Wednesday, November 26, 2008

Waziri awatembelea akina Mramba gerezani

Waziri wa mambo ya Ndani, Lawrence Masha, jana alifanya ziara ya ghafla katika gereza la Keko ambako mawaziri waandamizi wawili wa zamani wamehifadhiwa baada ya kukosa dhamana katika kesi yao ya kutumia vibaya madaraka yao inayowakabili.
mawaziri hao wa zamani, basili Mramba na Daniel Yona walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, wakikabiliwa na jumla ya mashitaka 13 ya kutumia vibaya madaraka yao, kuhusiana na mkataba wa kampuni ya Alex Steward Asseyers, iliyoingia mkataba wa kufanya ukaguzi wa biashara ya dhahabu.
Masha alifika gerezani hapo kinyemela kwani alikuwa anatumia gari binafsi, akiwa amevaa mavazi ambayo yanaweza kuhesabiwa kuwa si rasmi kwa kazi kwa mtu mwenye hadhi yake.
Maofisa wa Magereza hiyo walikataa kuzungumzia suala hilo lakini Masha mwenyewe amethibitisha kwua kweli alikwenda katika gereza hilo.
Alipoulizwa ziara yake hiyo ilikuwa na lengo gani, Masha alisema ilikuwa ni ziara ya kikazi, ingawa alipotakiwa kueleza kwa nini anafanya ziara ya kikazi akitumia gari binafsi, alishindwa kufanya hivyo.
Wakati huo huo, Mawakili wa Yona na Mramba walirejea mahakamani hapo wakiwa na barua ya kuomba kupatia mwenendo wa kesi hiyo ili wakate urfaa Mahakama Kuu kupinga masharti magumu ya dhamana waliyowekwa wateja wao.
hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Hezron Mwankenja, amewaamuru makarani kuiabndaa nyaraka hiyo haraka ili mawakili hao watimize dhamira yao.

No comments: