Wanafunzi wa vyuo vikuu vya umma vilivyofungwa, wamegoma kuyakubali masharti yaliyotolewa na serikali. Serikali iliagiza uongozi wa vyuo vikuu vya umma nchini, kuwabagua wanafunzi kati ya wale wanaokubaliana na mfumo wa uchangiaji wa elimu ya juu na wale wasiokubaliana nao.
Baada ya hapo, wanafunzi hao walitakiwa kuandika barua ya kueleza kukubaliana kwao na mfumo huo na kujaza fomu maalum, ambayo itakuwa kama mkataba baina yao na uongozi wa vyuo kuhusiana na makubaliano hayo.
Akizungumza leo, rais wa serikali ya Wanafunzi wa UDSM, Anthony Machibya, alisema kuwa uongozi wa UDSM ulishawapatia masharti hayo na wao wameyakataa.
Akizungumza kwa niaba ya marais wenzake saba kutoka vyuo sana vya umma vilivyofungwa kutokana na migomo ya wanafunzi, Machibya alisema kuwa hakuna atakayeandika barua wala kujaza fimu kama sharti la kumtaka arejee chuoni.
Alisisitiza kuwa wanafunzi watarejea chuoni iwapo tu serikali itaondoa mfumo wa uchangiaji wa elimu ya juu uliopo.
Alisisitiza kuwa iwapo serikali haitotekeleza madai yao, hawatarejea vyuoni na iwapo watarejea, wataendelea na migomo hadi sera hiyo ya uchangiaji iondolewe.
Lakini, mgawanyiko baina ya wanafunzi hao kwani wale wanaounda umoja wa viongozi wa vyuo vya umma, (Tahliso) wenyewe wameonekana kupingana na wenzao.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Tahliso, Nicholaus Mtindya, alisema kuwa umoja wao haukubaliani na mgomo uliofanywa na wanafunzi hivi karibuni.
Alisema kuwa hawakubaliani na mgomo huo kwa sababu Tahliso tayari ilishaongea na serikali na wakaipatia miezi miwili ili iyashughulikie madai yao.
Anasema kuwa miezi miwili haijapita kwa sababu kikao hicho kilifanyika Oktoba 23 na inashangaza kwa nini wanafunzi waligoma kabla ya kumalizika kwa muda huo.
Aidha, anasema kuwa mgomo uliofanywa na wanafunzi hivi karibuni ulishinikizwa na baadhi ya watu kwa maslahi yao binafsi. Hakufafanmua.
No comments:
Post a Comment