CHAMA cha Wananchi (CUF), kimerusha makombora mazito ya lawama dhidi ya mahasimu wao, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiibua shutuma mpya ambazo hazikupata kuwekwa hadharani kabla.
Katika hatua inayoonyesha kuendelea kujikita kwa hali ya uhasama wa kisiasa kati ya vyama hivyo viwili, CUF imefikia hatua ya kuwahusisha viongozi wakuu wa CCM hususan wale wa Zanzibar kuwa na uhusiano wa moja kwa moja wa kikazi na kinasaba na chama cha kisultani cha Hizbu.
Kauli hizo nzito za CUF zilitolewa jana Buguruni, jijini Dar es Salaam mbele ya wana habari na viongozi wa juu watatu wa chama hicho, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa ameongozana na Katibu Mwenza wa Kamati ya Pamoja (na CCM) ya Mazungumzo ya Muafaka, Ismael Jussa Ladhu na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho (Zanzibar), Juma Haji Duni.
Katika mkutano huo wa jana, viongozi hao wa CUF walisambaza miniti za vikao vyao vya siri na CCM ambazo zinaonyesha kuwa mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa kisiasa Zanzibar kati ya vyama hivyo viwili yalikamilika, tofauti na ilivyoelezwa juzi na viongozi wa juu watatu wa CCM walioongozwa na Katibu Mkuu, Yussuf Makamba.
Akizungumza kwa kujiamini, Jussa, mmoja wa viongozi wenye ushawishi ndani ya CUF, aliwataja Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na mke wa Rais wa Zanzibar, Shadya Karume, kuwa wana CCM wawili wenye uhusiano ama wa kikazi au kinasaba na chama hicho cha kisultani cha Hizbu.
Jussa ambaye alikuwa akikanusha madai ya kada mkongwe wa CCM aliyepata kuwa msoshalisti kiitikadi, Kingunge Ngombale-Mwiru, aliyeihusisha CUF na U-Hizbu, alisema chama hicho tawala ndicho ambacho kina historia ya kuwa na uhusiano na chama hicho cha kisultani.
Alisema inapofika mahali mtu mzima kama Kingunge akasema uzushi, ni dhahiri chama hicho (CCM) kimefikia mahala pagumu na kimepoteza dira na mwelekeo.
“CCM ndiyo ina sifa zote za mahusiano na Hizbu, na si CUF. Na kwa msingi huo, kama kuna hoja pia ya kurudisha Waarabu, hilo linapaswa kuhofiwa kutoka CCM na si kutoka CUF.
“CUF kiliasisiwa mwaka 1992, na viongozi wake wanne wakuu kutoka Zanzibar ni Seif Sharif Hamad, Ali Haji Pandu, Shaaban Khamis Mloo na Machano Khamis Ali. Wote ni wana-ASP wasio na chembe ya shaka.
“Lakini mawaziri wa Zanzibar wa hivi sasa, yupo ambaye anajulikana kuwa alikuwa mwanachama wa Hizbu. Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yusuf Himid, ambaye ni ndugu wa mama mmoja na Shadya Karume, mke wa Amani Karume, wote wawili ni wajukuu wa Sheikh Mohammed Salim Jinja, ambaye alikuwa mwasisi wa Hizbu na ambaye wenyewe Hizbu wakimwita ‘‘Founding Father of Zanzibar Nationalism,” alisema Jussa.
Pia alisema yupo waziri mmoja katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka Zanzibar ambaye amekuwa akiandika makala katika magazeti kuipinda CUF, alipata kuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Hizbu uliokuwa ukijulikana kama Youth Own Union (YOU).
Ingawa hakumtaja kwa jina, waziri anayetoka Zanzibar ambaye amekuwa akiandika makala kuiponda CUF kupitia magazetini ni Muhammad Seif Khatib, ambaye sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano.
Khatibu kabla ya kuingia serikalini alipata kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (zamani UVT) kwa muda mrefu, miaka ya 1980.
Mbali na hao, alisema viongozi wastaafu, kama Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi na Spika mstaafu wa Baraza la Wawakilishi, Mzee Ali Khamis Abdallah, baada ya Uhuru wa Desemba 1963 (miezi kadhaa kabla ya mapinduzi ya Januari 12, 1964) waliteuliwa na serikali ya Hizbu kuwa makatibu wa kwanza (First Secretaries) wa Ofisi za Kibalozi za Zanzibar huko Indonesia na Misri.
“Ni bahati mbaya sana kwamba lugha zinazochochea ubaguzi na kujidai kuwakataa ma-Hizbu zilizotolewa katika Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM hazikukemewa hata na Mwenyekiti wa CCM mwenyewe.
“Ulitumiwa Uhizbu kukataa ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar wakati hao waliokuwa wakiwakataa ma-Hizbu ndio ma-Hizbu wenyewe,” alisema Jussa katika kauli inayoweza kuamsha mtazamo mpya wa siasa za Zanzibar siku zijazo.
Kutokana na hayo, Jussa, aliwataka wana CCM kutambua kuwa, uzushi na upotoshaji hauwezi kukisaidia chama hicho tawala ambacho alisema sasa kimeanza kupoteza kwa kasi, uhalali wa kisiasa kama chama chenye dira na mwelekeo nchini.
Alisema CCM inapaswa ijirudi, ikiwa ni pamoja na kujisahihisha kama inataka ikubalike kuwa ni chama makini mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa.
“Kujidanganya kwamba wataendelea kufanya mchezo wa kitoto wa mazungumzo yasiyokwisha na baadaye kufikia miafaka ambayo hawana nia ya kuitekeleza sasa, hakuwasaidii tena, maana Watanzania wameamka.
Zanzibar kuna tatizo kubwa la kisiasa ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi wa kweli, makini, wa dhati na wa haki.
“Ni lazima pia tuseme tumesikitishwa sana na kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya wakati chama chake kikichezea shere suala zito linalohusu mustakbali wa taifa kama hili linalohusu mpasuko wa kisiasa Zanzibar,” alisema Jussa.
Huku akitumia msemo usemao: ‘Sadaka huanzia nyumbani’, Jussa alisema Watanzania wanahitaji kumuona Kikwete akiifanyia kazi Zanzibar, kwa mfano ule ule wa anavyojishughulisha na masuala ya Kenya, Comoro, Zimbabwe na hivi karibuni mgogoro wa DRC Kongo na Uganda.
Kuhusu mazungumzo yao ya muafaka, huku akisoma miniti zote za vikao vyao na CCM, Jussa alisema, wamefikia hatua hiyo ili kuweka kumbukumbu sahihi za mwenendo mzima wa mazungumzo baada ya kufedheheshwa na upotoshaji wa makusudi wa CCM.
Akitumia nakala za kumbukumbu za vikao hivyo zilizokuwa katika buku hilo lililopewa jina la ‘Ukweli unaofichwa na CCM kuhusu mazungumzo ya muafaka’, Jussa alisema kwa makusudi CCM wameamua kuficha ukweli wa mazungumzo hayo, na kuihusisha na tuhuma nzito CUF na viongozi wake, akiwemo Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad.
Kuhusu kukamilika kwa mazungumzo hayo, Jussa alisema Kamati ya Mazungumzo ya CCM inawapotosha wananchi na jumuiya ya kimataifa kwamba mazungumzo hayakukamilika.
Alisema katika kikao cha mazungumzo kilichowashirikisha makatibu wakuu wa CUF na CCM cha Januari 21 mwaka huu, pamoja na mambo mengine, wajumbe wa pande zote mbili walikubaliana mwishoni mwa mwezi huo, lazima wawe wamepeleka taarifa ya mwisho ya mazungumzo hayo na kupatiwa maamuzi.
“Ujumbe wa CUF ulishauriwa kwa sasa usitishe hatua ya kufikisha taarifa ya mazungumzo katika vikao vyake, ili kusubiri mazungumzo yakamilike na baadaye vyama vyote viwili viwasilishe taarifa hiyo katika kipindi kimoja,” alisema Jussa akinukuu kumbukumbu za kikao hicho.
Alisema kutokana na hali hiyo, walikubaliana taarifa za mazungumzo ziwasilishwe kwa pamoja katika vikao vyake vya juu baada ya mazungumzo kukamilika.
Alisema CUF na CCM kuwasilisha taarifa ya mazungumzo katika vikao vyao vya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Halmashauri Kuu ya Taifa Machi mwaka huu, ni ushahidi kuwa mazungumzo yalishakamilika.
Katibu huyo mwenza alisema walikubaliana kwamba mazungumzo hayo yakikwama, itakuwa fedheha kwa nchi na viongozi kutokana na matumaini yaliyojengwa kwa wananchi na jumuiya ya kimataifa.
“Tulikubaliana kwa kuwa mazungumzo yamechukua muda mrefu, hatua zichukuliwe kuyakamilisha ili ikifika Machi 2008 yawe yamemalizika.
“Mazungumzo hayo yalikamilishwa katika kikao cha 20 cha Februari 24 – 29 mwaka huu, ambapo ajenda namba tano ilijadiliwa. Ni bahati mbaya kwamba kwa sababu hakujafanyika tena vikao vya mazungumzo kutokana na ubabaishaji uliofanywa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM huko Butiama, hakujakuwa na kumbukumbu za kikao hicho zilizopitishwa rasmi,” alisema.
Alisema kama kuna ajenda iliyobaki ambayo haijajadiliwa, hiyo itakuwa agenda ya sita iliyozushwa na CCM inayohusu kura ya maoni.
Kuhusiana na kuwepo kwa rasimu ya makubaliano, alisema kamati ya mazungumzo ya CCM iliwapotosha wananchi kwamba hakukuwa na rasimu ya makubaliano iliyokubaliwa na CUF na CCM katika mazungumzo hayo.
Alisema rasimu ya makubaliano ipo na ilipitishwa kwa pamoja na Kamati ya Makatibu Wakuu wa CUF na CCM katika kikao cha mazungumzo cha 18 cha Januari 3-4 mwaka huu.
Jussa, alisema katika kikao hicho, kwanza walikubaliana kupokea rasimu ya makubaliano yaliyofikiwa na baadaye kujadili njia za kujengeana imani.
Alisema Kaimu Katibu wa kamati kutoka upande wa CCM, Dk. Masumbuko Lamwai, kwa niaba ya mwenzake kutoka CUF, aliwasilisha rasimu waliyoitayarisha.
Alisema rasimu hiyo ilikuwa na kichwa cha habari kisemacho: ‘Rasimu ya Makubaliano kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) katika kuupatia Ufumbuzi wa Kudumu Mpasuko wa Kisiasa Zanzibar’.
Aidha, alisema CCM walipotosha kwamba Katibu Mkuu wa CUF aliwapotosha wananchi kwamba katika serikali shirikishi kutakuwepo nafasi ya Waziri Kiongozi ambaye atatoka katika chama kitakachopata ushindi wa pili na kwamba jambo hilo halijakuwepo kabisa katika makubaliano.
Pia alisema CCM ilipotosha kuwa hakuna makubaliano kuwa serikali ya pamoja itaanza baada ya kutiwa saini makubaliano.
“Wajumbe wa CCM wamepotosha kwa makusudi suala hili. Wangetaka kuwa wakweli wangesema kwamba nafasi ya Waziri Kiongozi ilikubaliwa ifutwe katika muundo wa serikali shirikishi ambayo ilikubaliwa itaanza mwaka 2010.
“Hata hivyo, katika mazungumzo, ilikubaliwa kuwa CUF ishirikishwe katika Serikali ya Zanzibar katika kipindi hiki (baada ya kutiwa saini makubaliano ya mwafaka), ambapo serikali itaendelea kuwa na muundo wake kama ulivyo sasa.
“Hata hivyo, katika kipindi hiki cha kuelekea 2010, kuwe na njia za kujengeana imani ambazo katika hatua za kisiasa zitajumuisha na Rais wa Zanzibar aliyepo madarakani kuteua mawaziri kadhaa kutoka CUF, ili waingie serikalini,” alisema.
Alisema suala la CUF kuingizwa serikalini kabla ya 2010 yalikuwa ni makubaliano ya Kamati ya Makatibu Wakuu na kwamba mapendekezo ya CUF yalihusu kiwango cha ushirikishwaji na yaliwasilishwa kwa barua kwa Katibu Mkuu wa CCM Januari 22, mwaka huu.
Akifafanua, alieleza katika mapendekezo hayo CUF ilitaka Rais wa Zanzibar na Waziri Kiongozi watoke upande tofauti kati ya CCM na CUF, ili kujenga kuaminiana kwa kweli na kuendesha serikali kwa mashirikiano ya pamoja.
Pia mawaziri wagawiwe kwa idadi, wanane watoke CCM na saba CUF.
Chama hicho kilipendekeza manaibu waziri wanne watoke CCM na watatu CUF kwa utaratibu kwamba waziri na naibu waziri wa wizara watatoka vyama tofauti.
“Pande zetu mbili zilikubaliana kuwa iwapo mapendekezo ya CUF yataonekana yamekwenda mbali, viongozi wa CCM watarudi kwa wenzao wa CUF kuyazungumza kabla ya kuyafikisha kwa viongozi wa dola.
“Pamoja na barua hiyo, hakuna barua au mawasiliano yoyote mengine yaliyowasilishwa kwa CUF yaliyoashiria kutokubalika au kutaka marekebisho katika suala hilo mpaka kikao cha mwisho,” alisema Jussa.
Kuhusu hoja ya kura ya maoni, alisema CUF imeikataa hoja hiyo kwa kuwa haijawahi kuwa miongoni mwa ajenda zilizokubaliwa katika mazungumzo ya kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
Alisema iwapo CCM ingekuwa na nia ya kuwasilisha ajenda hiyo, ingeiwasilisha wakati wa mazungumzo, lakini imefanya hivyo baada ya mazungumzo kwa lengo la ‘kuipiku CUF kisiasa’.
“Mgogoro wa kisiasa Zanzibar kimsingi ni mgogoro uliotokana na kuendeshwa vibaya na kuvurugika kwa chaguzi za mwaka 1995, 2000 na 2005. Katika hali hiyo, uchaguzi kwa njia ya kura ya maoni hauwezi kuwa ufumbuzi wa mgogoro wa uchaguzi bila ya kwanza taasisi zote zinazohusika na masuala ya uchaguzi kufanyiwa marekebisho.
“CCM na CUF wote wanakubaliana kupitia rasimu ya makubaliano kuwa taasisi zote zinazohusika na uendeshaji na usimamizi wa uchaguzi, zikiwemo Tume ya Uchaguzi, Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, vyombo vya ulinzi na usalama na vyombo vya habari vya serikali zina kasoro kubwa ambazo zinahitaji kurekebishwa. Vipi unaweza ukafanya kura ya maoni iliyo huru na ya haki katika hali kama hiyo?” alihoji katibu mwenza huyo.
Hata hivyo, alisema maamuzi makubwa na mazito zaidi nchini yamefanywa bila ya kupigiwa kura ya maoni na kutoa mifano ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, kufutwa kwa mfumo wa vyama vingi, Azimio la Arusha, kuunganishwa kwa TANU na ASP, kupitishwa kwa Katiba ya kudumu ya Muungano na marekebisho yake yote, kupitishwa kwa Katiba ya Zanzibar ya 1979 na 1984, na muafaka wa kwanza wa 1999 na muafaka wa pili wa 2001.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CUF ambaye amekuwa mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho mara tatu, Maalim Seif, alisema anaamini Kikwete anaweza kuingilia kati suala hilo na kulimaliza, kwani hajapata kuyumba katika kauli zake.
“Sijui huko Butiama walimroga? Ninavyomjua ana uwezo wa kulisimamia na kulimaliza...bado anayo nafasi na sisi tutampa ushirikiano katika hilo, ” alisema.
Hata hivyo, alisema kamwe chama hicho hakipokei amri za CCM kurejea katika mazungumzo, kwani hali hiyo haiwezekani kamwe.
Alisema kurudi kwenye mazungumzo hayo ni kupoteza muda na kuwahadaa Watanzania.
Maalim, alisema hivi sasa chama hicho kimeanza jitihada za kuzunguka nchi nzima kuwashawishi kunusuru mazungumzo hayo.
“Hivi sasa Profesa Lipumba ameanza ziara za kuzungumza na viongozi wa dini, watu mashuhuri na asasi za kijamii kuhusu suala hilo. Pia tunashirikisha mabalozi mbalimbali katika suala hilo, ” alisema.
Mbali ya hayo CUF walimtaka Rais Kikwete achukue hatua za haraka kuitisha mkutano wa pamoja utakaoshirikisha wadau wakuu wa masuala hayo kwa Zanzibar na kujadili mapendekezo yaliyotolewa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kisha kuhitimisha makubaliano hayo kati ya vyama hivyo.
Walisema endapo hayo hayatafanyika, CUF itatoa wito kwa marafiki wa Tanzania na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti, za uhakika na za haraka kuingilia kati suala hilo, ili kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa yanatiwa saini.
“Baada ya Tanzania yenyewe kushindwa katika utatuzi wa mgogoro wake huu wa muda mrefu, sasa ni wakati muafaka kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati kwa kuhakikisha makubaliano ya dhati yanafikiwa yatakayotoa ufumbuzi wa kweli na wa haki wa mpasuko wa kisiasa Zanzibar.
“CUF inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuepuka fedheha iliyoipata katika nchi nyingine za Kiafrika, ambazo iliziachia hadi hali ikachafuka na ndipo ikaingilia kati. Hali ya Zanzibar ni mbaya. Ilitulia kwa sababu ya matumaini ya Wazanzibari na Watanzania kwamba mazungumzo ya CCM na CUF yataleta suluhisho la utulivu na umoja.
“Makubaliano yaliyofikiwa yanapokosa uongozi wa Rais Kikwete katika kuyakamilisha, yanahitaji kuona jumuiya ya kimataifa inaingilia kati, kwa hatua za wazi na madhubuti kuinusuru Zanzibar na Tanzania isitumbukie kule nchi nyingine za Kiafrika zilikotumbukia, ” alisema.
No comments:
Post a Comment