa ya Mara, Shinyanga, Mwanza na hata mkoa wa Tabora. Mauaji haya hufanywa na magenge ya watu wanaokodishwa na watu ambao wamepata maelezo potofu kutoka kwa waganga wa jadi baada ya kuuguliwa au kufiwa na jamaa zao, na wao kuamua kulipiza kisasi kwa watu waliotajwa kuwa ndio waliowaroga jamaa zao.
Vilevile, mauaji mengi ya kishirikina hufanyika kutokana na imani potofu walizonazo baadhi ya watu kwamba kwa kutumia viungo vya watu wengine wanaweza kufanikiwa katika biashara wazifanyazo au katika shughuli zao za uchimbaji wa madini na uvuvi.
Kutokana na imani hizo potofu, watu hao wanaowania utajiri wa haraka haraka huenda kwa waganga wa jadi na kupata maelekezo ya viungo vinavyotakiwa kutoka kwenye mwili wa binadamu. Katika mazingira haya, tumeshuhudia baadhi ya watu wakiuawa na kukutwa wamenyofolewa baadhi ya sehemu za miili yao kama vile sehemu za siri, ndimi, viganja, matiti na wengine kuchunwa ngozi.
Katika nyakati zingine, huvumishwa habari za watu wenye maumbile au mapungufu fulani kwenye mwili kama vile watu wenye vipara au maalbino kwamba viungo vyao vina mchango mkubwa katika kufanikisha utajiri wa haraka. Kwa sababu hiyo katika kipindi cha mwezi Julai, 2007 hadi sasa tumeshuhudia ndugu zetu wa jamii ya maalbino wakivamiwa na kuuawa na wengine kutoweka katika mazingira ya kutatanisha na hadi sasa bado hawajapatikana. Kuanzia mwezi Machi 2007 hadi 01 Aprili, 2008, jumla ya maalbino 19 wameuawa na wengine wawili wametoweka na hadi sasa hawajapatikana, lakini inasadikika kwamba nao wameuawa.
Tatizo hili la mauaji yanayotokana na imani za ushirikina limekuzwa zaidi na baadhi ya watu ambao hawana taaluma ya uganga (waganga pandikizi) kwa kujiingiza kwenye shughuli za uganga wa jadi hivyo kuzidisha upotoshwaji wa watu kwa kupiga ramli chonganishi au maelekezo yasiyosahihi kwa lengo la kujipatia kipato kwa njia ya udanganyifu.
Ndugu Watanzania wenzangu,
Kama nilivyosema, mauaji haya ni ya kusikitisha na ni ukatili usio na mfano. Ni aibu kubwa kwa jamii yetu. Nawasihi wale wanaojihusisha na vitendo hivi, waachane na dhana ya kwamba utajiri unaweza kuja kwa njia ya miujiza bila ya kufanya kazi kwa bidii.. Utajiri unakuja kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Pia unakuja kwa kuwa na nidhamu ya kazi na matumizi ya fedha uzipatazo.
Tiba ya asili na uganga wa jadi ni sehemu ya asili ya Mtanzania, na hiyo Serikali inaitambua na wala haiikatazi. Hata hivyo, nawasihi Watanzania wenzangu tujiepushe na matapeli na wahuni walioingilia fani hii na wao wakiwa na nia ya kuwalaghai wananchi kwamba wanaweza kuwafanya wapate utajiri wa haraka haraka kwa kutumia baadhi ya viungo vya wanadamu.
Hatua za Serikali Kukabiliana na Tatizo Hili
Ndugu Wananchi,
Serikali kwa upande wake itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kudhibiti mauaji haya kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo wale waganga wa jadi waliosajiliwa Serikali.
Kwa kushirikiana na Chama vya Maalbino nchini, Serikali inaendelea na zoezi la kupata orodha ya maalbino wote nchini na kutambua sehemu wanazoishi ili kwa kushirikiana na Serikali za Mitaa, Manispaa, Kata na Vijiji kubuni kwa pamoja namna ya kutengeneza mazingira ya ulinzi yanayoweza kuwahakikishia usalama wao. Zoezi hili ni muhimu liambatane na matumizi ya Ulinzi-Shirikishi ili kuwashirikisha wananchi katika kuyatambua makundi ya waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi na makundi yanayoendesha mauaji hayo na wale wanayoyakodisha.
Vilevile, Serikali itaendelea kutoa elimu ya uhamasishaji kwa wananchi wetu ili wasaidie kutoa taarifa kwa vyombo vya dola dhidi ya wahalifu wote wanaofahamika kushiriki katika mauaji yanayotokana na imani za kishirikina.
Ningependa Jeshi la Polisi nalo liharakishe zoezi la kuwaorodhesha waganga wote wa Tiba Asili walioko nchini ili kudhibiti wale wanaotoa maelekezo ya kuua watu. Nina imani waganga wa jadi wa kweli watatoa ushirikiano, kwani wanawajua wenzao wanaotoa maelekezo kinyume na sheria za nchi.
Vilevile, Jeshi la Polisi lijipange upya kuyatambua na kuyakamata magenge ya watu wanaokodishwa kufanya mauaji kwa wanawake vikongwe, au kwa watu wengine ili kunyofoa sehemu zao za mwili au kuchuna ngozi kama inavyotokea kwa maiti zinazopatikana zimeuawa wakiwemo maalbino.
Ndugu Wananchi,
Kila mtu ana imani yake. Na Serikali haiwezi kuingilia imani za watu kwa mambo ya asili na jadi. Hata hivyo, pale imani yako inapoingilia uhuru na haki ya msingi ya mtu mwingine, ikiwemo haki yake ya kuishi, Serikali haiwezi kukaa kimya. Lazima ichukue hatua.
Nina imani kabisa kwamba tukishirikiana kwa pamoja, wananchi, Serikali, asasi za kiraia, vyombo vya habari, waganga wa jadi na wadau mbalimbali, tunaweza kulimaliza kabisa tatizo hili ili lisije likaonekana kama ni sehemu ya maisha na utamaduni wa Mtanzania.

Muafaka Kati ya CUF na CCM
Sasa napenda kulizungumzia suala la tatu nalo ni Mazungumzo ya Muafaka kati ya CCM na CUF. Suala ambalo limetawala vichwa vya habari vya vyombo vya habari nchini na duniani tangu Butiama mpaka sasa. Na sasa, naona inaanza kujitokeza dhana potofu hasa kuhusu nini kilichoamuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
Ndugu Wananchi;
Moja ya ajenda katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichokutana Butiama hivi majuzi ilikuwa ni kujadili taarifa ya Kamati ya Mazungumzo baina ya CCM na CUF ya kutafuta ufumbuzi wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Kwa kweli haikuwa nia yangu kulizungumzia suala hilo katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi. Lakini kutokana na yanayoendelea sasa, nisipolisema sitaeleweka. Nitaongeza maswali mengi yasiyokuwa na majibu na kuishia kuwafanya wanachama wa CCM, wananchi na hata wenzangu wa CUF wachanganyikiwe zaidi.

Ndugu Wananchi,
Nianze kwa kutamka moja kwa moja kwamba, tofauti na yanayosemwa na baadhi ya watu, sisi katika CCM tunaamini kwamba maamuzi yaliyofanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa ni ya kujenga na wala siyo ya kubomoa. Kimsingi ni maamuzi yanayotusogeza hatua kubwa sana mbele kwenye kufikia muafaka.
Labda nirudi nyuma kidogo. Chimbuko la mazungumzo yanayoendelea sasa ni ahadi yangu, wakati nikizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 30 Desemba 2005, kwamba nitaanzisha na kuwezesha mjadala wa kisiasa kwa lengo la kumaliza mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Dhamira yangu ilitokana na kusoneshwa na uhasama, chuki, kejeli, dharau na hata fujo na vurugu, hasa nyakati za uchaguzi, na hata baada ya uchaguzi, baina ya wakazi wa Zanzibar. Kwangu mimi, hali hii, ambayo imefanya hali ya kisiasa na kiusalama kutokuwa ya utulivu, haiendani na taswira ya Tanzania tunayotaka kuijenga na Tanzania tunayoijua sisi na wanaoijua marafiki zetu wote duniani.
Kutokana na uhasama wa kisiasa, ilifika mahali ambapo watu walikuwa hawaoleani, Bibi na Bwana wanapeana talaka, wazazi na watoto wanatengana na hata ndugu kufarakana. Watu wamekuwa wanasusiana misiba, hawasalimiani, wanaachiana safu misikitini, na hawabebani kwenye vyombo vya usafiri na hawauziani bidhaa hadi wawe wa Chama kimoja. Hiyo sio Tanzania ninayoijua mimi, na wala siyo tunayoijua sote. Hiyo sio Tanzania ambayo waasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Aman Karume waliyokuwa nayo mioyoni mwao walipojitolea muhanga kuongoza harakati za ukombozi wa nchi zetu mbili zilizokuja kuungana na kuwa nchi moja.


Ndugu zangu,
Siku zote nimekuwa natambua kwamba dhamira yangu pekee haitoshi kwenye kuifikia Tanzania tunayoitaka. Kimsingi, kutekelezwa kwa ahadi niliyoitoa Bungeni kulitegemea ridhaa ya Chama changu na Chama cha Wananchi, CUF. Aidha, kulitegemea utayari na ushirikiano wa viongozi wa siasa wa Zanzibar na wananchi wanaowaongoza. Na, nilisema hivyo kwenye hotuba yangu Bungeni.
Bahati nzuri, nilipolipeleka suala hili kwenye vikao vyote vikubwa husika vya Chama chetu (CCM), viongozi wenzangu wa Chama, kutoka Bara na Visiwani, waliunga mkono hoja na haja ya kufanya mazungumzo na Chama cha CUF. Vilevile, sote tulifarijika kwamba wenzetu wa CUF nao walikuwa tayari kufanya mazungumzo nasi. Haya hayakuwa mazungumzo ya kwanza baina ya vyama vyetu lakini safari hii tulikuwa na dhamira ya kutafuta suluhu ya kudumu.
Katika miezi yote kumi na minne, tumeendesha mazungumzo haya katika mazingira ya udugu na kuheshimiana, wote tukiwa na dhamira ya kupata suluhu mapema kadri inavyowezekana. Palipotokea vizingiti vya hapa na pale, wote tulishirikiana kuvimaliza na kuendelea na mazungumzo.
Ndugu Wananchi,
Kama mnavyojua, tuliamua kufanya mazungumzo haya kwa mfumo wa Kamati ya pamoja, kila Chama kikiwa na Wajumbe walioongozwa na Katibu Mkuu wa Chama husika. Kila Chama kilitengeneza hadidu za rejea kwa Wajumbe wake. Lakini, Kamati ya Pamoja ilitengeneza agenda ya pamoja ya mazungumzo yao. Bahati nzuri vikao vya uamuzi vya vyama vyetu kila kimoja kwa wakati wake viliridhia agenda hiyo.
Agenda ya Mazungumzo ilikuwa na mambo matano:
(i) Uchaguzi Mkuu wa 2005 na athari zake.
(ii) Usawa na haki kuendesha siasa.
(iii) Masuala ya Utawala wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
(iv) Njia za kuimarisha maelewano katika uendeshaji wa Uchaguzi Huru na Haki.
(v) Utaratibu wa Utekelezaji na Programu ya Utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo hayo.

Ndugu Wana-CCM;
Kwa miezi kumi na minne, yaani tangu Februari, 2007 mazungumzo yamefanyika baina ya Wajumbe wa vyama vyetu viwili kwenye Kamati hiyo. Pamoja na tofauti au migongano ya hapa na pale, mazungumzo yalifanyika katika mazingira ya uwazi, ukweli na moyo wa udugu. Mara kwa mara Wajumbe wa Vyama vyetu walitoa taarifa kwa uongozi wa juu wa vyama na vikao vyake. Kwa upande wa CCM, Wajumbe wetu walitoa taarifa kwangu na kwa Kamati Kuu, na kila Halmashauri Kuu ya Taifa ilipokutana, taarifa ya maendeleo ya mazungumzo ilitolewa. Maoni yalitolewa na Wajumbe walielekezwa ipasavyo kuhusu yale yaliyofikiwa na yale ambayo walitakiwa kurudi kwa wenzao na kuzungumza nao. Nao walifanya hivyo na kutoa taarifa ipasavyo. Zipo nyakati Wajumbe wetu walilazimika kurudi kwetu kutoa taarifa kuhusu baadhi ya maelekezo tuliyowapa kutoafikiwa na upande wa wenzetu. Pale ilipoonekana kuwa wenzetu wanayo hoja bora zaidi ilikubaliwa.
Ndugu Wananchi;
Nalisema hili kutaka kuwathibitishia kuwa kilichofanywa Butiama na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM si jambo la ajabu, ndiyo utaratibu wetu. Katika vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM vilivyofanyika Musoma, hususan Butiama, wajumbe wetu wa Kamati waliwasilisha taarifa ya mwisho ya mazungumzo yao wa wenzao wa CUF. Hivyo walileta taarifa ya mazungumzo na makubaliano kuhusu agenda zote tano. Wajumbe walijadili agenda moja baada ya nyingine. Kwa jumla Wajumbe wamepokea kwa furaha taarifa hiyo, wameridhika na kazi nzuri iliyofanywa na kuwapongeza wajumbe wake na wenzi wao wa CUF kwa kazi nzuri waliyoifanya. Kazi ambayo waliitambua kuwa ni hatua kubwa katika safari yetu ya pamoja kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa uliopo Zanzibar.
Mjadala ulikuwa wa kina, tena mrefu. Ilituchukua saa 6 kwenye Kamati Kuu na karibu saa 8 kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa. Agenda hii siyo tu ilichukua muda mwingi wa mkutano wetu wa Butiama bali ilipunguza hamu ya wajumbe kujadili kwa urefu agenda nyingine. Hii ilikuwa ndiyo ilikuwa ndiyo mama wa agenda zote.
Kuna nyakati mjadala ulikuwa mkali na kuwatisha baadhi, wakidhani kuwa huenda tusifikie makubaliano. Lakini kama ilivyo kawaida ya Chama chetu, mwishowe tulikubaliana na mapendekezo ya Kamati. Kwangu mimi ukali wa baadhi ya wajumbe unaimarisha imani yangu kuhusu umuhimu wa kuhakikisha kuwa juhudi za kupata muafaka zinafanikiwa. Kushindwa hakuna maslahi kwa Zanzibar na kwa nchi yetu kwa jumla.
Pamoja na kukubaliana na mapendekezo ya Kamati, Halmashauri Kuu iliona haja ya kufanya marekebisho fulani fulani katika baadhi ya mapendekezo hasa kuhusu mapendekezo ya muundo wa Serikali Shirikishi. Shabaha ya mapendekezo hayo ni kuboresha na kuimarisha mfumo huo unaopendekezwa. Marekebisho yanapendekezwa kwenye utaratibu wa uteuzi wa Wasaidizi Wakuu wawili wa Rais na Baraza la Mawaziri. Marekebisho mengine yanahusu pendekezo la kuwepo Baraza la Usuluhishi. Mimi naamini marekebisho yote ambayo Halmashauri Kuu imetaka yafanywe kwa nia ya kuboresha mapendekezo ya Kamati yetu yasingekuwa mambo magumu. Naamini wenzetu na wao wangegundua hekima ya Halmashauri Kuu kupendekeza inavyopendekeza. Bahati mbaya wenzetu wanakataa jambo kabla ya kuliona. Hata kabla Katibu Mkuu wa CCM hajawaandikia kuwasilisha kile kinachopendekezwa, wenzetu wamekaa na kukataa, sijui wamekataa nini. Wamekataa Halmashauri Kuu kutoa maoni ya kuboresha kitu ambacho inabidi sote tukubaliane ndipo kitekelezwe. Je, ni sawa hivyo?


Ndugu Wananchi;
Pamoja na marekebisho hayo yahusuyo mapendekezo ya Kamati kuhusu mfumo wa Serikali Shirikishi, katika mjadala, Wajumbe ndani ya Kamati Kuu na baadaye Halmashauri Kuu walikuja na mawazo mawili mapya. Nia ya mawazo hayo ni kuimarisha na kuboresha huo mfumo mpya unaopendekezwa uwepo. Jambo la kwanza linahusu kuwashirikisha wananchi katika kufanya uamuzi huu mkubwa. Halmashauri Kuu ya Taifa inaamini kuwa mabadiliko yanayopendekezwa ni makubwa sana na ya msingi. Yanahusu kuubadili kabisa mfumo wa sasa wa utawala na uendeshaji wa shughuli za Serikali Zanzibar. Halmashauri Kuu ya Taifa inaona kuwa ipo haja ya msingi ya kuwashirikisha wananchi wa Zanzibar kuamua.
Halmashauri Kuu inaona kuwa sahihi za Maalim Seif na Mzee Makamba au za viongozi tu pekee hazitoshi. Ridhaa ya wananchi ni muhimu na hili ni jambo la msingi na la kawaida katika mifumo yote ya kidemokrasia.. Kama suala ni muda, napenda kuwahakikishia kuwa hata CCM inapenda mambo hayo yaishe mapema iwezekanavyo.
Jambo la pili jipya lililojitokeza kwenye Halmashauri Kuu linahusu haja ya kujipa muda wa kuufanyia mapitio mfumo huu mpya unapendekezwa hapo utakapokubaliwa na kutumika. Tofauti na ilivyo sasa ambapo mshindi anaunda Serikali hata kama ameshinda kwa tofauti ndogo (hata iwe chini ya asilimia moja), mfumo mpya nao unaleta utaratibu ambapo hata kama mshindi kapata ushindi mkubwa lazima awashirikishe wenzake. Halmashauri Kuu inaafiki hoja ya mfumo wa sasa wa kutokidhi haja ya kuwepo utulivu wa kisasa na kiusalama hasa kwa historia yetu tangu 1995 na hivyo kuafiki dhana ya kushirikiana katika Serikali kama jawabu.
Pamoja na hayo, Halmashauri Kuu inasema mahali pote mfumo wa Serikali Shirikishi ulipotumika ilifanyika hivyo kwa muda maalum. Wakati wote lengo kuu likiwa kuivusha nchi katika mazingira magumu ya wakati huo. Baada ya hapo, watu hurejea kwenye mfumo wa kawaida wa mshindi kuunda Serikali akiwa na hiari ya kuwashirikisha wenzake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa Afrika ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na ndivyo ilivyo hata sasa hapo Kenya. Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM inataka hata kwenye huu mfumo wetu tuweke utaratibu wa kuutazama upya kila baada ya wakati. Kwa jinsi ilivyo sasa dhana hiyo haipo. Ni mfumo utakaokuwepo daima dumu.
Ndugu Wananchi;
Kwa kweli hayo ndiyo yanapendekezwa na CCM. Na ndiyo mambo ambayo Halmashauri Kuu imeagiza Wajumbe wake waende wakazungumze na wenzi wao wa CUF. Tukubaliane ili tuendelee na hatua zinazofuatia. Kwa kweli sikutegemea yale mliyoyasikia ya kusemwa na viongozi wa CUF kuhusu maamuzi hayo. Upande mmoja siwalaumu kwa sababu walitoa matamko kabla ya kupata undani wa kila kilichoamuliwa na CCM. Lakini, upande mwingine nawalaumu kwa kutokusubiri taarifa rasmi kutoka kwa CCM juu ya mapendekezo yetu. Mimi bado naamini kuwa wangeyapata na kuyatafakari huenda wasingesema hayo wanayoyasema au kama wangesema wangefanya hivyo kwa namna na lugha tofauti.
Kwetu sisi katika CCM, tulichotegemea kutoka kwa wenzetu wa CUF, siyo tamko la kujitoa kwenye mazungumzo na kutishia kuvurugika kwa amani. Tulichotegemea ni kwamba hata kama wangekuwa na wazo la kujitoa kwenye mazungumzo, angalau wangetusikiliza ili kujua ni marekebisho gani ambayo wana-CCM wanaona yangeimarisha na kuyapa uhalali zaidi makubaliano ambayo Kamati zetu zilikuwa zinaelekea kuyapata.
Napenda kuwahakikishia wana-CCM wenzangu, wenzetu wa CUF na wananchi kwa jumla kuwa CCM haifanyi, wala haitafanya usanii wa kisiasa kwa jambo kubwa kama hili. CCM ina nia ya dhati ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa migogoro inayojirudia ya kisiasa na kiusalama Zanzibar. CCM inaamini kuwa mahali pa kuanzia ni kwenye mazungumzo baina yake na CUF. Ni kutokana na imani hiyo ndiyo maana tarehe 20 – 21 Desemba, 2006, Halmashauri Kuu iliamua kuanzisha mazungumzo na CUF.
Baada ya miezi 14 ya mazungumzo, CCM inaridhika kuwa tumefika mahali pazuri. Kilichobaki ni kukamilisha vizuri ili tupate makubaliano ambayo yatakuwa endelevu kama vile shabaha yetu ilivyo ya kupata suluhisho la kudumu. Kwa ajili hiyo pamoja na yote yaliyotokea na kusemwa CCM itawasilisha mapendekezo yake kwa wabia wetu kwenye mazungumzo haya, yaani CUF. Katibu Mkuu wa CCM, Lt. Yusufu Makamba tayari ameshaandika barua hiyo kwenda kwa Maalim Seif Shariff Hamadi, Katibu Mkuu wa CUF. Ni matumaini yetu kuwa tutapata majibu mazuri na vyama vyetu vitakaa chini baada ya muda si mrefu kukamilisha mazungumzo yetu.
Mimi naamini ni kwa maslahi ya wananchi wa Zanzibar na wananchi wa Tanzania kwa vyama vya CCM na CUF kukamilisha mazungumzo hayo. Haya shime tufanye hivyo! Inawezekana sote hatuna budi kutimiza wajibu wetu.
Ndugu Wana-CCM, Ndugu Wananchi;
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.

Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!

Kidumu Chama cha Mapinduzi

No comments: