Thursday, February 14, 2008

JESHI KATIKA KASHFA

Hospitali ya Jeshi la Lugalo Jijini Dar es Salaam imeingia katika kashfa ya kuwageuza watanzania kuwa nguruwe wa majaribio kwa kuruhusu kufanyika kwa utafiti kwa kutumia dawa iliyopigwa marufuku.

Kashfa hiyo imebainishwa Bunbgeni jana kufuatia swali lililoulizwa na Mbunge machachari wa Karatu, Dk. Wilnrod Slaa na Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Aisha Kigoda kukiri kutokea kwa jambo hilo.

Dk. Aisha Kigoda alisema kuwa licha ya taasisi ya serikali, Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), kupiga marufuku kufanyika kwa utafiti huo, Jeshi, huku likionyesha kiburi, liliiruhusu kampuni moja ya Afrika Kusini, sit u kuleta dawa hizo ziitwazo virodene PO 58 kuzifanyia utafiti kwa kuwatumia watanzania, bali pia kampuni hioyo ilianza kuziuza dawa hizo kiholela mitaani.

Taarifa zilizotolewa na Dk. Slaa akilinukuu gazeti la Washington Post la Marekani, zinaonyesha kuwa watanzania 64 wamefanyiwa majaribio ya dawa hiyo ya ukimwi iliyotengenezwa Afrika Kusini lakini meshapigwa marufuku nchini humo.

Dk. Slaa aliitaka serikali kueleza ni chombo gani cha sheria kilitoa kibali cha watanzania kufanyiwa majaribio ya dawa ambayo imeshapigwa marufuku.


Dk. Slaa alisema kuwa pamoja na Hospitali ya Lugalo, kuna taarifa kuwa majaribio hayo yalifanywa pia katika zahanati binafsi inayomilikiwa na Mkuu wa Jshi la Polisi mstaafu ambaye hakumtaja jina.

Kwa kawaifda, vyombo vya serikali vinavyohusika na utoaji wa vibali vya utafiti wa kisayansi ni Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja na COSTECH.

Hata hivyo, hakuna hata moja ya taasisi nilizozitaja iliyowahi kutoa kibali kwa ajili ya utafiti huo na kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kuwa ombi la kibali cha kufanya utafiti liliwasilishwa NIMR Julai 2000.

Baada ya NIMR kufanya tathimini ya utafiti huo, ililikataa ombi hilo kwa kuwa andiko kuhusu utafiti wa dawa hiyo lilikuwa na upungufu mkubwa kisayansi na kimaadili.

Lakini katika hali ya kushangaza, hata baada ya kukataliwa kwa ombi la kufanya utafiti, wanasayansi hao waliingiza dawa bila kibali cha serikali na kuanza kufanya utafiti katika hospitali ya Lugalo.

Alipopewa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, Dk. Slaa alimtaka Naibu waziri huyo kueleza hatua zilizochukuliwa kwa watanzania ambao walishirikiana na watafiti hao kutoka nje kufanya uhalifu huo.

Dk. Slaa alisema anazo taarifa kuwa ombi la utafiti lilipokataliwa na NIMR, viongozi wa Jeshi walisema wazi wazi kuwa Wizara ya asfya haihusiki kutoa vibali vya utafiti.

Dk. Kigoda hakulijibu swali hilo ipasavyo kwani hakueleza viongozi wa jeshi walioshiriki kuwaleta watafiti hao walichukuliwa hatua gani.

Badala yake, alilieleza Bunge kuwa Wizara ilikaa na Jeshi la kukubaliana kuwa utafiti huo usiendelee na kuwa iwapo wanataka utafiti huo unedelee basi wafuate sheria na taratibu zilizopo.

Thursday, February 7, 2008

BREAKING NEWS: Lowassa Aomba Kujiuzulu

Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ameandika barua kjwa Rais Jakaya Kikwete akiomba kujiuzulu wadhifa huo.
Lowassa alitangaza hayo Bungeni leo wakati alipotakiwa kuchangia ripoti ya Kamati nTeule ya Bunge kuhusu kampuni ya Richmond.
Lowassa amesema kuwa ameamua kujiuzulu ili kuonyesha uwajibikaji ingawa hakubaliani na jinsi kamati hiyo ilivyomhukumu bila kumhoji.
Alisema kuwa baada ya kuisoma taarifa ya kamati hiyo amebaini kuwa kinachotakiwa ni Uwaziri Mkuu, hivyo kwa manufaa ya serikali, chama chake na nchi, ameamua kuuachia wadhifa huo.
Huku akiongea kwa masikitiko makubwa, Lowassa alisema kuwa imemshangaza kuwa wakati ripoti hiyo inamtuhumu yeye, hakuhojiwa wakati yeye alikuwa tayari kutoa maelezo yake. Alisema ahata aliponong'onezwa suala hilo na Spika, samwel Sitta, alimletea ushahidi wa maandishi.
Habari kutoka Ikulu zinaeleza kuwa tayari barua hiyo imeshapokelewa na maamuzi yatakapofanywa yatatangazwa.
Mwandishi wa Habari wa rais, Premmy Kibanga aliiambia tovuti hii kuwa suala hilo litatangazwa hadharani ingawa hakusema lini maamuzi hayo yatafanywa na kutangazwa

Wednesday, February 6, 2008

BREAKING NEWS: Lowassa ananuka Richmond

Kamati teule ya Bunge, iliyopewa kazi ya kuangalia mkataba wa uzalishaji umeme wa dharura kati ya kampuni ya Richmond Development ya Marekani na serikali, imemkuta waziri Mkuu, Edward Lowassa, akiwa mchafu kimaadili na kumshauri kujiuzulu.

Kwa maneno yake, kamati hiyo inahitimisha: “Kamati teule haikufurahishwa hata kidogo na taarifa zinazomgusa moja kwa mowa moja Mhe waziri Mkuu katika kuipendelea Richmond Development Company LLC. Hata hivyo, Kamati teule imetimiza wajibu wake kwa uwazi na ukweli kama ilivyoagizwa na Bunge letu tukufu.

“Kwa kuzingatia umuhimu wa nafasi aliyonayo Mhe. Waziri Mkuu katika uendeshaji wa shughuli za serikali na uongozi wan chi kwa ujumla, ni wajibu wake yeye mwenyewe kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huu na wajibu wake kikatiba ndani na nje ya Bunge.

“Vile vile ni wajibu wa Bunge ambalo linathibitisha uteuzi wake kwa mujibu wa Ibara ya 51 inayothibitisha uteuzi wake, kuangalia ikiwa matokeo ya uchunguzi huu hayajaathiri hadhi na uzito wake ndani ya Bunge.”

Kwa maneno mengine, Kamati hiyo iliyokuwa inaongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela-CCM) ilikuwa inamtaka waziri Mkuu kujiuzulu kutokana na kuhusika kwake na kashfa hiyo.

Aidha, iwapo Lowassa angeshindwa kuchukua uamuzi wa kumwajibisha kwa kumpigia kura ya kutokwua na imani naye.

Kwa ujumla, Kamati hiyo imebaini kuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, wanahusishwa moja kwa moja na kuipatia kampuni hiyo kazi ya kuzalisha umeme wa dharura wakati ikiwa haina sifa.

Aidha, wengine wanaotajwa katika ripoti hiyo na kushauri wawajibishwe kutokana na ushiriki wao katika sakata hilo ni waziri wa sasa wa Nishati na Madini, nazir Karamagi, katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Ather Mwakapugi pamoja na Kamishna wa Madini, Bashir Mrindoko.

Wengine ni Mwanassheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, ambaye kwa mujibuw a ripoti hiyo ameonekana kutojua alichokuwa anakifanya wakati baadhi ya viongozi wakiwa wanatekjeleza njama za kupindisha sheria na taratibu ili kuhakikisha kuwa Richmond inapatiwa kazi hiyo.

Uchunguzi wa Kamati pia ulibaini kuhusika kwa aliyekuwa waziri katika serikali ya awamu ya tatu, Daniel Yona, jinsi ambavyio naye alishiriki katika kuhakikisha kuwa Richmond inapata kazi hiyo.

Inaelezwa katika ripoti hiyo kuwa Dk. Msabaha aliamua kukiuka maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na mchakato wa kuipata kampuni itakayozalisha umeme wa dharura, na kuilazimisha Tanesco kupindisha taratibu na kuikumbatia Richmond ingawa ilidhihirika wazi kuwa haikuwa na sifa ya kupata kazi hiyo.

Hata hivyo, Msabaha anakaririwa na ripoti hiyo akisema kuwa katika suala hilo, yeye amefanywa kuwa kondoo wa kafara tu.

Mtiririko wa ripoti hiyo unaonyesha kuwepo kwa maelekezo na maagizo kutoka kwa Lowassa, kwenda kwa Dk. Msabaha kuhakikisha kuwa Richmond inapatiwa kazi hiyo kwa njia yoyote ile.

Pia ripoti hiyo imeonyesha jinsi Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Nchini (Takukuru), kwa jinsi ambavyo ilitumia mamlaka yake kuficha ukweli wa mambo na kuisafisha Richmond pamoja na viongozi wasio waadilifu walioileta kampuni hiyo.

Kwa msingi huo, Kamati hiyo imependekeza kuwa uongozi wa Takukuru ufanyiwe mabadiliko makubwa ili kulinda hadhi ya taasisi hiyo muhimu katika mapamvbano dhidi ya rushwa.

Friday, February 1, 2008

Masuala Nyeti Yapigwa Danadana Bungeni

KIU ya watanzania kufahamu hatma ya hoja nyeti zinazosubiri maamuzi ya Bunge itabidi kusubiri kwa wiki moja zaidi.
Hii ni kutokana na Spika wa Bunge, Samuel Sitta, kutangaza kuwa masuala hayo nyeti, hayatajadiliwa Bungeni wiki hii hadi atakaporejea kutoka Marekani.
Spika Sitta alitangaza kuwa atakuwa na ziara ya wiki moja nchini Marekani alikoalikwa na Baraza la Wawakilishi na kutoa maelekezo kuwa katika muda ambao hatokuwepo, masuala nyeti yaliyo Bungeni yatapaswa kusubiri.
Alisema kuwa anatarajia kuondoka Jumatatu na kurejea Alhamisi hivyo Naibu Spika, Anne Makinda, atakaimu nafasi yake lakini kati ya majukumu yake hayatahusisha kushughulikia masuala hayo nyeti.
Sitta aliyataja masuala hayo kuwa ni pamoja na suala la ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoangalia mchakato wakuipata kampuni ya Richmond Development (RDC) ya Marekani, iliyopewa kandarasi ya kuzalisha umeme za dharura wakati taifa lilipokabiliwa na upungufu wa nishati hiyo mwaka juzi.
Pia aliitaja hoja nyingine nzito kuwa ni lile linalohusiana na sakata la kashfa ya akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA) ya Benki Kuu (BoT).
“Sikutaka Naibu Spika akurupuke na kuvamia masuala haya nyeti, itabidi yasubiri mpaka pale nitakaporejea… tunayo wiki nzima ya kuyaangalia haya,” alisema.
Hata hivyo, dalili za kupigwa danadana kwa suala la EPA zilianza kuonekana mapema Bungeni jana wakati wa kipindi cha maswali na majibu, pale ambapo masuali kuhusiana na suala hilo yalipozuiliwa na Spika, kwa maelezo kuwa suala hilo bado linajadiliwa.
Wakati fulani, Spika alizima swali la nyongeza lililoulizwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF), ambaye baada ya Naibu Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo kubainisha kuwa suala la EPA linafanyiwa kazi kutokana na maelekezo ya Rais Jakaya Kikwete.
Aliposimama kuuliza swali la nyongeza, Hamad Rashid alikumbusha kwua kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, taasisi hiyo ambayo ni moja ya mihimili ya utawala, haizuiliwi kujadili suala ambalo linachunguzwa na taasisi nyingine, ukiacha masuala ambayo yapo mahakamani.
Lakini Spika badala ya kumwita Mkulo kujibu suala hilo, alisimama na kutoa maelezo kuwa alishatoa maelezo awali kuwa majadiliano kuhusu suala hilo yanaendelea na atalitaarifu Bunge hatma ya majadiliano hayo.
Baada ya jitihada za Hamad Rashid kugonga mwamba, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisimama kwa lengo la kuuliza swali la nyongeza, na kwa kudhani kuwa anakusudiakuuliza swali kuhusiana na suala hilo, Spika alimzuia akisema kuwa maelezo aliyoyatoa yameizima hoja hiyo kuendelea kuhojiwa.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mapema wiki hii, Spika aliliambia Bunge kuwa ndani ya wiki huii angetoa taarifa kuhusiana na matokeo ya mashauriano kati ya ofisi yake na serikali kuhusiana na suala la kuwasilishwa Bungeni kwa ripoti kamili iliyoandaliwa na kampuni ya kimataifa ya ukaguzi wa hesabu ya Ernst & Young kuhusiana na EPA.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili nje ya Bunge baada ya kipindi cha maswali na najibu, Zitto alisema kuwa lengo lake la kusimama halikuwa kuulizia masuala ya EPA.
“Inaonekana mzimu wa EPA umevawaa serikalini, kila kitu wao wanaona kama EPA… mimi sikutaka kuulizia kuhusu EPA, hoja yangu ilikuwa ni kuwa Naibu Waziri hakujibu swali lililoulizwa.
“Swali liliuliza kuhusu Debt Conversion Scheme, hizi ni fedha ilizoliwa na wafanyabishara waliouziwa madeni, hilo ndilo lililoulizwa lakini waziri alikwepa kulijibu hilo,” alisema Zitto.