Wednesday, July 30, 2008

Kwa heri Wangwe

(KWA HISANI YA TANZANIA DAIMA)

RAIS Jakaya Kikwete, jana aliwaongoza viongozi mbalimbali wa serikali, wabunge, majaji, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Chacha Wangwe, katika shughuli ya kuaga mwili wake.

Shughuli ya kuuaga mwili wa Chacha, ilifanyika katika maeneo ya Bunge, kuanzia majira ya saa 12:15, jioni.

Rais Kikwete alikuwa Dodoma kuhudhuria mkutano wa Baraza la Mawaziri, uliofanyika katika Ikulu ya Chamwino, mjini hapa, ambapo alitumia fursa hiyo kuuaga mwili wa Wangwe, aliyefariki dunia juzi kutokana na ajali ya gari, iliyotokea katika eneo la Pandambili, wilayani Kongwa, takriban kilometa 20 kutoka Dodoma mjini.

Shughuli ya kuuaga mwili wa Wangwe ambao ulikuwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, ilitawaliwa na kwikwi ya vilio vya wabunge, ndugu, jamaa na marafiki na wake wawili wa mbunge huyo, waliokuwa wameongozana na watoto watatu wa marehemu.

Kabla ya kuanza shughuli hiyo, zilitolewa salamu za rambirambi, na wa kwanza alikuwa Kiongozi wa upinzani Bungeni, Hamad Rashad, aliyemwelezea Wangwe kuwa ni kiongozi shupavu na mtetezi mkubwa wa watu wake wa Tarime.

Katika kulithibitisha hilo, Hamad Rashidi, alisema uamuzi wake kutaka kuwasilisha hoja binafsi inayozungumzia mgogoro wa ardhi katika jimbo lake, ni dhamira ya wazi ya namna mbunge huyo alivyokuwa akiwapigania watu wake.

Wa pili kutoa salamu za rambirambi alikuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa niaba ya serikali.

Pinda alimwelezea Wangwe kuwa ni kiongozi mwenzao na Bunge limepoteza kiongozi stadi, akiwa ni mbunge wa tano kupoteza maisha, tangu Serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani.

Wengine waliopoteza maisha ni pamoja na Juma Akukweti (Tunduru), aliyefariki kutokana na ajali ya ndege, mkoani Mbeya na Salome Mbatia (Viti Maalumu) ambaye pia alifariki dunia kwa ajali ya gari.

Wengine ni Benedict Losurtia (Kiteto) na Amina Chifupa (Viti Maalumu), ambao walifariki dunia kutokana na maradhi.

Wa tatu kutoa salamu za rambirambi, alikuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye alianza kwa kusoma histori fupi ya maisha ya Wangwe.

Alisema Wangwe alizaliwa Julai 15, 1956, huko Tarime. Alimwelezea Wangwe kama kiongozi aliyejiamini na mtu madhubuti aliyetetea hoja zake hata kama hoja hizo zingesababisha kuhitilafiana na watu wengine.

Aidha, Spika alisema kifo cha Wangwe kimesababisha Bunge lipoteze mtu aliyekuwa akihitajika sana katika taifa lake na katika familia.

Alitumia fursa hiyo kuwaeleza kuwa Bunge, lilitoa ubani wa sh milioni tano kama rambirambi yake kutokana na kifo cha mbunge huyo.

Kwa upande wake kaka wa marehemu Wangwe, Profesa Samweli Wangwe, alimwelezea mdogo wake kuwa alikuwa kiungo mhimu katika familia.

Alisema alikuwa jasiri na mtetezi wa haki, hasa katika masuala ya kifamilia na kusisitiza kuwa mdogo wake alikuwa mtu mwenye moyo mweupe hata ilipotokea kukorofishana na kutetea ndugu zake.

Kabla ya shughuli hiyo ya kuaga, katika hali isiyokuwa ya kawaida, Spika Sitta, alishindwa kujizuia na kububujikwa machozi wakati akitoa taarifa za kifo hicho bungeni.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Pinda na wabunge wengine waliokuwemo ukumbini humo, baadhi yao walifuta machozi na kusababisha kuwepo utulivu kwa muda kabla ya Bunge hilo kuahirisha shughuli zake jana.

“Waheshimiwa wabunge, kwa mara nyingine tena tumeangukiwa na msiba mzito wa mwenzetu Chacha Wangwe.

“Kifo cha mwenzetu kilitokea jana (juzi) usiku kwenye eneo la Pandambili, baada ya gari lake kupinduka na kugonga miti, hali iliyosababisha kifo chake papo hapo.

“Ndani ya gari hilo alikuwepo kijana mwingine alitwaye Deus Mallya…kwa kweli hali ilivyokuwa pale hatuna maelezo zaidi.

“Natoa pole kwa familia yake, CHADEMA na mwenyekiti wa chama hicho…kwa kuzingatia kanuni ya 149 naliahirisha Bunge, hadi saa sita mchana kwa ajili ya kuangalia namna ya kufanikisha hili.

“Hivyo basi, nawaomba wajumbe wa Kamati ya Uongozi…(kilio), na Tume ya Huduma za Bunge kukutana kwenye Ukumbi wa Spika,” alisema Sitta aliyekuwa akipangusa machozi yake kwa kitambaa cheupe huku akiliahirisha Bunge.

Aidha, kanuni ya 149 ya Bunge toleo la mwaka jana, inaeleza kwamba, endapo mbunge atafariki dunia wakati Bunge likiwa katika shughuli zake, Spika ataahirisha shughuli za Bunge kwa siku hiyo kwa ajili ya maombolezo.

Baada ya kukutana kwa Kamati ya Uongozi na Tume ya Huduma za Bunge, Spika huyo aliwaeleza wabunge kuhusu utaratibu wa mazishi.

Alisema bungeni hapo kwamba mwili wa marehemu Wangwe utasafirishwa leo kuelekea kijijini kwao kilometa 12 kutoka Tarime mjini kwa mazishi.

Aidha, Ofisi ya Bunge imeshughulikia mazishi hayo ambapo ndege maalumu imekodiwa kwa ajili ya kubeba mwili wa marehemu na ndugu zake akiwemo mjane na watoto.

Alisema, wabunge 20 na maofisa wa Bunge watahudhuria mazishi hayo, ambapo watakwenda kwa ndege ya kukodi kesho asubuhi na kurudi baada ya mazishi.

Spika, alisema hatahudhuria mazishi hayo kwa sababu anasafiri kuelekea Malaysia kwenye uchaguzi wa viongozi wa Commonwealth Parliamentary Association (CPA), kwa kuwa ni miongoni mwa wagombea.

Kuhusu udhuru wa Naibu Spika, Anne Makinda, Sitta alisema naye atashindwa kwenda Tarime kwenye mazishi hayo, kwa kuwa Rais Kikwete atakuwa kwenye ziara ya kikazi wilayani Njombe.

“Kutokana na udhuru wetu, Bunge limemteua Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu inayoshughulikia Nishati na Madini, William Shelukindo, kuwa kiongozi wa msafara huo,” alisema Sitta.

Hata hivyo, alisisitiza uwiano katika uwakilishi huo, ambapo Bunge limezingatia jinsia na uwakilishi wa Bara na Visiwani.

Sitta pia, alisema uchunguzi wa kina utafanyika na taratibu za kipolisi zitafuatwa kuhusu mwili wa mbunge huyo.

Aidha, timu ya uchunguzi iliongozwa na daktari bingwa kuchunguza maiti kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, ndugu mmoja wa marehemu, ofisa wa Bunge na askari polisi.

Baadhi ya wabunge kutoka vyama mbalimbali vya siasa, wameelezea masikitiko yao kuhusu kifo cha Wangwe.

Kifo cha Wangwe, kilitokea juzi usiku baada ya gari alilokuwa akisafiria kuelekea Dar es Salaam kutoka Dodoma, kupinduka kwenye eneo la Pandambili, Kongwa mkoani hapa.

Akizungumza kwa masikitiko, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, alisema kifo hicho ni pigo kwa kambi ya upinzani bungeni.

Dk. Slaa ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, alisema licha ya kushtushwa na msiba huo wa ghafla, chama kimempoteza mtu aliyekuwa na misimamo.

Alisema, baada ya kupokea taarifa hizo kutoka kwa mtu ambaye hakumtaja, alikwenda kwenye eneo la tukio ili kuhakikisha alichosikia.

Alisema, kabla hajafika gari alilokuwamo lilisimamishwa na askari polisi walioweka kizuizi, hali iliyosababisha magari kutoka pande zote kusimama.

Baada ya kusimama kwa muda alifuatilia mazungumzo ya polisi na gari la upande wa pili, ndipo alipogundua kwamba gari lile lilibeba mwili wa Wangwe kwa ajili ya kuupeleka hospitali na kuuhifadhi.

“Nilipogundua hivyo, niliamua kugeuza gari nikaongozana na lile lililobeba maiti hadi Hospitali ya Mkoa hapa Dodoma.

“Hapo sasa ndipo niliamini kwamba aliyekuwa amekufa ni Wangwe…hapo ilikuwa saa saba usiku, kwa kweli hali ya gari lake inasikitisha,” alisema Dk. Slaa na kusisitiza kwamba kifo hicho ni pigo kwa CHADEMA, kambi ya upinzani na Bunge zima.

Alimwelezea Wangwe kuwa mtu mwenye misimamo, jasiri, aliyesimamia kila alichokiamini na kwamba alikuwa changamoto pia kwa wabunge wengine kutokana na hoja zake.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge alisema kifo hicho ni pengo kwa Bunge na wabunge wengine kutokana na kauli zake, misimamo na maamuzi yake.

Hata hivyo alibainisha kwamba juzi ilikuwa awasilishe maelezo yake binafsi kuhusu hali ya wakazi wa Tarime, nguvu inayotumiwa na polisi kuwahamisha kwenye baadhi ya maeneo na tatizo sugu la mapigano ya koo na wizi wa mifugo hasa ng’ombe.

“Ijumaa iliyopita aliniletea maelezo yake nikamwambia ratiba haitamruhusu hadi jana (Jumatatu), ilipofika asubuhi aliniuliza vipi mheshimiwa nitapata nafasi ya kutoa maelezo yangu? Nikamwambia tumsubiri Spika anaweza kukupa muda.

“Kweli Spika akasema muda utapatikana baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, kuhitimisha hoja ya bajeti ya wizara yake. Hapo napo Spika alimpa dakika 20, nikamwambia ‘hang around’ yaani asiende mbali nafasi imepatikana.

“Nadhani kifo chake kilifika kwa kweli maana saa 12, Spika aliwaagiza maofisa wa Bunge kumtafuta Chacha Wangwe ili muda utakapofika wa kutoa maelezo yake, afanye hivyo lakini hakupatikana,” alisema Naibu Spika huyo.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (CHADEMA), alimwelezea Wangwe kuwa ni mtu aliyesimamia alichokiamini hata kama anapingwa na watu wengi.

“Wangwe namuelezea kama mtu mwenye misimamo, asiyeogopa kupingwa kwa kila alichoamini. Tumempoteza mtu muhimu. Ni pengo kubwa kwa upinzani na Bunge pia,” alisema Lyimo.

Naye Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema amepokea kwa mshituko mkubwa kifo cha Wangwe, na kuongeza kuwa kifo hicho ni pigo kwa chama chake kwani kimempoteza kiongozi mwenye msimamo.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka nchini Afrika Kusini alikokwenda kwenye ziara ya kikazi, Mbowe alisema amelazimika kukatiza ziara hiyo na kurejea nchini ili kuwahi mazishi ya Wangwe.

Saturday, July 19, 2008

Dk. Migiro yupo likizo Dar

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha Rose Migiro, yupo nchini kwa ajili ya likizo. Akizungumza leo, ameisifu Tanzania kwa jitihada za kukuza elimu na kupunguza vifo vya akina mama na watoto.

Amesema sifa hizo kwa Tanzania zinatokana na mafanikio hayo ambayo yanaendana na utekelezaji wa Malengo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa, yanayopaswa kufikiwa ifikapo mwaka 2015.

Amesema hatua zinazochukuliwa na Tanzania katika kukabiliana na umaskini ni za kujivunia na za kuigwa.

Dk. Migiro, ambaye yuko nchini kwa likizo yake ya kwanza tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo mwaka jana, alieleza kuwa ongezeko la uandikishaji wa wanafunzi nchini, uboreshaji wa huduma za afya ambazo zimepunguza idadi ya vifo vya akina mama na watoto pamoja na usawa wa kijinsia ni maeneo ya msingi ambayo Tanzania imefanya vizuri kuliko mataifa mengine ya Afrika.

Kuhusu upatikanaji wa ajira katika Umoja wa Mataifa, alisema habari kwamba Watanzania wananyimwa fursa za ajira katika Umoja huo kulinganisha na wenzao wa Kenya, Uganda na nchi za Afrika Magharibi si za kweli kwa vile unatoa fursa sawa kwa wote wanaotimiza vigezo ikiwamo kufaulu mitihani inayotolewa.

Aliwahamasisha vijana wa kitanzania kusoma lugha zaidi ya moja zinazotumiwa na umoja huo kwa sababu kujua Kiingereza pekee si kugezo kinachotosha kupata ajira katika umoja huo.

Dk. Migiro ambaye ni Mwanamke Mwafrika wa Kwanza duniani kuteuliwa katika wadhifa huo, yupo nchini kwa likizo yake ya kwanza na anatarajiwa kukutana na Rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Aman Abeid Karume.

Friday, July 18, 2008

Ndege ya rais yagongwa

Gari la usalama la Ikulu linaelezwa kuigonga ndege ya rais iliyokuwa imepaki katika hangar katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere.

Haijaelezwa tukio hilo limetokea lini lakini Rubani Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali amebainisha kuwa ndege hiyo iliyogongwa haijaharibika sana.

Taarifa zilizopatikana hata hivyo, hazijaeleza gari hilo lilikuwa linatafuta nini karibu na ndege hiyo ya rais iliyonunuliwa kwa bei mbaya, ambayo haitumiki kwenye safari nyingi za rais ingawa wakati inanunuliwa ilidaiwa ni kwa ajili ya kumuondolea rais aibu ya kusafiri na ndege za abiria.

Mtikila amtisha Rostam

Wakati mfanyabiashara na mwanasiasa, Rostam Aziz amefungua kesi dhidi ya Mchungaji Chritopher Mtikila, akimtaka athibitishe madai yake kuwa yeye (Rostam) ni raia wa Iran, Mtikila naye amempelekea barua Rostam, akimtaka amwombe radhi kwa kumdhalilisha.

Katika Demand Note hiyo, Mtikila ametoa siku 14 kwa Rostam kumwomba radhi na kumlipa fidia y ash bilioni tatu. Pia Demand Note hiyo inavihusu vyombo vya habari kadhaa, ambavyo viliripoti hayo maneno ya Rostam ambayo Mtikila anadai kuwa yamemdhalilisha.

Maneno anayoyalalamikia ni yale yaliyotolewa na Rostam alipokutana na waandishi wa habari hivi karibuni kuwa ‘Mtikili hastahili heshima ya kujibiwa na mimi (Rostam).

Pia Mtikila analalamikia maneno ya Rostam yanayobainisha kuwa kauli za Mtikila ni za kinyaa na zinachochea machafuko nchini.

Tuesday, July 8, 2008

BAJETI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI 2008/09

HOTUBA YA WAZIRI WA NISHATI NA MADINI MHESHIMIWA WILLIAM MGANGA NGELEJA (MB), AKIWASILISHA KATIKA BUNGE MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA ZA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA 2008/09

1. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na Taarifa iliyowasilishwa leo mbele ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyochambua Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa kazi za Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2007/08. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2008/09.

A: UTANGULIZI

2. Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza makadirio ya matumizi ya fedha za Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2008/09.

3. Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena kutoa shukurani kwa Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Waziri wa Nishati na Madini mwezi Februari, 2008, uteuzi ambao umenipa fursa kwa mara ya kwanza kuwasilisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia, nawashukuru wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa William Hezekia Shellukindo (Mb) na Makamu Mwenyekiti Mhe. Dkt. Harrison George Mwakyembe (Mb) kwa mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2008/09. Nakushukuru wewe binafsi Mhe. Spika, Naibu Spika pamoja na wenyeviti wote wa Bunge kwa kuliongoza Bunge hili Tukufu kwa umahiri mkubwa. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri wanaonipa mimi na wenzangu katika kusimamia na kuongoza sekta za nishati na madini. Nina imani kuwa ushirikiano huo utaendelea ili tuweze kufikia malengo ya Taifa hasa katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

4. Mheshimiwa Spika, pia, naomba kutumia fursa hii, kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika. Hiyo ni heshima kubwa kwa Taifa letu. Pia, nampongeza Mhe. Rais kwa juhudi zake katika kuvutia wawekezaji na ukuzaji mahusiano na nchi nyingine ikiwa ni pamoja na kufanikisha ziara ya Mhe. George W. Bush, Rais wa Marekani na kufanikisha kufanyika kwa mkutano wa Leon Sullivan jijini Arusha mwezi Juni 2008. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kufanikisha kusuluhisha mgogoro wa kisiasa uliotokana na vurugu za uchaguzi nchini Kenya akiwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.

5. Mheshimiwa Spika, vilevile, nampongeza Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb), kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, nakupongeza wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa kuteuliwa kwako kuwa Makamu wa Rais wa Chama cha Wabunge wa Nchi za Jumuiya ya Madola (CPA). Aidha, nawapongeza Mhe. Celina Ompeshi Kombani (Mb), kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI); Mhe. Profesa Peter Msolla (Mb), Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia; Mhe. Dkt. Shukuru Kawambwa (Mb), Waziri wa Miundombinu; Mhe. Stephen Wassira (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika; Mhe. Aggrey Mwanri (Mb), Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Mhe. Hezekiah Chibulunje (Mb), Naibu Waziri wa Miundombinu na Mhe. Dkt. Milton Makongoro Mahanga (Mb), Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kwa uteuzi wao kufuatia mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Mhe. Rais mwezi Mei, 2008. Napenda kuwapongeza Mawaziri na Naibu Mawaziri wote walioteuliwa na Mhe. Rais mwezi Februari, 2008 kushika nyadhifa hizo akiwemo Mhe. Adam Kighoma Ali Malima, Mbunge wa Mkuranga, aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Aidha, nampongeza Mheshimiwa Benedict Ngalama Ole-Nangoro (Mb), kwa kuchaguliwa kwake kuwa Mbunge wa Jimbo la Kiteto. Pia, nawapongeza Mheshimiwa Al-Shymaa John Kwegyr (Mb), na Mheshimiwa Mchungaji Dkt. Getrude P. Rwakatare (Mb), kwa kuteuliwa kwao kuwa Wabunge wa Bunge hili Tukufu.

6. Mheshimiwa Spika, mwezi Oktoba, 2007 Bunge lako lilimpoteza Mheshimiwa Salome Joseph Mbatia (Mb), aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, aliyefariki dunia kufuatia ajali ya gari. Aidha, mwezi Desemba, 2007 Bunge lako lilimpoteza Mheshimiwa Benedict Kiroya Losurutia aliyekuwa Mbunge wa Kiteto. Pia, nampa pole Mhe. Adam Kighoma Ali Malima, Naibu Waziri wa Wizara ya Nishati na Madini kwa kufiwa na mke wake. Natoa pole kwako, familia zao na wote walioguswa na misiba hiyo. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amin!

7. Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Machi, 2008, kulitokea maafa yaliyosababishwa na mafuriko katika baadhi ya machimbo ya madini ya tanzanite Merelani, Wilayani Simanjiro ambapo wachimbaji wadogo 78 walipoteza maisha. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilifanikiwa kuopoa miili ya watu wote 78 waliopoteza maisha. Natoa pole kwa Mhe. Christopher Ole Sendeka, Mbunge wa Simanjiro, ndugu, jamaa na Taifa kwa ujumla. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi, Amin.

8. Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Sengerema na viongozi wa wilaya ya Sengerema kwa ujumla kwa ushirikiano wao wanaonipa na juhudi zao katika kazi mbalimbali ambazo zinachangia maendeleo ya Jimbo na wilaya yetu kwa ujumla. Ni matumaini yangu kuwa tutaendelea kushirikiana zaidi kwa manufaa ya Jimbo letu na Taifa kwa ujumla.

9. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naishukuru familia yangu, wazazi na ndugu zangu kwa jinsi wanavyoendelea kuniimarisha katika utekelezaji wa majukumu yangu, hususan, mke wangu Blandina ambaye anaendelea kuisimamia familia yetu pamoja na kumlea binti yetu mwenye umri wa mwezi mmoja na nusu sasa. Nakushukuru sana mke wangu Blandina.

B: MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO
NA BAJETI YA MWAKA 2007/08

10. Mheshimiwa Spika, Mpango na Bajeti kwa mwaka 2007/08, ulitekelezwa kwa kuzingatia:- Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2005; malengo ya MKUKUTA; Mwongozo wa Kutayarisha Mpango na Bajeti 2007/08 – 2009/10; ushauri na maelekezo ya Mhe. Rais alipotembelea Wizara ya Nishati na Madini Januari, 2006; na ushauri uliotolewa na iliyokuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara. Kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mwaka 2007/08 zilikuwa ni:- kukamilisha uanzishwaji wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rural Energy Agency - REA) pamoja na Mfuko wa Nishati Vijijini (Rural Energy Fund - REF); kukamilisha mkakati wa kurekebisha sekta ya umeme; kuimarisha mfumo wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme; kuanzisha miradi ya hifadhi ya mafuta na kuiwezesha TPDC kushiriki katika biashara ya mafuta; kuratibu utekelezaji wa miradi ya gesi asilia; kukamilisha maandalizi ya sheria ya mafuta na sheria ya gesi asilia, kuhamasisha matumizi bora na uendelezaji wa nishati jadidifu na mbadala; kuendelea kukuza uwekezaji katika sekta za nishati na madini kwa kuweka mazingira shindani ya kuvutia wawekezaji; kuendelea kuhamasisha ujasiriamali kwenye miradi ya kuongeza thamani madini kama ukataji na usanifu wa madini na utengenezaji wa bidhaa za madini ya vito; kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata mikopo na teknolojia mwafaka katika utafutaji, uchimbaji na uchenjuaji wa madini; kuongeza maduhuli ya Serikali yatokanayo na madini; na kuimarisha masuala ya usalama, afya na utunzaji wa mazingira katika shughuli za utafutaji na uchimbaji madini.

Mafanikio

11. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2007/08, Wizara ilipata mafanikio yafuatayo:- kupitishwa kwa Sheria ya Umeme na Sheria ya Mafuta mwezi Aprili, 2008; kuanza kazi rasmi kwa Wakala wa Nishati Vijijini mwezi Oktoba, 2007; kukamilika kwa kazi ya kukarabati jenereta yenye uwezo wa KVA 320 mjini Mbinga mwezi Septemba, 2007; kununuliwa kwa jenereta mbili zenye uwezo wa KVA 1,250 kila moja kwa ajili ya mji wa Mbinga na mbili zenye uwezo wa KVA 600 kila moja kwa ajili ya mji wa Ludewa; kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme chenye uwezo wa MW 100 katika eneo la TANESCO-Ubungo Dar es Salaam; kugundulika kwa gesi asilia katika kisima cha Kiliwani Kaskazini Namba 1 Kilwa; kupanuka kwa matumizi ya gesi asilia ambapo viwanda vinne (4) vilivyopo Dar es Salaam vilipatiwa huduma hiyo, viwanda hivyo ni Serengeti Breweries, Simba Plastic, Namera Textile na Simba Steel; kujadiliwa na kukamilika kwa mikataba mitatu [3] mipya ya utafutaji wa mafuta; kuanzishwa kwa Kitengo cha Ukaguzi wa Shughuli za Uzalishaji na Biashara ya Madini ya Dhahabu katika Migodi Mikubwa (Gold Audit Programme - GAP) mwezi Agosti, 2007; kuunganishwa kwa Mfumo wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini (Mining Cadastre Information Management System – MCIMS) katika ofisi 22 za madini mikoani na Makao Makuu ya Wizara; kufunguliwa kwa ofisi ya afisa madini mkazi mkoani Kigoma mwezi Septemba, 2007; kupitishwa kwa muundo mpya wa Wizara mwezi Agosti, 2007; na kujitokeza kwa watumishi 117 wa Wizara kupima afya zao kuhusu UKIMWI.

Changamoto

12. Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyotajwa hapo juu, kumekuwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na:- kuhimili kasi kubwa ya upandaji wa bei ya mafuta katika soko la dunia; kasi ndogo ya kufikisha umeme vijijini kwa Watanzania walio wengi; kutokuwepo rasilimali fedha inayokidhi mahitaji halisi ya kuwezesha ukarabati na upanuzi wa mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme; kukabiliana na ongezeko kubwa la gharama za utekelezaji wa miradi; kupunguza hujuma [vandalism] zinazofanywa kwenye miundombinu ya umeme; mitaji isiyokidhi uwekezaji katika miradi ya gesi asilia ya Songo Songo na Mnazi Bay; kuanzisha hifadhi ya Taifa ya mafuta ya Petroli; upungufu wa watumishi wa taaluma mbalimbali; na kupata rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuharakisha upatikanaji wa huduma bora za nishati vijijini.


SEKTA YA NISHATI

Ukuaji wa Sekta na Mchango wake katika Pato la Taifa

13. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007, shughuli za kiuchumi za umeme na gesi asilia zilikua kwa asilimia 10.9 ikilinganishwa na ukuaji hasi wa asilimia 1.9 mwaka 2006, kwa bei za mwaka 2001. Miongoni mwa sababu za ukuaji huo ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji umeme kutoka katika mitambo ya dharura; kuwepo kwa maji ya kutosha kwenye mabwawa ya kuzalisha umeme; kukua kwa matumizi ya umeme viwandani kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji katika viwanda vya chuma na saruji. Aidha, mchango wa kiuchumi wa umeme na gesi asilia katika Pato la Taifa ulikuwa asilimia 2.1 mwaka 2007 ikilinganishwa na asilimia 2.0 mwaka 2006, kwa bei za mwaka 2001.

14. Mheshimiwa Spika, mwaka 2007, umeme uliozalishwa ulikuwa Megawatt-hour (MWh) 4,204,620 ikilinganishwa na MWh 3,592,470 mwaka 2006, sawa na ongezeko la asilimia 17. Ongezeko hilo lilitokana na kuwepo kwa maji ya kutosha, hususan, katika mabwawa ya Mtera na Kidatu yanayotumika kuzalisha umeme.

Kupeleka Umeme Vijijini

15. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/08, miradi ya usambazaji umeme vijijini ilitekelezwa kwa kasi ndogo kutokana na upungufu wa fedha baada ya Serikali kuelekeza rasilimali nyingi katika kukabiliana na matatizo mbalimbali yaliyosababishwa na ukame. Pia, miradi mingi ya kupeleka umeme vijijini inahitaji fedha nyingi ikilinganishwa na mapato madogo ya TANESCO yatokanayo na malipo ya huduma hiyo.

Wakala wa Nishati Vijijini

16. Mheshimiwa Spika, Wakala wa Nishati Vijijini ulianza kazi rasmi mwezi Oktoba, 2007 na umeajiri jumla ya watumishi 21 kati ya 30 wanaohitajika. Wakala unakusudia kuwa na wafanyakazi makini wachache ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuelekeza rasilimali katika kupeleka umeme vijijini.

17. Mheshimiwa Spika, majukumu makuu ya Wakala ni:- kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji katika upatikanaji wa huduma za nishati bora vijijini, kwa kutoa ruzuku kwa wawekezaji kutoka sekta binafsi na ya umma; na kuwasaidia wawekezaji kuandaa miradi ya nishati itakayowasilishwa kwenye Bodi ya Nishati Vijijini kwa ajili ya uamuzi wa miradi hiyo kupatiwa ruzuku. Mfumo wa utendaji wa Wakala unahamasisha ubia wa sekta ya umma na binafsi (Public-Private Partnership – PPP) ili kuiwezesha sekta binafsi kushiriki vilivyo katika kuchangia kutoa huduma za nishati kwa wananchi vijijini. Uwezeshaji wa miradi utazingatia uwiano wa kijiografia na vigezo vingine vilivyoainishwa katika Sheria ya Nishati Vijijini ya mwaka 2005 na kama ilivyoelezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005, Ibara ya 43 (c).

18. Mheshimiwa Spika, pamoja na uchanga wake, Wakala tayari umeanza kujenga mtandao (network) wa wadau mikoani na wilayani ikiwa ni pamoja na wamiliki na waendelezaji wa vyanzo mbalimbali vya nishati vijijini. Hata hivyo, changamoto zilizojitokeza ni pamoja na:- kutopata rasilimali za kutosha kwa ajili ya kuharakisha upatikanaji wa nishati bora vijijini; kuwaelimisha wadau majukumu ya Wakala; na uwezo mdogo wa kifedha vijijini hivyo kusababisha uwekezaji katika miradi ya nishati kushindwa kuwa kivutio kwa wawekezaji.

Upelekaji Umeme Makao Makuu ya Wilaya

19. Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2005 ilielekeza kuongeza kasi ya kupeleka umeme vijijini kupitia mfuko wa Nishati Vijijini. Katika mwaka 2007/08, Wakala wa Nishati Vijijini kupitia Mfuko wa Nishati Vijijini (REF) umetoa ruzuku kwa ajili ya kupeleka umeme katika makao makuu ya wilaya tano (5) za Kilolo, Kilindi, Mkinga, Bahi na Uyui. Pia, baadhi ya maeneo ambayo yalipatiwa fedha kutoka katika Mfuko huo ni Mto wa Mbu, Matema Beach na Shule ya Sekondari ya Chief Oswald Mang’ombe iliyopo Musoma. Aidha, Mfuko pia ulitoa fedha kwa ajili ya kulipa fidia ya mali za wananchi zilizoathirika wakati wa kutathmini njia ya usambazaji umeme kwenye mradi wa njia ya bomba la gesi ya kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam.

20. Mheshimiwa Spika, kuhusu miji ya Mbinga na Ludewa, jenereta mpya zimenunuliwa na ufungaji unaendelea. Aidha, mifumo ya usambazaji umeme katika miji hiyo imekamilika. Mipango ya muda mrefu ni kuipatia miji hii pamoja na Songea na Namtumbo umeme wa gridi ya Taifa. Serikali ya Uswidi (Sweden) wamethibitisha ufadhili wa mradi wa Makambako hadi Songea pamoja na miji ya Mbinga, Ludewa, Namtumbo, na vijiji vilivyoko katika laini zitakazojengwa. Mradi pia utahusu upanuzi wa mifumo ya usambazaji umeme katika miji ya Makambako, Njombe na Songea. Gharama ya mradi ni US$ 70.4 milioni. Asilimia 90 zitatolewa kama msaada na asilimia 10 kama mkopo wa masharti nafuu.

Sheria Mpya za Umeme, Mafuta ya Petroli na Gesi Asilia

21. Mheshimiwa Spika, Muswada wa Sheria ya Umeme ulipitishwa na Bunge mwezi Aprili, 2008, na kuridhiwa na Mhe. Rais tarehe 6 Juni, 2008. Sheria mpya itaimarisha udhibiti wa uzalishaji, usafirishaji, usambazaji pamoja na matumizi bora ya umeme, itawezesha biashara ya umeme na nchi jirani, na pia itaweka mipango ya kusambaza umeme vijijini. Aidha, Sheria hii imetambua umuhimu wa kuiimarisha TANESCO katika kipindi cha mpito ili iweze kuhimili ushindani kutoka sekta binafsi muda utakapowadia. Sheria mpya vilevile imefafanua jukumu la wawekezaji katika sekta ya umeme kutoa huduma kwenye maeneo ya vyanzo vya nishati, pamoja na maeneo yote ambayo yanapitiwa na njia kuu za kusafirisha umeme.

22. Mheshimiwa Spika, pamoja na masuala mengine, Sheria hiyo imefafanua majukumu na mamlaka ya Waziri mwenye dhamana ya nishati ikiwa ni pamoja na kusimamia sekta ya umeme katika utekelezaji sera na uandaaji wa mipango na mikakati ya kuhamasisha soko lenye ushindani kwa lengo la kuvutia wawekezaji binafsi na kulinda maslahi ya Taifa.

23. Mheshimiwa Spika, Muswada wa Sheria ya Mafuta ya Petroli ulipitishwa na Bunge mwezi Aprili, 2008, na kuridhiwa na Mhe. Rais tarehe 6 Juni, 2008. Aidha, Rasimu ya Sheria ya Gesi Asilia imeandaliwa na Wizara ipo katika hatua za kupata ridhaa ya Serikali.

24. Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa mchakato wa kutungwa Sheria Mpya za Umeme na Mafuta ya Petroli, Wizara inaratibu utayarishaji wa kanuni na taratibu husika kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa sheria hizo. Wizara itashirikiana na wadau muhimu kuhakikisha kuwa kanuni hizo zinakamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2008.

Mfumo wa Uendeshaji wa TANESCO

25. Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa TANESCO na muundo wake yanaendelea kufanyika yakilenga katika uboreshaji wa huduma, ufanisi na kujiendesha kibiashara. Pamoja na kufikia kiwango cha ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 96 katika mwaka 2006 na 2007, TANESCO imeendelea kuathiriwa na upungufu wa fedha uliosababishwa na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji hususan, katika uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.

Mifumo ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme

26. Mheshimiwa Spika, tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara kwenye gridi ya Taifa limeanza kupungua kutokana na ukarabati uliofanywa katika miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme katika gridi ya Taifa. Ukarabati uliendelea kufanyika katika baadhi ya maeneo na nguvu zaidi zilielekezwa katika maeneo yaliyokuwa na uchakavu mkubwa.

Umeme Sumbawanga

27. Mheshimiwa Spika, tatizo la kukatikakatika kwa umeme Sumbawanga linatarajiwa kwisha mwishoni mwa mwaka 2008 kufuatia ahadi iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Maji wa Zambia katika kikao kati yake na Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania kilichofanyika tarehe 30/06/2008 mjini Dodoma.
Umeme Kigoma

28. Mheshimiwa Spika, mkakati wa muda mfupi wa kuongeza upatikanaji wa umeme wa Kigoma ni ununuzi wa mitambo mitano yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya MW 6. Fedha za ununuzi huo takriban Shilingi bilioni 13.8 zimetengwa na ufungaji wa mitambo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2009.

29. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Japani ilikuwa na mpango wa kujenga kituo cha kupozea umeme cha New Oysterbay ili kuboresha upatikanaji wa umeme katika jiji la Dar es Salaam. Hata hivyo, mradi haukuweza kuanza katika muda uliopangwa kutokana na upeo wa mradi kubadilika na kuchelewa kupata umiliki wa kiwanja. Kazi zilizofanyika ni pamoja na kumwajiri mshauri na kukamilisha kazi za awali za ujenzi.

Mradi wa kuendeleza na kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati Nchini (Tanzania Energy Development and Access Expansion Project – TEDAP)

30. Mheshimiwa Spika, makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa kuendeleza na kupanua wigo wa upatikanaji wa nishati nchini (Tanzania Energy Development and Access Expansion Project –TEDAP) yalifikiwa kati ya Serikali na Benki ya Dunia mwezi Januari, 2008. Utekelezaji wa mradi ulianza mwezi Aprili, 2008. Lengo la mradi huu ni kuboresha mifumo ya usafirishaji na usambazaji umeme katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro (Dola za Marekani milioni 85.8); na kuendeleza mifumo ya umeme nje ya gridi (off-grid electrification) kwa kutumia nishati jadidifu kwa ajili ya matumizi majumbani, katika taasisi na kwenye shughuli za uzalishaji mali (Dola za Marekani milioni 22.5). Mradi pia umelenga katika kujenga uwezo wa kitaalamu wa Wakala wa Nishaji Vijijini, TANESCO na Wizara, ambapo kiasi cha Dola za Marekani milioni 3.2 zitatumika.

Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Umeme PSMP (Power System Master Plan)

31. Mheshimiwa Spika, maandalizi ya kutayarisha Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Umeme (Power System Master Plan – PSMP) ambao utatumika kuongoza maendeleo endelevu ya sekta yalikamilika katika mwaka 2007/08. Utayarishaji wa PSMP umezingatia Sera ya Taifa ya Nishati, hususan, upanuzi wa wigo wa vyanzo vya nishati kwa ajili ya kuzalisha umeme ili kupunguza utegemezi katika umeme utokanao na maji. Aidha, wataalamu wa Wizara na TANESCO walishiriki katika hatua na maeneo mbalimbali ya kutayarisha PSMP, kwa mfano, uandaaji wa mipango inayozingatia unafuu wa gharama (Least-Cost Expansion Plans) katika uzalishaji na usafirishaji wa umeme. Wizara iko katika hatua za mwisho za kupata ridhaa ya Serikali kwa ajili ya kutumia Mpango Kabambe.

32. Mheshimiwa Spika, Mipango ya muda wa kati kulingana na PSMP inahusisha miradi ya Mchuchuma (MW400), Rusumo (MW60), Ruhudji (MW358) na katika kipindi cha muda mrefu, miradi ya Stiegler’s Gorge (MW2,400), Rumakali (MW222), Mpanga (MW158) na Masigira (MW144).

Hifadhi ya Taifa ya Mafuta

33. Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko mbalimbali yaliyotokea duniani yakiwemo ya kisiasa, kiuchumi, hali ya hewa pamoja na uzoefu kutoka nchi nyingine, Serikali iliridhia kuanzishwa kwa hifadhi ya Taifa ya mafuta nchini kwa ajili ya kutumika inapotokea dharura na kutengemaza mwenendo wa bei za mafuta ya petroli nchini. Uamuzi huu ulifikiwa mwezi Machi, 2008. Ili kufanikisha hilo, Serikali kupitia TPDC inaendelea na mchakato wa utekelezaji wa uamuzi huo.

Ujenzi wa Kiwanda cha kusafisha mafuta na bomba la mafuta la Dar es Salaam – Mwanza

34. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na majadiliano na mwekezaji aliyeonesha nia ya uendelezaji wa miradi ya kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta ya petroli. Aidha, Serikali inakamilisha uchunguzi wa kampuni husika ya Noor - Oil and Industrial Technology (NOIT) na wabia wake. Endapo uhakiki utaleta matokeo mazuri, Serikali itaridhia NOIT kuanza upembuzi yakinifu.

Shughuli za Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta na Gesi Asilia

35. Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005 (Ibara ya 43 (h)) inatutaka kuendelea kutafuta mafuta kwa kasi zaidi. Kuanzia mwezi Julai, 2007 hadi Juni 2008, Serikali imesaini mikataba mitatu ya utafutaji mafuta ya petroli na kampuni zifuatazo:- Dodsal Hydrocarbon & Power ya India eneo la Ruvu; Funguo Petroleum ya Australia, magharibi mwa eneo la Songo Songo; na Hydrotanz ya Visiwa vya Morisi (Mauritius), eneo la Kaskazini ya Mnazi Bay. Hii inafanya idadi ya mikataba yote ya utafutaji mafuta nchini kufikia 22, makampuni 13. Kampuni hizo zinaendelea na shughuli mbalimbali za utafutaji mafuta na gesi asilia ikiwemo kudurusu takwimu za kijiolojia na kijiofizikia katika maeneo husika, kuchukua takwimu za mitetemo, na kufanya maandalizi ya uchimbaji wa visima vya utafiti.

36. Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa utafutaji wa mafuta na gesi asilia uliofanywa na Kampuni ya Ndovu Resources katika Mkoa wa Lindi, umethibitisha kuwepo kwa gesi asilia katika kisima cha Kiliwani Kaskazini Namba 1. Kampuni hiyo inajiandaa kuchimba visima zaidi ili kubaini kiasi cha gesi kilichopo. Kampuni ya Maurel & Prom kutoka Ufaransa inayofanya utafiti katika maeneo ya Mkuranga imekamilisha tathmini ya taarifa za mitetemo na imeainisha maeneo ambayo vitachimbwa visima vya kuhakiki (appraisal wells) kiasi cha gesi kilichopo. Aidha, inachimba kisima kingine cha utafutaji (exploratory well) katika eneo la Mafia.

Gesi Asilia ya Songo Songo

37. Mheshimiwa Spika, gesi asilia ya Songo Songo ilianza kutumika kuanzia Julai, 2004 kwa ajili ya kuzalisha umeme Dar es Salaam na kutumika kama nishati viwandani. Kufuatia ongezeko la mahitaji ya gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme, umejitokeza ulazima wa kuongeza uwezo wa mtambo wa kusafisha gesi kutoka futi za ujazo milioni 70 kwa siku hadi futi za ujazo milioni 140 kwa siku ili kusafisha gesi zaidi kwa ajili ya mitambo iliyopo na mipya. Kazi ya upanuzi inategemewa kukamilika mwezi Agosti, 2009.

38. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kupitia mikataba ya mradi wa Songo Songo na kufanya marekebisho ya mikopo husika ili kupunguza capacity charge. Hii ni hatua muhimu kwani marekebisho husika yatapunguza capacity charge kwa Dola za Marekani takriban milioni 1.0 kwa mwezi. Aidha, Serikali inaendelea kupitia mikataba yote ya nishati.

Mradi wa Gesi Asilia ya Mnazi Bay

39. Mheshimiwa Spika, kazi ya kupima na kutathmini kiasi cha fidia ya mali kwa ajili ya bomba la gesi asilia toka Mnazi Bay hadi Mtwara imekamilika na tayari bomba limetandazwa. Visima vitatu (Mnazi Bay 2, 3 na Msimbati 1) vimechimbwa na vimetoa matokeo ya kuwepo kwa gesi asilia ya kutosha kutekeleza mradi wa umeme wa MW 30 na miradi mingine.

40. Mheshimiwa Spika, katika kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005 (Ibara ya 43 (a) (ii) mikoa ya Lindi na Mtwara iliwekwa katika mpango wa kupatiwa umeme unaozalishwa na Kampuni ya Artumas kwa kutumia gesi asilia ya Mnazi Bay. Miji ya Lindi na Mtwara tayari imeanza kupata umeme unaotokana na mradi huo tangu Desemba, 2006. Aidha, mikataba ya kuiwezesha Artumas kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme katika maeneo mengine ya mikoa hiyo inatarajiwa kukamilishwa mwishoni mwa mwezi Julai, 2008.

Usimamizi na Udhibiti wa Shughuli za Nishati

41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/08, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) iliendelea na kazi ya kutoa leseni kwa watoa huduma wa umeme na mafuta, kuhakiki bei za umeme na kanuni ya kupanga ushuru kwa kutumia miundombinu ya gesi asilia ya Songas katika soko la nishati, kukagua na kuhakiki uwezo, ubora na usalama wa vituo vya kuzalisha umeme pamoja na vituo na maghala ya kuhifadhia mafuta ili kuleta nidhamu katika biashara ya mafuta. Aidha, EWURA ilitoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Mamlaka hiyo kwa wadau kupitia warsha na makongamano. Vilevile EWURA kwa kushirikiana na Shirika la Viwango Nchini (TBS) ilifanikiwa kuvinasa na kuvifungia vituo 154 kati ya 194 vilivyogunduliwa kutokana na kujihusisha katika kuchakachua mafuta ya petroli.

42. Mheshimiwa Spika, kama Waheshimiwa Wabunge wanavyofahamu, uhusiano kati ya TANESCO na IPTL umekuwa wa mashaka kufuatia kutokubaliana na kiwango cha capacity charge kinachotozwa. Maamuzi yaliyotolewa na Kituo cha International Centre for Investment Disputes, mwaka 2001 wakati wa usuluhishi wa shauri lililowasilishwa na TANESCO dhidi ya IPTL, iliamriwa kuwa capacity charge itakokotolewa kwa kutumia mtaji (equity) wa asilimia 30 na faida ya asilimia 22.31. Kiwango cha equity kilichotumika kilikuwa Dola za Marekani milioni 86.54.

43. Mheshimiwa Spika, kufuatia uchunguzi uliofanywa na TANESCO imegundulika kuwa equity halisi iliyotumika ilikuwa shilingi 50,000. Kwa maana hiyo, malipo ambayo TANESCO imekuwa ikiilipa IPTL kama capacity charge ni zaidi ya kiasi kilichostahili. Huu ndio msingi wa mgogoro wa sasa ambao Serikali/TANESCO na IPTL wanaendelea kujadili.

Gharama za Uendeshaji na Bei za Umeme

44. Mheshimiwa Spika, wakati EWURA inapotafakari maombi ya kurekebisha bei za umeme hutumia vigezo vyenye mwelekeo wa ufanisi wa gharama katika uwekezaji na ubora wa huduma kwa mteja. Aidha, maelekezo hutolewa kuhusu hatua za kuchukua za kupunguza gharama za uendeshaji bila kumtaka mlaji kulipia.

45. Mheshimiwa Spika, Gharama za uzalishaji za TANESCO zimepanda kutoka shilingi 96/kWh mwaka 2005 hadi shilingi 120/kWh mwaka 2007. Gharama za ujenzi wa njia za umeme zimepanda kutokana na kupanda kwa bei ya chuma na shaba kwenye soko la dunia. Gharama ya ujenzi wa njia ya kV 33 zimepanda kutoka shilingi milioni 18 kwa kilometa mwaka 2006 hadi shilingi milioni 35 kufikia Januari, 2008. Bei za nguzo zimepanda kutoka shilingi 96,000 mwaka 2005 hadi shilingi 153,017 kwa mwaka 2007 kwa nguzo za futi 10. TANESCO imelazimika kununua nguzo kutoka nje, ikiwemo Afrika Kusini kutokana na bei kuwa nafuu zaidi.

Uendelezaji wa Nishati Jadidifu na Mbadala

46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/08, Wizara iliendelea kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu na mbadala kwa kuzindua mradi wa umemenuru unaofadhiliwa na Sida katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Mtwara na Mbeya. Jumla ya mafundi sanifu na wafanyabiashara 72 katika mikoa hiyo walifundishwa namna ya kufunga mifumo ya umemenuru majumbani - solar home systems na jinsi ya kuboresha uendeshaji wa biashara zao. Aidha, utekelezaji wa mradi wa majaribio wa Mwanza unaofadhiliwa na Global Environment Facility, (GEF) uliendelea katika mikoa ya Kagera, Mara na Shinyanga. Ili kuendeleza uzoefu uliopatikana mkoani Mwanza katika mikoa jirani iliyotajwa, mafunzo yalitolewa kwa mafundi mchundo 170. Mafunzo hayo pia yalitolewa kwa walimu 12 kutoka vituo sita vya VETA ili vituo hivyo vipate uwezo wa kutoa mafunzo ya umemenuru kwa wananchi wengine. Aidha, shughuli za ufungaji wa mifumo ya umemenuru ziliendelea katika vituo 47 vikiwemo vya afya na shule za sekondari.

47. Mheshimiwa Spika, mradi huo pia ulifanikiwa kukopesha SACCOS mbili kwa majaribio, ambapo wanachama 40 kutoka SACCOS hizo waliweza kufungiwa mifumo ya umemenuru ili kuhamasisha teknolojia hii. Semina zilifanyika kwa ajili ya maafisa maendeleo ya jamii 130 kutoka mikoa ya Kagera, Shinyanga na Mara kuanzia ngazi ya mkoa hadi kata.

48. Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2005 inatambua umuhimu wa kutumia nishati mbadala, ikiwemo nishati ya upepo. Tafiti zimefanywa na zinaonesha kuwa Tanzania ina maeneo kadhaa ambayo yana uwezekano wa kuzalisha umeme utokanao na nishati ya upepo. Maeneo hayo ni pamoja na mkoa wa Singida, Iringa, Kilimanjaro, Manyara na Rukwa. Kwa kuzingatia umuhimu wake, Serikali kwa kushirikiana na TANESCO iliendelea kujadiliana na wadau wenye nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa umeme utokanao na nishati ya upepo ili kupanua wigo wa vyanzo vya nishati kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Mpango wa Kuzalisha Bayofueli Nchini

49. Mheshimiwa Spika, Suala la bayofueli limeendelea kufuatiliwa kwa makini. Kama unavyofahamu bayofueli inaweza kuzalishwa kutokana na mimea mbalimbali ikiwemo miwa, mtama, mibono na michikichi. Serikali iliendelea kushauriana na Serikali ya Uswidi kuhusu uwezekano wa kuchangia katika kutekeleza Mradi wa kuandaa Sera, Sheria na Muundo Kiasasi (Strengthening the Policy, Legal, Regulatory and Institutional Framework). Mradi huu una lengo la kuandaa mazingira sahihi ya uendelezaji endelevu wa bayofueli nchini. Hata hivyo, inatarajiwa kwamba kilimo cha mazao ya bayofueli kitazingatia maslahi ya Taifa kuhusu ajira, ardhi, mazingira na upatikanaji wa chakula. Tangu mwaka 2005, kampuni nane (8) zimepata hati ya uwekezaji kutoka Kituo cha Taifa cha Uwekezaji, na zipo taasisi 30 zinazohusika na masuala ya bayofueli nchini.

50. Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa rasimu ya Mwongozo wa bayofueli (Biofuels Guidelines) ikiwa ni hatua za awali na muda mfupi za kuwaongoza wawekezaji na wadau mbalimbali wakati maandalizi kuhusu masuala ya sera, sheria pamoja na kanuni na miundo kiasasi yakishughulikiwa. Rasimu ya Mwongozo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2008.

Maporomoko madogomadogo ya Maji na Jotoardhi

51. Mheshimiwa Spika, ubainishaji wa maporomoko madogomadogo ya maji uliendelea katika mikoa ya Iringa na Mbeya ambapo maeneo 30 mapya yenye uwezo wa takriban MW 29 yalifanyiwa tathmini ya awali. Aidha, Wizara imeendelea kutafiti uwezekano wa kuwepo rasilimali ya kutosha ya jotoardhi kwa ajili ya kuzalisha umeme. Sampuli zilizochukuliwa katika eneo la Songwe na Ziwa Ngozi zilifanyiwa utafiti wa kimaabara nchini Ujerumani. Matokeo ya utafiti yaliashiria uwezekano wa kuwepo rasilimali kubwa ya jotoardhi hapa nchini. Uhakika wa ukubwa wa rasilimali hiyo utathibitishwa baada ya uchimbaji wa visima vya utafiti kufanyika.

Matumizi Bora na Uendelezaji wa Vyanzo Mbadala vya Nishati

52. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuendeleza elimu ya matumizi bora ya nishati mbadala hapa nchini kupitia mradi wa SADC-ProBEC, mafunzo ya utengenezaji majiko sanifu yalitolewa kwa mafundi 40 katika wilaya za Songea na Mufindi. Aidha, matanuri 60 ya kukaushia tumbaku yatumiayo teknolojia sanifu yalijengwa kwa ajili ya majaribio mkoani Tabora na matokeo ya awali yanaonesha uokoaji wa kuni kwa asilimia 50 ikilinganishwa na matanuri ya kawaida.

53. Mheshimiwa Spika, katika kuhamasisha uendelezaji wa vyanzo mbadala wa kuni na mkaa kwa kupikia, Wizara kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi ilifanya utafiti kuhusu gesi itokanayo na matumizi ya vitofali vya makaa ya mawe wakati wa kupika. Matokeo ya awali yameonesha kuwepo umuhimu wa kuboresha teknolojia ya utengenezaji wa vitofali ili kupunguza gesi yenye sumu hususan itokanayo na sulphur kwa lengo la kulinda afya za watumiaji. Ili kutekeleza hilo, majadiliano kati ya Wizara, Kampuni iliyotengeneza vitofali na Tume ya Sayansi na Teknolojia yameanza ili kutafuta namna ya kuboresha teknolojia hiyo.

54. Mheshimiwa Spika, ukaguzi wa vifaa vinavyotumia umeme mwingi katika viwanda (kwa mfano mota, viyoyozi na taa) ulifanyika katika viwanda vikubwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Mwanza na Mbeya. Matokeo yanaonesha upotevu mkubwa wa umeme kutokana na uchakavu na kutokidhi kwa viwango vya ubora vya matumizi bora ya nishati. Upotevu huo unaweza kupungua kwa asilimia 30 hadi 40 iwapo vifaa vyenye viwango vya ubora unaotakiwa vitatumiwa.

SEKTA YA MADINI

Ukuaji na Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa

55. Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2005 (Ibara za 38 na 39) inabainisha hatua za kuchukua ili kuharakisha ukuaji wa mchango wa sekta ya madini kwenye uchumi wa Taifa. Hatua hizo ni pamoja na: kuendelea kukuza ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi; kuweka mazingira bora ya kuvutia wawekezaji; kuimarisha usalama migodini; kuwaendeleza wachimbaji wadogo; kuboresha mahusiano kati ya wachimbaji wadogo na wakubwa; na kuendeleza utafutaji wa madini nchini. Ilani hiyo pia inaelekeza kuendelea kuboresha Sera ya Madini kwa lengo la kuboresha ushiriki wa Serikali katika umiliki wa migodi, mfumo wa kodi katika sekta ya madini ili sekta ya madini iwe na manufaa zaidi kwa Taifa.

56. Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo yaliyoainishwa na Ilani ya Uchaguzi ya CCM kama nilivyoeleza hapo juu Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuiendeleza sekta ya madini kwa kuimarisha usimamizi wa sekta na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kama nitakavyoeleza katika hotuba hii.

57. Mheshimiwa Spika, kiwango cha ukuaji halisi wa sekta ya madini mwaka 2007 kilikuwa asilimia 10.7 ikilinganishwa na asilimia 15.6 mwaka 2006 kwa bei za mwaka 2001. Upungufu huo ulitokana na kupungua kwa uwekezaji mpya kwenye sekta ya madini na pia migodi mingine kama Buhemba kusimamisha shughuli za uzalishaji. Mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa mwaka 2007, ulikuwa asilimia 2.7 ikilinganishwa na asilimia 2.6 mwaka 2006. Ongezeko hili lilitokana na kuongezeka kwa shughuli za utafutaji, uchimbaji na biashara ya madini nchini na kuongezeka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia. Mauzo ya madini yote nje ya nchi kwa mwaka 2007 yalikuwa ni takriban Dola za Marekani milioni 886.5 ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 836.8 mwaka 2006.

Kuboresha Sera na Sheria ya Madini
58. Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Bajeti ya Mwaka 2007/08, Wizara ilipanga kukamilisha durusu ya Sera ya Madini ya mwaka 1997 ili kuongeza mchango wa sekta katika Pato la Taifa. Rasimu ya Sera hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia changamoto zilizotokana na ukuaji wa sekta ya madini, maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mapendekezo ya Kamati mbalimbali zilizoundwa. Kamati hizo ni Kamati ya Kudurusu Sera ya Madini ya mwaka 2005 na Kamati ya Kupitia Mikataba ya Madini ya mwaka 2006.

59. Mheshimiwa Spika, itakumbukwa mwezi Novemba, 2007 Mheshimiwa Rais aliunda Kamati ya Kuishauri Serikali Kuhusu Usimamizi wa Sekta ya Madini. Kamati hiyo ilimaliza kazi na kuwasilisha taarifa yake kwa Mheshimiwa Rais mwezi Mei, 2008. Serikali imepokea na kuchambua mapendekezo ya Kamati hiyo na inaandaa mpango mkakati wa kurekebisha Sera ya Madini, Sheria ya Madini na sheria nyingine zinazohusu sekta ya madini ili kuyatekeleza mapendekezo hayo. Matarajio ya Wizara ni kuwa ifikapo mwezi Aprili, 2009 Sera ya Madini ya mwaka 1997 na Sheria ya Madini ya mwaka 1998 vitakuwa vimerekebishwa.

Mfumo wa Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini

60. Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza utafutaji wa madini nchini kulingana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni za madini umeimarishwa ili usaidie kuharakisha na kuweka wazi shughuli za utoaji na usimamizi wa leseni kwa kuongeza ufanisi katika uchambuzi wa maombi ya leseni za madini. Utoaji wa leseni umeongezeka takriban maradufu kwa wastani wa leseni 500 kwa mwezi kwa mwaka 2007/08 ikilinganishwa na wastani wa leseni 240 kwa mwezi kwa mwaka 2006/07.

Majadiliano na Kampuni za Madini
61. Mheshimiwa Spika, mwezi Machi, 2008, Serikali ilianza majadiliano na Kampuni ya De Beers ambayo ni mbia na Serikali (kupitia kampuni yake tanzu ya Willcroft katika mgodi wa almasi wa Williamson Diamonds Limited (WDL), ili kuona namna ya kuboresha uzalishaji wa almasi katika mgodi huo na kuhakikisha kuwa Serikali inafaidika na mapato yatokanayo na mgodi huo. Majadiliano hayo bado yanaendelea.

Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo
62. Mheshimiwa Spika, Katika kutekeleza lengo la kuwaendeleza wachimbaji wadogo, kama ilivyoelekezwa na Ilani ya Uchaguzi, Serikali ilitenga maeneo katika sehemu mbalimbali za nchi, ambayo yanajumuisha Kilindi mkoani Tanga, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro ambako ilitenga hekta 269,842; Maganzo, Kishapu na Ibadakuli mkoani Shinyanga, hekta 14,870 na Merelani mkoani Manyara hekta 10,490. Pia, Serikali imefanikiwa kupata eneo la hekta 4,000 huko Winza wilayani Mpwapwa, ambako mchakato wa taratibu za kisheria kwa ajili ya kulitenga na kuligawa rasmi kwa wachimbaji wadogo unaendelea. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2007/08 Serikali ilitenga maeneo ya Nyarugusu na Rwamgasa Wilayani Geita na maeneo ya Londoni na Sambaru Wilayani Manyoni kwa ajili ya wachimbaji wadogo ambapo leseni za uchimbaji mdogo zinaendelea kutolewa.

Kuimarisha Uwezo wa Serikali Kusimamia Sekta ya Madini

63. Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini, muundo wa Wizara ya Nishati na Madini umeimarishwa kwa kuipanua Idara ya Madini na kuendelea kuajiri wataalamu zaidi wa kusimamia sekta hiyo. Aidha, ofisi ya Afisa Madini Mkazi, Kigoma ilifunguliwa mwezi Septemba, 2007. Lengo ni kuongeza ufanisi katika usimamizi wa shughuli za madini na kuboresha utoaji wa huduma.

Udhibiti wa Shughuli za Madini Nchini

64. Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha udhibiti wa shughuli za madini, Wizara ilianzisha kitengo cha ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya madini ya dhahabu katika migodi mikubwa (Gold Audit Programme (GAP)) mwezi Agosti, 2007. Kitengo hicho kilipewa majukumu ya msingi yafuatayo:- kuhakiki uzalishaji na biashara ya madini kwenye migodi mikubwa ya dhahabu kwa kuchukua sampuli za madini yanayozalishwa kwenye migodi hiyo na kuyafanyia uchunguzi kwenye maabara ili kujua aina, ubora na wingi wa madini yaliyozalishwa; kuhakiki gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi mikubwa ya dhahabu; na kufanya ukaguzi wa shughuli za utunzaji na ukarabati wa mazingira kwenye migodi mikubwa na kuhakiki gharama za utunzaji wa mazingira wa migodi hiyo. Kitengo hicho kina wafanyakazi 35 ambao wote ni Watanzania. Kati ya hao, wafanyakazi 25 walikuwa wameajiriwa na kampuni ya (ASAGBC) na wafanyakazi waliobaki wameajiriwa na Wizara kutoka kwenye soko la ajira na wengine walipewa uhamisho wa ndani ya Wizara.

65. Mheshimiwa Spika, tangu kuundwa kwa GAP, kumekuwa na ufanisi katika kazi ya ukaguzi na udhibiti wa shughuli za madini na kujenga uwezo wa watumishi wake kwa kuwapatia uzoefu unaohitajika. Aidha, pamoja na uwepo wa ufanisi katika kazi za ukaguzi, gharama za kufanya ukaguzi zimepungua kuanzia shilingi bilioni 16.4 zilizokuwa zinalipwa kwa kampuni ya ASAGBC hadi shilingi bilioni 3.4 zinazotumiwa na Serikali kufanya kazi hiyo kwa sasa.

66. Mheshimiwa Spika, sambamba na shughuli zinazofanywa na Kitengo cha GAP, Idara ya Madini imeimarisha shughuli zake za ukaguzi wa usalama, afya ya wafanyakazi na utunzaji wa mazingira katika migodi mikubwa na midogo. Kazi hii hufanywa na wakaguzi wa migodi waliopo katika ofisi za madini za kanda.

Migogoro katika Shughuli za Madini

67. Mheshimiwa Spika, katika kufikia lengo la kuboresha sekta ya Madini ili iwe na mafanikio yanayotarajiwa, Ilani ya Uchaguzi inaitaka Serikali kuboresha mahusiano kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo. Wizara ilifanya tathmini na kuona kuwa migogoro mingi kati ya wachimbaji wadogo na wakubwa inatokana na sababu kuu mbili: Kwanza, wachimbaji wasiokuwa na leseni kuendesha shughuli za uchimbaji madini ndani ya maeneo yanayomilikiwa na watafutaji na wachimbaji wakubwa wa madini. Pili, ni malalamiko ya fidia ndogo inayotolewa kwa wananchi wanaohamishwa makazi yao kupisha ujenzi wa migodi.

68. Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hizo, Wizara imechukua hatua mbalimbali za kutatua migogoro hiyo ikiwa ni pamoja na: kuendeleza majadiliano ambapo wawekezaji wakubwa walikubali kuachia baadhi ya maeneo ya leseni katika maeneo ya Rwamgasa na Nyarugusu wilayani Geita; Makoro, Ngembambili na Kitai wilayani Mbinga; Seza Kofi na Mumbwi wilayani Handeni; na Winza wilayani Mpwapwa. Kuhusu fidia, tatizo hili linahitaji marekebisho ya Sheria ya Madini na Sheria ya Ardhi ili kurekebisha kasoro zilizopo.

Uongezaji Thamani Madani

69. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM kuhusu kuhakikisha kwamba sehemu ya madini inayosafirishwa nje ya nchi yakiwa yameongezwa thamani kuongezeka kutoka asilimia 0.3 hadi asilimia 3.0 ifikapo mwaka 2010, Wizara inaendelea na mchakato wa kutunga Sheria ya Uongezaji Thamani Madini ikiwemo Usonara. Lengo kuu la Sheria hiyo ni kuhakikisha kuwa shughuli za uongezaji thamani madini ya vito na dhahabu zinakua kwa kasi na kusimamiwa ipasavyo ili kukuza mauzo nje ya nchi na kuongeza mapato na ajira nchini. Aidha, Wizara iliendelea kuimarisha Arusha Gemstone Carving Centre ili iweze kutoa mafunzo ya usanifu wa madini ya vito, miamba na usonara.
KITENGO CHA TANSORT

70. Mheshimiwa Spika, Kitengo cha Uchambuzi na Uthamini wa Almasi (Tanzania Government Diamond Sorting Organisation - TANSORT) kiliendelea na majukumu yake ya kuchambua na kuthamini almasi zinazozalishwa katika mgodi wa Almasi wa Mwadui, uliopo Kishapu, Shinyanga, ili zipate bei nzuri na hivyo kuongeza mapato ya Serikali. Katika mwaka 2007, jumla ya karati za almasi 282,786 zilizalishwa ikilinganishwa na karati 272,204 mwaka 2006.

71. Mheshimiwa Spika, katika mchakato wa kukihamishia nchini Kitengo cha TANSORT kutoka Uingereza na kutokana na Kitengo kuwa na wafanyakazi wawili (2) tu Watanzania, Wizara ilipeleka wafanyakazi wanne (4) kwenye mafunzo ya fani ya kuchambua na kuthamini almasi nje ya nchi ili kukijengea uwezo. Kwa sasa Wizara ipo kwenye hatua za kupata ofisi Jijini Dar es Salaam itakapowekwa TANSORT baada ya kurejeshwa nchini. Aidha, tathmini inafanyika kupata gharama halisi za kuweza kutekeleza uhamisho huo. Lengo la Wizara ni kuwa ifikapo mwaka wa fedha wa 2009/10 wataalamu wa kutosha watakuwa wamepatikana na bajeti itatengwa kutekeleza kikamilifu uamuzi wa kukihamishia nchini.

CHUO CHA MADINI

72. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/08, Chuo cha Madini kilitoa mafunzo ya ufundi sanifu katika kozi za utafutaji madini, uhandisi migodi na uchenjuaji madini. Mafunzo hayo yaliendeshwa kwa wanafunzi 71 wa mwaka wa kwanza, 67 wa mwaka wa pili na 32 wa mwaka wa tatu ambao ndio wahitimu kwa mwaka 2007/08.

73. Mheshimiwa Spika, natumia nafasi hii kuwashukuru wenye migodi nchini kwa kutoa ajira kwa wahitimu wa Chuo cha Madini. Aidha, nawashukuru wenye migodi na shughuli za utafutaji mkubwa wa madini nchini kwa kutoa fursa kwa wanafunzi wa Chuo cha Madini kufanya mafunzo kwa vitendo katika migodi yao.

74.Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa Chuo cha Madini, Wizara katika mwaka 2007/08, iliendeleza ujenzi wa miundombinu ya Chuo ikijumuisha maktaba, karakana ya uchimbaji madini, nyumba za watumishi wa Chuo, zahanati na maabara mbalimbali. Chuo kina changamoto ya kutoa wahitimu wengi zaidi ili waweze kutosheleza soko la ajira. Pamoja na sababu nyingine changamoto hii inatokana na kutokuwepo kwa miundombinu ya kutosha ambapo idadi ya wahitimu wenye taaluma ya ufundi sanifu katika sekta ya madini ni ndogo.

WAKALA WA JIOLOJIA TANZANIA - GST

75. Mheshimiwa Spika, shughuli za upimaji wa ramani za jiolojia zilifanyika katika maeneo ya Sikonge mkoani Tabora ambapo ramani tano (5) za jiolojia zilikamilika. Ramani maalumu kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika sekta ya madini kwa maeneo ya Mpanda-Kigoma, ukanda wa Ziwa Rukwa na ukanda wa Ziwa Victoria zilitengenezwa. Pia, ramani zinazoonesha maeneo yanayokumbwa na matetemeko ya ardhi mara kwa mara na maeneo yenye mionzi (radiation) zilichapishwa.

76. Mheshimiwa Spika, Wakala ulikamilisha ujenzi wa kituo kipya cha kupima matetemeko katika eneo la Isanga-Dodoma. Tathmini ya matukio ya matetemeko ilifanyika katika vituo vya Kibaya, Kondoa, Singida, Dodoma, Manyoni na Mbeya. Pia, uchunguzi ulifanyika wa tukio la mlipuko wa volkano huko Oldonyo Lengai – Arusha. Viongozi wa maeneo yaliyoathirika na mlipuko huo walipewa ushauri juu ya kukabiliana na athari zitokanazo na tukio hilo, ikiwa ni pamoja na mikakati ya kuchukua tahadhari kwa ajili ya kuimarisha usalama.

77. Mheshimiwa Spika, sampuli za miamba ya dhahabu kutoka Nzuguni - Dodoma, Sambaru na Londoni – Singida, zilikusanywa na kazi ya kutafiti uchenjuaji bora wa sampuli hizo ilikamilika. Pia, uchunguzi wa nishati kutokana na maji moto katika Ziwa Ngozi, wilayani Rungwe ulifanyika na kubaini uwezekano wa kuwepo kwa mashapo katika ziwa hilo. Aidha, GST kwa kushirikiana na STAMICO na BGR ya Ujerumani ilichapisha kitabu cha mwongozo kwa wawekezaji katika madini ya viwanda.

SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA - STAMICO

78. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa Shirika la Madini la Taifa – STAMICO na kwa kuzingatia mapendekezo ya kamati mbalimbali, Wizara iliwasilisha kwenye ngazi za maamuzi pendekezo la kuliondoa Shirika hilo kutoka orodha ya mashirika ya umma ya kubinafsishwa, na kulipa majukumu mapya ya ushiriki wa Serikali katika sekta ya madini na kuhudumia uchimbaji mdogo.

79. Mheshimiwa Spika, Shirika la Madini la Taifa liliendelea na shughuli za utafutaji wa madini ya dhahabu katika ukanda wa Ziwa Victoria kwa ubia na kampuni binafsi. Aidha, Shirika lilifanya utafiti wa awali wa madini ya fluorite katika eneo la Sengeri, Mkoani Mbeya na lilitoa huduma ya uchorongaji miamba katika mikoa ya Tanga, Lindi na Mbeya.

KITUO CHA SEAMIC (Southern and Eastern African Mineral Centre)

80. Mheshimiwa Spika, Kituo kimeendelea kutoa mafunzo katika sekta ya madini pamoja na kufanya uchunguzi na uchambuzi wa sampuli mbalimbali za madini katika maabara kwa ajili ya nchi wanachama ambazo ni Tanzania, Ethiopia, Angola, Kenya, Uganda, Komoro na Msumbiji. Aidha, Kituo kina maabara ya mazingira ambayo ni mahsusi kwa ajili ya uchunguzi na uchambuzi wa sampuli za mazingira katika maeneo ya uchimbaji mkubwa na mdogo wa madini.

AJIRA NA MAENDELEO YA WATUMISHI

81.Mheshimiwa Spika, mwaka 2007/08, Wizara iliimarisha uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa kuwapatia mafunzo watumishi, kuajiri watumishi wapya wa kada mbalimbali, kudurusu muundo wa Wizara, kushughulikia maslahi ya watumishi, kukarabati majengo na kununua vitendea kazi, kutoa elimu na vifaa vya kujikinga na maambukizi ya UKIMWI, na kutoa huduma kwa watumishi wanaoishi na virusi vya UKIMWI.

82. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza kampeni ya kupima virusi vya UKIMWI kwa hiari zoezi lililoanzishwa na Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete mwezi Julai, 2007, jumla ya watumishi 117 wa Wizara walijitokeza kupima na kujua hali ya afya zao katika zoezi la awali lililofanyika mwezi Desemba, 2007. Aidha, katika zoezi lingine lililofanyika mwezi Machi, 2008 jumla ya watumishi 82 walijitokeza kurudia kupima kwa lengo la kuhakiki majibu ya awali. Wizara ilifanikiwa kuwahamasisha watumishi walioambukizwa virusi vya UKIMWI kujitokeza na kupata huduma kulingana na Waraka wa Watumishi wa Umma Namba 2 wa Mwaka 2006 unaohusu huduma kwa watumishi wa umma wanaoishi na virusi vya UKIMWI. Wizara imeendelea kutoa huduma ya mlo kamili pamoja na huduma nyingine kwa watumishi waathirika wa UKIMWI waliojitokeza. Aidha, warsha na semina kuhusu njia za kujikinga na kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI zilifanyika kwa waelimishaji rika na watumishi wa Wizara.


83. Mheshimiwa Spika, katika utekelezaji wa mpango wa mafunzo wa mwaka 2007/08, uwezo wa utendaji kazi wa watumishi uliendelea kuimarishwa, ambapo watumishi 73 walipelekwa mafunzoni. Kati yao, watumishi 36 walishiriki mafunzo ya muda mfupi na 37 mafunzo ya muda mrefu. Aidha, Wizara iliajiri watumishi wapya 67 wa fani mbalimbali. Pia, jumla ya watumishi 61 wa kada mbalimbali walipandishwa vyeo.

84. Mheshimiwa Spika, marekebisho ya Muundo wa Wizara yamefanyika ili kuendana na ongezeko la majukumu ya Wizara na kukabiliana na changamoto zilizopo. Muundo mpya wa Wizara uliidhinishwa na Kamati ya Rais mwezi Agosti, 2007. Muundo huo umewezesha kuwepo ongezeko la vitengo viwili ambavyo ni Kitengo cha Sheria (Legal Services Unit), na Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira (Environmental Management Unit). Aidha, Idara ya Madini itakuwa na sehemu tano ambazo ni:- Ukaguzi Migodi - Mines Inspection; Uendelezaji Wachimbaji Wadogo - Small Scale Mining Development; Usimamizi wa Baruti na Milipuko - Explosive Management; Biashara ya Madini na Uchumi - Mineral Economics and Trade; na Utoaji na Usimamizi wa Leseni za Madini - Licensing and Mineral Rights Management zitakazosimamiwa na Makamishna Wasaidizi. Pia, ofisi za madini za kanda nane zitasimamiwa na Makamishna Wasaidizi.

C: MPANGO NA BAJETI KWA MWAKA 2008/09

SEKTA YA NISHATI

85.Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua nyingi zilizochukuliwa kipindi cha nyuma za kuboresha upatikanaji wa nishati, bado uwezo uliopo wa kupata nishati kwa wingi haujatumika vilivyo. Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2005 imeelekeza hatua zichukuliwe zenye lengo la kuongeza nishati, na hasa umeme na kuongeza uhakika wa upatikanaji na usambazaji wake ili uwafikie wananchi wengi zaidi. Ili kutekeleza azma hiyo na kuiwezesha sekta ya nishati kuwa endelevu na kuweza kuchangia ipasavyo katika kuendeleza uchumi wa Taifa maeneo ya kipaumbele katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Wizara katika mwaka 2008/09 ni:- kutekeleza miradi chini ya Wakala wa Nishati Vijijini; kupeleka umeme makao makuu ya wilaya; kuimarisha mfumo wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme nchini; maandalizi ya kuunganisha gridi ya Taifa na nchi jirani; kukamilisha majadiliano na kampuni zilizoshinda zabuni ya kutafuta mafuta katika maeneo mbalimbali nchini; kukamilisha maandalizi ya sheria ya gesi asilia; kukamilisha majadiliano ya uendelezaji wa mradi wa gesi asilia ya Mnazi Bay; kuanza maandalizi ya miradi ya hifadhi na uagizaji wa mafuta wa pamoja (bulk procurement); kuhamasisha matumizi bora na uendelezaji wa nishati jadidifu na mbadala; kukamilisha mipango endelevu ya uendelezaji wa bayofueli nchini; kuhamasisha matumizi bora ya nishati; na kusimamia kazi ya mshauri wa namna ya kugawana gharama na mapato ya mafuta katika pande mbili za Muungano.

Miradi chini ya Wakala wa Nishati Vijijini

86.Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, miradi itakayotekelezwa chini ya Wakala wa Nishati Vijijini ni pamoja na kukamilisha upelekaji wa umeme katika makao makuu ya wilaya za Kilindi, Kilolo, Rufiji, Bahi, Uyui, Mkinga na Simanjiro. Aidha, baadhi ya miradi iliyoainishwa chini ya mradi wa TEDAP itatekelezwa kupitia Wakala chini ya usimamizi wa Wizara. Wakala pia utatoa mafunzo ya kuandaa na kuendeleza miradi ya nishati vijijini.

Miradi Iliyo Chini ya AfDB

87. Mheshimiwa Spika, katika kufanikisha lengo la Serikali la kusambaza umeme vijijini, Benki ya Maendeleo ya Afrika iliidhinisha takriban Dola za Marekani milioni 50 ili kuwezesha usambazaji wa umeme vijijini katika mikoa ya Arusha, Shinyanga na Mwanza. Ni matarijio ya Serikali kuwa fedha hizo zitasaidia katika kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya umeme vijijini katika mikoa husika. Kwa sasa mchakato unaendelea wa kumpata mtaalamu mshauri na matarajio ni kuwa atakuwa ameanza kazi ya kuandaa makabrasha ya zabuni na kushauri kuhusu uteuzi wa wakandarasi mwishoni mwa mwezi Julai, 2008.

Tozo la Wakala wa Umeme Vijijini

88. Mheshimiwa Spika, fedha za utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme vijijini zitatokana na ruzuku ya Serikali, michango ya washirika wa maendeleo wa Serikali, wawekezaji binafsi pamoja na tozo mbalimbali. Waziri wa Nishati na Madini alisaini tangazo la kuanzishwa tozo ya asilimia tatu kwa kila uniti ya umeme unaozalishwa nchini kuanzia tarehe 01 Julai, 2008. Sheria ya Wakala inaruhusu tozo hadi asilimia tano. Tozo itaanza kutumika baada ya kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.

Kupeleka Umeme Makao Makuu ya Wilaya

89. Mheshimiwa Spika, miji mikuu ya wilaya za Ngorongoro, Kibondo, Nanyumbu na Nkasi inatafutiwa fedha kwa ajili ya kutekeleza mipango ya kupeleka umeme huko. Upembuzi yakinifu wa kupanua gridi ya Taifa hadi kufikia mikoa ya Kigoma, Kagera na Rukwa umekamilika ambapo wilaya za Kibondo, Kasulu na Bukombe zimejumuishwa. Mpango wa usambazaji umeme katika makao makuu ya wilaya utaendelea kutekelezwa kulingana na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Kuimarisha na Kuendeleza mfumo wa Usafirishaji na Usambazaji Umeme

Miradi chini ya TEDAP

90. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme itatekelezwa kutokana na misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo. Mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia wa Dola za Marekani milioni 111.5 kupitia mradi wa TEDAP unalenga kuboresha miundombinu katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Kilimanjaro; kusambaza umeme katika maeneo yaliyo nje ya gridi (off-grid electricity distribution); na kujenga uwezo wa Wakala wa Nishati Vijijini na wataalamu katika sekta ya nishati ikiwa pamoja na Wizara na TANESCO. Mchakato wa kupata wataalamu washauri wa kutayarisha makabrasha ya zabuni mbalimbali na kusimamia utekelezaji utakamilika mwishoni mwa Agosti, 2008.

Miradi chini ya MCC na JICA

91. Mheshimiwa Spika, Serikali kwa upande mwingine imepata kiasi cha Dola za Marekani milioni 206.5, kutoka Millenium Challenge Corporation (MCC) ya Marekani kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa umeme. Kiasi hicho kitatumika kwa ajili ya kuimarisha mifumo ya usafirishaji na usambazaji umeme kwa mikoa sita (6) ya Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Mbeya na Mwanza kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 89.7. Kiasi cha Dola za Marekani milioni 53.7 kitatumika kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwenye mto Malagarasi cha MW 8 kwa ajili ya Kigoma, Uvinza na Kasulu, na pia kujenga sub-marine cable kutoka Ras Kilomoni, Dar es Salaam hadi kisiwa cha Unguja kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 63.1. Wataalamu washauri kwa ajili ya kusimamia Mradi wanatarajiwa kuanza kazi katikati ya Julai, 2008. Aidha, Shirika la Maendeleo la Japani (JICA) limetoa Dola za Marekani milioni 10 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kuboresha miundombinu ya usambazaji umeme katika maeneo ya Masaki, Mikocheni na Oysterbay jijini Dar es Salaam.

92. Mheshimiwa Spika, gridi ya Kaskazini Magharibi ya njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 itaendelea kuimarishwa sanjari na miradi mipya ya laini ya msongo wa kV 400 kutoka Iringa kupitia Dodoma, Singida hadi Shinyanga. Aidha, ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 inajengwa kupeleka umeme wa gridi katika migodi ya dhahabu ya Buzwagi na North Mara kwa makubaliano maalumu kati ya migodi hiyo na TANESCO.

Kuimarisha Uzalishaji Umeme

93. Mheshimiwa Spika, katika kupanua wigo wa aina za vyanzo vya nishati kwa ajili ya kuzalisha umeme, mradi wa kuzalisha umeme wa MW 200 kwa kutumia makaa ya mawe ya Kiwira utaendelea kutekelezwa, ambapo yatafanyika maandalizi ya ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kV 220 kutoka Kiwira hadi Uyole, Mbeya itakayounganishwa kwenye gridi ya Taifa. Mtambo wa Ubungo wa MW 100 utakaomilikiwa na TANESCO unategemewa kuanza uzalishaji umeme mwanzoni mwa Agosti, 2008. Mkataba wa Alstom Power Rentals uliokwisha muda wake Machi, 2008 haukuhuishwa na Mkataba wa Aggreko muda wake utaisha Novemba, 2008.

94. Mheshimiwa Spika, kufuatia utata uliojitokeza kuhusu uhalali wa Mkataba wa Richmond/Dowans TANESCO/Serikali imechukua hatua ya kusitisha Mkataba huo kuanzia tarehe 1 Agosti, 2008.

Kuunganisha Gridi ya Taifa na Nchi Jirani

95. Mheshimiwa Spika, matayarisho yanaendelea ili kuziunganisha gridi za Zambia, Tanzania na Kenya. Mshauri mwelekezi ataendelea kuzishauri Serikali za nchi hizi tatu kwa lengo la kuanza utekelezaji wa mradi.

Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia ndani ya Muungano

96. Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza juhudi za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini, Wizara itaendelea kushirikiana na Wizara inayohusika na Nishati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kukamilisha kazi ya mtaalamu atakayezishauri Serikali mbili ndani ya Muungano jinsi ya kugawana gharama na mapato endapo mafuta ya petroli au gesi asilia itagundulika upande mmojawapo wa Muungano. Mtaalamu huyo ni kampuni ya AUPEC kutoka Uingereza ambayo imeanza kazi mwezi Juni, 2008. Kazi hiyo itakamilika mwezi Novemba, 2008.

97. Mheshimiwa Spika, Serikali inatarajia kuanza na kukamilisha majadiliano na kampuni zilizoshinda zabuni ya kutafuta mafuta na gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini. Kampuni hizo ni Tower Resources ya London, Ansco Petroleum (T) Limited, Motherland Homes Limited ya India na Beach Petroleum Limited ya Australia zilizoshinda zabuni ya kutafuta mafuta na gesi asilia katika maeneo ya ziwa Eyasi-Manyara, Natron na bonde la Wembere, Ruhuhu, Malagarasi na eneo la kusini mwa Ziwa Tanganyika.

Maandalizi ya Sheria ya Gesi Asilia

98. Mheshimiwa Spika, kufuatia kukamilika kwa rasimu ya mapendekezo ya kutunga Sheria ya Gesi Asilia, taratibu za kupata ridhaa ya ngazi za maamuzi zitaendelea ili Rasimu ya Sheria iweze kufikishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano mwezi Novemba, 2008.

Mradi wa Gesi Asilia ya Mnazi Bay

99. Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika na kuanza utekelezaji wa mkataba wa muda wa mpito wa ununuzi wa umeme kati ya TANESCO na Artumas, majadiliano ya mkataba wa muda mrefu yatakamilishwa mwaka 2008/09. Kukamilika kwa majadiliano kutaharakisha usambazaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara. Aidha, vipaumbele vya Serikali kuhusu matumizi ya gesi asilia ya ziada inayopatikana Mnazi Bay ni kutengeneza mbolea, saruji na kuzalisha umeme.

Hifadhi na Uagizaji wa Mafuta wa Pamoja

100.Mheshimiwa Spika, ili kuwa na uhakika wa kuwa na mafuta ya kutosha na ya dharura nchini, Wizara itakamilisha mchakato wa kuanzisha hifadhi ya mafuta. Aidha, EWURA itawasilisha mapendekezo kuhusu uagizaji wa mafuta wa pamoja (bulk procurement) kwa lengo la kuanza kutekeleza utaratibu huo mwaka 2008/09. EWURA imetoa tangazo la kukaribisha washauri wa kusimamia taratibu za bulk procurement na walioonekana kuwa na uwezo wameorodheshwa na watapewa makabrasha ya zabuni. Orodha hiyo inatarajiwa kupitishwa kwenye Bodi ya Zabuni ya EWURA katikati ya mwezi Julai, 2008.

Nishati Jadidifu na Mbadala

101. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Mradi wa umemenuru utaendelea kutekelezwa kwa kuhamasisha soko la teknolojia hiyo katika mikoa ya Dodoma, Ruvuma, Singida na Tabora. Mafanikio ya mradi wa majaribio ya umemenuru Mkoani Mwanza yataendelea kutekelezwa (replicated) katika mikoa ya Mara, Kagera na Shinyanga kwa kutumia uzoefu uliopatikana mkoani Mwanza. Aidha, ukusanyaji wa taarifa za nishati ya upepo, jotoardhi, maporomoko madogomadogo ya maji kwa ajili ya uzalishaji umeme (small-scale hydropower generation) utaendelea ili kuongeza mchango wa nishati jadidifu katika kuzalisha umeme. Pia, Serikali itaendelea kuhamasisha viwanda vyenye kuzalisha taka nyingi kama vya sukari na mbao, kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa kutumia taka husika.

102. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Serikali kwa kushirikiana na TANESCO itaendelea kujadiliana na wadau wenye nia ya kuwekeza katika matumizi ya nishati ya upepo. Aidha, Wizara itaanza maandalizi ya kutengeneza Wind Atlas ili kurahisisha jitihada za wawekezaji katika nishati hiyo hapa nchini kwa kuwezesha kuwepo kwa takwimu sahihi za maeneo yanayoweza kuzalisha nishati ya upepo.

103. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Serikali itaendelea na uandaaji wa mazingira ya kuwezesha uendelezaji endelevu wa bayofueli nchini na itakamilisha mwongozo wa uendelezaji bayofueli ikiwa ni utaratibu wa mpito kabla sera na sheria mahsusi ya bayofueli kukamilika. Aidha, baadhi ya masuala ambayo yatazingatiwa ni mazingira, ardhi kwa mazao ya chakula, ajira, matumizi na wajibu wa wawekezaji kutoka nje katika kuhakikisha kwamba wananchi wananufaika ipasavyo na faida zitokanazo na bayofueli.

Matumizi Bora ya Nishati

104. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi bora ya nishati katika sekta mbalimbali za uchumi ili kuokoa nishati, fedha na mazingira. Maandalizi kuhusu masuala ya uhamasishaji wa viwango vya ubora katika matumizi ya nishati na nembo majumbani na viwandani (energy efficiency standards and labels) yatafanyika.


105. Mheshimiwa Spika, Wizara itaendelea kuhamasisha wadau kuendeleza vyanzo vya nishati kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa matumizi ya bayogesi, Liquified Petroleum Gas (LPG), gesi asilia, moto poa (gel-fuel), vitofali vya tungamotaka na makaa ya mawe (biomass and coal briquettes) kama mbadala wa kuni na mkaa. Lengo ni kuchangia katika kupunguza kasi ya ukataji miti na kuhifadhi mazingira. Aidha, Serikali kupitia mradi wa SADC-ProBEC kwa kushirikiana na wadau, itaendelea kuhamasisha matumizi endelevu ya kuni katika ukaushaji wa tumbaku na majiko bora ya kuni, hasa vijijini na katika taasisi kubwa kwa ajili ya kupikia.

SEKTA YA MADINI
Mipango ya Sekta ya Madini kwa Mwaka 2008/09

106. Mheshimiwa Spika, mipango ya sekta ya madini kwa mwaka 2008/09, itaendelea kuongozwa, pamoja na miongozo mingine, na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Mipango hiyo ni pamoja na kurekebisha Sera na Sheria ya Madini; kuendeleza majadiliano na kampuni za madini; kuanzisha mfuko maalumu wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo; kukamilisha maandalizi ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali ya Madini (Sustainable Management of Mineral Resources Project) kusimamia utafutaji na uchimbaji wa urani (uranium) nchini; uimarishaji wa miundombinu katika ofisi za madini; na kuimarisha shughuli za ukaguzi wa gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi mikubwa.


Sera na Sheria ya Madini

107. Mheshimiwa Spika, Wizara itakamilisha marekebisho ya Sera ya Madini ya mwaka 1997 na Sheria ya Madini ya mwaka 1998 kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya CCM, changamoto za ukuaji wa sekta ya madini na mapendekezo ya kamati mbalimbali zilizoundwa na Serikali. Lengo ni kuwa na mabadiliko ya msingi katika uendeshaji wa sekta ikiwa ni pamoja na kupitia upya vivutio vya kodi na kuongeza ushiriki wa Serikali katika uwekezaji ili kuhakikisha manufaa kwa Taifa yanaongezeka. Marekebisho hayo pia, yatajumuisha kuirekebisha na kuipa majukumu mapya STAMICO.

Majadiliano na Kampuni za Uchimbaji wa Madini

108. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendeleza majadiliano na Kampuni ya De Beers kupitia kampuni yake tanzu ya Willcroft katika mgodi wa almasi wa Williamson Diamonds Limited (WDL). Katika majadiliano hayo Serikali itaangalia upya suala la hisa zake kwenye mgodi huo, ambapo kampuni ya Willcroft ina asilimia 75 ya hisa na Serikali asilimia 25. Aidha, Serikali itaendelea na majadiliano na kampuni ya AngloGold Ashanti kuhusu kuondoa kipengele cha asilimia 15 kwenye mtaji wa uwekezaji ambao haujarejeshwa.

Mfuko Maalumu wa Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo

109. Mheshimiwa Spika, Suala la kuendeleza wachimbaji wadogo limepewa kipaumbele na Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kuelekeza kuwa wachimbaji wadogo wasaidiwe kupata mikopo na maarifa mapya katika fani ya uchimbaji madini. Katika kipindi cha fedha cha mwaka 2008/09 Wizara itaanzisha mfuko maalumu wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo (Mineral Revolving Fund) ili utumike kuwakopesha mitaji wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini Watanzania. Aidha, Wizara itaendelea kuwahamasisha wachimbaji wadogo nchini kuanzisha SACCOS ili waweze kukopeshwa mitaji na kuendeleza maeneo yaliyotengwa na kupimwa viwanja vya uchimbaji.


Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali ya Madini


110. Mheshimiwa Spika, ili Taifa liendelee kunufaika ipasavyo na rasilimali ya madini nchini, Serikali imekamilisha maandalizi ya awali ya mradi wa miaka mitano wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali ya Madini (Sustainable Management of Mineral Resources) utakaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Mradi huu pamoja na mambo mengine utasaidia kujenga uwezo wa Wizara kusimamia Sekta ya Madini, kusaidia kukuza shughuli za uongezaji thamani ya madini nchini na kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za madini. Mwezi Januari, 2008 Benki hiyo ilitoa Dola za Marekani milioni 1.4 kwa ajili ya maandalizi ya mradi huo.



Utafutaji na Uchimbaji wa Urani Nchini

111. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2007, kumekuwa na ongezeko kubwa la shughuli za utafutaji wa madini ya urani hapa nchini ambapo kampuni kubwa za kigeni zipatazo 20 zinaendelea na shughuli za utafutaji wa madini hayo katika mikoa ya Kusini na Kanda ya Kati. Madini haya ni ya kimkakati (strategic) kwa nchi nyingi duniani kwani hutoa nishati ya umeme ya uhakika. Aidha, madini haya yana madhara makubwa kwa binadamu kama uchimbaji wake usipozingatia taratibu maalumu. Serikali itaanza maandalizi ya kutunga sera na sheria zitakazosimamia utafutaji na uchimbaji wa urani nchini.

Ujenzi wa Ofisi za Madini

112. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Serikali itaendelea na mpango wa kusogeza huduma za usimamizi wa sekta ya madini mikoani kwa kuanza kujenga ofisi tatu za kanda ya Kusini Magharibi - Mbeya, Kanda ya Ziwa - Mwanza na Kanda ya Kati - Singida pamoja na ofisi moja ya Afisa Madini Mkazi katika wilaya ya Ludewa.


Ukaguzi wa Gharama za Uwekezaji na Uendeshaji wa Migodi Mikubwa

113. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza azma ya Serikali katika kuimarisha shughuli za ukaguzi wa gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi na kuhakikisha kuwa migodi inachangia ipasavyo kwenye ukuaji wa uchumi, Serikali itaendelea kuimarisha Kitengo cha GAP ili kipate uwezo wa kukagua na kudhibiti madini yote yanayozalishwa hapa nchini na wachimbaji wakubwa na wadogo. Aidha, Idara ya Madini itaimarishwa kwa kutekeleza muundo wake mpya ili iweze kusimamia na kukagua masuala ya usalama na afya ya wafanyakazi migodini, utunzaji wa mazingira na utoaji wa huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo.


WAKALA WA JIOLOJIA TANZANIA - GST

114. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Wakala utafanya kazi zifuatazo:- kutengeneza ramani katika maeneo ya Urambo – Tabora; kukamilisha ramani zilizopo ndani ya Mtwara Development Corridor; kukusanya na kuhifadhi takwimu za matetemeko ya ardhi; kukarabati na kujenga miundombinu; kufanya utafiti maalumu wa makaa ya mawe; na kutoa mafunzo kwa wachimbaji madini wadogo wa Sambaru, Londoni na Nzuguni kuhusu namna bora za uchenjuaji wa dhahabu. Kwa kushirikiana na NDC, Wakala utafanya tathmini ya kina kubaini wingi na ubora wa madini ya chuma yaliyoko Liganga - Ludewa na makaa ya mawe yaliyoko Mchuchuma – Ludewa na Mbalawala - Mbinga. Aidha, Wakala utawapeleka mafunzoni baadhi ya wafanyakazi hususan katika fani za jiofizikia, jiokemia na utunzaji wa mazingira.


CHUO CHA MADINI

115. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Chuo kinatarajia kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya Chuo na kuendelea kutoa mafunzo kwa wanafunzi zaidi ili Taifa liwe na mafundi sanifu wengi wenye kiwango bora cha ujuzi katika sekta ya madini. Kutokana na miundombinu iliyopo, Chuo kitaendelea kusajili wanafunzi 60 wa mwaka wa kwanza. Aidha, Chuo kitaandaa mpango mkakati wa kukiendeleza (Corporate Strategic Plan) ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka 2009/10.

KITENGO CHA TANSORT

116. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Kitengo cha TANSORT kitaendelea na kazi za kuchambua na kuthamini almasi za mgodi wa Mwadui. Aidha, Wizara imepanga kupeleka wafanyakazi wawili zaidi katika mafunzo ya fani ya kuchambua na kuthamini almasi. Lengo ni kukiongezea Kitengo uwezo wa kuchambua na kuthamini almasi zaidi. Kazi nyingine zilizopangwa ni kukamilisha tathmini na maandalizi ya kununua vifaa vitakavyohitajika ili kukiwezesha Kitengo kufanya kazi zake kwa ubora na ufanisi. Wizara inatarajia kuwa ifikapo mwaka wa fedha 2009/10 Kitengo kitakuwa kimehamia Tanzania.

SHIRIKA LA MADINI LA TAIFA - STAMICO

117. Mheshimiwa Spika, baada ya Serikali kutoa uamuzi wa msingi kuhusu hatima ya STAMICO inatarajiwa kwamba Shirika hilo litarekebishwa ili liweze kuwekeza kwenye sekta ya madini kwa niaba ya Serikali (Government Investment Arm) hususan, kwenye madini mkakati (strategic minerals). Aidha, Shirika hilo litahamasisha uwekezaji kwenye madini ya viwanda (industrial minerals) na kusimamia juhudi za Serikali za kuwaendeleza wachimbaji wadogo nchini ikiwa ni pamoja na kutoa huduma za ugani.

Southern and Eastern African Mineral Centre – SEAMIC

118. Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2008/09, Kituo kitafanya kazi zifuatazo:- kutoa mafunzo yanayohusu sekta ya madini; kuchambua sampuli za madini; kufanya utafiti wa teknolojia bora za kuendeleza madini ya viwanda; na kutoa huduma za ushauri kwa nchi wanachama na sekta binafsi.

D: AJIRA NA MAENDELEO YA WATUMISHI

119. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Wizara inatarajia kuajiri watumishi 65 watakaogawanywa katika idara mbalimbali. Pia, Wizara imepanga kuwapeleka mafunzoni baadhi ya watumishi wake ili kuwajengea uwezo katika utaalamu mahsusi ili kutekeleza majukumu yao kwa umahiri na ufanisi zaidi. Aidha, mazingira ya kufanyia kazi yataendelea kuboreshwa kwa kujenga na kukarabati majengo ya ofisi na kununua vitendea kazi.

120. Mheshimiwa Spika, katika kuboresha mfumo wa utoaji huduma kwa wadau Wizara itaanza kutekeleza Mkataba wa Huduma kwa Mteja - Client Service Charter mwaka 2008/09. Mkataba huo haukuweza kuzinduliwa mwaka 2007/08 kutokana na mabadiliko ya msingi yaliyofanyika katika muundo wa Wizara na maoni yaliyotolewa na wadau. Mkataba huo utazinduliwa katika mwaka 2008/09, baada ya kuzingatia mabadiliko na maoni ya wadau.

121. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Wizara itaendelea kuimarisha mfumo wa teknolojia ya habari na mawasiliano; kuimarisha mawasiliano kati ya Wizara na umma kuhusu huduma na taarifa mbalimbali za kisekta; kusimamia shughuli za manunuzi na utoaji wa zabuni unaozingatia sheria na kanuni; pamoja na kusimamia utekelezaji wa Mfumo wa Mapitio na Upimaji wa Utendaji Kazi wa Wazi (OPRAS) kwa watumishi.

122. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2008/09, Wizara itaendelea kutoa mafunzo kwa watumishi kwa lengo la kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI; kuwahamasisha watumishi kupima afya zao; kuanzisha mfumo wa mawasiliano wa namna ya kupashana habari kuhusu masuala ya UKIMWI; na kutoa huduma kwa watumishi waliojitokeza wanaoishi na virusi vya UKIMWI kulingana na Waraka wa Watumishi wa Umma Namba 2 wa mwaka 2006.

E: USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

123. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2007/08, Wizara ya Nishati na Madini ilinufaika kwa misaada na ushirikiano kutoka kwa washirika mbalimbali wa maendeleo. Kwa niaba ya Serikali napenda kutoa shukurani kwa Serikali za nchi za Denmaki, Hispania, Japani, Kanada, Marekani, Norwe, Uswidi, Uholanzi na Ujerumani. Vilevile, natoa shukurani kwa Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Rasilimali ya Ulaya, Umoja wa Nchi za Ulaya, pamoja na mashirika ya ADF, GEF, IAEA, IDA, JICA, MCC, NDF, NORAD, Sida, UNDP, UNIDO na WEC.

F: SHUKURANI

124. Mheshimiwa Spika, naomba kutumia nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Adam Kighoma Ali Malima, Mbunge wa Mkuranga na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, kwa ushirikiano wake mkubwa anaonipa katika kusimamia utekelezaji wa shughuli za Wizara. Aidha, nawashukuru Katibu Mkuu, Bwana Arthur Gwanaloli Mwakapugi, wakuu wote wa idara na vitengo, viongozi wa taasisi zilizopo chini ya Wizara wakiwemo wenyeviti na wajumbe wa Bodi na watendaji wakuu, kamati zinazosimamiwa na Wizara na wafanyakazi wote wa Wizara ya Nishati na Madini pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini.

G: MAJUMUISHO

125. Mheshimiwa Spika, sasa naliomba Bunge lako Tukufu likubali na kuidhinisha mapendekezo ya Bajeti ya shilingi 362,922,265,600 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na taasisi zake kwa mwaka 2008/09. Mchanganuo wa Bajeti hiyo ni kama ifuatavyo:-

(a) Bajeti ya Maendeleo ni shilingi 320,067,385,600, kati ya fedha hizo shilingi 96,598,691,000 ni fedha za hapa na shilingi 223,468,694,600 ni fedha za nje; na

(b) Bajeti ya Matumizi ya Kawaida ni shilingi 42,854,880,000 ambapo shilingi 3,305,639,000 ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 39,549,241,000 ni matumizi mengineyo (OC).

126. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.