Monday, May 12, 2008

Kamata Kamata Pemba

ZAIDI ya watu 12 kutoka kisiwani Pemba wametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio la kupelekwa kwa barua katika ofisi za Umoja wa Mataifa (UN) wakidai kujitenga kwa kisiwa hicho kutoka Zanzibar.

Watu wao walikamatwa kwa nyakati tofauti kuanzia usiku wa kuamkia Jumatatu, na familia zao zilithibitisha kukamatwa kwao kuanzia majira ya saa 5: 30 usiku wakiwa wamelala majumbani mwao.

Baadhi ya watu waliokamatwa wametambuliwa kwua ni ni Salim Mohammed Abeid, mkazi wa Mtambile, Mohammed Mussa Ali, mkazi wa Kiwani, Hidaya Khamis Haji wa Mkoani, Ahmed Marshed, Khamis Machomane na Mariam Hamad Bakar, wote wakaazi wa Kichangani Wawi, mkoa wa Kusini Pemba, Gharib Omar Ali, mkaazi wa Wete na Jirani Ali Ahmed wa Micheweni Kaskazini Pemba .

Sharifa Mussa, mke wa kiongozi wa kundi la watu 12 ambao walikwenda katika ofisi za UN wakiwakisha watu 10,000 waliotia saini barua hiyo, alithibitisha kukamatwa kwa mumewe, Ahmed Marshed Khamis, nyumbani kwake Mkanjuni mkoa wa Kusini Pemba.

Akielezea tukio hilo, Sharifa alisema mume wake alichukuliwa usiku na watu watano ambao hawakuwa na sare za polisi, ambao waligonga mlango wao wa nje na wao kulazimika kuamka haraka na kutoka nje kuangalia kinachoendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Ameir Khatib, hakutaka kuzunguzia chochote kuhusiana na kukamatwa kwa watu hao, ingawa alikiri na kuwataka waandishi wawasiliane na Makao Makuu ya Polisi Unguja.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Khamis Mohamed Simba, alisema hana taarifa zaidi na kuahidi kutoa taarifa baadaye.

Taarifa zaidi kutoka Kisiwani Pemba zinaeleza kuwa hofu imetanga katika kisiwa hicho, kutokana na kukamatwa kwa watu hao ambao wengine hadi sasa hawajulikani wamepelekwa wapi.

Zainab Omar Hamad, ambaye ni Mtoto wa Fatma Abdallah Hamad, ambaye ni miongoni mwa watu 12 waliowasilisha waraka wa barua katika ofisi za UN jijini Dar es Salaam, alisema alifuatwa na askari majira ya saa 6 usiku akitakiwa kueleza alipo mama yake huyo.

Fatma Abdallah Hamad, Katibu wa watu waliokwenda kuwasilisha waraka huo, ambaye alieleza kuwa lengo lao ni kuomba msaada wa UN kuwasaidia kuunda serikali shirikishi kutokana na wakazi wa kisiwa cha Pemba kunyanyaswa na serikali hivi sasa.

Imeelezwa kuwa baada ya kuwakamata watu hao, polisi pia walizipekuwa nyumba wanamoishi, kwa maelezo kuwa walikuwa wakitafuta nyaraka nyingine, lakini hawakufanikiwa kupata chochote na kuondoka.

Wananchi wa Pemba wapatao 10,000 kwa mara ya kwanza waliwasilisha mapendekezo yao katika ofisi ya umoja huo, wakiongwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimboi la Ole (CUF) Hamad Ali Mussa.

Wanafamilia wa watu hao walisema kwamba baada ya watu hao kukamatwa walijaribu kuwatafuta asubuhi katika vituo vya Polisi vya Pemba bila ya mafanikio na walielezwa kuwa walisafirishwa nje ya kisiwa cha Pemba kwa ndege.

Hata hivyo, walisema hadi Jumatatu mchana walikuwa hawafahamu jamaa zao iwapo wamesafirishwa kupelekwa kisiwani Unguja au Tanzania Bara.

Walieleza kwamba baada ya kuzunguuka katika vituo mbali mbali vya Polisi kisiwani Pemba walipata taarifa kutoka kwa baadhi ya askari kuwa watu hao wamesafirishwa usiku huo kwa ndege ya Jeshi kuelekea Bara.

Akilizungumzia tukio hilo, Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, alisema kwamba wamepata malalamiko kutoka kwa wanachama wa CUF Pemba kuwa usiku wa kuamkia jana, Polisi walifanya operesheni majumbani na kukamata baadhi ya watu.

Wiki iliyopita, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais anayeshughulikia Muungano, Mohammed Seif Khatib, alikaririwa akisema kitendo cha wananchi hao kutaka Pemba ijitenge ni uhaini.

Alisema kwamba kitendo hicho hakina tofauti na kile kilichofanywa na muasi wa Anjouan, Kanali Mohammed Bacar.

1 comment:

Anonymous said...

Your blog keeps getting better and better! Your older articles are not as good as newer ones you have a lot more creativity and originality now keep it up!