Wakazi kadhaa wa eneo la Tabata Dampo katika Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, ambao nyumba zao libomolewa hivi karibuni, wamekataa kupokea fidia ya sh milioni 20 kila mmoja, walizoahidiwa na serikali.
Wakazi hao wamesema hawawezi kupokea fedha hizo kwa sababu ni kidogo ukilinganisha na hali halisi inayowakabili hivi sasa baada ya kubomolewa nyumba zao.
Aidha, wakazi hao wamekataa viwanja vya bure walivyopewa na serikali kwa madai kuwa eneo la Buyuni, wakisema kuwa eneo hilo halina huduma zozote za kijamii na hakuna miundombinu kwa sasa.
Tamko la kutaka kuwalipa fuidia wananchi hao lilitolewa na waziri wa Sertikali za Mitaa, Stephen Wassira kama hatua ambazo serikali imezichukua baada ya kukabidhiwa ripoti ya timu iliyochunguza sakata hilo.
Wassira alisema fedha hizo zinalipwa kutokana na uvunjwaji wa haki za binadamu waliofanyiwa wakazi hao kwa kuvunjiwa nyumba zao kinyama.
Timu ya watu wanne ilifanyakazi yake kwa siku 16 na kubaini ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu uliofanywa na watendaji wa Manispaa ya Ilala katika kusimamia zoezi hilo, na kusababisha kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi, Mhandisi na Mwanasheria.
Timu ilibaini kuwa ubomoaji huo haukuzingatia uamuzi wa Baraza la Ardhi ulioisisitiza Halmashauri ya Ilala kuangalia taratibu zilizopo za kuwaondoa wavamizi katika eneo husika.
Aidha, timu hiyo pia iligundua kuwa taratibu za uendeshaji wa Halmashauri hazikuzingatiwa kwa kuwa ilipaswa dhamira ya kubomoa makazi hayo, ilitelewe katika vikao vya menejimenti na baraza la madiwani.
Wassira alisema, timu hiyo ilibaini mambo yaliyojitokeza wakati wa zoezi hilo ambayo ni kunyanyasika na kuteseka kisaikolojia kwa wakazi hao na familia zao na kubainisha kuwa leseni za makazi zilitolewa kimakosa.
Kwa mujibu wa kanuni na sheria kama ilivyoelezwa na Wassira, notisi ya kuondoka katika maeneo hayo ilitakiwa kutolewa siku 30 kabla ya ubomoaji huo kwa vile hilo ni eneo la makazi.
Baraza la ardhi, Februari 27 mwaka huu lilitoa hukumu yenye kueleza kuwa kiwanja namba 52 eneo la viwanda Tabata dampo ni mali ya Kampuni ya Allied Cargo na baada ya siku mbili watendaji wa Manispaa ya Ilala ilibomoa makazi ya watu hao kinyume cha sheria na taratibu.
“Hilo ni kosa, serikali wajibu wetu ni kulinda haki za raia hasa kuishi salama…nataka tuelewane vizuri. Ninachosema hapa ni kwamba tunashughulikia ukiukwaji wa sheria uliofanywa na watendaji wetu.
“Katika hili, kanuni za ubomoaji zimekiukwa na tunachokitoa hapa siyo malipo ya makazi yao, hapana hii ni pole kwa yaliyowakuta. Na mimi kama Waziri wa TAMISEMI, nawashauri kuhamia buyuni kwenye viwanja vya bure.
“We are concerned with human right (tunafuata haki za binadamu) kutokana na makosa ya maofisa wetu wachache, hii watalipwa wenye nyumba tuu,” alisisitiza Wassira.
Alisema, serikali imejifunza kutokana na ukiukwaji huu hivyo imeziagiza mamlaka zote za halmashauri nchini zinazoshughulikia mipango miji kuwawajibisha watendaji wote wanaokiuka sheria, taratibu na kanuni za kuwahamisha wananchi.
Wassira pia, alisema iwapo kuna baadhi ya watendaji wa Manispaa hiyo wanaotuhumiwa kwa ruhwa au uzembe, mamlaka husika ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) itawashighulikia.
No comments:
Post a Comment