Wednesday, May 21, 2008

Ballali afariki

(Habari hii ni kwa hisani ya Tanzania Daima)

*Kuzikwa huko huko Marekani Ijumaa hii
*Serikali kutoa taarifa rasmi ya msiba leo
*Baadhi wanahofia huenda alilishwa sumu

Na Absalom Kibanda


ALIYEKUWA Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) amefariki dunia mwishoni mwa wiki nchini Marekani, Tanzania Daima imethibitisha.

Habari ambazo gazeti hili limezipata kutoka Marekani na Dar es Salaam zinaeleza kwamba, Ballali alifariki dunia Ijumaa iliyopita nyumbani kwake Washington alikokuwa akiishi.

Jamaa wa karibu wa Ballali walioko Dar es Salaam na Washington walilithibitishia Tanzania Daima kuhusu kutokea kwa msiba huo.

“Ni kweli amefariki nyumbani kwake Ijumaa usiku. Na sasa hivi tuko katika maandalizi ya kwenda funeral home (taasisi ya kuandaa shughuli zote za mazishi) kwa ajili ya kuanza kufanya maandalizi kwa ajili ya msiba,” alisema ndugu wa karibu wa Ballali kutoka Washington.

Habari zaidi zinaeleza kwamba, tayari familia ya gavana huyo wa zamani wa BoT imeshaitaarifu serikali kuhusu kutokea kwa msiba huo na kwamba taarifa rasmi kuhusu kifo hicho zitatolewa leo hii.

Ndugu mwingine wa karibu wa Ballali aliyezungumza na Tanzania Daima majira ya saa 4:00 usiku jana alisema mazishi ya gavana huyo wa zamani wa BoT yanatarajiwa kufanyika Ijumaa hii huko huko Marekani.

Mmoja wa wanasiasa aliye karibu na familia ya Ballali aliyezungumza na Tanzania Daima jana alithibitisha pia kupokea taarifa za kifo cha Ballali kutoka kwa mkewe, Anna Muganda.

Ndugu mmoja wa Ballali alipoulizwa na Tanzania Daima sababu za kushindwa kutangazwa kwa taarifa za kifo hicho mapema alisema walilazimika kufanya hivyo ili wapate fursa ya kuwasiliana na serikali kwanza na kisha ndugu, jamaa na marafiki wa familia yao kabla ya habari hizo kusambazwa.

Kifo hicho cha Ballali ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Jakaya Kikwete Januari mwaka huu zimekuja siku chache tu baada ya serikali kupitia Ofisi ya Rais Ikulu kutangaza kwamba ilikuwa haimtafuti gavana huyo wa zamani wa BoT.

Baadhi ya jamaa za Ballali waliozungumza na Tanzania Daima walisema kulikuwa na wasiwasi kwamba kifo cha gavana huyo wa zamani wa BoT kikawa kikawa si cha kawaida.

“Kuna wasiwasi kwamba huenda alilishwa sumu wakati akiwa nchini mwaka jana na hili limekuwa likizungumzwa sana ndani ya familia,” alisema mmoja wa jamaa za karibu wa Ballali aliyezungumza na Tanzania Daima jana.

Taarifa za kuwapo kwa wasiwasi wa Ballali kulishwa sumu zilipata kusikika mwaka jana na wakati fulani ilielezwa kwamba alipelekwa Marekani kwa matibabu kutokana na sababu hizo.

Tamko hilo la serikali lilitolewa mbele ya waandishi wa habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Salvatory Rweyemamu.

Rweyemamu alisema kuwa serikali ina mkono mrefu na iwapo itafikia hatua ya kumtafuta gavana huyo wa zamani wa BoT ili aje atoe maelezo yake kuhusu wizi wa zaidi ya shilingi bilioni 133 uliogundulika katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) haitashindwa kamwe kumfikia alipo.

Alisema kutokuwepo nchini kwa Ballai, au kutojulikana alipo, si jambo linaloisumbua serikali kwa sasa kwa sababu hivi sasa yeye ni raia wa kawaida, hivyo anao uhuru wa kuishi popote anapopenda.

“Serikali haimtafuti Ballali (kwa sasa), lakini ikiamua kufanya hivyo haitashindwa. Kwanza ni private citizen (raia huru) siyo mwajiriwa wa serikali tena,” alisema Rweyemamu na kuongeza kuwa, mkono wa serikali ni mrefu hautashindwa kumpata Ballali iwapo itamhitaji.

Akifafanua zaidi, alisema baada ya kutenguliwa kwa uteuzi wake, serikali iliunda timu ya kuwachunguza watuhumiwa wa EPA, kuhakikisha fedha zilizoibwa zinarudi na kuwachukulia hatua waliohusika, akiwemo Ballali.

Alisema: “Ninachofahamu ni kwamba, timu iliyopewa kazi kuhusu ubadhirifu wa EPA inaendelea na kazi yake na tunaona jinsi fedha zinavyorudishwa.”

Mkurugenzi huyo pia alikiri kwamba serikali haifahamu hospitali aliyokuwa akitibiwa Ballali, licha ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo, kukaririwa akisema alimtafuta Ballali bila mafanikio alipokuwa jijini Washington, Marekani.

“Kwa kweli sifahamu hasa Ballali alikuwa akitibiwa katika hospitali gani, lakini najua alikuwa nchini Marekani katika Jimbo la Boston, ila hospitali kwa kweli siijui.

“Lakini huyu ni mtu huru hivyo anaweza kuishi popote… huyu ana nyumba yake nchini Marekani… yupo huko anaishi na familia yake,” alisisitiza Rweymamu katika ufafanuzi wake.

Wiki iliyopita, ikiwa ni siku chache tu baada ya taarifa hiyo ya Ikulu, vyombo kadhaa vya habari viliandika habari zilizokuwa zikieleza kuwa makachero kutoka hapa nchini, walikuwa wamekwenda nchini Marekani katika miji ya Boston na Washington kufuatilia nyendo na maisha ya gavana huyo wa zamani.

Kwa mujibu wa habari hizo, ambazo zilikariri taarifa za ndani kutoka serikalini, makachero hao walikuwa wamekwenda huko ili kujua mahali anakoishi ili wakati wa kumhitaji utakapofika iwe rahisi kumpata.

Ballali aliondoka nchini, Agosti mwaka jana kwenda Marekani kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kwa matibabu, na tangu wakati huo taarifa zake zilikuwa ni zenye utata mkubwa.

Mara ya mwisho kwa Ballali kuonekana hadharani ilikuwa ni Julai 12 mwaka jana alipozungumza na wanahabari na akasema alikuwa hatarajii kujiuzulu wadhifa wake kutokana na kukabiliwa na tuhuma za ubadhirifu.

Katika mkutano huo, Ballali alisema madai ya ubadhilifu yanayotolewa dhidi yake ni uzushi na uongo mtupu.

Huku akionekana kujiamini alisema; “Niko Comfortable, moyo wangu mweupe, ari yangu ya kazi iko juu kwani tuhuma hizo ni uongo na uzushi mtupu na siwezi kujiuzulu kwa tuhuma zisizo na ushahidi.

“Tuhuma zote dhidi yangu ni za uongo mtupu. Kwanza sijui zimetoka wapi, nani mtunzi na kwanini amefanya hivyo. Hilo tunawaachia wanaofanya uchunguzi na naamini siku moja atajulikana na ukweli utajulikana, lakini mimi siwezi kujiuzulu kwa mambo ya uzushi,” alisisitiza.

Kashfa ya BoT kupitia mtandao wa Internet, uliibuliwa mara ya kwanza Bungeni na Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa (CHADEMA).

Akichangia maoni ya kambi ya upinzani wakati wa mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha, Dk. Slaa alisema kambi ya upinzani imefarijika baada ya Waziri wa Fedha kukiri kufahamu taarifa aliyoitoa Bungeni kuhusu ubadhirifu mkubwa ndani ya BOT unaomgusa Ballali, pamoja na wafanya biashara wengine wakubwa akiwemo Mbunge wa Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya (CCM), kupitia kampuni anayoimiliki.

Dk. Slaa alisema Dk. Mzindakaya alichukua mkopo kwa shughuli za kampuni yake ya SAAFI wa sh 6.217 bilioni, uliogawanyika kama ifuatavyo.

Alisema aliomba ‘Overdraft facility ya 450 millioni zitakazolipwa kwa miaka 5; mkopo wa shs 2.8 bilioni zitakazolipwa katika miaka mitano; na Dola za Marekani 2.528. Jumla yote ni Bilioni 6.217.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, fedha zote zilikopwa Benki ya Standard Charter na Benki Kuu ilitoa (Guarantee) mdhamana wa asilimia 100. Mwaka huu wa 2007 Benki kuu kutokana na Mdhamana huo tayari imelipa kiasi cha sh 8.1 Billion kwa niaba ya Mzindakaya na fedha hizo pamoja na riba zinakisiwa kufikia 9.7 billioni hadi sasa (Hati ref. CIBD-14662 ya tarehe 24 May, 2007, na mkopo kutolewa 2005. Kutokana na tuhuma hizo, Meghji wakati akifanya majumuisho ya hoja yake, alisema Serikali imeagiza kuanza kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje zinazoikabili Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Alikiri serikali kupata taarifa za kuwapo kwa vitendo vya rushwa na nyingine za matumizi mabaya ya fedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Waziri Meghji alisema, tayari alikuwa ameshamwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali, kuanza uchunguzi kuhusu tuhuma hizo. Meghji alisema, serikali ilikuwa ikitarajia kukamilisha kazi hiyo na taarifa kamili ya uchunguzi huo kutangazwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu. Mbali ya BoT kutuhumiwa kutumia fedha nyingi kuliko inavyostahili katika ujenzi wa majengo yake mapya ya ‘minara miwili pacha’ (Twin Towers), kiasi cha Dola za Marekani milioni 30.8 sawa na shilingi bilioni 40 kinatuhumiwa kufujwa katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje. Taarifa zinaonyesha kuwa, wakopeshaji wa kimataifa kutoka nchi 12 waliingia mkataba wa kusimamia akaunti hiyo na kampuni ya Kitanzania ijulikanayo kwa jina la Kagoda Agriculture Ltd kati ya Septemba na Novermba mwaka jana. Uchunguzi wa awali wa wakaguzi wa nje wa mahesabu ya akaunti hiyo unaonyesha kuwapo kwa mazingira yenye utata mkubwa unaozingira makubaliano kati ya wakopeshaji na kampuni hiyo iliyolipwa dola milioni 30.8. Akichangia hotuba ya Waziri Mkuu, Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe (CHADEMA) alihoji kwa nini Serikali ilikalia kimya suala la kashfa ya BoT mara baada ya habari za kashfa kutangazwa kupitia mtandao wa internet tangu Novemba 2006 na kuonya kuwa hali hiyo inaathali kubwa kiuchumi iwapo kashfa kama hizi zinaachwa bila ya ufuatiliaji wa serikali. Taarifa za awali za uchunguzi huo zinaonyesha kuwa, BoT ilifikia hatua ya kuipa kampuni hiyo fedha zote hizo ikidai kuingia mkataba na wakopeshaji hao katika mazingira ambayo nyaraka zilizopatikana zinaonyesha kuwa na hitilafu nyingi. Miongoni mwa hitilafu zilizobainishwa katika uchunguzi wa awali ni, kukosekana kwa karatasi rasmi zenye majina ya makampuni hayo ya kimataifa.
Mwisho

No comments: