ALIPOLIHUTUBIA Bunge wakati analizindua Desemba 30, 2005, rais Jakaya Kikwete alitoa kauli iliyowahakikishia watu wengi kuwa sit u amedhamiria, bali pia atafanya kila lililo katika uwezo wake (kama rais) kumaliza mpasuko wa kisiasa unaokwamisha mambo mengi Zanzibar. Kauli aliyoitoa haikuonyesha mashaka yoyote kuhusu dhamira yake ya kukabiliana na suala hilo.
Kauli hiyo, ilionyesha kwa mara ya kwanza kuwa kiongozi mkuu wa nchyi ametambua matatizo yanayoikabili Zanzibar. Hili lilimpa sifa sana. Hata wakati mazungumzo hayo yaliposuasua, hili lilitumika kama sehemu ya ushawishi kwa Chama cha Wananchi (CUF) kisijitoe katika mazungumzo kama ambavyo kilikuwa kimetishia.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja, watanzania walivumilia wakati mazungumzo hayo yakivuta miguu na hatimaye, mwezi uliopita, CUF ilipasua jibu kwa kueleza hadharani kile ambacho kilikubalika katika mazungumzo hayo yaliyokihusisha pia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Lakini kabla ya hapo, itakumbukwa kuwa masuala yaliyokuwa yakijadiliwa katika kamati ya mazungumzo yalikuwa yakivuja na kuufikia umma. Kwa mfano, ilipobainishwa kuwa moja kati ya masuala ambayo yanaelekea kuafikiwa ni kuundwa kwa serikali ya mseto, baadhi ya watu wasiopendelea mfumo huo wa utawala, walijitokeza na kueleza wazi wazi jinsi ambavyo hautokubalika hata kama kamati hiyo ya mazungumzo itaafiki hilo.
Na hivyo ndivyo ilivyotokea.
Lakini hakuna mtu ambaye aliuona mtego alioutega rais Kikwete katyika hotuba yake hiyo ya kihistoria. Katika sehemu ya hotuba hiyo, kwa kutaka kkujivua uwajibikaji katika suala hilo siku za usoni, Kikwete alisema: “Natambua kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu hatma ya siasa na utawala Zanzibar ni wa Wazanzibari wenyewe.”
Maana ya kauli hii ni kuwa chochote kitakachoafikiwa katika yale atakayoayaanzisha kuhusiana na mazungumzo hayo, itapaswa kipate baraka za Wazanzibari wenyewe. Kauli hii ni kichaka ambacho CCM wanekitumia kujificha, hasa wale wahafidhina ambao hawapendi kuona CUF ikihusishwa serikalini.
Ilichofanya NEC ya CCM huko Butiama ni kwenda nje kabisa ya yale yaliyoafikiwa katika mazungumzo na kutafuta namna ya kuliingiza hilo la kura ya maoni. Kilichokuwa kinafahamika ni kuwa yaliyokubaliwa kwenye kamati ya mazungumzo ndiyo yafikishwe kwenye vyama husika ili yajadiliwe na kupata baraka. Inavyoelekea, kamati ya mazungumzo haikuweka kipengele chochote kinachohusisha kura ya maoni (ndio maana CUF wameng’aka).
Lakini hata kama itakubalika kuwa kura ya maoni kama ilivyopendekezwa na NEC ya CCM, kitakachotokea kinaweza kujulikana tangu sasa. Mgawanyo wa kura huko Zanzibar tangu 1995 unajulikana. Ni dhahiri kuwa kura hiyo itapigwa kwa kufuata itikadi ya vyama hivyo.
Wale wa CUF, kwa sababu chama chao kimekubali kuingia kwenye serikali ya mseto, wataliunga mkono suala la kuanzishwa kwa serikali hiyo. Kwa upande mwingine, wale wa CCM, ambao wameapa kutoishirikisha CUF kwenye serikali, watalipinga suala hilo.
Kutokana na mgawanyiko uliopo visiwani humo, matokeo ya kura hii hayatatofautiana sana na matokeo ya chaguzi kuu zilizopita. Tofauti ya kura utakuwa chache sana na hili litazusha mabishani upya huku CCM wakishangilia ushindi katika kura ya maoni na CUF ikibishia matokeo hayo kwa sababu wameibiwa kura.
Hapa tutakuwa tuinarudi tena kule kule tulikotoka. Kwa maana hiyo inabidi tujiandae na muafaka mwingine tena wa kupatanisha ugomvi utakaotokana na malumbaano ya kura za maoni. Hivi ndilo lengo letu?
Ilichokifanya CCM ni kutaka kuliingiza taifa katika aibu kubwa. Naamini kuwa kamati ya mazungumzo walijua fika kuwa upo uwezekano wa kupiga kura ya maoni kuhusiana na jambo lakini kwa kutambua ukweli wa hali halisi, waliamua kulikwepesha wakiamini kuwa walikuwa wanawakilisha maslahi ya watu wote. Kumbe huku nyuma kuna genge jingine ambalo lina malengo yake.
Haikuwa na maana kwa Kikwete kuanzisha mazungumzo haya akihusishsa akikundi kidogo cha watu, wakati akijua kuwa suala hilo linahitaji maamuzi ya Wazanzibari wote. Haikuwa na maana kwa Kikwete kuanzisha mazungumzo hayo wakati anafahamu kuwa kitakachokubaliwa kitageuzwa na chama chake kwa maslahi ya nani sijui.
Inavyoonekana, baada ya wawakilishi wa CCM na CUF kukubaliana jambo hili katika mazungumzo yao, CUF katika umoja wao wameamua kulikubali suala hilo wakati wale wa CCM wameamua kulikataa. Je, katika hali kama hiyo suluhisho ni kwenda kwenye kura ya maoni? Na ni nani atatoa uhakikisho leo kuwa kura ya maoni itakuwa ya huru na haki na kuwa matokeo yake yataheshimiwa?
Ieleweke kuwa kinachojadiliwa hapa ni mustakabali wa Zanzibar yote na Tanzania kwa ujumla. Ifahamike kuwa katika mfumo wa utawala ambao tumeamua kuufuata, hakuna maana kuvihusisha vyama viwili tu katika mazungumzo haya hata kama vyama hivyo ndivyo vyenye ushawishi mkubwa visiwani hum oleo hii.
Haipendezi na wala haitosaidia kutengeneza muafaka wa CCM na CUF wakati nchi sit u inafuataa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi, bali pia kuna vyamka lukuki ambavyo vinaendesha siasa na vimeshaonyesha upinzani wa kweli katika masuala kadhaa.
Hata kama serikali ya mseto itakubalka Zanzibar, tumepata kujiuliza, iwapo tutafikia muafaka baina ya CUF na CCM leo hii, hivi itakuwaje wakati ambapo NCCR-Mageuzi itafanikiwa kupata nguvu ya kiaisasa Zabnzibar ka kushika nafasi ya pili katika matokeo ya kura? Nayo itahusika na mfumo wa kugawana madaraka au mfumo huu ni kwa ajili ya bCCM na CUF peke yao?
Kama na NCCR au chama kingine chochote kitakuwa kinahusika kutekeleza maamuzi haya, kwa nini nao hawakuhusishwa katika mazungumzo haya aambayo yamezaa mtafaruku mwingine badala ya muafaka?
CCM wanapozungumzia kura ya maoni hivi sasa wanafahamu kuwa suala hilo linahusu pia matumizi ya fedha? Zipo? Au ni namna nyingine ya kukwamisha maafikiano? Kwamba kura ya maoni haitofanyika mapema kwa sababu hakuna fedha na serikali zote mbili zipo katika juhudi ya kutafuta fedha ili kufanikisha suala hilo. Kuna aina fulani ya mchezo unafanyika hapa lakini umeshagunduliwa.
Nani atasimamia kura hii ya maoni? Chombo pekee kinachoweza kusimamia kura hii ni Tume ya Uchaguzi, ambayo inaweza kupewa jukumu hili. Lakini ni tume hii hii ambayo imekuwa ikilalamikiwa mara zote kuwa haitendi haki. Hivi sasa nani ataamini matokeo ya kura ya maoni iwapo mmojawapo wa wahusika atalalamika kuwa haki haikutendeka?
Kuna makosa ambayo kama nchi tumekuwa tukiyafanya kwa muda mrefu sana. Pamoja na kuwa suala hili linaweza lisionekane kuwa na uhusiano wa moja kwa moja, lakini hali ya Zanzibar na uhuru wake kama nchi nalo lina mchango wake humu.
Kwa muda mrefu, Zanzibar inajichukulia na kujiheshimu kama nchi (si taifa kama ilivyoamriwa na Mahakama). Lakini pamoja na mahakama kueleza kuwa hili si taifa, lakini yanayofanyika, jinsi ambavyio Zanzibar imeonekana katika harakati zake za kujiongezea mamlaka na madaraka, inaonekana ni jinsi gani ambavyo inapenda kuwa taifa kamili.
Kosa hapa ni kuwa wakati Zanzibar ikiwa na mwelekeo huo, inaonekana kuwa maamuzi makubwa mengi kuhusiana na nchio hiyo hufanywa aidha na Bara au kuathiriwa sana na Bara. Kwa Wazanzibari wengi, hasa wale wenye msimamo mkali, hili ni tusi.
Katika hili la mpasuko wa kisiasa ilipaswa ieleweke mapema iwapo ni suala lililopo katika malaka ya Zanzibar au la. Kikwete alipaswa kulijua hili kabla hajatoa kauli yake iliyoonyesha dhamira yake ya kulitafutia suala hilo ufumbuzi.
Inaelekea kuwa hata hakupata ushauri wa Wazanzibari kuhusiana na hili kama ambavyo wamemuonyesha juzi huko Butiama kwa kukataa mapendekezo ya kamati aliyoiunda. Kama angekuwa ameshauriana na kukubaliana na Wanzazibari kabla ya kuchukua hatua, ni dhahiri kuwa tusingefikia hali hii.
CCM wasipoanglia wanaweza kuwa wanafanya kosa la kuipa CUF nafasi ya kuendeleza mapambano ya kisiasa bila ya wao wenyewe kujua kuwa wanakipa faida chama hicho. Kwa kuwa kinaonekana kushindwa uchaguzi kila mara, CUF kinapata nafasi ya kuwa chama cha upinzani na kazi yake kubwa kuwa ni kuikosoa serikali iliyopo madarakani. Hili unaweza kulifanya kwa ufanisi iwapo utakuwa na hoja za msingi.
Mchezo unaofanywa na CCM kuhusiana na muafaka unakipa CUF hoja ambazo kwa kutumia uzoefu wake wa upinzani, kinaweza kuisumbua sana CCM hata kama kipo nje ya serikali. Inawezekana CCM wakaona kuwa harakati za CUF ambayo iko nje ya serikali kama keleleza mlango. Huo ni uamuazi wao.
Lakini kuna hatari nyingine kubwa zaidi ambayo inaweza kutokea ndani ya CCM yenyewe. Kwa muda mrefu sana kumekuwa na malalamiko kutoka kwa CUF kuwa wanaonewa, wanadhulumiwa na kunyanyaswa visiwani Zanzibar. Lakini habari kutoka kwenye kikao cha NWEC cha CCM cha Butiama, zinaeleza kuwa hata wana CCM, hasa wale walioko Pemba, nao wameanza kulalamika.
WanaCCM hao wa Pemba wanasema kuwa kutokana na mgawanyo wa kisiasa uliopo, wanafanya kazi kaatika mazingira magumu kisiwani humo, hasa kutokana na CUF kujiimarisha na kuwa hiyo ni ngome yake.
Kwao hawa, serikali ya mseto ilikuwa ni namna fulani ya kuwapunguzia ugumu wa kazi na maumivu wanayoyapata kukitumikia chama chao. Pale ambapo wenzao wa Unguja wameshindwa kusikiliza kilio chao, machozi yao yanaweza yasipotee hivi hivi. Lakini nani anayejua kuwa wanaweza kusikilizwa na kupozwa kwa namna nyingine?
Iwapo hali itaachwa iendelee kuwa hivi, ni dhahiri kwua itafika wakati, kutokana na kuimarika kwa harakati za CUF kutokana na kupatia hoja za msingi kisiasa, hali ya wanaCCM hawa wa Pemba ikawa mbaya zaidi kiasi cha kufikia kubadili msimamo wao.
Wazungu wana msemo kuwa iwapo huwezi kupambana nao basi jiunge nao. Itafika siku ambayo wanaCCM hawa kisiwani pemba wataona dhahiri kuwa hawawezi tena kuhimili vishindo na mikiki ya CUF, hivyo busara pekee watakayobakiwa nayo ni kujiunga nao.
No comments:
Post a Comment