Monday, November 10, 2008

Wengi zaidi washitakiwa kwa EPA

WATU walioshitakiwa kwa makosa yanayohusiana na wizi wa fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ya Benki Kuu (BoT) sasa wamefikia 20 baada ya watuhumiwa wengine watatu kufikishwa katika Mahakaha ya hakimu Mkazi Kisutu leo.

Waliofikishwa mahakamani hapo ni wafanyabiashara ndugu; Ajar Sryakant Somani na Jai Chhotalal Somani. Pamoja nao alikuwemo pia Mwesiga Lukaza, ambaye aliunganishwa kwenye kesi ya ndugu yake, Jonson Lukaza. Katika kesi hiyo wanatuhumiwa kujipatia kwa njia ya udanganyifu kiasi cha sh. Bil 6.3 kutoka katika akaunti hiyo.

Kama kawaida, watu walikuwa wengi mahakamani hapo. Watu wengine walifika mapema sana saa 1 asubuhi baada ya taarifa kuenea jijini Dar es Salaam kuwa mmoja wa wafanyabiashara maarufu jijini, leo angefikishwa mahakamani hapo kuhusiana na kesi hizo.

Ndugu hao, Ajar Sryakant Somani na Jai Chhotalal Somani) wanatuhumiwa kujipatia kwa njia ya udanganyifu kiasi cha sh bil 5.91.

Katika moja ya matukio ya jana katika kesi hiyo, Chhotalal Somani alishindwa kujizuia na kububujikwa na machozi ndani ya mahakama wakati akisubiri kusomewa mashitaka.

Akiwasomea mashitaka, Wakili wa Serikali, Fredrick Manyanda aliiambia mahakama hiyo iliyokuwa mbele ya hakimu mkazi Victoria Nongwa kuwa ndugu hao, Sryakant na Chhotalal, waliiba fedha hizo mnamo Septemba 2, 2005.

Manyanda alidai kuwa walijipatia fedha hizo baada ya kughushi nyaraka wakionyesha kuwa wamenunua deni la kampuni ya nje iitwayo Society Alsacienne Construction de Machines Textiles. Watu hao wana kampuni yao iliyosajiliwa nchini ya Liquidity Service Limited, ambayo waliitumia kama iliyonunua deni hilo.

Mwesiga Lukaza yeye alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Euphemia Mingi na kuunganishwa kwenye kesi ya ndugu yake.

Wanadaiwa kuwa nao waliwasilisha nyaraka za kughushi, wakidai kuwa kampuni ya Kernel Limited Company of Tanzania, imenunua deni la kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan.

Watuhumiwa wote watatu walipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutekeleza masharti ya dhamana ambayo yalihusisha kuweka kiasi cha fedha ambacho ni nusu ya kiasi wanachodaiwa kuibaau kutoa hati za mali zisizohamishika zenye thamani hiyo.

Watuhumiwa hao wanatetewa na wakili maarufu, Majura Magafu, ambaye anawatetea pia watuhumiwa wengine wawili wanaokabiliwa na kesi za EPA. Kesi hizo zitatajwa tena Novemba 21.

Watuhumiwa wengine walioshitakiwa kwa makosa hayo wafanyabiashara na watumishi wa BoT.

No comments: