RAIS Kikwete, amefanya mabadiliko ya makatibu wakuu na naibu katibu wakuu wa wizara 13 na Gray Mgonja wa fedha amekwenda likizo ya kustaafu.
Makatibu kadhaa na manaibu wamehamishwa na wengine wapya wameteuliwa baada ya wengine kustaafu.
Mabadiliko hayo yamegusa wizara kadhaa ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ulinzi, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki na nyingine tisa.
Kikwete amewateua wasaidizi wake wawili wa Ikulu kuwa naibu makatibu wakuu wa wizara.
Alhaj Ramadhan Kijja anakuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Uchumi, Dk Florens Turuka Katibu Mkuu wa Habari Utamaduni na Michezo, Joyce Mapunjo anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara na Andrew Nyumayo anakuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Kabla ya uteuzi Kijja alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Uchumi, Dk Turuka alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Joyce Mapunjo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Miundo Mbinu na Andrew Nyumayo alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu.
Makatibu wakuu waliohamishwa Wizara ya ni pamoja na Paniel Lyimo aliyekuwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Masoko sasa anakwenda Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Ladislaus Komba amehamishiwa Maliasili na Utalii, Kijakazi Mtengwa amepekewa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana na Mohamed Muya amehamishiwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.
Awali Dk Ladislaus Komba alikuwa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Kijakazi Mtengwa alikuwa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ambapo Mohamed Muya alikuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Makatibu wakuu wengine waliohamishwa ni Patrick Rutabanzibwa amepangiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kutoka Maji na Umwagiliaji, Dk Sergomena Tax - Afrika Mashariki akitokea Viwanda, Biashara na Masoko, Wilson Mukama anakwenda Maji na Umwagiliaji kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, pamoja na Blandina Nyoni anayekwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii akitokea Maliasili na Utalii.
Naibu makatibu wakuu wapya walioteuliwa ni pamoja na Dk. Philip Mpango- Fedha na Uchumi, Celestine Gesimba - Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Seti Kamuhanda - mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Dk Mpango alikuwa msaidizi wa rais (Uchumi) Ikulu, Seti Kamuhanda pia alikuwa msaidizi wa rais (Hotuba) Ikulu na Gesimba alikuwa Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Fanuel Mbonde aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu.
No comments:
Post a Comment