Monday, April 14, 2008

Serikali ya mseto si suluhu ya matatizo Zanzibar

INASIKITISHA kuwa watu wameanza kubishana juu ya jambo ambalo hata kama wakikubaliana na kulitekeleza kama lilivyo, haliwezi kuwa suluhu ya matatizo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi yanayoikabili Zanzibar hivi sasa. Achilia mbali mlolongo wa migogoro iliyosababisha kukua kwa mpasuko visiwani humo, hivi sasa wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wa Chama cha Wananchi (CUF) wapo katika malumbano makubwa, kuhusiana namna ya kutekeleza makubaliano ya kuunda serikali ya mseto, kama moja ya dawa za kumaliza mpasuko huo, zilizokubaliwa katika mazungumzo yaliyofanywa na kamati iliyowakilisha vyama hivho.

Malumbano ya sasa yanayokana na msimamo wa CCM, ilioibuka katika vikao vyake vya juu vilivyofanyika hivi karibuni kijijini Butiama, mkoani Mara.

Matatizo ya Zanzibar yalianza tangu zamani lakini malumbano ya sasa, inaaminika kuwa yametokana na uamuzi wa CCM kubadilisha makubaliano ya namna ya kuundwa kwa serikali ya mseto. Wakati kwa mujibu wa rasimu moja pendekezo ni kuunda serikali hiyo mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, inadaiwa kuwa CCM imechomeka kipengele kinachopendekeza kufanyika kwa kura ya maoni kama sehemu muhimu ya kuushirikisha umma kuamua juu ya hatma ya mfumo wa utawala visiwani humo.

Lakini ieleweke kuwa tatizo hili halikuanzia na CCM kama wengi tunavyodhani na kuamini. Tatizo (hili la sasa) lilianzishwa na CUF bila ya wao wenyewe kujua kuwa wanatengeneza tatizo.

CUF ililianza tatizo hili pale ilipoamua kutangaza makubaliano ya mazungumzo peke yao bila kuwashirikisha wenzao wa CCM. Hili lilikuwa ni kosa la kiufundi na ndio maana Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, alipotakiwa atoe maoni yake kuhusiana na tamko hilo la CUF, yeye alikataa akisema kuwa hilo lilikuwa ni tamko la CUF. Alijiepusha hata kusema tu kuwa yaliyotangazwa na chama hicho ni sehemu ya makubaliano waliyoyafikia, alisisitiza kuwa hilo ni tamko la CUF!

Kwa kuonyesha kuwa alikuwa anamaanisha kuwa hilo lilikuwa tamjko la CUF, Makamba aliwataka wote wanaohoji wasubiri vikao vya juu vya CCM, kwa kuwa ndivyo vitakavyotoa maamuzi kuhusiana na muafaka wa Zanzibar .

CCM ilipokaa Butiama liliibuka na pendekezo la kura ya maoni ambalo CUF imeanza kulipinga kwa nguvu zote kwa maelezo kuwa halikuwa sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa. Wakati nyaraka zimevuja kutoka katika vikao vya CCM zikionyesha kilichowasilishwa na Makamba kama rasimu ya makubaliano, CUF nayo imesambaza nyaraka nyingine, ikidai kuwa hiyo ndiyo rasimu halisi ya makubaliano. Katika hali kama hii ni vigumu sana kuamini ipi ni nyaraka halisi.

CUF wamelifanya jambo hilo liwe gumu kwa haraka yao ya kutaka kuipiga pini CCM na kuamua kutangaza makubaliano haraka bila kuwashirikisha wenzao. Katika kufanya hivyo, CCM sasa ina nguvu ya kuiruka CUF kimanga na kusema kuwa ilichokitangaza chama hicho ni chake chenyewe na wala CCM haihusiki nacho. Huu ni mwanzo wa mgogoro mwingine ambao nao unaongeza mpasuko ambao Rais Jakaya Kikwete alidhamiria kuumaliza kupitia mazungumzo hayo.

Lakini wapo ambao walishangilia nab ado wanaamini kuwa kuundwa kwa serikali ya mseto ndio suluhu ya matatizo ya Zanzibar . Hawa, naamini kuwa wakati walipoliangalia tatizo linaloikabili Zanzibar leo hii, walipofushwa na kile kinachotokea hivi sasa, bila kuchunguza kwa kina na sababu ya hayo yanayotokea.

Ni kweli kuwa serikali ya mseto inaweza kuwa sehemu ya dawa ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar , lakini siamini kuwa aina ya serikali iliyopendekezwa, (ambayo imefafanuliwa katika nyaraka zote mbili za rasimu ya makubaliano) inaweza kuwa ndiyo dawa yenyewe. Wala siamini kuwa serikali ya aina hiyo inaweza kuwa dawa katika mazingira yaliyopo sasa.

Mfumo wa utawala unaopendekezwa katika serikali hiyo ya mseto Zanzibar ni wa kuwa na rais atakayesaidiwa na manaibu wawili, wakati nafasi ya Waziri Kiongozi ikifutwa. Kwa mujibu wa rasimu hizo na maelezo ya wanasiasa waliohusika katika mazungumzo hayo na wasioshiriki, rais atatokana na chama kitakachoshinda uchaguzi.

Chini yake atakuwa na makamu wa kwanza, ambaye atatokana na chama kitakachoshika nafasi ya pili katika idadi ya kura katika uchaguzi. Huyu atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa rais ambaye atamsaidia katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa kila siku wa kazi za serikali. Pia huyu atakaimu nafasi ya urais wakati rais atakapokuwa nje ya nchi.

Kwa kuwa hakuna kipengele cha makamu wa rais katika katiba ya Zanzibar , imeazimiwa kuwa katika mabadiliko ya katiba ya Zanzibar yatakayofanyika, maudhui ya ibara ya 47 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano yaingizwe katika katiba ya Zanzibar .

Katika utekelezaji wa kazi za serikali, haiwezekani kwa rais na makamu wa rais wa kwanza wakaw wanatekeleza sera, mipango, programu na mikakati tofauti. Ni lazima wawe wanafanya kitu kimoja. Je, inaeleweka sera zitakazokuwa zinatekelezwa ni zile za chama cha rais au makamu wake?

Pia kutakuwa na makamu wa pili wa rais ambaye atatoka katika chama cha rais. Atakuwa kiongozi wa shughuli za serikali katika Baraza la Wawakilishi. Atakaimu urais wakati rais na makamu wa kwanza hawapo nchini.

Kama kweli haya ndiyo makubaliano, nayaona yana matatizo kadhaa ambayo yatasababisha matatizo zaidi ya yaliyopo hivi sasa iwapo yatakubaliwa kama yalivyo.

Kwanza, madaraka ya rais yatakuwa kama yalivyoainishwa katika katiba ya sasa ya Zanzibar kupitia ibara za 51, 52 na 53. Ajabu na kweli! Hivi hatujawahi kulalamika katika nchi hii kuwa katiba zetu zinawapa watawala wa juu kabisa madaraka makubwa kiasi cha kuwafanya wawe madikteta iwapo wataamua kuyatumia ipasavyo?

Iwapo katiba hiyo hiyo tuliyowahi kuilalamikia ndiyo itakayoendelea kutoa madaraka ya rais, hivi huyo makamu wake, atakayetokana na chama kitakachoshika nafasi ya pili kwa idadi ya kura, atakuwa na nafasi kweli ya kufurukuta? Au atakuwa kama kibaraka wa rais wa chama kilichoshinda uchaguzi?

Hivi rais huyu atakapoamua kuyatumia madaraka hayo dhidi ya makamu wake, nini kitamzuia? Kwa sababu atakuwa anatekeleza matakwa ya katiba. Kinachochukuliwa kama zawadi hapa ni kuwa watanzani ni mabingwa wa kutotekeleza katiba,hivyo inaaminika tu kuwa utamaduni huo utaendelea. Lakini tufahamu kuwa huu ni mchezo wa saisa.

Pili, sioni ni namna gani, katika mazingira ya Zanzibar , chama kitakachopata nafasi ya makamu wa kwanza wa rais, kiache kuhubiri sera zake na kijikite katika si tu kuhubiri, bali kutekelza pia sera za chama hasimu. Sioni urahisi wa CUF kukubali kutekelza sera za CCM au CCM kutekeleza za CUF katika mazingira yaliyopo sasa Zanzibar .

Tatu, kiongozi wa shughuli za serikali anapaswa kuwa mmoja ili kutoleta mgongano katika kinachofanywa na serikali. Katika makubaliano haya, makamu wa kwanza wa rais na yule wa pili watakuwa na jukumu la kuwa wasimamizi wa shughuli za serikali lakini maeneo mawili tofauti.

Makamu wa kwanza atakuwa akifuatilia utekelezaji wa kila siku wa kazi za serikali nje ya Baraza la Wawakilishi wakati makamu wa pili atahusika na kuangalia maslahi ya serikali katika Baraza.

Hapa naona kuna naibu mmoja anataka kufanywa kanyaboya. Na kwa kuwa makamu wa pili wa rais atatokana na chama kilichoshinda, ambacho ndicho kilichotoa rais, ninaweza kubashiri kwa uhakika kabisa kuwa makamu wa kwanza wa rais anaweza kufanywa kuwa kama kanyaboya.

Nne, kutokana na ukubwa wa Zanzibar na uwiano wake na idadi ya watu, nadhani mfumo huu utaleta serikali kubwa ambayo itakuwa mzigo mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ). Ikumbukwe kuwa hata katika serikali ya Muungano, Rais Kikwete alikiri wakati alipounda Baraza jipya la Mawaziri mwezi Februari kuwa kati ya vitu alivyokuwa amevifikiria katika kuunda baraza hilo , ni ukubwa wake.

Kwa hali ya Zanzibar , sioni ni kwa namna gani itaweza kuhimili serikali kubwa namna hii.

Tano, sidhani kuwa kinachotakiwa ili kumaliza mpasuko huo ni kuwapa watu madaraka. Kama lengo litakuwa kuwapa watu madaraka, hilo nalo litazaa matatizo mengine kwa sababu atakayepewa madaraka atataka kuonyesha nguvu za madaraka yake.

Katika mazingira niliyoonyesha kuwa baadhi ya viongozi wanaweza kuwa kama kanyaboya tu, ubingwa huo wa kutaka kuonyesha madaraka katika mazingira ya ukanyaboya, yatasababisha misuguano itakayopanua zaidi mpasuko.

Sita, ni suala laujumla zaidi. Ili kuleta maelewano, ninaamini kuwa kikubwa kinachotakiwa ni viongozi kuonyesha utayari na hiari (will) yao ya kufanya kile kitakachokubaliwa. Hili limekosekana tangu hapa mwanzoni na mabishano tunayoyashuhudia na tuhuma kuwa rasimu imebadilishwa, ni dalili za wazi za kukosekana kwa utayari wa viongozi.

Inatisha kuwa hilo limejitokeza katika hatua ya kufikia makubaliano kabla hatuajakubaliana na kuanza safari ya utekelezaji. Ni vigumu kufikiria hali itakuwaje watakapokubaliana na kuanza safari ya kutekeleza makubaliano hayo wakati katika hatua ya kufikia kukubaliana tu wanabishana namna hii?

Haraka ya CUF kutaka kuundwa kwa serikali ya mseto mara baada ya makubaliano hayo kusainiwa, na mbinu za CCM kutaka kuchelewesha utekelzaji wa makubaliano hayo, ni ishara nyingine ya kukosekana kwa utayari wa vyama hivyo kumaliza matatizo Zanzibar .

Saba, sioni ni namna gani serikali ya mseto itafanya kazi katika mazingira ya kutoaminiana yaliyopo Zanzibar hivi sasa. Ikimbukwe kuwa haraka ya kutaka kutekeleza kile kinachoonekana kuwa ndio suluhu, bila kuandaa mazingira yatakayofanikisha utekelezaji wa hilo lililoafikiwa, kunaweza kusababisha kushindwa kwa makubaliano hata kama kilichokuwa kimekubaliwa kweli ni dawa ya matatizo hayo.

Hili ni kama lile linalotokea Kenya hivi sasa. Baada ya Rais Mwai Kibaki na Raila Odinga kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja, watu walifanya haraka ya kushangilia kuwa hatimaye suluhu imepatikana, bila kujiuliza iwapo mahasimu hao walikuwa wamejiandaa namna gani kutachana na misimamo mikali waliyokuwa nayo saa chache tu kabla ya kufikia makubaliano?

Kinachotakiwa kuanza kufanywa Zanzibar , kama njia ya kuelekea katika suluhu ya kweli, wala si haraka ya kuunda serikali ya mseto. Pamoja na kuwa matatizo ya Zanzibar ni ya kihistoria, lakini tatizo lililopo hivi sasa linatokana na kutokubalika kwa matokeo ya chaguzi, hasa baadaya ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Tunaweza tusirudi sana kwenye historia ya zamani na kuamua kuanza kuiangalia historia ya sasa katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hili.

Kwanza itafutwe namna ambayo itahakikisha kuwa chaguzi si tu zinakuwa huru na haki, bali zionekane kuwa ni huru na haki. Tukiweza kufikia mazingira kama hayo, kila mgombea ataweza kukubaliana na matokeo ya uchaguzi hata kama atashindwa kwa kura moja.

Katika mazingira ya kuamini hivyo, hatutahitaji serikali ya mseto kwa sababu atakayeshindwa atakuwa anajua kuwa ameshindwa kwa haki, hivyo hatokuwa na sababu wala kitu cha kulalamikia. Atabaki kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi ujao.

Kukosekana kwa mazingira ya uchaguzi huru na wa haki Zanzibar ni kikwazo kwa serikali ya mseto itakayoundwa. Hata kama itakubaliwa kuwa serikali ya mseto ianze sasa, mpaka utakapofika wakati wa uchaguzi, viongozi waliopo katika serikali ya mseto watakuwa wameshagongana sana kuhusiana na hili la marekebisho ya taratibu za uchaguzi kiasi kwamba hawatakuwa tena serikali moja halisi. Itakuwa ni serikali moja ambayo kila upande una mambo yake. Huo si aina ya mseto utakaoisaidia Zanzibar .

Pamoja na kuwa CCM imependekeza kura ya maoni, inapaswa kufahamu kuwa chimbuko la migogoro ya sasa ni sanduku la kura. Hivyo, kuweka mazingira ya kupiga kura kama njia ya kupata jawabu la matatizo yaliyotokana na upigaji kura, ni kurudia kosa kabla hujatafuta dawa ya kosa la awali.

Hata kama pendekezo la kura ya maoni litakubalika, inapaswa kwanza yaandaliwe mazingira ambayo yataifanya kura hiyo ionekane na wote kuwa ni huru na ya haki, kinyume na hayo, tutakuwa tunaandaa mgawanyiko mwingine.

Yapo matatizo mengi yanayoikabili Zanzibar katika nyanja mbalimbali lakini ufunguo wa hayo upo katika kukubalika kwa matokeo ya chaguzi. Hilo ndilo linapaswa kufanywa sasa kwani litazaa serikali, iwe ya mseto au vinginevyo, itakayokuwa na uhalali wa kuanza kuyashughulikia matatizo mengine bila ya kukumbana na vikwazo.

No comments: