Thursday, May 8, 2008

Serikali haina shida na Ballali

SERIKALI imesema haimtafuti aliyewahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Daudi Ballali, ambaye mapema mwaka huu alifutwa kazi na Rais Jakaya Kikwete kutokana na kubainika kwa wizi wa mamilioni ya shilingi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salvatory Rweymamu, amesema kuwa serikali haina shida yoyote na Ballali kwa hivi sasa.

Alisema kutokuwepo nchini kwa Ballali, au kutojulikana alipo, si jambo linaloisumbua serikali kwa sasa kwa sababu hivi sasa Ballali ni raia wa kawaida, hivyo anao uhuru wa kuishi popote anapopenda.

Hata hivyo, alisema kuwa serikali ina mkono wa serikali, hivyo haitashindwa kumpata itakapomuhitaji wakati wowote.

Akifafanua zaidi, alisema baada ya kutenguliwa kwa uteuzi wake, serikali iliunda timu ya kuwachunguza watuhumiwa wa EPA, kuhakikisha fedha zilizoibwa zinarudi na kuwachukulia hatua waliohusika, akiwemo Ballali.

Mkurugenzi huyo pia alikiri kwamba serikali haifahamu hospitali aliyokuwa akitibiwa Ballali, licha ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mustafa Mukulo, kukaririwa akisema alimtafuta Ballali bila mafanikio alipokuwa jijini Washington, Marekani.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alitengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa BoT, baada ya taarifa ya uchunguzi wa hesabu uliofanywa na Kampuni ya Ukaguzi ya Ernst & Young na kubaini ubadhirifu wa zaidi ya sh bilioni 133.

Taarifa hiyo ilibaini kuwapo kwa kampuni hewa 22 zilizolipwa mamilioni ya fedha kutoka kwenye akaunti hiyo kati ya mwaka 2005 na 2006.

Hata hivyo, ilibainika kwamba, baadhi ya kampuni hizo zilidanganya kuhusu usajili na wamiliki wake huku nyingine zikimilikiwa na vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wengine wakitumia nyaraka za kughushi kuiba mabilioni hayo.

Mbali na udanganyifu huo, fedha za EPA zinadaiwa kusaidia kampeni za CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

No comments: