AJALI nyingine mbaya imetokea leo mkoani Morogoro na watu 12 wamepoteza maisha yao. Ajali hiyo, iliyotokea katika kipindi cha wiki moja tangu itokee ajali nyingine iliyosababisha vifo vya watu 18, nayo ililihusisha basi pamoja na malori mawili.
Ajali hiyo ilitokea huko gairo majira ya saa 4 asubuhi wakati basi hilo la kampuni ya Al-Hushoom likielekea Dodoma kutokea Morogoro.
Malori yaliyohusika yote yalikuwa yakitokea Dodoma kuelekea Morogoro. Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Thobias Andengenye alisema kuwa ajali ilitokea wakati lori moja lilipokuwa linalipita loji jingine na ghafla likakutana na basi hilo.
Katika harakati za kulikwepa basi, dereva wa lori alilivaa trela la lori jingine ambalo lilikatika na kuligonga basi.
Waliofariki wanajumuisha wanaume wanane na wanawake wanne. Hadi hivi sasa marehemu waliotambuliwa ni pamoja na watawa wawili wa shirika la Carmelite la Kanisa Katoliki Kihonda, ambao ni Renatha Joseph na Anitha Bay, dereva wa basi Thomas Magosha, Khalid Mahai na Rehema Mzuwanda, mkazi wa Manispaa ya Morogoro.
Watu 32 walijeruhiwa na isipokuwa mmoja ambaye amelekwa Morogoro, wengine wamelazwa katika hospitali ya misheni ya Berega, iliyopo Gairo wilayani Kilosa na mmoja. Charles Kalekwa (39) ndiye aliyekimbizwa hospitali ya Mkoa kwa matibabu zaidi.
Hii ni ajali ya pili ndani ya wiki moja katika barabara hiyohiyo baada ya siku chache zilizopita watu wanane kufariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka wilayani kahama kuelekea Dar es Salaam kukwaruzana na lori. Watu 16 walijeruhiwa.
No comments:
Post a Comment