Sunday, November 25, 2007


Jamani, jamani, jamani! Eti wanasema huyu alifanyiwa operesheni MOI, badala ya kumuweka mkono, akaunganishwa kipande cha mguu!

Safari Si Kifo

Ndugu zangu, nimeadimika kwa siku kadhaa kwa sababu baada ya kutoa A town, nilikatiza anga moja kwa moja hadi makao makuu ya Afrika-Addis Ababa. Nilikuwepo hapo kwa wiki moja na ndio kwanza nimerejea nyumbani. Kutokana na sababu za kiufundi, nilishindwa kuwa pamoja nayi kwa muda huo wote. Lakini kwa kuwa nimesharejea, naandaa mambo ya huko Addis na mengine na nitaanza kuwarushia hivi karibuni.

Thursday, November 15, 2007

Arusha inaangamia?

Jamani bado nipo A town. Baada ya kuzunguka hapa na pale mjini hapa na kuzungumza na wenyeji, nimebaini kuwa mambo si shwaji mjini hapa na mkoani Arusha ka ujumla.
Ni kwamba uchumi wa mji wa Arusha ulikuwa ukitegemea sana madini ya tanzanite huko Mererani. Lakini kwa bahati mbaya sana, upatikanaji wa madini hayo, hasa miongoni mwa wachimbaji wadogo, umeshuka sana, ni kama hakuna kitu kinapatikana hivi sasa.
Matokeo yake, watu wengi wamekosa kazi. Vijana wengi wamelazimika kukimbia kutoka Mererani na kukimbilia katika miji jirani ya Moshi na Arusha. Si ajabu matukio ya uhalifu yanazidi kushika kasi ingawa Polisi hawataki kukiri hivyo (nadhani wanahofia kitumbua chao).
Sasa hivi kampuni ya Tanzanite One pekee ndiyo inayoendelea na uchimbaji na hata madini machache yanayoonekana mitaani inasemekana yanaibwa kutoka Tnzanite One kwa sababu kwenye machimbo ya wachimbaji wadogo hakuna kinachopatikana kabisa!
Hii ni hatari na nadhani mamlaka zinazohusika zinapaswa kuchukua hatua mara moja kunusu maisha ya hao waliokosa kazi pamoja na wananchi wengine ambao wameaza kuwa walengwa wa vijana hao waliokosa kazi. Wanachokijua hivi sasa ni kuvuzia maduka na kuiba, kweli ni hatari.

Wednesday, November 14, 2007

Karibuni Arusha

Jamani, nipo katika mji wa kitalii wa Arusha. Nimewasili hapa jana majira ya saa 1 jioni (kwa saa za Afrika Mashariki). Sijazunguka sana kutokana na kwuasili muda huo mbaya lakini katika mizunguko michache niliyoifanya nimegundua kuwa zile taxi aina ya baloon ambazo zilikuwa zinaupamba mji huu katika miaka michache iliyopita, hazipo tena barabarabi. Hivi sasa taxi nyingi ni magari ya kawaida na nyingi ni mbovu mno.
Katika ulizauliza yangu, mtu mmoja alinifahamisha kuwa baloon zilichangamkiwa sana na watu waliokuwa wakifanya biashara ya taxi lakini baadaye wakabaini kuwa si gari imara za kuhimili kazi hiyo, wengi waliozinunua waliishia kupata hasara na sasa wanaziogopa kama ukoma. Hayo ni madhara mengine ya bidhaa feki zinazoingizwa nchini kwani nyingi ya baloon hizo zilitokea mashariki ya mbali.
Nitaendelea kuwajuvya mambo nitakayokumbana nayo mjini humu kwani nitakuwepo hadi Jumamosi Mungu akipenda.

Sunday, November 11, 2007

Uchaguzi Zanzibar Ulikuwa huru?

MCHAKATO wa Uchaguzi Mkuu uliopita Visiwani Zanzibar ulitawaliwa na malalamiko mengi. Kati ya hayo yapo, na kwa hakika malalamiko mengi, yalielekezwa kwa Tume ya Uchaguzi visiwani humo (ZEC).

Malalamiko hayo yalihusu mwenendo wa uchaguzi huo, katika masuala kama uandikishwaji wa wapiga kura, uendeshwaji wa vituo vya kupigia kura na kuvunjwa kwa haki za wapiga kura.

Katika suala la uandikishwaji wa wapiga kura mathalan, yalikuwepo malalamiko kuwa wapo watu waliokuwa wamejiandikisha zaidi ya mara moja. Hili, kwa kiasi fulani lilikubaliwa na ZEC, wakalifanyia kazi na kutoa taarifa kuwa takriban watu 5,000 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja.

Lilikuwepo pia suala la kuandikishwa kwa watu ambao walikuwa hawajafikisha umri rasmi wa kujiandikisha (miaka 18).

Yapo malalamiko yaliyoelekezwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) hasa kuhusiana na matumizi ya vyombo vya dola. Ilidaiwa kuwa sehemu nyingi vyombo hivyo vilitumika kukandamiza wapinzani, hasa wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ndicho chenye wafuasi wengi wa upinzani visiwani humo.

Wakati huo, mengi ya madai haya, pamoja na mengine mengi yalikanushwa kwa nguvu zote na taasisi ambazo zilituhumiwa. ZEC ni mojawapo ya taasisi ambazo zilikanusha kasoro kadhaa walizotuhumiwa.

Vyombo vya dola navyo vilikanusha kuhusika na unyanyasaji wowote dhidi ya vyama na wapiga kura. ZEC ilikaa kimya wakati vyombo hivyo vya dola vikikanusha kuhusika na kuvunja taratibu za uchaguzi.

Lakini Tume hiyo ilipomaliza muda wake wa kuwa madarakani, iliandaa ripoti ambayo imewasilishwa kwa Rais Amani Karume, aliyewateua wajumbe na mwenyekiti wake. Kwa bahati nzuri sana, ingawa si yote, lakini mambo muhimu yaliyomo katika ripoti hiyo, yamewekwa hadharani.

Pamoja na hongera hiuzo, lakini lazima mshangao unaosababishwa na ripoti hiyo uonyeshwe wazi. Kikubwa kinachoshangaza ni kuwa kasoro nyingi zilizokuwa zimeanishwa wakati wa uchaguzi, ambazo ZEC na taasisi nyingine ilizikanusha, ndizo ambazo kwa kiasi kikubwa zinabainishwa kwenye ripoti ya ZEC.

Kwa sababu rekodi ya ZEC kukanusha mambo haya bado zipo, na sasa wanaibuka na ripoti inayoonyesha kuwa yale waliyoyakanusha yalitokea kweli, inabidi waje na msimamo ambao utatuweka sote kwenye uelewa mmoja kuhusiana na mambo hayo; yalitokea au hayakutokea? Ufafanuzi huo unatakiwa kwa sababu baadhi ya yaliyomo kwenye ripoti yanazua maswali mengi ambayo majibu yake hayapaswi kuwa ya kufikirika.

Mathalan, katika ripoti yao ZEC wanabainisha kuwa jumla ya watu 1,197 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja. Lakini ripoti za awali zinaonyesha kuwa watu zaidi ya 5,000 walibainika kujiandikisha zaidi ya mara moja. Kimetokea nini mpaka namba hii ikabadilika kiasi hiki?

Pia inapaswa ielezwe kinagaubaga, hao watu waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, wamechukuliwa hatua gani? Inafahamika wazi kabisa zipo sheria zinazoharamisha mtu kujiandikisha katika daftari wa kudumu la wapiga kura zaidi ya mara moja, pamoja na mambo mengine sheria hiyo imepanga adhabu kwa mtu au watu watakaobainika kutenda kosa hilo. Inapaswa ielezwe hapa watu hao ambao ZEC imebaini kuwa wamejiandikisha zaidi ya mara moja wamechukuliwa hatua gani.

Hili linapaswa kuelezwa kwa sababu kuna tetesi kuwa kati ya watu waliobainika kujiandikisha zaidi ya mara moja ni vigogo serikalini. Haiyumkini hawa wakaachwa hivi hivi. Hii ni kwa sababu iwapo wao hawakuona haya kutaka kuliingiza Taifa katika madhila yanayotokana na njama za kuvuruga uchaguzi, Serikali nayo haipaswi kuona haya kuwashughulikia ipasavyo.

Aidha, ripoti ya Tume hiyo yenye kurasa 70, imetoa lawama kali kwa vikosi vya SMZ, vikiwemo KMKM, JKU, Zimamoto, mafunzo na Valantia kwamba viliingilia kazi za ZEC. Vikosi hivyo vinashutumiwa kuwa wakati mwingine vilifanya maamuzi yanayohusu ulinzi wakati wa uchaguzi bila kuihusisha Tume.

Baya zaidi, ZEC inaeleza kuwa vikosi hivyo vilishiri katika kuwaandikisha askari bila ya kuihusisha Tume. Sote tunafahamu kuwa jukumu la uandikishaji wapiga kura ni la Tume, iwapo askari au mtu yeyote anataka kujiandikisha katika daftari la wapiga kura, analazimika kufuata taratibu zilizowekwa.

ZEC inaeleza kinagaubaga kuwa pamoja na kuchukua hatua ya kuwaita viongozi wa vikosi hivyo, lakini walikataa katika nyakati walizoombwa ili kwenda kurekebisha hali mbaya ya mambo iliyokuwa ikijitokeza wakati wa uandikishaji wapiga kura hasa katika mkoa wa Mjini Mgharibi.

Ripoti imesema viongozi wa Serikali za mitaa (Masheha) ambao ni
mawakala wa Tume hiyo, wakati wa uandikishaji wapiga kura walisikiliza ziadi maelekeo ya wakubwa wao kutoka Serikali za Mikoa na kupuuza maelekezo ya Tume hiyo.

Imeelezwa katika ripoti hiyo kwamba kuna baadhi ya vyama vya siasa
Vilifanya mbinu ya kuandikisha watoto wadogo chini ya umri wa miaka 18 kwenye daftari, huku wakijua kitendo hicho ni kinyume cha sheria.

Ripoti hiyo ilisema mbali kukubali kusaini maadili ya uchaguzi, baadhi ya vyama viliyavunja maadili hayo kwa sababu hayakuwa na nguvu za kisheria. Ndiyo maana sasa ZEC inapendekeza maadili ya uchaguzi yawe ni sehemu ya sheria za uchaguzi.

ZEC inagusia pia mambo nyeti likiwemo la taasisi yenye mamlaka ya kuongeza au kupunguza majimbo ya uchaguzi. Kwa mujibu wa Tume hiyo, suala hili lina utata wa kikatiba. Wakati Tume inaamini kuwa yenyewe ndiyo yenye mamlaka ya kufanya hivyo, lakini kwa utaratibu uliotumika, Baraza la wawakilishi ndilo lililopitisha uamuzi kuhusiana na suala hilo.

Kasori hizi pamoja na nyingine zilisababisha mivutano ambayo ilihatarisha uchaguzi huo. Lakini uchaguzi Zanzibar haukuishia mwaka 2005. Tunatarajia kuwa utafanya uchaguzi mwingine mwaka 2010 na nyingine nyingiz zitafuatia.

Ni vema tukaangalia tunakokwenda ili kujiepusha na matatizo yoyote ambayo yanaweza kutukwamisha katika jitihada zetu za kujenga taifa tajiri.

Hatupaswi kuangalia nyuma kwani tukifanya hivyo tunaweza kujikuta tunajiuliza maswali ambayo kimsingi yanaweza kutufanya tuone giza mbele na kushindwa kujua njia ambayo tunapaswa kuienenda.

Hata hivyo, yapo ambayo tunapaswa kujiuliza kwa ajili ya kuweka msimamo wa pamoja na kupanga mustakabali utakaotufikisha tunapokusudia kwenda. Ni lazima tujiulize na kupata jibu la iwapo hivi uchaguzi huo uliofanyika ukigubikwa na kasoro hizo zote, ulikuwa huru na wa haki kama ilivyoelezwa?

Friday, November 9, 2007

Rafiki wa Kweli...



Awali sikufahamu kuwa urafiki baina ya makomredi hawa (John Magufuli-kushoto na Raila Odinga-kulia) ni mkubwa kiasi cha Odinga aliposikia hivi karibuni kuwa Magufuli yupouwanja wa ndege jijini Nairobi akisubiri kuunganisha ndege kuelekea Kigali, aliamua kukatisha kampeni zake na kwenda kuteta naye. Na unajua nini? Waliteta kwa takriban saa moja ila walichozungumza hadi sasa inabakia kuwa siri yao. Hakika rafiki wa kweli....

Ni Siasa au Mwendelezo wa Vichekesho?

NIMESHANGAZWA, na kwa muda sasa nimekuwa nikijiuliza swali ambalo sipati jibu lake; Kwa nini ni rahisi kuwatofautisha Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yussuf Makamba na Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete? Si kuwatofautisha kwa umri, umbo, wajihi au sura, bali kwa kauli na hoja wanazotoa kuhusiana na chama wanachokiongoza na masuala makubwa yanayolihusu taifa.

Itakumbukwa kuwa nchi imegubikwa na mjadala kuhusiana na ufisadi na rushwa. Mjadala huu ulipamba moto kuanzia katikati ya mwezi Septemba, pale Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Dk. Wuilbrod Slaa, alipoamua kuyataja majina 11 ya viongozi wa serikali, akiwatuhumu kwa ufisadi.

Wakati majina haya yanatajwa, Rais Kikwete alikuwa nje ya nchi. Kabla ya waliotajwa hawajajitokeza hadharani, Kingunge Ngombale Mwiru (labda kwa niaba ya serikali) na Aggrey Mwanri, akitumwa na CCM wakati huo akiwa Katibu wa Uenezi, walitolea ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo. Watu wengi sasa wanajua walichokisema kilikuwa na mantiki gani.

Alipopata fursa ya kulizungumza hili, Kikwete alitoa kauli ambayo licha ya kutafsiriwa tofauti, lakini ujumbe wake mkuu ulikuwa thabiti; kuwa taarifa kuhusiana na tuhuma hizo zimefika serikalini na sasa zinafanyiwa kazi.

Na ndio maana akawataka waliotoa tuhuma watulie na kuviachia vyombo vingine vifanye kazi zake. Alisema si busara kwa watoa tuhuma wakajivika majoho ya taasisi nyingine. Wao wameshatekeleza wajibu wao kama raia wema. Hakumtisha mtu wala kumkejeli.

Makamba naye alipata nafasi ya kulizungumzia hili mjini Dodoma.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa ukimya wa CCM katika tuhuma zinazotolewa na wapinzani, zinatokana na busara waliyonayo viongozi wa chama hicho.

Aliendelea kusema kuwa viongozi wa chama hicho wanajua siri nyingi sana za hao wanaokirushia makombora. Kwa hiyo, iwapo kama CCM wakiamua kuwaumbua wapinzani, hata vyama vyao vinaweza kufa.

Lakini wiki chache kabla ya hapo, baada ya rais Kikwete kirejea toka Marekani ambako alikuwa wakati majina ya wanaotuhumiwa kwa ufisadi yalipotajwa kwa mara ya kwanza, alitoa kauli iliyoonyesha kuwa yanayosemwa yameifikia serikali na yanafanyika kazi. Na ndio maana akawataka baada ya kazi ya kutoa tuhuma, waviachie vyombo vingine kufanya kazi zake.

Kikwete alikuwa akizungumzia hoja za ufisadi lakini Makamba ameamua kuachana na hoja za ufisadi, sasa anaangalia boriti lililo katika jicho la mtoa tuhuma.

Inashangaza Makamba anamaanisha nini anaposema kuwa viongozi ndani ya CCM wanazifahamu siri nyingi za wapinzani wanaotoa tuhuma? Anawatisha, anawapa rushwa, anawakejeli au ndio kujibu mapigo huko?

Wakati ambapo mwenyekiti wake alishatoa msimamo wa serikali (unaweza vilevile kuwa wa chama), Makamba alipaswa kuwa mwangalifu sana na anachokisema kuhusiana na suala hili.

Ingekuwa vema iwapo Makamba angeelezea kwanza kutuhumiwa kwa viongozi wa Serikali ya chama chake, na jinsi wasivyohusika au wanavyohusika na ufisadi, alafu akatoa maelezo yanayotosheleza kujibu sakata la mikataba ya madini kabla hajageuka na kuanza kuwachambua wapinzani.

Labda aeleze kuwa hizo siri za wapinzani zitasaidia vipi kujibu hoja kuhusu tuhuma za ufisadi na rushwa katika mikataba. Kwa bahati mbaya sana, Makamba anazungumzia kuhusu siri za wapinzani wakati ambapo kumekuwa na taarifa zinazosambazwa kupitia mtandao wa intaneti kuhusiana na kashfa za baadhi ya viongozi wa wapinzani.

Taarifa hizo zinasambazwa kupitia barua pepe na moja ya taarifa hizo jina la msambazaji lifanana na la Makamba. Anataka tuelewe nini? Au ndio siasa yenyewe hiyo?

Wednesday, November 7, 2007

Tuogope kwenda Muhimbili?

KATIKA kipindi cha wiki mbili zilizopita, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imejiwekea rekodi mbili tofauti ambazo zitachukua muda mrefu kuvunjwa.

Kwanza iliibuka kashfa ya kuuzwa maiti. Ingawa watawala hospitalini hapo walijitahidi kulifunika suala hilo, lakini kila mwenye akili alifahamu kuwa kuna kosa kubwa la kitaaluma lilifanyika.

Ilibainika kuwa mtu aliyepewa dhamana ya kuangalia chumba cha kuhifadhia maiti, aliigeuza kazi hiyo kuwa ni aina fulani ya kujipatia ulaji. Labda ni katika muendelezo wa falsafa ya ‘kila mtu atakula mahali pake.’

Watu walibainisha kuwa si ajabu tukio limetokea kwani mtu aliyepewa jukumu la kuangalia chumba hicho, hana taaluma husika.

Katika utetezi wao, watawala hospitalini hapo walitaka jamii ielewe kuwa suala la kuuza maiti ni la kawaida. Sawa, ni la kaida. Lakini, kuna taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa katika kutekeleza suala hilo ambalo ni la kawaida. Je zilifuatwa? Kama zilifuatwa, manung’uniko yalitokea ya nini?

Lazima kuna jambo hapa, kwani haiwezekani suala lifanyike kwa kufuata taratibu zote alafu lije lizue manung’uniko. Kwa bahati mbaya sana, mtu aliyehusika na kashafa hii alitetewa na wakubwa nab ado anaendelea ‘kutesa’ kwenye nafasi yake.

Kwa kuwa uongozi ulikiri kuwa mtu huyo kweli aliuza maiti bila kufuata taratibu, itawawea vigumu watu kuamini sasa kuwa anapoendelea na kazi yake hatouza tena maiti bila kufuata taratibu. Huo ndio mtindo wake wa maisha kazini, hiyo ndiyo tabia yake, kutuambia kuwa atakuwa amebadilika kwa muda wa siku hizi chache zilizopita, tena bila kumchukulia hatua yoyote, itakuwa ni kutuongopea.

Huyo mtu hafai kuwepo katika chumba hicho. Maiti, pamoja na kuwa thamani yake ya uhai inakuwa imetoweka, lakini ni kitu ambacho bado kina thamani katika utu wa mtu. Haivumiliki kwa ndugu ambao wanajiandaa kumzika marehemu wao, wagundue kuwa maiti yake haipo. Uongozi Muhimbili unapaswa kufikiria upya juu ya kumuachia ofisa huyu wa chumba cha kuhifadhi maiti kuendelea na kazi hiyo.

Kana kwamba hiyo haitoshi, hospitali hiyo kubwa kuliko zote nchini imejiwekea rekodi nyingine. Kwa sababu ambazo zitaelezwa siku chache zijazo (kama zitakuwa ni za kweli au za kutetea uzembe haijalishi sana kwa sababu makosa yameshafanyika), madaktari hospitalini hapo waliamu kumchua mgonjwa aliyekuwa anaumwa goti, wakamfanyia operesheni ya kichwa. Na pia, wakamchukua yule aliyekuwa anahitaji matibabu ya kichwa, wakaenda kumfanyia upasuaji wa goti. Hatuna haja ya kusubiri maajanu na tisa ya dunia, haya yanatosha kuwa na sifa hiyo!

Tumeshaelezwa kuwa tutulie tusubiri matokeo ya uchunguzi unaofanywa na kamati iliyoundwa. Kamati hiyo bila shaka itaangalia sana mambo ya kitaluma na kujaribu kutafuta sababu ni nini kilisababisha makosa hayo yakatokea.

Lakini hata kwa mtu wa kawaida, ni vigumu sana kuamini kuwa lililotokea lilikuwa ni bahati mbaya tu. Si kwamba hakuna bahati mbaya, lakini iwapo taratibu zote kuhusiana na hatua za kumfanyia mgonjwa upasuaji zingefuatwa, hili lisingetokea.

Kimsingi taratibu hizo zimewekwa ili kuzuia makosa kama hayo. Haielezeki kuwa pamoja na taratibu hizo zote, bado suala hilo limetokea. Rekodi ya muda mrefu ya kutotokea kwa suala hilo, inaweza kutumika kama utetezi kuonyesha utendaji mzuri wa hospitali hiyo.

Lakini kwa upande wa pili, rekodi hiyo ya utendaji inaonyesha ni jinsi gani madaktari hao walivyo wazembe kwa sababu rekodi ya hospitali ni kufanya vizuri, hivyo makosa yanaweza kutokea tu kutokana na uzembe.

Suala la kuuza maiti lilitokana na kutofuatwa kwa taratibu na sasa suala hili la kuchanganya upasuaji wa wagonjwa, dalili zinaonyesha kuwa limetokana na kutofuatwa kwa taratibu. Huku kutofuatwa kwa taratibu ambako kunaibuka katika hospitali hii kubwa ndiko kunakonifanya nijiulize kuwa hivi sasa tunapaswa kuogopa kwenda Muhimbili? Kwa sababu yule jamaa aliyepasuliwa kichwa wakati anahitaji operesheni ya goti tu, hajaamuka hadi hivi sasa!

Joto Hili la Kidini Linatisha

SASA ni dhahiri kuwa mamlaka zinazohusika zinapaswa kuchukua hatua kuhakikisha kuwa masuala ya kidini yanawekwa katika mukhtadha unaofaa ili kuepusha migongano mikubwa kijamii.

Kuna kila dalii kuwa migongano mikubwa ya kijamii, ikisababishwa na tofauti za kidini ipo njiani na mtu anayefuatilia kwa makini malumbano na matukio kutokana na kuhusiana na hoja ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, atabaini hilo.

Uamuzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuliweka suala la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi katika Ilani yake ya uchaguzi unaweza kutajwa kuwa ndicho chanzo cha migongano hii inayozidi kukua.

Uamuzi huo ndio uliowafanya baadhi ya Waislamu, mwishoni mwa mwaka jana, waanzishe haratakati, kama aina ya shinikizo, wakiitaka serikali iharakishe uundwaji wa Mahakama hiyo kama ilivyoahidiwa katika Ilani.

Mmoja wa wanaharakati maarufu wa kidini, Sheikh yahya Hussein, aliitisha mkutano katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na kutoa historia ya suala hilo, kwa lengo la kuonyesha kuwa hakukuwa na ubaya wowote kwa Tanzania kuwa na mahakama ya aina hiyo.

Lakini suala hilo limepata sura mpya tangu Mchungaji Chritopher Mtikila wa Kanisa la Wokovu Kamili, aibuke siku za hivi karibuni na kufungua kesi Mahakama Kuu, akiitaka isitishe harakati zozote za taasisi yoyote, ikiwemo Serikali, kuanzisha Mahakama ya kadhi, kwa kuwa hatua hiyo inakinzana na katiba na nchi.

Tangu hapo, suala hilo limetawaliwa na vitisho na mabishano ya jazba, wakati mwingine bila kujali kuwa suala hilo tayari limeshafikishwa mahakamani.

Hali hiyo labda ndiyo iliyosababisha Mtikila aandike barua yenye maneno makali kwenda wa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na kusababisha akamatwe na polisi, ahojiwe na hatimaye kufikishwa mahakamani, akikabiliwa na kesi ya uchochezi.

Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa kesi mbili zinazohusiana na uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, makundi kadhaa ya kidini yameendelea kutoa maoni yao kuhusiana na suala hilo, na sasa taasisi nyingine zimeanza kuhusishwa katika kile kinachoonekana kutaka kuupanua mjadala wa kidini nchini.

Katika taarifa yake, Umoja wa Wainjilisti wa Kikristo Tanzania (Uwakita), sasa unalilaumu Jeshi la Polisi, kwa kuonyesha kile umoja huo unachokiita upendeleo wa kidini.

Uwakita unaamini kuwa Jeshi la Polisi wamekuwa wepesi kushughulikia Wakristo wanaotoa vitisho na kuwaachia Waislamu (tena baadhi yao viongozi) kwa kutoa vitisho na uchochezi wa aina hiyo hiyo.

Kauli hii ya Uwakita inatokana na hatua ya Jeshi la Polisi kumkamata, kumhoji na kunfungulia mashtaka Mtikila. Kwa mujibu wa Bullegi, Umoja huo unaamini kuwa Jeshi la Polisi halitendi haki linapowashughulikia viongozi wa kidini wanaortuhumiwa kutoa kauli zinazoashiria uchochezi na uvunjifu wa amani.

Umoja huo unasema kuwa kinachoendelea hivi sasa ni matokeo ya kufumbiwa macho kwa mihadhara ya dini ya Kiislamu, iliyoibuka enzi za utawala wa Awamu ya Pili, chini ya rais Ali Hassan Mwinyi.

Hili linadhihirishwa na matukio na kauli kadhaa za viongozi wa dini. Kabla ya kufikia hatua ya kuandika barua kwa Lowassa, Mchungaji Mtikila alikuwa ametishiwa maisha yake mara kadhaa na baadhi ya viongozi wa Kiislamu, tena wengine wakitumia vyombo vya habari, bila wahusika kuchukuliwa hatua zozote na Jeshi la Polisi, licha ya Mtikila kufikisha malalamiko yake.

Sheikh Yahya Hussein amewahi kutamka kuwa bila Mahakama ya Kadhi, damu itamwagika, lakini hajaeleza damu itakayomwagika ni ya nani. Haya si maneno ya kupuuza.

Yapo matamshi yaliyotolewa na Sheikh Khalifa Khamis na Ponda Issa Ponda, kuwa watamkata kichwa Mchungaji Mtikila kwa kutoa maoni yake juu ya Mahakama ya Kadhi.

Kwa maelezo yoyote yale, mwenendo huu wa mambo unaonekana dhahiri kuanza kulipeleka Taifa hili kule lisikostahili kwenda.

Ilani ya Uchaguzi ya CCM ni moja ya vyanzo vya tatizo hili na kimsingi viongozi wake na wale wa serikali wanapaswa kukaa na makundi ya kidini ili kuliweka suala hili sawa.

CCM inatambua kuwa, Serikali ya Tanzania kwa maelekezo ya waasisi wake waliokuwa wakitambua vyema athari za masuala ya kidini iliweka bayana kutokuwa na dini na hivyo kutojihusisha moja kwa moja na masuala yote ya kiimani.

Uamuzi chama hicho tawala, kwa sababu inazojua, iliamua kwa vitendo kukiuka misingi ya kisera na kimuelekeo wa waasisi wake ambao siku zote imekuwa ikitamba kuwaenzi na sasa taifa limeanza kuonja machungu ya maamuzi haya mabaya.

Kwa kutambua hilo, viongozi wetu wanapaswa kuchukua kila hatua ya wazi inayowezekana kuyaweka chini makundi yote ya kidini na kuiondoa serikali kuchukua mwelekeo wa kiimani kwa maslahi ya taifa hili ambao msingi wake tulishajengewa na waasisi wetu.

Si kwamba Mahakama ya Kadhi ni mbaya, la hasha. Kwa Waislamu ni chombo muhimu sana katika utekelezajiw a imani yao. Hivyo kuanzishwa kwake ni kwa manufaa makubwa kwao. Lakini kuanzishwa kwa Mahakama hii kusigeuke kuwa zahma kwa watu wengine.

Zipo njia mbazo zikitumika, kuna uwezekano wa kuwanzisha Mahakama ya Kadhi, bila kuathiri utendaji wa Serikali na imani za watu wengine. Utafutwe upenyo huo ili susla hili lisilete madhara kwa jamii.

Tuesday, November 6, 2007

Haya Ndiyo Mashitaka ya Dalali wa Rada

Mnaweza kuwa mmesikia kuwa yule bwana mkubwa aliyekuwa mtu wa kati katika deal ya ununuzi wa rada amefunguliwa mashitaka na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU). Lakini mnaweza kuwa hamjapata mashitaka halisi yanayomkabili bwana mkubwa huyo.
Nimebahatika kuiona hati ya mashitaka (Charge sheet) yanayomkabili, na nimeamua kuiweka hapa kwa tafsiri yake ambayo si rasmi (yenyewe imeandikwa kwa kiingereza na nimeacha mambo kadhaa ambayo nimehisi si ya msingi na hayabadili maana sana yaliyomo).
Inasomeka ifuatavyo;

KOSA LA KWANZA
Perjury (hii ni lugha ya kisheria wala sijui maana yake nini)
Kinyume na kifungu 102 cha kanuni ya adhabu.

MAELEZO YA KOSA
SHAILESH PRAGJI VITHLAN, mnamo Jumatano Julai 25, 2006, ulipokuwa mbele ya Hakimu Mkazi Katarina Revocati katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wilayani Ilala katika mkoa wa Dar es Salaam, ukitoa ushahidi kwa mujibu wa sheria, wakati ukifahamu, ulitoa ushahidi ambao si kweli kuhusiana na suala la serikali ya Tanzania kununua rada iliyoigharimu USD 39,972.450 kuwa ENVERS TRADING CORPORATION ilikuwa inamilikiwa na Pablo J. Espino na Adelina M. Estriby, jambo ambalo si kweli kwa sababu kampuni hiyo ilikuwa chini ya umiliki wake (Vithlan) kama mkurugenzi na alilipwa asilimia 31 ya bei ya rada ambayo ni sawa na USD 12,391,459 kama kamisheni ya kile kilichoitwa kuwa ni ushauri kwa mujibu wa mkataba kati ya RED DIAMONG TRADING CORP na ENVERS TRADING CORP.

KOSA LA PILI
Chini ya kidungu hicho hicho kilichotajwa hapo juu.

MAELEZO YA KOSA
SHAILESH PRAGJI VITHLAN, manmo Julai 28, 2006 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akiwa katika kiapo, alitoa ushahidi wa uwongo kwamba alilipwa na British Aero Space System (Bae System) USD 390,000 tu ambazo ni sawa na asilimia moja ya bei ya rada iliyonunuliwa na serikali ya Tanzania kutoka Bae Sysytem kama malipo ya ushauri alioutoa kwa kampuni hiyo.

KOSA LA TATU
Kusema uwongo mbele ya afisa wa serikali

MAELEZO YA KOSA
SHAILESH PRAGJI VITHLAN, mnamo Desemba 27 katika hoteli ya Sea Cliff, Dar es Salaam alimueleza KASSIM EPHREM ambaye ni afisa mwandamizi wa TAKUKURU kuwa yeye (Vithlan) alikuwa amelipwa asilimia moja tu ya bei ya rada kutoka Bae System, kauli ambayo alifahamu kwa si kweli na aliitoa kwa lengo la kuathiri upelelezi uliokuwa unaendeshwa na KASSIMU EPHREM kuhusiana na taratibu za ununuzi wa rada.

***********
Hati inaonyesha kuwa mashitaka yalifunguliwa Novemba Mosi, 2007 na hii ni kesi ya jinai iliyopewa namba 1474 ya mwaka 2007 na wala aihusiani na uhujumu uchumi au rushwa.

Monday, November 5, 2007

Kunani NEC?

Habari zinakuja toka Dodoma hivi sasa kuwa baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa, wapo waliozimia na wengine kuangusha vilio kama watoto wadogo. Hivi walipokuwa wanagombea hawakujua kuwa kuna kushindwa? Au walishajihakikishia ushindi? Kama ndio hivyo, sasa hiyo inayoitwa demokrasia ipo wapi?
Kwanza wanalilia nini? NEC yenyewe hukutana kama mara nne kila mwaka, hata kama posho yake ni sh 100,000 kwa siku, hivi vipesa hivyo ambayo wanalipwa kama posho vinalingana na mamilioni ambayo wameyatumia kufanya kampeni? Si afadhali wangebaki na mamilioni yao wakayatumbua kidogokidogo.
Kama hawalilii fedha, hivi kuna nini hasa kwenye NEC?

Kumbe wazungu wanapokuwa watoto wanakuwa hawana akili!!!


Kutoka asilimia 80 hadi kuzomewa

USEMI wa Rais Jakaya Kikwete, alipochukua uongozi wa nchi, kwamba anakusudia kuendesha uongozi wake akijenga katika yale yaliyofanywa na mtangulizi wake, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, unaweza kuwa na tafsiri nyingi sana. Wakati alipotoa msemo huo, (utabakia kuwa msemo mpaka utekelezaji wa yaliyoahidiwa utakapoanza kuonekana), wengi waliufasiri chini ya matumaini yao juu yake na kuuona kama sehemu ya ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

Wakati huo watu tayari walikuwa wameshayapima kwa undani yale yaliyofanywa na mtangulizi wake. Hivyo matumaini ya watu wengi yalikwenda kwenye muendelezo wa hayo na ndiyo maana watu walimuamini sana Kikwete alipoahidi kuwaletea kila mmoja wao maisha bora.

Na watu walifahamu nini kuhusu mtangulizi wa Kikwete? Walikuwa wakimfahamu Mkapa kama mtu ambaye alitumia muda wake wa uongozi kujenga uchumi wa Tanzania. Walimfahamu hivyo kutokana na yale yaliyofanyika ambayo yalikuwa yanaonekana dhahiri. Haikuhitajika kuwa na darubini au hadubini kuyajua hayo.

Katika kipindi cha miaka kumi ya kuwepo kwake madarakani, jambo kubwa na la msingi ambalo Mkapa alilifanya ni kufanikiwa kuutengamanisha uchumi mkuu (macro-economy).

Huu ulikuwa ni msingi ambao ulimjengea sifa ndani na nje ya nchi. Hapa nchini, hivi sasa, sifa hii ya Mkapa, pamoja na nyingine nyingi, zimeanza kupata tafsiri nyingine baada ya upande wa pili wa shilingi ya mambo aliyoyafanya Mkapa akiwa madarakani, kuanza kuwekwa wazi.

Tumesikia upande mmoja tu unaotoa tuhuma hizo, hatujasikia Mkapa mwenyewe anasema nini. Na haiyumkini kuwa tutamsikia akisema. Lakini hata kama tunapaswa kufanya uamuzi kuhusu tulichokisikia na ushahidi wake, na kuamua kuwa Mkapa aliyafanya yote anayotuhumiwa kuyafanya, haitafuta sifa zake, ikiwamo hii ya kuujenga uchumi mkuu.

Pamoja na mabaya yake yote (na kwa hakika anayo mabaya kwa sababu yeye ni binadamu tu), sifa hiyo itaendelea kuwepo na kudumu, hata kama baadhi ya watu hawatakubaliana na hilo.

Nalichukulia hili la kujenga uchumi mkuu kama msingi wa yote aliyoyafanya Mkapa, kwa sababu hilo ndilo jambo ambalo lilikuwa na mwelekeo wa kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania. Na kwa watu wa kawaida, iwapo watapata mahitaji yao muhimu, mambo mengine wala hayatawasumbua sana.

Iwapo mtu ana uhakika wa mlo kila siku, anapata uwezo wa kulipia ada watoto wake, anaweza kuipatia familia mahitaji yake yote muhimu na mwisho wa siku kuweza kuweka akiba, hata kama Mkapa aliiba mamilioni mangapi, hayatamuathiri sana kisaikolojia.

Ila itamuuma sana iwapo maisha yake yatakuwa ya shaka. Kila mara, anapokuwa na uhitaji wa kitu fulani alafu akakosa uwezo wa kukipata, mawazo yake yatamfanya aamini kuwa wizi uliofanywa na Mkapa ndio unaomsababishia leo hii akikose kitu hicho.

Na ukiangalia alipofikia Mkapa katika kuujenga uchumi, aliwafikisha Watanzania mahali pa kuleta matumaini. Na ninarudia kusema kuwa ndiyo maana Kikwete alipoahidi kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania akijenga katika yale aliyoyakuta, watu walimuamini sana. Walimuamini kwa sababu waliyaona hayo ambayo yamejengwa na Kikwete kuyakuta. Waliona kuwa ilibakia kazi ndogo tu ya kuufanya uchumi mkubwa uujenge uchumi mdogo (micro-economy), ambao kimsingi ndio unaomjaza mtu mafedha mfukoni.

Na kwa jinsi ilivyokuwa, uwezo wa uchumi mkuu wakati Mkapa anaondoka madarakani, ulionyesha dhahiri kuwa kazi ya kuujenga uchumi mdogo ni rahisi kwa kiasi fulani kwa sababu misingi ilikuwa imeshajengwa.

Mfumuko wa bei ulikuwa umeshuka kutoka tarakimu mbili na ulikuwa ukizidi kushuka. Hii ilimaanisha kuwa uwezo wa mtu kununua (purchasing power) ulikuwa ukiongezeka.

Akiba ya fedha za kigeni nchini ilikuwa ya kuridhisha, iliyotoa uhakika wa uchumi wa nchi kuhimili misukosuko ya muda mfupi na wa kati iwapo itabidi.

Makusanyo ya kodi yalikuwa yakiongezeka kila mwezi na kwa hakika kila mwisho wa mwaka, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ilikuwa ikitangaza kuvuka malengo iliyojiwekea.

Hii inamaanisha kuwa nchi ilikuwa na uwezo wa kulipia zaidi ya sehemu ya bajeti ambayo ilijipangia kulipia na mapato ya ndani, ndiyo maana kila mwaka asilimia ya utegemezi katika bajeti ilikuwa ikipungua.

Thamani ya sarafu yetu ilikuwa inajizatiti. Ni kweli kuwa ilikuwa ikishuka, lakini si kwa kasi ambacho tunaishuhudia hivi sasa. Hii ilionyesha kuwa mambo hayakuwa mabaya sana.

Lakini leo hii, takriban miaka miwili baada ya Kikwete kuingia madarakani tupo wapi? Mfumko wa bei unaelekea kwenye tarakimu mbili, kule ambako Mkapa alitutoa. Hapa mtu unaweza kujiuliza ni jinsi gani Kikwete anajenga uongozi wake katika yale aliyoyafanya Mkapa.

Ushahidi kwamba mfumko wa bei unapanda, unatolewa na Benki Kuu kila mwezi. Lakini hata katika maisha ya kawaida, hili linaonekana. Bei za bidhaa zimepaa kiasi kwamba watu wameanza kujiuliza maswali mengi yanayokosa majibu.

Mtafaruku kuhusu bei ya saruji wala bado haujatulia. Bei za vyakula zinabadilika kwa kasi kuliko kinyonga anavyoweza kubadili rangi zake. Kibaya zaidi ni kuwa mabadiliko hayo yanahusisha si tu kupanda, bali kupanda kwa tofauti kubwa mno. Leo si ajabu ukakuta bidhaa ikiwa imepanda bei mara mbili ya uliyoiona jana.

Lakini serikali imekuwa haiishiwi na visingizio na kutoa matumaini kwa kutumia takwimu. Tulitarajia kuwa hali ingekuwa mbaya mwaka jana baada ya msukosuko uliotokana na kukosekana kwa umeme. Lakini wakati wa tatizo hilo, serikali yenyewe iliwatoa Watanzania wasiwasi na kuwaeleza kuwa kila kitu kilikuwa kimedhibitiwa ipasavyo.

Na kama kawadia yao wakatumia takwimu, zilizoonyesha kupanda kwa makusanyo ya kodi ya kila mwezi kuhalalisha kauli yao kuwa kila kitu kipo sawa. Hamkujua kuwa kutoyumba kwa uchumi wa nchi kulitokana na misingi ya kuweka akiba ya kutosha fedha za kigeni kulikofanywa na Mkapa.

Leo hii uchumi wa nchi upo matatizoni. Hakuna kiongozi wa serikali au chama anayetaka kukiri hili hadharani. Wengi wanauchukulia uchumi kama sehemu ya siasa wanazopiga majukwaani. Na ndiyo maana tunaumia na tutaendelea kuumia iwapo viongozi wetu wataacha kuuona uchumi kama siasa.

Ndio wanauona uchumi kama siasa. Hii inatokana na jinsi wanavyotukoga. Haiwezekani mtu apange safari, akiwa ametinga magwanda ya kijani kibichi na nyeusi, akitumia gari la serikali, alafu anasema kuwa anaelezea uzuri wa bajeti huku hotuba yake ikianza na salamu za kidumu chama.

Uchumi haujui chama, unajua mipangilio na mambo kimahesabu. Ni utaalamu wa kimahesabu, si ujuzi wa kupiga domo jukwaani. Wanaweza kuwa mabingwa wa kuelezea uzuri wa bajeti kwa lugha tamu, zinazonakshiwa na vikorombwezo na vichekesho, lakini kama hesabu za kiuchumi hazijakaa sawa, kesho yake itajionyesha wazi kwa mfumko wa bei kupanda.

Hayo maneno matamu hayawezi kuifanya thamani ya shilingi isishuke. Thamani ya shilingi itaendelea kushuka na tofauti kati ya riba ya kuweka na kukopa kupanuka iwapo tutaishia kutoa maneno matamu jukwaani bila kuchukua hatua za kuidhibiti hali hiyo.

Iwapo watafanya mambo yanayotakiwa kudhibiti viashiria vya uchumi, wala hawatahitaji wajuzi wa kutunga mashairi ili kuwashawishi watu. Kila kitu kitaonekana dhahiri; hali ya mambo itabadilika, maisha yatazidi kuwa bora na hapo hata wasipowaambia Watanzania lolote, watafahamu kwa kweli serikali yao ipo kazini.

Miaka miwili iliyopita, asilimia 80 ya Watanzania waliichagua serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyopo madarakani. Huu ni ushindi ambao hadi hii leo bado umewalevya baadhi ya watu ndani ya CCM, kiasi kwamba hawaachi kuutajataja kana kwamba shida za Watanzania zitamalizwa na asilimia 80.

Hivi hawa viongozi wameshawahi kujiuliza kwa nini hao asilimia 80 waliowachagua juzi tu, leo wanaanza kuwazomea majukwaani? Yanatokea haya mara nyingi sana, na yanapaswa kuwa somo kwa viongozi wetu.

Lakini wao inaelekea wameamua wasiyaone. Inatisha sana kuwa wanaozomewa ni wao, lakini wakitoka hapo wanakanusha kuwa hawakuzomewa! Hivi ni kuwa wamelewa sana madaraka kiasi kwamba kelele za kuzomewa wao wanaziona kama za kushangiliwa? Siamini.

Kuzomea huku ni aina fulani ya wananchi kutoa hasira zao. Na namna yao ya kueleza manung’uniko yao. Lengo lao ni kutaka kilio chao kisikiwe na viongozi. Lakini viongozi wasiposikia kuzomea huko, na hata kufikia hatua ya kukanusha kuwa hawakuzomewa, wananchi watajua kuwa salamu zao hazijafika.

Watatafuta njia na mbinu nyingine ya kufikisha kilio chao. Na huu ndio utabiri ambao CCM siku zote imekuwa wakiambiwa lakini hawataki kuamini. Kwamba ipo siku, wananchi ambao wanajihisi kudharauliwa kwa kiasi cha juu na viongozi wao, ambao wakiwafikishia ujumbe na kilio chao hawakisikii, wataamua kutafuta njia na mbinu nyingine ya kufikisha kilio chao. Watafanya nini? Ni vigumu kujua sasa.

Lakini ni dhahiri kuwa chaguo la watakachokifanya litakuwa si kuwakumbatia viongozi wasiowasikia.

pnyanje@yahoo.com
pnyanje@gmail.com

KARIBUNI

Ninajilaumu sana kwa nini nimechelewa kuingia kwenye tekinolojia hii. Lakini kama walivyotueleza wahenga, kuchelewa si sababu ya kutufanya tusifike safari yetu. Nadhani hata kwa kuchelewa huku, bado tunaweza kuienenda safari hii na kufika. Hivyo waungwana, ningependa kuwakaribisha kwenye uwanja huu kwani sikuuanzisha kwa ajili yangu, bali kwa ajili yetu.
Naamini kuwa mchango wenu wa mawazo, katika kuchambua na kunyambulisha masuala, utatusaidia si tu kupanua uelewa wetu, bali kupanga mikakati ya kuleta mabadiliko yatajkayofanya maisha yetu ya leo yawe bora kuliko yalivyokuwa jan.
KARIBUNI SANA