Wednesday, November 12, 2008

Chuo Kikuu chafungwa

Baraza la Chuo Kikuu cha dar es Salaam limekifunga chuo hicho kwa muda usiojulikana baada ya wanafunzi kugoma kwa siku tatu mfululizo.
Tangazo la kufungwa kwa chuo hicho limetolewa leo asubuhi na kubandikwa katika mbao kadhaa za matangazo chuoni hapo.
Jana, waziri wa Elimu na Mafunzo ya ufundi, Prof. Jumanne maghembe aliwataka wanafunzi hao kuachana na mgomo huo na kurejea madarasani leo. Kwa upande wake, uongozi wa Chuo Kikuu uliwataka wanafunzi hao kuwa madarasani leo saa moja asubuhi.
Lakini wanafunzi hao waliendelea na mgomo wao ambao walisema hautakuwa na mwisho hadi madai yao yasikilizwe na serikali.
Wanafunzi hao wanataka kuondolewa kwa sera ya kuchangia elimu inayotoa maelekezo kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutoa mikopo kwa kiwango kulingana na hali za waombaji.
Wanafunzi wanasema kigezo hicho hakitumiki ipasavyo, ni cha unyanyasaji na kinawabagua wanafunzi wasio na uwezo.
Walianza mgomo wao Jumatatu na kwa mujibu wa sheria, Chuo kinalazimika kufungwa iwapo wanafunzi watagoma kwa siku tatu mfululizo.

No comments: