SIKU moja baada ya maofisa usalama kuingia majumbani na kuwakamata wananchi waliopeleka barua Umoja wa Mataifa kutaka kuundwa kwa serikali shirikishi katika Kisiwa cha Pemba, baadhi ya watu wameingia mafichoni, wakihofia kukamatwa.
Wananchi hao ambao wameingia mafichoni kwa hofu ni miongoni mwa watu 12 waliokwenda Ofisi za UNDP jijini Dar es Salaam, wakitaka umoja huo usaidie utekelezaji wa mchakato wa kuundwa kwa serikali hiyo.
Polisi jana ilithibitisha kuwakamata watu kadhaa na ikasema wanashikiliwa kwa ajili ya mahojiano kuhusu hatua yao ya kwenda UNDP kuomba Pemba ijitenge kutoka Zanzibar.
Watu hao 12 waliwawakilisha wenzao zaidi ya 10,000 walioweka saini zao katika tamko hilo ambalo sasa linachukuliwa kuwa ni lenye dhamira ya kujitenga.
Licha ya Kamishna wa Polisi Zanzibar, Khamis Mohammed Simba, kukiri kukamatwa kwa wananchi hao, hakutaka kutoa maelezo, zaidi ya kuwataka waandishi kuwa na subira akisema chungu bado kiko jikoni kinatokota na kikiiva watapewa taarifa sahihi badala ya kukurupuka.
Kamishna Simba alisema, hakuna haja ya kufanya papara juu ya suala hilo, kwani bado linashughulikiwa na iwapo litakamilika umma utapewa taarifa zote kupitia vyombo vya habari.
Alisema Jeshi la Polisi nchini lina jukumu la kulinda uhuru na mipaka ya nchi yake na jaribio lolote la kutaka kumega nchi, lazima lishughulikiwe ipasavyo na vyombo vya ulinzi, ili kusitokee madhara.
Hata hivyo, akizungumza kwa njia ya simu ya kiganjani, mmoja wa watu walioshiriki kuandaa waraka uliopelekwa UNDP, alisema wamelazimika kuingia mafichoni wakihofia usalama wao, kutokana na taarifa za kutafutwa na vyombo vya usalama.
“Wenzetu wameshatiwa mbaroni na sisi tunatafutwa… bado tutaendelea kuishi huku (mafichoni) kwanza hadi hapo tutakapopewa taarifa za usalama wetu,” alisema Hamad Ali Mussa.
Alisema bado wataendelea kudai haki licha ya baadhi ya wananchi wenzao kukamatwa, kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakionewa na kudhulumiwa katika nchi yao kama wakimbizi, wakati wanastahiki kuheshimiwa na kupewa haki zote za kiutu, ikiwemo huduma za kijamii.
Hamad alisisitiza kuwa, huo si mwisho, kwani azma yao ni kujipanga upya na kuwafikisha mahakamani wale wote walioshiriki kuwaua raia wasio na hatia tangu mwaka 1964 baada ya mapinduzi na mauaji ya mwaka 2001 yaliyofanyika chini ya utawala wa Rais Amani Karume.
“Huu ni mwanzo tu. Tutachukua hatua nyingine zaidi, tulikuwa tumejipanga kuchukua hatua za kisheria tuwafikishwe mahakamani wale wote walioua tokea mwaka 1964 hadi 2001 kwa sababu tumechoka kudhalilishwa na kuonewa katika nchi yetu,” alisema Hamad.
Alibainisha kuwa, awali walikuwa na matumaini makubwa baada ya kusikia kauli ya Rais Jakaya Kikwete kusononeshwa na hali ya kisiasa Zanzibar, na ahadi yake ya kuumaliza mgogoro huo, pamoja na kuundwa kwa kamati ya mazungumzo ya mwafaka, lakini baada ya Halmashauri Kuu ya CCM kutaka kuitishwe kura ya maoni, ndipo walipovunjika moyo na kuamua kuandika waraka huo.
Alipotakiwa kueleza viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) wamewasaidiaje katika suala hilo wakati huu ambapo wenzake hawajulikani walipo, Hamad alisema chama hicho hakihusiki na suala hilo kwa kuwa wao wameamua kufanya hivyo bila ya kutaka ushauri wa chama. “Hili si la CUF, ni la sisi Wapemba na tumepeleka ombi tutambuliwe kama raia wenye haki katika nchi yao… sisi sio wageni, lakini haya madhila na manyanyaso yametutosha sasa na ndio tumeamua kujitolea,” alisema.
“Nisamehe bibi simu yangu itakatika sasa hivi kwa kukosa chaji nimeshawasiliana na watu wengi kama wewe, kwa hivyo ikikatika nakuomba samahani, lakini kwa ufupi sisi tutaendelea kudai haki zetu, watatutafuta wakitupata watupeleke mahakamani…tukitoka tutadai tena,” alisema na muda mfupi baadaye ikakatika.
Akizungumza kwa njia ya simu, mtu mwingine ambaye hakutaka kutajwa jina lake, ambaye naye yupo mafichoni huko, alisema kukamatwa kwa wenzake si jambo la ajabu kwani wapo wananchi kadhaa waliowahi kukamatwa bila ya sababu yoyote huko Pemba na kushitakiwa kwa kesi za kubambikiziwa, lakini hatimaye waliachiwa.
Mtu huyo alitoa wito kwa serikali zote mbili kuacha kujidanganya kuwa kuwakamata au kuwatisha wananchi hao ndio suluhisho la matatizo ya kisiwani Pemba, kwani tatizo kubwa linatokana na mfumo wa serikali pamoja na muundo wa ubaguzi dhidi ya Wapemba.
Akizungumzia kwamba kauli zao hizo zinaweza kuhusishwa na uhaini, alisema kuliwahi kutokea kundi la wabunge Tanzania Bara waliojiita G55 na kudai serikali ya Tanganyika, lakini hawakuhesabiwa kuwa ni wahaini, na kueleza kushangazwa na wao kupakaziwa kuwa ni wahaini.
Mzee huyo alisema kilichowasukuma na kulalamika kudai kuundwa kwa serikali shirikishi huko Pemba ni uonevu na dhuluma dhidi yao wanaofanyiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambapo hakuna uwiano wa kiuchumi na hata kukoseshwa nyadhifa muhimu serikalini.
Akitoa mfano alisema hivi sasa kati ya mawaziri 15 ni mmoja tu anayetoka Pemba.
“Kuwepo uwiano basi… na sisi tupewe nafasi za mawaziri kwani ni kweli hakuna Mpemba anayeweza kuwa waziri? Hakuna Mpemba anayeweza kuwa naibu waziri? Nafasi za makatibu wakuu na watendaji wakuu wa serikali wote kutoka Unguja! Huu uonevu mpaka lini tutaendelea nao? Ifike pahali tuseme enough is enough (inatosha) jamani,” alisema mtu huyo ambaye alisema alipata kufukuzwa kazi wakati wa utawala wa Dk. Salmin Amour Juma.
Akizungumza kwa simu jana, Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda naye alieleza kushangazwa na hatua ya serikali kuwakamata wananchi hao wa Pemba bila ya sababu za msingi.
Ponda alisema hoja za Wapemba hao ziko wazi, na akahoji ni kwa nini wabunge wa kundi la G 55 nao hawakukamatwa kwa uhaini, wakati walipodai ndani ya Bunge haja ya kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika.
Ingawa polisi hawajaeleza idadi ya watu waliokamatwa, habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa waliokamatwa ni watu saba.
Habari kutoka ndani ya Jeshi la Polisi Zanzibar zinaeleza kuwa watu hao walikamatwa na maofisa wa usalama kutoka Bara na kupakiwa katika ndege ya jeshi na hivi sasa wanahifadhiwa katika vituo kadhaa vya polisi kisiwani Unguja.
Taarifa hizo zinapasha kuwa vituo ambamo watu hao wanahifadhiwa ni Mwembe Madema, Mazizini na Ng’ambo.
Miongoni mwa watu waliokamatwa ni kiongozi wa wazee wa Pemba, Ahmed Marshed Khamis, Maryam Hamad Bakar (Wete), Jiran Alli Hamad (Micheweni), Gharib Omar Gharib (Wete), Mohammed Mussa (Mkoani), Salim Abeid (Mkoani) na Hidaya Khamis Haji (Mkoani).
No comments:
Post a Comment