Sunday, November 16, 2008

Mgomo wa walimu-Kesho ndio kesho

Juhudi za serikali kuhakikisha mgomo wa walimu hautokeo, zimeshindikana. walimu wamethibitisha kuwa liwake jua inyeshe mvua, kesho lazima watagoma.
rais wa Chama Cha walimu, Gratian Mukoba, amesema kuwa baada ya hukumu ya Mahakama ya Rufaa mapema wiki hii, hakuna tena kunachoweza kuwazuia walimu nchini kugoma.
Aidha, Mukoba anasema vitisho na ahadi zinazotolewa na serikali hivi sasa zinathibitisha kuwa madai ya walimu ni ya kweli na halali.
Kupitia kwa katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo, serikali juzi ilitishia kuwa mwalimu atakayegoma hatolipwa mshahara. Pia, waziri wa TAMISEMI, Celina Kombani, naye amepiga mkwara akiwa humo Mwanza kuwa walimu waliowasilisha nyaraka za kughushi katika madai yao watafikishwa mahakamani.
Luhanjo alisema katika taarifa yake kuwa Serikali imekwenda mahakamani kuomba mgomo huo usitishwe na Chama cha walimu kimeshapelekewa wito wa kuitwa mahakamani.
Lakini, Mukoba anasema kuwa wao bado hawajapata wito huo, na hata kama wakiupata hauwezi kuwafanya waahirishe mgomo wao wka sababu vitu hivyo viwili havihusiani.
Anasema kuwa walimu walishajiandaa kugoma tangu siku nyingi na hivi sasa wanaisubiri kesho ifike kwa hamu waonyeshe kile ambacho wana uwezo kukifanya.
Mukoba alisema CWT haiwezi kuvutwa na ahadi ya serikali kuwa fedha zimeanza kusambazwa wilayani kwa ajili ya malipo ya walimu kwa sababu wao madai yao si fedha kusambazwa wilayani, bali walipwe malimbikizo ya madai yao.
Walimu wanasema kuwa wanadai zaidi ya Sh bilioni 16 kama malimbikizo ya posho za likizo, usafiri, matibabu na madai mengineyo lakini serikali inasema karibu nusu ya madai hayo ni feki.

No comments: