THE CIVIC UNITED FRONT
HOTUBA YA MWENYEKITI WA TAIFA WA CHAMA CHA WANANCHI (CUF), MHE. PROF. IBRAHIM LIPUMBA, KATIKA MKUTANO NA WAZEE, WANAWAKE NA VIJANA VIONGOZI WA CHAMA WA MKOA WA DAR ES SALAAM, KUTOA UFAFANUZI KUHUSIANA NA MAZUNGUMZO YA KUTAFUTA UFUMBUZI WA KUDUMU WA MPASUKO WA KISIASA ZANZIBAR
UKUMBI WA DIAMOND JUBILEE, DAR ES SALAAM
TAREHE 06 APRILI, 2008
UTANGULIZI
Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kuwa wazima na kuweza kukutana leo hii. Naamini ataendelea kutupa baraka na mwongozo wake ili tuweze kuutekeleza wajibu wetu kama viongozi ambao ni watumishi wa Watanzania kuweza kuwapa uongozi thabiti wenye hekima na busara na utakaoiepusha nchi yetu na shari ambayo watawala waliopo madarakani hivi sasa wanaonekana kuiandaa. Nawashukuru nyinyi pia Wazee, viongozi wa Chama chetu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kina mama na vijana kwa kufika kwa wingi kuja kutusikiliza licha ya taarifa ya muda mfupi ya kufanyika kwa mkutano huu. Najua mmeacha shughuli zenu muhimu kuja kunisikiliza na kwa hilo, nasema Ahsanteni sana.
Watanzania wenzangu, sina haja ya kuwaficha, nimelazimika kuja kuzungumza nanyi ili kutumia fursa hii kuweka kumbukumbu sahihi kuhusiana na mchakato mzima wa mazungumzo kati ya Chama Cha Wananchi (CUF) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) yenye lengo la kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar na hasa hii hali ya mtafaruku iliyopo sasa ambayo tumefikishwa na CCM. Nimeamua kufanya hivi baada ya kumsikiliza Mwenyekiti mwenzangu wa upande wa pili ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, akitoa maelezo kuhusiana na mazungumzo hayo katika ukumbi huu huu wa Diamond Jubilee tarehe 2 Aprili, mwaka huu wa 2008 lakini kwa bahati mbaya maelezo hayo yakiwa yamejaa upotoshaji na ubabaishaji wa hali ya juu. Rais anatumia usanii wa kisiasa kukanusha kwamba yeye na chama chake hawafanyi usanii wa kisiasa. Nchi inapoongozwa na watu wa aina hii, Watanzania tuna kila haki na sababu ya kujiuliza iwapo kweli tuko salama hivi sasa na huko mbele tunakokwenda.
Wakati wa ufunguzi wa kampeni za Uchaguzi Mkuu za chama cha CUF mjini Tabora Septemba 2005 niliwatahadharisha Watanzania kuwa Mheshimiwa Kikwete ni Mtu wa mzaha mzaha, hana kauli thabiti hafai kuwa Rais na tukimchagua matokeo yake itakuwa rushwa na ufisadi itaongezeka kwa kasi, mpya na nguvu mpya. Uchambuzi wa kina wa rushwa nitaufanya katika mikutano ifuatayo leo nitachambua mazungumzo ya CCM na CUF. Hata hivyo la kuzingatia ni kuwa Mafisadi wamejikita na kujenga kambi ndani ya CCM. Hawataki demokrasia kwa sababu itawaumbua na kuwanyima nafasi ya kuendelea na ufisadi wao.
MCHAKATO WA MAZUNGUMZO
Watanzania wenzangu, mtakumbuka kuwa mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005, ambao kwa mara ya tatu mfululizo uliendelea kutawaliwa na wizi wa kura uliofanywa na CCM na kumuweka madarakani kwa nguvu Mheshimiwa Amani Karume kinyume na matakwa ya Wazanzibari, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lilikutana tarehe 5 Novemba, 2005 kutafakari hali mbaya ya kisiasa iliyokuwapo wakati huo ambayo ingeweza kuzaa maafa makubwa kwa nchi yetu. Wazanzibari walikuwa tayari kwa lolote baada ya kuchoshwa na wizi wa kura wa CCM katika chaguzi zote tatu, yaani 1995, 2000 na 2005. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama chetu likaamua kutumia busara na kuepusha shari kwa kuwataka Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla watulie na kuwapa nafasi viongozi wao kutafuta ufumbuzi wa suala hilo kwa njia za amani.
Wengi waliomsikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, wakati akilihutubia na kulizindua Bunge jipya tarehe 30 Desemba, 2005, pamoja na mambo mengine akilieleza Taifa nia yake ya kuutafutia ufumbuzi wa kudumu mpasuko wa kisiasa Zanzibar walidhani hiyo ilikuwa ni hoja yake mwenyewe tu. Hamkuelewa kwamba maelezo hayo ya Rais hayakuja kwa sababu ya nia yake tu bali yalitokana na mawasiliano baina ya baadhi ya wasaidizi na washauri wake wa karibu na baadhi ya viongozi wa CUF ambayo yalianza mara baada ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005 kumalizika na kabla hata ya yeye kushika madaraka ya Urais. Tukakubaliana kuwa tusubiri hadi baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Muungano na tutachukua hatua za pamoja za kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Rais alipotoa hotuba yake Bungeni, hata kama haikuwakilisha kisawa sawa mtazamo wa CUF kuhusiana na mgogoro wa kisiasa Zanzibar, tuliamua kumpa ushirikiano wetu katika kutimiza ile ahadi tuliyokubaliana. Siku moja tu baada ya hotuba yake, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alitoa taarifa kwa vyombo vya habari na akamuandikia barua rasmi Rais Kikwete tarehe 31 Desemba, 2005 akimhakikishia ushirikiano wetu. Kuanzia hapo mazungumzo yasiyo rasmi yakawa yanafanyika kati ya baadhi ya wasaidizi na washauri wa Rais aliowaamini na baadhi ya viongozi wa CUF tuliowapa ridhaa ya kuendeleza mawasiliano hayo. Ubalozi wa nchi moja iliyo rafiki mkubwa wa Tanzania nao ukajitolea kuratibu mawasiliano hayo ili kujenga maelewano mazuri.
Jambo moja ambalo nataka niliweke wazi na Watanzania wote walielewe ni kwamba tokea hatua hizo za mwanzo kabisa, ambazo hazikuwa zikitangazwa hadharani, tulikubaliana kuwa ufumbuzi tunaoutafuta utapatikana kwa CUF kusamehe madai yake ya kutaka Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar urudiwe na badala yake itapewa nafasi ya Waziri Kiongozi na idadi kadhaa ya mawaziri kama itakavyokubaliwa. Kwa maneno mengine, makubaliano hayo yalikuwa na sura kama ile iliyokuja kujitokeza baadaye katika suluhisho la mgogoro wa Uchaguzi Mkuu wa Kenya ambao Rais Kikwete amejisifia sana kuwa aliweza kuumaliza kwa masaa matano tu.
Kilichokuwa kikizungumzwa katika duru hizo za awali kilikuwa ni utaratibu upi utakuja kutumika kufanikisha malengo hayo. CUF ilimweleza wazi Rais kupitia wasaidizi wake kwamba haikuwa na imani kwamba Mheshimiwa Karume na wahafidhina wenzake wa CCM Zanzibar watakubaliana na ufumbuzi huu. Naye, kupitia wasaidizi hao hao, akatuhakikishia kuwa hilo ni la ndani ya CCM na tuwaachie wao. Tulipouliza lini utaratibu huu utaanza kazi rasmi tukaambiwa tusubiri miezi sita hadi Juni 2006 pale Rais Kikwete atakapokabidhiwa uenyekiti wa Chama chake kwani atakuwa na mamlaka kamili na muhimu yatakayomuwezesha kulifanikisha suala hili.
Juni 2006 ilifika na Rais Kikwete akawa Mwenyekiti wa CCM. Tukahimiza haja ya sasa kuyawekea utaratibu wa kuyatekeleza yale tuliyokuwa tumeelewana tokea Januari 2006, tukaambiwa tumpe nafasi zaidi ya miezi sita mingine ili aweze kuweka safu vyema na kuimarisha mamlaka yake katika Chama kusudi awe na nguvu za kupitisha maamuzi mazito kama hayo. CUF kwa maslahi ya Taifa, tukakubali kusubiri hadi Desemba 2006. Ilipofika Desemba 2006, badala ya kuwa na utaratibu wa kutuelekeza kule tulikokuwa tayari tumeshaelewana kuwa ndiyo suluhisho, tukapokea tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuwa imeagiza yafanyike mazungumzo kati ya CCM na CUF kwa lengo la kuanzisha siasa za maelewano Zanzibar. Pamoja na kuona hatua hiyo inaturejesha nyuma na ina lengo la kuchelewesha kufikia malengo tuliyokubaliana, CUF kwa nia njema ya kuwaamini wenzetu na hasa Rais Kikwete, tukatoa tamko kuridhia mazungumzo hayo.
Januari 17, 2007, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akiambatana na Mhe. Hamad Rashid Mohamed na Mhe. Ismail Jussa, walikutana na Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. Yusuf Makamba akiwa amefuatana na Mhe. Ali Ameir Mohamed na Mhe. Saleh Ramadhani Feruzi kukubaliana utaratibu wa kuendesha mazungumzo. Miongoni mwa mambo waliyokubaliana ilikuwa ni kubadilishana hadidu za rejea ambazo kila upande utaeleza matarajio yake katika mazungumzo hayo na baadaye hadidu hizo ndizo zitumike kutengeneza agenda za mazungumzo.
Katibu Mkuu wa CUF aliwasilisha hadidu za rejea zetu kwa Katibu Mkuu wa CCM kupitia barua ya tarehe 26 Januari, 2007 ambazo zilikuwa kama ifuatavyo:
Kurudiwa kwa Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar:
(a) chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa; au
(b) chini ya usimamizi wa Serikali ya Mpito ya CCM na CUF
kutokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 30, 2005 kutokuwa huru na wa haki ambako kulisababishwa na ama kutotekelezwa kikamilifu au kutotekelezwa kabisa kwa maeneo mengi ya Muafaka wa CCM na CUF wa 2001 na pia kutumika kwa nguvu kubwa na ya kupita kiasi ya Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Vikosi vya SMZ na makundi ya vijana wa CCM ya ’Janjaweed’ katika kuwatisha wananchi wasiweze kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa uhuru na uwazi.
Kutengwa, kubaguliwa, kunyanyaswa na kukandamizwa kwa wanachama na wafuasi wa CUF walioko Zanzibar na hasa Pemba ikiwemo kunyimwa haki zote za kiraia kutokana na itikadi zao za kisiasa na kufanywa hawana haki katika nchi yao, hali inayotishia hata umoja na usalama wa nchi kwa kukuza hisia za sehemu kubwa ya wakaazi wa Pemba kuanza kufikiria hawatakiwi katika Zanzibar na katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuendelea kuizuia na kuiwekea vikwazo CUF kufanya shughuli zake halali za kisiasa katika visiwa vya Zanzibar kama inavyopaswa kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Vyama vya Siasa (Nam. 5/1992).
Askari wa Polisi na Vikosi vya SMZ pamoja na vijana wa ’Janjaweed’ waliohusika katika matukio ya uhalifu na uvunjwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wasio na hatia kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Utaratibu wa Utekelezaji na Programu ya Utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa katika mazungumzo haya.
Kwa upande wa Katibu Mkuu wa CCM, kama ilivyo kawaida yao, akakiuka makubaliano hayo ya mapema kabisa kwa kutowasilisha hadidu zao. Hiyo ilikuwa hatua ya awali ya CCM kutokuwa wakweli katika mazungumzo haya na kama itavyokuja kudhihirika huko mbele, mara zote kutoheshimu yale yaliyokwisha kubaliwa au kujitia hamnazo kwamba hakukuwa na makubaliano kama hayo.
Badala ya kuwasilisha hadidu za rejea, CCM wakawasilisha barua ya kutaka ziteuliwe timu za watu sita kutoka kila upande na mazungumzo yaanze na kwamba wao wangetoa hadidu za rejea na mapendekezo ya agenda zao katika kikao cha kwanza cha timu hizo.
Tarehe 1 Februari, 2007, kikao cha kwanza cha timu zetu kikafanyika mjini Dodoma bila ya CCM kuwasilisha hadidu za rejea zake kama walivyokuwa wameahidi na badala yake wakasema wametumia hadidu za rejea za CUF tulizowapelekea kuandaa mapendekezo ya agenda. Baada ya mvutano wa muda, hatimaye timu yetu ilikubali yaishe na kwa pamoja kukubaliana agenda tano za mazungumzo zifuatazo:
Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005: Uhalali na Taathira zake.
Usawa na Haki katika Kuendesha Siasa.
Masuala ya Utawala wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Njia za Kuimarisha Mazingira ya Maelewano na Uendeshaji wa Uchaguzi Huru na wa Haki Zanzibar.
Utaratibu wa Utekelezaji na Programu ya Utekelezaji wa makubaliano yatakayofikiwa.
Hata baada ya hatua hiyo, katika kila walichokieleza ni kumridhisha Mhe. Amani Karume ili asiwe na kinyongo na mazungumzo hayo, CCM ikarudi tena kutuomba upande wa CUF tukubali kuliondoa neno “Uhalali“ katika agenda ya kwanza inayohusu uchaguzi mkuu na badala yake iwe “Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa Oktoba 30, 2005 na Taathira zake“. CUF kwa mara nyingine tena ikaonyesha uungwana kwa kukubali ombi hilo la CCM bila ya kipingamizi chochote. Uzuri wa haya ninayoyaeleza ni kwamba yote yamo katika Kumbukumbu za Vikao vya Kamati ya Mazungumzo ambazo zimetiwa saini na pande zote mbili.
Ni baada ya hatua hiyo, ndipo mjadala wa agenda moja baada ya nyingine ukaanza, na kila hatua makubaliano yakifikiwa. Kwa yale maeneo ambayo hayakuwa na makubaliano, ikakubaliwa kila upande ubaki na msimamo wake. Jumla ya vikao 21 vya mazungumzo vimefanyika katika kipindi cha miezi 14 tokea Januari 2007 hadi Februari 2008. Katika hatua zote hizo, kila upande ulikuwa ukitoa taarifa kwa viongozi wake wakuu na katika vikao vya maamuzi vya vyama vyetu ambavyo ni Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa upande wa CUF na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa kwa upande wa CCM.
Watanzania wenzangu, mtakumbuka kwamba mwezi Agosti mwaka jana ulizuka mtafaruku mkubwa kuhusu mazungumzo hayo pale CUF ilipobaini kwamba CCM haikuwa na nia ya dhati ya kuyakamilisha na kutekeleza yale tuliyokubaliana tokea hatua za awali kabisa za mazungumzo yasiyo rasmi. Mimi kwa niaba ya CUF nikatoa tamko tarehe 7 Agosti, 2007 kuiomba jumuiya ya kimataifa iingilie kati ili kuyanusuru mazungumzo yetu na kuiepusha nchi yetu na shari. Nilichukua hatua hiyo baada ya kuona tarehe 15 Agosti, 2007 ambayo Makatibu Wakuu wa CCM na CUF walikubaliana kuwa mazungumzo yawe yamekamilika inakaribia na hakuna dalili zote za kufanya hivyo huku CCM ikijikurupusha huku na kule kwa visingizio kemkem. Mwenyekiti mwenza wa CCM katika kamati ya mazungumzo alikuwa anadai kuwa kinyume na na uchaguzi wa mwaka 2000 na matukio ya 2001, safari hii CUF haina hoja kwa sababu hakuna mtu aliyekufa kwenye uchaguzi wa 2005. Katika jitihada za kuyanusuru mazungumzo haya nikiambatana na Mhe. James Mbatia, Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, niliwasiliana na viongozi wakuu wa dini akiwemo Muadhama Kadinali Polycap Pengo wa Kanisa Katoliki, Askofu Mstaafu Elinaza Sendoro wa Kanisa la Kilutheri Tanzania na Mufti Shaaban Simba wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) na kuwaomba wayaombee Mazungumzo ya CCM na CUF yanusurike na watumie nyadhifa zao kuhakikisha Rais Kikwete hayafanyii mzaha mazungumzo haya. Vile vile niliende Dodoma kuzungumza na aliyekuwa Makamu wa Mwenyekiti wa CCM Bara, Mhe. John Samuel Malecela na aliyekuwa Waziri Mkuu Mhe. Edward Lowasa kuwaomba watumie nyadhifa zao kuyanusuru mazungumzo.
Rais Jakaya Kikwete hatimaye akatoa tamko tarehe 14 Agosti, 2007 akiinasihi CUF ikubali kuendelea na mazungumzo hata baada ya kupita tarehe 15 Agosti iliyokuwa imekubaliwa kuwa yawe yamekwisha na akaahidi binafsi atayasimamia kuona yanafanikiwa. CUF ikaheshimu kauli ya Rais na ikakubali kuendelea na mazungumzo kwa sharti kwamba hatua zichukuliwe kuyakamilisha. Imepita miezi mingine saba baada ya ahadi hiyo ya Rais kabla ya mazungumzo hayo kukamilishwa.
Timu ya CUF iliporudi katika mazungumzo, ujumbe wa CCM ukawaeleza wenzao kuwa kwa vile makubaliano yanayotarajiwa kufikiwa yanahusu mambo makubwa, ni vyema CUF ikaonyesha ustahmilivu hadi umalizike Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM hapo Novemba, 2007 ili kumruhusu Rais Kikwete kujipanga vyema na safu mpya za Chama kuweza kukabili maamuzi mazito kwa maslahi ya taifa. CUF ikawakubalia tena.
Watanzania wenzangu, ni vyema mkaelewa kuwa ustahmilivu na uungwana huo uliokuwa ukionyeshwa na CUF haukutokana na kwamba labda CUF ni dhaifu bali ni maumbile ya chama chetu, misingi yake ya ukweli na uaminifu na kujali kwake amani ya nchi yetu. Ni bahati mbaya sana kwamba CUF ilikuwa ikiyazingatia haya mbele ya CCM, chama ambacho kinaamini katika hadaa, udanganyifu, upotoshaji, ubabaishaji na usanii wa kisiasa.
Waswahili wanasema njia ya mwongo fupi. Hatimaye Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ulimalizika na mazungumzo yakaendelea na yakahitimishwa katika kikao cha tarehe 25 – 29 Februari, 2008. Tukakubaliana kuwa sasa rasimu ya makubaliano yaliyohusu agenda zote zilizowasilishwa na kujadiliwa ifikishwe kwenye vikao vya juu vya vyama vyetu ili kuidhinishwa na kisha kupanga tarehe ya kutiwa saini makubaliano na utekelezaji kuanza.
Hii ilikuwa ni hatua ya mwisho ya utaratibu (formality) tu kwa sababu kila hatua ya mazungumzo na makubaliano, viongozi wakuu wa vyama vyetu na vikao vya juu vya vyama vyetu vilikuwa vinashirikishwa na kutoa miongozo yake. Yapo mambo mengi yakiwemo hata yale yanayohusu muundo wa Serikali Shirikishi ambayo yaliwahi kufikishwa mbele ya vikao na vikao hivyo vikaagiza marekebisho yafanywe na yakafanywa. Hatua ya mwisho ilikuwa ni kuyaweka pamoja tu katika rasimu ya makubaliano ili iidhinishwe, siyo kufungua upya mjadala wa mambo yaliyokuwa yameshakubaliwa.
aik
Watanzania na ulimwengu ni mashahidi kuwa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la CUF lilikutana na kuridhia makubaliano hayo tarehe 17 Machi, 2008. Timu ya CUF katika mazungumzo na CCM iliwasilisha taarifa ya mazungumzo kwa kusoma rasimu ya makubaliano ya CCM na CUF iliyokubaliwa na kupitishwa katika vikao vya kamati ya mazungumzo. Siyo kama hakukuwa na wajumbe wa Baraza Kuu la CUF ambao hawakutaka marekebisho katika makubaliano yaliyowasilishwa au waliokuwa wakiyakataa kabisa kwa kutowaamini CCM kutokana na uzoefu wa Muafaka wa Kwanza wa 1999 na Muafaka wa Pili wa 2001. Walikuwepo, lakini wajumbe wa timu ya mazungumzo ya CUF chini ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, na mimi nikiwa Mwenyekiti wa kikao, tulitumia busara na hekima zote kuwaeleza kwamba hatua ya sasa hairuhusu tena mabadiliko bali ni ya kuidhinisha tu kwa ajili ya kutiwa saini na utekezaji kuanza. Tulifanya hivyo kwa sababu misingi ya Chama chetu ni uungwana, ukweli, uaminifu na uadilifu.
Tulitarajia na CCM nayo kupitia vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama chao ingefanya hivyo. Kwa mshangao mkubwa, wetu na hata wa watu waadilifu na waaminifu wote wa hapa Tanzania na katika Jumuiya ya Kimataifa, tumeshuhudia CCM ikiyapiga teke makubaliano hayo. Huku wakitumia makada wao waliochoka wa propaganda zilizopitwa na wakati na mabingwa wa kisasa wa siasa za kisanii maarufu kama ’spin doctors’ wamekuja na hoja mpya ya kura ya maoni na pia wakisema wamefanya mabadiliko katika baadhi ya vifungu vya makubaliano.
Katika waraka walioupeleka Butiama, ambao CUF inao nakala yake, wanasema kwa kuibua hoja ambayo haikuwepo ya kura ya maoni, CCM itakuwa imeipiku CUF kisiasa.
“Liko wazo ambalo ujumbe wetu umelipata kutoka kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Aman Abeid Karume linalohusu uzito wa makubaliano juu ya kuanzisha mustakabali mpya wa kisiasa kwa msingi wa Serikali shirikishi (power sharing arrangement) katika Zanzibar. Yeye alikuwa na fikra kwamba jambo kubwa na la kutia matumaini kama hili isingefaa maamuzi yake yakahitimishwa na viongozi katika Kamati Kuu na NEC tu. Kwa vile wadau wakuu katika hili ni wananchi wenyewe wa Zanzibar, ingekuwa bora kama suala hili likafikishwa kwao. Sisi (yaani Katibu Mkuu, ndugu Yusuf Makamba, Ndugu Ali Ameir Mohamed na Ndugu Kinguge Ngobale- Mwiru) tulivutiwa sana na pendekezo hili na tuliliunga mkono. … Kwa kukubali wazo hili CCM itakuwa imeipiku CUF katika ubunifu wa kujenga.”
Katika hali ya kawaida, waraka huu usingeweza kufikishwa mbele ya vikao bila ya Mwenyekiti wa vikao kuuona na hivyo ni wazi kuwa Rais Kikwete aliijua hoja hiyo ya kura ya maoni tokea mapema, kama si kuwa ameshiriki hata kuiandaa. Halafu eti wanataka Watanzania wawaamini kuwa hoja hiyo iliibuliwa na wajumbe wa vikao. Rais Jakaya Kikwete na CCM yake wanafanya usanii wa kisiasa katika masuala mazito yanayohusu mustakbali wa taifa letu na maisha ya wananchi wetu.
HOTUBA YA RAIS KIKWETE NA UTETEZI WAKE
Kufuatia usanii huo wa Butiama, CUF ilitoa tamko rasmi kupitia Katibu Mkuu wetu, Maalim Seif Sharif Hamad, kuzikataa hoja zote mbili za CCM, ile ya kutaka mabadiliko ya yaliyokwishakubaliwa na ile ya kura ya maoni. Katibu Mkuu wa CUF alishatoa hoja zetu za kwa nini hatuzikubali hoja hizo lakini naomba nizirejee kwa ufupi hapa:
Kuhusu hoja ya CCM kutaka marekebisho katika yaliyokubaliwa.
Kwanza, CCM haikutaja ni maeneo gani inataka yafanyiwe marekebisho. Pili, hoja hii inashangaza kwa sababu wajumbe wa Kamati ya Mazungumzo kutoka upande wa CCM walikuwa wakiwaarifu wajumbe wa Kamati kutoka upande wa CUF kwamba wao walikuwa wakiwasilisha taarifa kwa kila hatua inayofikiwa katika vikao vya chama vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa na pia kwa viongozi wao wa juu, Rais Jakaya Kikwete na Mheshimiwa Amani Karume, na kupata maelekezo na miongozo inayohitajika. Hatua hii ya mwisho ilikusudiwa kubariki makubaliano hayo yaliyokuwa yakifikiwa hatua kwa hatua na siyo kufungua mjadala mpya kupitia duru mpya ya mazungumzo.
Kuhusu hoja ya CCM makubaliano yanapaswa kuridhiwa na wananchi wenyewe kwa njia ya kura ya maoni.
Muda wote wa mazungumzo ambayo yamechukua miezi 14 na yakiwa yamehusisha vikao 21, wajumbe wa Kamati ya CCM wanaoshiriki mazungumzo hawakuleta hoja hii ya kura ya maoni. Kama nilivyoeleza, pendekezo la kutaka kura ya maoni halikuwa limeibuliwa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM bali lilikuwemo katika Taarifa ya Kamati ya CCM inayoshiriki mazungumzo likiwa ni pendekezo walilotaka liridhiwe na Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa. Kitendo hicho cha Kamati ya CCM kuwasilisha kitu kipya nje ya makubaliano yaliyofikiwa ni upotoshaji mkubwa wa yale yaliyokubaliwa. Iwapo pendekezo hilo lina nia njema ya kuwashirikisha wananchi, kwa nini wajumbe wa Kamati ya CCM wasiliwasilishe katika vikao vya mazungumzo na badala yake wakaamua kuliingiza kama mtego wa kisiasa wenye lengo la “kuipiku CUF”?
Kufuatia Tamko hilo la CUF, Rais Jakaya Kikwete alikuja katika ukumbi huu huu wa Diamond Jubilee na kutoa kile alichokiita ufafanuzi wa maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuhusu Muafaka. Katika hotuba yake hiyo aliilaumu CUF kwa kile alichokiita ‘kukurupuka’ katika kutoa Tamko lake kabla ya kupata undani na msingi wa maamuzi hayo.
Inaonyesha Rais Kikwete alikuwa amesahau kauli aliyoitoa katika hotuba yake ya ufunguzi ya tarehe 28 Machi 2008 aliposema na ninanukuu
“kama ilivyo kawaida yetu, tutatoa taarifa kwa ukamilifu mwishoni mwa kikao kuhusu nini kimezungumzwa na nini kimeamuliwa.”
Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Mhe. Pius Msekwa alisoma Tamko la Halmashauri Kuu ya Taifa kuhusu Mazungumzo ya Mwafaka baina ya CCM na CUF. Kwa kuzingatia kauli ya Mwenyekiti wa CCM katika hotuba yake ya ufunguzi hapakuwa na sababu ya kusubiri mawasiliano toka kwa Katibu Mkuu kwani ilikuwa wazi kuwa CCM hawataki kutekeleza yale tuliyokubaliana.
Katika hotuba yake ya tarehe 2 Aprili 2008 Rais Kikwete alisema kwamba amemuagiza Katibu Mkuu wa CCM kumuandikia barua Katibu Mkuu wa CUF kuyaeleza hayo kwa undani. Barua hiyo imeletwa kwetu juzi Alhamisi, tarehe 3 Aprili, 2008 ikiwa haina chochote kati ya yale yaliyoahidiwa na Rais. Kwa hakika, tamko lililosomwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Tanzania Bara), Mhe. Pius Msekwa, lina maelezo yanayoeleweka kuliko barua iliyoletwa kwetu ambayo bahati nzuri si siri maana katika utaratibu mpya wa utendaji kazi wa CCM imeisambaza nakala yake kwa vyombo vya habari vyote.
Katika barua hiyo, ambayo nakala pia imeletwa kwangu, Mhe. Makamba anasema: “Sasa naomba nikuarifu rasmi kuwa Wajumbe wa Kamati ya Mazungumzo kwa upande wetu tuko tayari kukutana na Kamati yako ili kuwasilisha uamuzi na maelekezo ya Halmshauri Kuu ya Taifa kama tulivyokubaliana.“ Ndiyo kusema kuwa uamuzi na maelekezo hayo hayamo katika barua hiyo isipokuwa sasa yanatumiwa kuitega CUF kwamba ikubali kurudi katika vikao visivyokwisha na huko ndiko yatakakoelezwa. Ni wazi kuwa Rais Kikwete hakusema kweli aliposema maamuzi na maelekezo hayo yatawasilishwa katika barua ya Katibu Mkuu wa CCM kwa Katibu Mkuu wa CUF. Ni ule ule usanii wa kisiasa kwa mara nyingine tena.
Tumesikitishwa zaidi kupata taarifa kuwa katika mkutano ulioitishwa kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard Membe, na Mabalozi wote wa nchi za kigeni wanaowakilisha nchi zao hapa nchini juzi Ijumaa, tarehe 4 Aprili, 2008, Waziri Membe aliamua kuwafungia ngulai mabalozi hao kwamba eti maelezo kamili ya maeneo CCM inayotaka marekebisho katika rasimu ya makubaliano pamoja na utaratibu mzima wa vipi kura ya maoni iliyopendekezwa utakuwa, umeelezwa kwa kina katika barua ya Mhe. Makamba kwa Maalim Seif. Serikali inapofikia hatua ya kuwadanganya hata mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, hatuwezi kutegemea kuwa wakweli kwa CUF na kwa Watanzania.
Rais Kikwete aliwaeleza mabalozi katika hotuba yake ya kuukaribisha mwaka mpya (Sherry Party) Januari 2006 na ninanukuu:
“I will offer the authority of my office to promote, assist and facilitate an inter-party, broad dialogue on the best way to reduce the polarisation of politics in Zanzibar.” Kwa tafsiri ya kiswahili isiyo rasmi
Nitatumia madaraka ya ofisi yangu kuendeleza, kusaidia na kuwezesha mazungumzo mapana baina ya vyama ili kupata njia bora ya kupunguza mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Sherry Party ya Januari 2007 aliwaeleza mabalozi:
“We are serious about the multi-stake holder dialogue on Zanzibar. We are doing the final touches to the process. Please continue to be as supportive as you have been.” Ambayo tafsiri yake ni
Tuko makini kuhusu mazungumzo baina ya wadau Zanzibar. Tuko katika kumalizia mchakato huo. Tafadhalini endeleeni kutuunga mkono katika suala hili.
Na sherry party ya mwaka huu Rais kawaeleza mabalozi kuwa
“Muafaka talks between the Civic United Front (CUF) and the ruling party, Chama cha Mapinduzi (CCM), over the situation in Zanzibar, are nearing conclusion. Hopefully, this time around we will succeed in building a firm basis for relegating divisive politics in Zanzibar as a relic of the past. I want to thank you all for being supportive of the process and for understanding its complexities, and therefore the nature of its slow pace.” Tafsiri ya kauli ya Rais ni “Mazungumzo ya Muafaka kati ya the Civic United Front (CUF) na Chama tawala Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhusu Zanzibar yanakaribia kuhitimishwa. Ni matumaini yangu safari hii tutafaulu kujenga msingi imara wa kumaliza mpasuko wa kisiasa na kuufanya historia ya zamani. Nataka kuwashukuru nyie nyote kwa kutuunga mkono katika mchakato huu na kwa uelewa wenu wa ugumu wa tatizo lenyewe na ndiyo maana limechukua muda mrefu.”
Kinachosikitisha Rais anashindwa kuheshimu wadhifa wake na kutoa kauli nzito kwa mabalozi na viongozi wa mataifa mengine kimzaha mzaha bila ya kuwa na nia thabiti ya kutekeleza. Anayachukua mambo mazito ya nchi kama vile alivyoahidi kuwa Real Madrid watakuja kucheza mechi ya kufungua uwanja mwaka 2007 bila kujua gharama za kuwaleta Real Madrid na uwanja utakamilika lini. Bila shaka Watanzania tutamvumilia Rais wetu na usanii wake katika mambo ya mpira. Kuendeleza usanii katika mambo mazito ya Muafaka na kuwahadaa mabalozi kunahatarisha amani ya nchi yetu na kulivunjia heshima taifa letu.
Katika hotuba yake ya tarehe 2 April 2008, Rais ameeleza kuwa
“Halmashauri Kuu iliona haja ya kufanya marekebisho fulani fulani katika baadhi ya mapendekezo hasa kuhusu mapendekezo ya muundo wa Serikali Shirikishi. Shabaha ya mapendekezo hayo ni kuboresha na kuimarisha mfumo huo unaopendekezwa. Marekebisho yanapendekezwa kwenye utaratibu wa uteuzi wa Wasaidizi Wakuu wawili wa Rais wa Zanzibar na Baraza la Mawaziri. Marekebisho mengine yanahusu pendekezo la kuwepo Baraza la Usuluhishi. “
Waheshimiwa wananchi pendekezo la Muundo wa Serikali Shirikishi lilitolewa na timu ya CCM katika kamati ya mazungumzo. Timu ya CCM ilieleza mapendekezo hayo yanatokana na mashauriano waliyoyafanya na Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete na Makamu wake Mhe. Aman Abeid Karume. Mapendekezo ya CUF ilikuwa kugawa nyadhifa za Rais na Waziri Kiongozi kati ya vyama vitakavyokuwa vimepata kura zilizokaribiana katika kura za Rais. CUF ikatoa concession, ikaachia pendekezo lake na kulikubali pendekezo la CCM. Pendekezo la kwanza la CCM ilikuwa pawepo na Makamu mmoja wa Rais. CUF ikaridhia. Baadaye wakabadilisha kuwepo makamu wawili wa Rais. CUF tukawakubalia. Rais anaeleza kuwa NEC inataka kulifanyia marekebisho pendekezo lililoletwa na ujumbe wa CCM baada ya kupokea ushauri wake na wa Makamu wake. Sisi tuwaeleweje CCM? Kama hii siyo mbinu na usanii wa kupoteza muda na kufanya mazungumzo yasiyokwisha ni kitu gani?
Katika kutapatapa na kujitetea, Rais Kikwete amesema kwamba eti yeye ni mwanademokrasia sana na hivyo aliamua kuruhusu mjadala wa wazi kuhusu suala hilo kusudi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa watoe maoni yao kwa uwazi. Akajigamba kwamba huo ndiyo utaratibu wa CCM. Lakini akashindwa kutueleza Watanzania kuwa iwapo huo ndio utaratibu wake na wa CCM, kwa nini hakuruhusu mjadala wa wazi na wa kidemokrasia katika vikao hivyo hivyo kuhusu mafisadi wa Richmond na fedha za akaunti ya nje ya Benki Kuu ya Tanzania, ambao inadaiwa ni marafiki zake wa karibu kisiasa.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete aliitaja mifano ya nchi kadhaa zilizotumia utaratibu wa kugawana madaraka kama njia ya kumaliza migogoro ya kisiasa kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda, Afrika Kusini na hata Kenya. Nilikuwa na hamu ya kumsikia akitutajia angalau mfano mmoja wa nchi iliyopiga kura ya maoni katika kuidhinisha makubaliano ya kumaliza mgogoro wa kisiasa kama ambavyo chama chake chini ya uongozi wake kimeamua kuhusu Zanzibar. Aliporudi kutoka Kenya, alijisifu sana kwamba ameweza kufanikisha kufikiwa makubaliano ya kugawana madaraka kati ya ODM na PNU, lakini hakutwambia kwa nini hakuwapa wazo la kura ya maoni ili wananchi wayaridhie makubaliano hayo.
Katika maamuzi mazito yaliyofanywa na CCM, TANU na ASP hakuna hata mara moja kura ya maoni ilitumiwa. Mwaka 1964, Tanganyika na Zanzibar ziliungana, hapakuwa na kura ya maoni. Mwaka 1965 mfumo wa vyama vingi vya siasa ulifutwa hapakuwa na kura ya maoni. Mwaka 1977 vyama vya TANU na ASP viliunganishwa, hapakuwa na kura ya maoni ya wanachama TANU na ASP. Kamati iliyounganisha vyama ikapewa kazi ya kuandika katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hapakuwa na kura ya maoni. Katiba ya Zanzibar ya kwanza ya 1979 na1984 haikupigiwa kura ya maoni. Waliodai kuwepo kura ya maoni kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar katika miaka ya mwishoni ya 1980 waliambiwa wamechafua hali ya hewa ya kisiasa na kuwekwa kizuizuni. Tuliporejea katika mfumo wa vyama vingi hapakuwa na kura ya maoni. Katika mabadiliko ya katiba ya 11 yaliondoa nafasi ya Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jambo ambalo ndiyo msingi wa mkataba wa kimataifa wa Muungano wa dola mbili wa 1964. Jambo hili linaloidhalilisha Zanzibar lilipingwa na Wazanzibari wakiwemo wana CCM, hapakuwa na kura ya maoni.
Katiba ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano haina kipengele chochote kinachoelezea kufanya maamuzi yeyote kwa kutumia kura ya maoni. Tanzania haina sheria ya kura ya maoni. Rais hakueleza kura ya maoni itakapopigwa itakuwa ya maamuzi ya mwisho au ni ya ushauri? Kama ni ya mamuzi ya mwisho, Katiba ya Zanzibar inaeleza kuwa Baraza la Wawakilishi ndilo lenye mamlaka ya kufanya marekebisho ya katiba. Au kwa kuwa CCM wamezoea kuvunja Katiba basi suala hili haliwapi shida? Kama ni ya ushauri kwa nini kupoteza gharama kubwa ya kura ya maoni kwa maamuzi ambayo siyo ya mwisho?
Kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa wanadai kushiriki kuandika katiba mpya yenye misingi imara ya demokrasia, CCM wamekataa kata kata. Bila kuona haya sasa wanadai kupanua demokrasia kwa kuitisha kura ya maoni kuwa ndio njia yakutatua mgogoro wa kisiasa Zanzibar.
Katika ufunguzi wa Mkutano wa Butiama, Rais Kikwete alisema wamekutana Butiama kuiweka “hai kumbukumbu ya Mzee wetu hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.” Hata hivyo CCM imeendelea kudharau ushauri wa Mwalimu Nyerere alioutoa mwaka 1995 kuwa suluhisho la Zanzibar ni serikali ya umoja wa kitaifa. Rais Kikwete alimnukuu Rais wa zamani wa Marekani, John F. Kennedy, aliyesema: “mifano ya watu mashuhuri huzaa watu wa kiwango hicho”. Kuja hapa kutatupa ari ya kuishi na kutumikia taifa na watu wake kwa mfano wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tulitegemea Rais ataiga alau mfano wa Mwalimu alivyokuwa akiendesha vikao vya CCM. Katika hotuba yake ya Aprili 2 inaonyesha wazi kuwa Uenyekiti wake ni dhaifu na hana dira wala msimamo. Mfano wa Uenyekiti wa Mwalimu Nyerere haujazaa Mwenyekiti wa CCM mwenye kiwango alau cha asilimia tano ya kiwango chake. Kwa Rais Kikwete kujikweza kuwa anafuata mikoba ya Mwalimu kama nukuu ya maneno ya JFK inavyolenga ni kuidhalilisha kumbu kumbu ya Baba wa Taifa.
Kwa ufupi, hotuba ya Rais Kikwete haikuwa na jipya ambalo lingetufanya CUF kufikiria upya msimamo wetu uliotolewa kupitia Katibu Mkuu wetu. Kama kuna jipya basi ni ule usanii wa Rais Kikwete wa kukanusha kufanya usanii kwa kisiasa kwa kurejea tena usanii wa kisiasa. Sasa ni rasmi kwamba Tanzania yetu inaongozwa na watu wanaosimamia usanii wa siasa na ufisadi wa uchumi. Watanzania tuna sababu na haki ya kutaka mabadiliko ili kuipatia nchi yetu uongozi makini unaohitajika kufanya maamuzi makini yanayohusu mustakbali wetu.
MUSTAKBALI WA MAKUBALIANO YETU:
Napenda nimalizie kwa kusema kuwa baada ya kumsikia Rais Jakaya Kikwete, na iwapo kweli anataka tumuamini tena kwamba dhamira yake katika kuumaliza mgogoro wa kisiasa Zanzibar iko pale pale, basi CUF iko tayari kumsaidia kwa kukubaliana na mojawapo ya njia hizi mbili:
CCM ikubali kuheshimu makubaliano yaliyofikiwa na Kamati ya Mazungumzo ya vyama vyetu viwili na endapo kweli Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho “imeyakubali kimsingi” makubaliano yaliyofikishwa kwake kama ilivyosema taarifa yake, basi ikubali kutia saini makubaliano hayo na utekelezaji wa yaliyokubaliwa uanze mara moja.
Kama kuna haja ya kutafakari maeneo hayo machache ambayo CCM inataka marekebisho, basi kwanza Rais Kikwete atembee juu ya maneno yake kwa kumuagiza Katibu Mkuu ayawasilishe kwa CUF maeneo hayo yakiwa na maelezo ya kina. Baada ya hapo, kama alivyofanya Kenya kwa kuwaweka pamoja Rais Mwai Kibaki na Mheshimiwa Raila Odinga kuhitimisha makubaliano, basi atumie kipaji chake na uwezo wake huo kuwaweka pamoja wadau wakuu wa masuala haya ambao ni Mheshimiwa Amani Karume na Maalim Seif Sharif Hamad kuhitimisha makubaliano hayo. Kwa njia hii, hata ile hoja inayojaribiwa kujengwa sana katika siku za karibuni kwamba viongozi wa CCM Zanzibar ndiyo kikwazo kwa kuwa hawashirikishwi katika maamuzi yanayoihusu Zanzibar na kwamba ndiyo waliokwamisha ‘nia njema’ ya Rais Kikwete itakuwa imeondoka.
Pendekezo la kufanya kiini macho cha kura ya maoni yenye lengo la kuchelewesha utiaji saini na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa HALIKUBALIKI KWA CUF.
Nawashukuru kwa kunisikiliza. Ahsanteni sana.
HAKI SAWA KWA WOTE
Dar es Salaam
06 Aprili, 2008
No comments:
Post a Comment