Monday, August 25, 2008

Kikwete ziarani Marekani

Rais jakaya Kikwete anaondoka leo kwenda Marekani kwa ziara ya siku tatu. Taarifa rasmi ya ziara yake iliyotolewa na ikului inasomeka ifuatavyo:

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameondoka nchini leo (Jumatatu, Agosti 25, 2008) mchana kwenda Marekani kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais George W. Bush.

Ziara hiyo inalenga kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa karibu zaidi kati ya Tanzania na Marekani, na shughuli zote za Rais Kikwete wakati wa ziara hiyo zinalenga kufanikisha jambo hilo.

Malengo makuu ya ziara hiyo yatakuwa ni kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili hasa katika nyanja za elimu, afya na uchumi.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake keshokutwa, Rais Kikwete atahudhuria hafla ya mfuko wa kwanza katika Marekani kujishughulisha na masula ya elimu miongoni mwa Wamarekani wenye asili ya Afrika na Waafrika wa The Phleps Stokes Fund.

Kwenye hafla hiyo, Rais atazungumzia hali ya elimu ya Tanzania, mafanikio yake na changamoto ambazo zinaendelea kuikabili sekta hiyo.

Baada ya hapo, Rais Kikwete atahudhuria mkutano kuhusu sekta ya afya na hasa jinsi ya kupambana na kuufuta ugonjwa wa malaria nchini kwenye kituo cha maendeleo cha Center for Global Development.

Wakati wa mkutano huo pia zitataganzwa juhudi mpya na misaada mingine ya Marekani katika kupambana na malaria katika Tanzania.

Baadaye siku hiyo hiyo, Rais atakwenda kwenye Bunge la Marekani, ambako itatangazwa rasmi kuwa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha wanyamapori cha International Conservation College kitajengwa Arusha.

Kwenye siku yake ya pili ya ziara hiyo, Rais Kikwete atakwenda Makao Makuu ya Shirika la Misaada la Marekani la USAID, ambako itatangazwa rasmi kuwa Marekani itatoa msaada wa kiasi cha dola za Marekani milioni 20 kusaidia maendeleo ya kilimo na usalama wa chakula nchini.

Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa atatia saini makubaliano ambako Marekani itasaidia usimamizi katika sekta za maji na nishati kupitia EWURA.

Rais pia atashiriki katika majadiliano kuhusu masuala mbalimbali ya sekta ya elimu, na baadaye kushuhudia tangazo ambako Marekani itaipa Tanzania msaada katika sekta hiyo ya elimu.

Msaada huo utakuwa wa vitabu vya kufundishia masomo ya sayansi wa kiasi cha dola za Marekani milioni 1.5, na kiasi cha dola 500,000 kwa ajili ya kufundishia walimu na ujenzi wa maabara tatu za kufundishia lugha ya Kiingereza.

Rais anatarajiwa kukutana na wawezekaji maarufu katika Marekani.

Kwenye siku ya tatu ya ziara yake, Rais Kikwete atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Rais George W. Bush katika Ikulu ya nchi hiyo ya White House.

Baada ya shughuli hiyo ya White House, Rais Kikwete atakwenda kwenye kituo maarufu cha waandishi wa habari katika Marekani cha National Press Center ambako Marekani itatangaza misaada zaidi kwa Tanzania katika nyanja ya afya, na hasa katika kupambana na ugonjwa wa ukimwi na magonjwa ya mlipuko.

Chini ya msaada huo wa kupambana na ugonjwa wa ukimwi, Marekani itasaidia ujenzi wa vituo viwili vya kisasa kabisa vya watoto, na pia itasaidia kuongeza uwezo wa Tanzania katika kupambana na magonjwa ya mlipuko.

Jioni ya siku hiyo ya tatu ya ziara hiyo, Rais Kikwete atahudhuria mchezo wa kikapu wa WNBA kati ya timu za Washington Mystics na Chicago Sky kwenye uwanja wa Veriton Center.

Wakati wa mechi hiyo, itatangazwa rasmi kuanzishwa kwa “Diplomasia ya Mpira wa Kikapu” ambayo itaanza kufanya kazi rasmi mwezi ujao (Septemba) wakati ujumbe wa wachezaji nyota wa mpira wa kikapu wa Marekani utakapotembelea Tanzania.


Salva Rweyemamu,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.

25 Agosti, 2008



No comments: