Tuesday, April 1, 2008

TAMKO RASMI LA CUF KUHUSU MAZUNGUMZO YA MUAFAKA

TAMKO LA CHAMA CHA WANANCHI (CUF) KUFUATIA TAMKO LA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CCM KUHUSIANA NA MAZUNGUMZO YA KUTAFUTA UFUMBUZI WA KUDUMU WA MPASUKO WA KISIASA ZANZIBAR


Tarehe 17 Machi, 2008, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi (CUF) lilifanya kikao chake mjini Zanzibar ambapo lilipokea na kuridhia makubaliano yaliyofikiwa na Kamati ya Mazungumzo ya CCM na CUF ya kuupatia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Siku hiyo hiyo, CUF iliwatangazia wanachama wake na Watanzania kwa jumla matokeo ya kikao hicho cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Demokrasia, mjini Zanzibar.

Hiyo ilikuwa ni hatua kubwa na muhimu kutekelezwa na upande wa CUF baada ya vyama vyetu viwili kukubaliana kuwa viwasilishe makubaliano hayo kwa vikao vya juu vya maamuzi vya vyama vyetu ili kuyaridhia kabla ya kutiwa saini. Baada ya CUF kutekeleza wajibu wake, yalikuwa matarajio na imani yetu kwamba na upande wa CCM nao ungefanya wajibu wake.

Kwa mshangao na masikitiko makubwa, jana tumepokea Tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuhusiana na mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa Zanzibar ambalo kimsingi limeyakataa makubaliano yaliyofikiwa na Kamati zetu mbili.

CCM imeamua kufanya usanii wa kisiasa kwa kutumia lugha ya mzunguko, ya ubabaishaji na ya upotoshaji kwa lengo la ama kuendelea kurefusha muda hadi mwaka 2010 au kuyakataa makubaliano ambayo wajumbe wake wameshiriki kuyaandaa katika miezi 14 ya mazungumzo kati ya vyama vyetu viwili.

Hali hiyo iko wazi kwa sababu mbili kuu zifuatazo:

CCM imetamka ‘kuyakubali kimsingi’ mapendekezo yaliyowasilishwa na Kamati ya chama hicho inayoshiriki mazungumzo lakini wakati huo huo inazungumzia marekebisho ambayo inataka yafanywe na hivyo kuiagiza Kamati yake kukutana na wajumbe wa CUF ili kuyajadili marekebisho hayo.

Kwanza, CCM haikutaja ni maeneo gani inataka yafanyiwe marekebisho. Pili, hoja hii inashangaza kwa sababu wajumbe wa Kamati ya Mazungumzo kutoka upande wa CCM walikuwa wakiwaarifu wajumbe wa Kamati kutoka upande wa CUF kwamba wao walikuwa wakiwasilisha taarifa kwa kila hatua inayofikiwa katika vikao vya chama vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa na pia kwa viongozi wao wa juu, Rais Jakaya Kikwete na Mheshimiwa Amani Karume, na kupata maelekezo na miongozo inayohitajika. Hata taarifa ya karibuni kabisa ya CCM iliyokuwa ikikanusha taarifa za vyombo vya habari kwamba Mheshimiwa Amani Karume si kikwazo cha kufikiwa makubaliano ya muafaka iliweka mkazo na msisitizo kwamba katika kila hatua, viongozi hao wameshauriwa ipasavyo. Hatua hii ya mwisho ilikusudiwa kubariki makubaliano hayo yaliyokuwa yakifikiwa hatua kwa hatua na siyo kufungua mjadala mpya kupitia duru mpya ya mazungumzo.

CCM imekuja na hoja mpya kwamba iwapo mapendekezo haya yatakubaliwa, yatakuwa yanaleta mabadiliko makubwa ya mfumo wa utawala katika Zanzibar na hivyo yanapaswa kuridhiwa na wananchi wenyewe kwa njia ya kura ya maoni.

CCM kuleta hoja hii ni kulifanyia mzaha jambo kubwa linalohitaji umakini wa hali ya juu kwani linagusa mustakbali wa taifa letu. Muda wote wa mazungumzo ambayo yamechukua miezi 14 na yakiwa yamehusisha vikao 21, wajumbe wa Kamati ya CCM wanaoshiriki mazungumzo hawakuleta hoja hii ya kura ya maoni. Kinachosikitisha zaidi ni kuwa tofauti na ilivyoelezwa, pendekezo la kutaka kura ya maoni halikuwa limeibuliwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM bali lilikuwemo katika Taarifa ya Kamati ya CCM inayoshiriki mazungumzo likiwa ni pendekezo walilotaka liridhiwe na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa. Hivyo, ni wazi liliandaliwa mapema kutokana na kile Kamati hiyo ya CCM ilichokiita “kuipiku CUF katika ubunifu wa kujenga”. Kitendo cha Kamati ya CCM kuwasilisha kitu kipya nje ya makubaliano yaliyofikiwa ni upotoshaji mkubwa wenye lengo la kulifanyia usanii wa kisiasa suala kubwa kama hili linalogusa maslahi ya taifa na watu wake moja kwa moja. Na iwapo pendekezo hilo lina nia njema ya kuwashirikisha wananchi, kwa nini wajumbe wa Kamati ya CCM wasiliwasilishe katika vikao vya mazungumzo na badala yake wakaamua kuliingiza kama mtego wa kisiasa wenye lengo la “kuipiku CUF”?

Hoja nyengine ni kwamba kura ya maoni hiyo itaendeshwa na chombo kipi na kwa utaratibu upi hasa ikitiliwa maanani tayari CCM na CUF wamekubaliana kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na Daftari la Kudumu la Wapiga Kura vina matatizo ya msingi ambayo yanahitaji kurekebishwa? Ni vipi basi Tume hiyo chini ya Daftari bovu liliopo itaweza kuendesha kura ya maoni ambayo itakuwa huru na ya haki?

Sisi tunaona suala hilo ni mbinu chafu tu yenye lengo la kuendelea kupoteza muda ili makubaliano yaliyofikiwa yasiweze kutiwa saini na utekelezaji kuanza. Kwa lugha yao CCM waliyoandika katika waraka wao ni njia ya “kuipiku CUF” na kamwe haikusudiwi kupata maoni ya wananchi.

Kwa msingi huo CUF haikubaliani na hoja hizo zote mbili.

Ni lazima tukiri kuwa tumeshtushwa sana na kiwango hiki cha CCM kulifanyia usanii wa kisiasa suala kubwa kama hili. Lakini pia tumepata faraja kuwa Watanzania sasa wameweza kujua ni nani kati ya CCM na CUF asiyeitakia mema nchi hii. Wamejua ni nani kati ya CCM na CUF asiyetaka amani na utulivu katika nchi hii. Wamejua ni nani kati ya CCM na CUF asiyetaka siasa za maelewano na mashirikiano katika nchi hii.

Sasa ni wazi kwamba CCM iliingia katika mazungumzo haya ikiwa haina dhamira ya kweli na ya dhati ya kuupatia ufumbuzi wa kweli mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Inaonekana lengo pekee la CCM katika mazungumzo haya lilikuwa ni kuwahadaa Watanzania na jumuiya ya kimataifa kwa kujidanganya kwamba wangeweza kuidhibiti kisiasa CUF kupitia utaratibu wa kuwapa matumaini ya uongo (strategic engagement) na kuyarefusha mazungumzo hayo kadiri inavyowezekana hadi kipindi kinachokaribia uchaguzi mkuu ujao pasina kuchukua hatua zozote za maana zenye kulenga kutoa ufumbuzi wa kweli wa mpasuko uliopo. CCM imeonesha wazi wazi kuwa haiitakii mema Tanzania yetu na wala haitaki kuona umoja wa kitaifa na utulivu wa kudumu vinapatikana Zanzibar ambayo ni sehemu moja ya Jamhuri ya Muungano.

Kwa upande mwengine, Watanzania wote na jumuiya ya kimataifa ni mashahidi kuwa CUF imefanya kila liliomo katika uwezo wake kuinusuru hali tete ya kisiasa Zanzibar isichafuke. CUF imechukua kila juhudi kuona mazungumzo haya yanafanikiwa. Imetoa kila ushirikiano unaohitajika kwa CCM na hata kuachia madai yake makuu (kutoa ‘concessions’) ili kuyanusuru mazungumzo hayo na kuyafanikisha.

CUF imeonesha ustahamilivu, ustaarabu na uelewa mkubwa katika mazungumzo haya. Tumeweza kukubaliana na CCM kwa kila hatua tuliyoombwa tuwe na subira ili kupisha mambo kadhaa ya kisiasa yapite. Mara nyengine, hata bila ya kutuomba, sisi wenyewe tumeonyesha uelewa na kuwapa nafasi pale yalipoibuka matukio ya kisiasa ambayo hayakutarajiwa na ambayo tulihisi yanahitaji tuwape muda wenzetu. CCM haionekani kujali au kuthamini juhudi hizo na imeamua kuzipiga teke.

Kama tulivyowahi kusema, hatukufanya hivyo kwa sababu CUF ni dhaifu kisiasa kama ambavyo CCM wangependa kujidanganya. Tulifanya yote hayo kwa sababu tunaongozwa na dhamira njema ya kuhakikisha nchi yetu inabaki katika hali ya amani na utulivu huku tukiamini kwa dhati kwamba mazungumzo ndiyo njia pekee ya kistaarabu ya kumaliza tofauti au migogoro ya kisiasa na kijamii. Lakini ni lazima tusisitize kuwa mazungumzo yenye lengo hilo ni lazima yawe mazungumzo makini yanayoongozwa na utashi wa kweli wa kisiasa uliojengeka juu ya nia njema na kuheshimiana baina ya pande zinazohusika. Hilo limekosekana kwa upande wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.

Kufuatia misukosuko iliyoyakumba mazungumzo haya mwaka jana, Rais Kikwete, alitoa taarifa kwa umma tarehe 14 Agosti, 2007 akiuomba upande wa CUF ukubali kuendelea na mazungumzo na akiwahakikishia Watanzania kuwa angechukua hatua kuona yanakamilishwa na yanafanikishwa. Wakati akiwahutubia Mabalozi wa nchi za nje wanaowakilisha nchi zao hapa nchini katika sherehe za kuukaribisha mwaka mpya, mapema mwaka huu, Rais Kikwete aliwaeleza kwamba mazungumzo yamefikia ukingoni na kwamba karibu suala la mpasuko wa kisiasa Zanzibar litakuwa historia. Kauli hiyo ilipokewa kwa matumaini makubwa na wananchi ambao wamekuwa wakifuatilia kwa makini kila hatua ya mazungumzo yetu. Ni bahati mbaya kwamba Rais Kikwete ameyaangusha matumaini hayo ya Watanzania kama ambavyo ameyaangusha matumaini yao katika masuala mengine yote aliyowaahidi wakati anaomba kura na anaingia madarakani.

CUF imevunjwa moyo sana na Mheshimiwa Jakaya Kikwete akiwa kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM. Imani tuliyokuwa nayo kwake kama kiongozi wa nchi na ambayo tulibaki nayo hadi CCM inaelekea katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa imetetereka sana. Kitendo cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM chini ya Uenyekiti wake kukataa kupitisha makubaliano yaliyofikiwa na Kamati ya Mazungumzo ya CCM na CUF na badala yake kuja na hoja mpya za ajabu ajabu zenye lengo la “kuipiku CUF” kisiasa kunamwonyesha Rais Kikwete ama hakuwa mkweli na mwaminifu tokea mwanzoni na kwamba alikuwa akifanya usanii wa kisiasa wakati alipotangaza kuwa anasononeshwa sana na mpasuko wa kisiasa Zanzibar au ni kiongozi dhaifu asiye na udhibiti wa chama anachokiongoza. Yote mawili hayampi sifa za kiongozi ambaye nchi inamhitaji inapopita katika vipindi vigumu.

Kama tulivyofanya mwaka jana, ni vyema tumkumbushe tena Mheshimiwa Jakaya Kikwete kauli yake mwenyewe aliyoitoa wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tarehe 16 Septemba, 2003 wakati anafungua Mkutano wa Kumi na Moja wa Hali ya Siasa Tanzania ambao ulihusu ‘Udhibiti na Utatuzi wa Migogoro’, pale aliposema:

“…[N]aelewa kuwa utaratibu wa kung’amua dalili za migogoro hauwezi kuwa na manufaa kama haukuambatana na vitendo vya haraka. Taarifa za dalili za uendelezaji wa migogoro zinapopatikana zitakuwa hazina manufaa katika uzuiaji wa migogoro hiyo kama zitashughulikiwa kwa njia ya mlolongo wa uamuzi wa kirasimu ambao unaweza kuchelewesha utekelezaji hadi migogoro inapotokea. Kwa hiyo ni wazi kuwa upatikanaji wa taarifa za dalili za migogoro unakuwa wa maana katika uzuiaji wa migogoro kama mara zipatikanapo, zinatafsiriwa kwa vitendo. Mtiririko wa hoja hapa unapaswa kuwa “dalili za mwanzo kujumlisha na vitendo halisi ni sawa sawa na uzuiaji wa migogoro.” Ili haya yatokee unahitaji kuharakisha au kurekebisha utaratibu wa utoaji wa maamuzi ili dalili za mwanzo ziweze kutafsirika kwa vitendo haraka iwezekanavyo.”

Maamuzi ya Chama chake kupitia kikao alichokiongoza yeye mwenyewe akiwa Mwenyekiti wake hayaonyeshi kuwa anayazingatia haya aliyowaasa wenzake mwaka 2003 maana maamuzi ya Halmshauri Kuu ya Taifa yanawakilisha hasa “mlolongo wa maamuzi ya kirasimu” ambayo kama alivyosema hayawezi kuwa msingi wa utatuzi wa mgogoro. Inasikitisha zaidi kwa Rais Kikwete kuwatangazia Watanzania na ulimwengu kuwa amefanikiwa kuwakutanisha Rais Mwai Kibaki na Mheshimiwa Raila Odinga wa Kenya na kufanikisha kufikiwa kwa makubaliano kati ya ODM na PNU nchini humo lakini anashindwa kulifanikisha hilo nchini mwake ndani ya chama anachokiongoza mwenyewe na kati ya CCM na CUF. Rais Kikwete anaona fakhari kuwa Tanzania imeongoza Jeshi la Umoja wa Afrika (AU) katika operesheni ya kijeshi iliyopewa jina la “Operesheni Demokrasia” kisiwani Anjouan, nchini Comoro lakini ameshindwa kuongoza operesheni ya kisiasa ya kusimamisha demokrasia visiwani Zanzibar.

Rais anapaswa ajue kuwa heshima ya ofisi yake na uadilifu wake binafsi ameutia doa kubwa kutokana na kushindwa kusimamia kwa vitendo ahadi yake aliyoitoa kwa Watanzania kupitia hotuba yake ya Desemba 30, 2005 Bungeni na pia ahadi aliyoitoa na kuirejea mara kadhaa kwa marafiki wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa katika ziara zake za nje ya nchi kila mara pale alipoulizwa kuhusiana na mgogoro wa muda mrefu wa kisiasa Zanzibar.

MSIMAMO WETU:

Chama Cha Wananchi (CUF) hakiko tayari kushirikiana na CCM kuwafanyia Watanzania usanii wa kisiasa. Huu sio utaratibu wa CUF katika uendeshaji wa siasa. Kwa CUF, siasa si proaganda zilizopitwa na wakati bali ni utumishi wa dhati na uliotukuka kwa umma uliowaamini viongozi wake. Kwa msingi huo, CUF haitakubali kurejea katika mazungumzo kwa utaratibu inaoutaka CCM.

CUF kinakitaka CCM kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na Kamati ya Mazungumzo ya vyama vyetu viwili na endapo kweli Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho “ imeyakubali kimsingi” makubaliano yaliyofikishwa kwake kama ilivyosema taarifa yake, basi kikubali kutia saini makubaliano hayo na utekelezaji wa yaliyokubaliwa uanze mara moja.

Kinyume na hayo, CUF inatoa wito kwa marafiki wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti, za uhakika na za haraka kuingilia kati suala hili ili kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatiwa saini. Baada ya Tanzania yenyewe kushindwa katika utatuzi wa mgogoro wake huu wa muda mrefu, sasa ni wakati muafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kuingilia kati kwa kuchagua Mpatanishi wa Kimataifa anayeheshimika kuja kuyasimamia hadi kuyafikisha ukingoni kwa kuhakikisha makubaliano ya dhati yanafikiwa yatakayotoa ufumbuzi wa kweli na wa haki wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar.

CUF inatoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kuepuka fedheha iliyoipata katika nchi nyengine za Kiafrika ambazo iliziachia hadi hali ikachafuka na ndipo ikaingilia kati. Hali ya Zanzibar ni mbaya. Ilitulia kwa sababu ya matumaini ya Wazanzibari na Watanzania kwamba mazungumzo ya CCM na CUF yataleta suluhisho la utulivu na umoja. Makubaliano yaliyofikiwa yanapokosa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuyakamilisha, yanahitaji kuona jumuiya ya kimataifa inaingilia kati kwa hatua za wazi na madhubuti kuinusuru Zanzibar na Tanzania isitumbukie kule nchi nyengine za Kiafrika zilipotumbukia.

Wakati tunawashukuru kwa dhati viongozi wa vyama vyengine vya siasa, viongozi wa dini, taasisi na jumuiya za kijamii, mabalozi wa nchi za nje wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania na vyombo vya habari hususan magazeti huru kwa mchango wao mkubwa walioutoa na ambao ulisaidia kuyafikisha mazungumzo hadi hatua ya kukamilishwa, CUF tunatoa wito tena kwao kuendelea kutoa ushirikiano wao na kutimiza wajibu wao kuona mgogoro huu unamalizwa kwa njia za amani na za haki.

CUF inawataka wanachama na wapenzi wake pamoja na Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki wakijua kuwa CUF iko upande wa amani, ukweli na haki na siku zote upande wa amani, ukweli na haki utashinda.

Kwa jinsi inavyoyachezea masuala mazito yanayohusu maslahi ya taifa kama ilivyodhihirika kwa mambo yote makubwa yaliyojitokeza hivi karibuni, ni wazi kuwa CCM imepoteza uhalali wa kuongoza nchi na wakati sasa umefika wa Watanzania kuchagua chama makini kitakachoipa Tanzania uongozi makini unaohitajika.

HAKI SAWA KWA WOTE


SEIF SHARIF HAMAD
KATIBU MKUU – CUF

Dar es Salaam
01 Aprili, 2008

No comments: